Correspondance Course - Lesson 58

Somo la 58:

NEEMA YA MUNGU

Somo: Wafilipi 3

Tunavyokaribia mwisho wa kozi hii, inafaa tuyaangalie masomo yote na kukumbuka kile ambacho tumetaka kukipata. Tumeona kutoka katika Biblia kuwa, maisha mapya katika Kristo ni tofauti sana na maisha watu wanayoishi kabla ya kubatizwa. Ufuasi unataka kujizatiti kuufuata mfano wa Bwana Yesu Kristo, na anawataka watu wajipime kwanza kabla hawajafanya uamuzi kumfuata. Anasema:

“Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kama anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu ya kumalizia. Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini? Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule angali mbali. Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa wanafunzi wangu” (Luka 14:28-33).

Kuchagua kuwa mfuasi wa Bwana Yesu, ni uamuzi wa maana kuliko uamuzi mwingine wowote tunaoweza kuufanya katika maisha yetu ya sasa. Ni uamuzi utakaokuwa na matokeo kwetu kwa sasa, na katika enzi ya Ufalme unaokuja.

Mara nyingine watu wanakataa kufanya uamuzi wa namna hii kwa kuwa, wanasema hawawezi kuishi kulingana na inavyotakiwa kwao. Hili linasikitisha sana. Ufuasi sio mzigo mzito tunaoubeba wakati tunapobatizwa; ni kinyume chake kabisa. Bwana Yesu ndiye anayetubebea mzigo mzito tunaoubeba kwa sasa. Mwenyewe anasema:

“Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu. Kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi” (Mathayo 11:28-30).

Mfuasi anapobatizwa, hali ya ajabu ya uhuru na amani inamwingia katika maisha yake. Mizigo inayomvunja ya dhambi inakuwa imepokelewa; sasa anakuwa sehemu ya familia ya Mungu. Kwa lolote linalomtokea katika maisha haya, anajua Mungu amesema:

“Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi (‘mridhike’) na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa. Hata twathubutu kusema, Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa; mwanadamu atanitenda nini?” (Waebrania 13:5, 6).

Kujisikia kwa namna hii kunakuja, kwa sehemu, kutokana na kujitambua kuwa umekuwa huru mbali na dhambi. Ni karama inayotoka kwa Mungu; ni kitu kinachotokana na ukarimu wake. Hakitokani na kazi; sio malipo kwa namna yoyote. Ni kitu tunachokipata kwa neema tu ya Mungu. Paulo anasema:

“Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda; hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu, alituhuisha pamoja na Kristo, yaani, tumeokolewa kwa neema….. Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu” (Waefeso 2:4-9).

Neno ‘neema’ (au ‘rehema’) ni gumu kulitafsiri. Hata hivyo tunatambua, linamaanisha ‘upendeleo wa namna fulani’. Hatutakustahili kuokolewa kutokana na dhambi zetu. Wokovu unaotujea unatokana na upendo wa Mungu ambao ni mkubwa kwetu; tunaokolewa kwa neema iliyopo katika upendo huo. Hakuna wokovu bila ya imani katika hiyo neema.

Neno ‘neema’ tunalikuta kwa mara ya kwanza, katika maisha ya Nuhu: “Lakini Nuhu akapata neema machoni pa BWANA” (Mwanzo 6:8).

Tugundue hapa ya kuwa, Nuhu alipata neema. Kinachomaanishwa hapa ni kwamba, neema ni kitu tunachopaswa kukitaka na kukitafuta. Sio kitu kinachopatikana tu hivi-hivi. Hili ni jambo alilolielewa vizuri mtume Yohana, kwa kuwa alipokuwa akiiandika Injili yake alifundisha kuwa, tunaipata neema hasa tunapouangalia mfano wa Bwana Yesu Kristo:

“Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona Utukufu wake, utukufu kama kwa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli” (Yoh. 1:14).

Yesu mwenyewe aliwaambia Wayahudi wenzake:

“Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia. Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima” (Yoh. 5:39, 40).

Tunaipata neema; huo upendeleo tusioustahili kwa Bwana Mungu, tunapolisoma Neno lake, na zaidi tunapoyaangalia maisha ya Bwana Yesu Kristo, na kumwona mtu huyu aliyekuwa kweli na huruma, aliyeijua rehema, aliyekuwa tayari kufa kwa ajili ya wengine.

Tunajua kuwa Sauli wa Tarso alikuwa adui mkubwa wa waliokuwa wafuasi wa Bwana Yesu. Alishiriki katika kifo cha Stefano; aliyekuwa mfuasi wa kwanza wa Yesu kuuawa kwa ajili ya imani yake. Sauli alitaka kuiangamiza Eklesia kwa kuwaweka wafuasi gerezani (Matendo 8:3). Tunaambiwa katika Matendo 9 jinsi alivyopanga safari ya kwenda Dameski kutoka Yerusalemu, ili aweze kuwakamata wafuasi waliokuwa huko.

Alipokuwa safarini, Yesu aliyefufuka alimtokea, na mchakato ukaanza, kwa mamlaka na utukufu kumbadilisha Sauli, na kuwa mtume Paulo tunayemfahamu. Paulo alitiwa upofu katika jambo hili na Yesu akamwelekeza kuendelea mbele kwenda Dameski. Akiwa huko aliunganishwa na mfuasi mmoja aliyeitwa Anania, aliyempa kuweza kuona tena. Neno linasema:

“Anania akaenda zake, akaingia mle nyumbani; akamwekea mikono akisema, Ndugu Sauli, Bwana amenituma, Yesu, yeye aliyekutokea katika njia uliyoijia, upate kuona tena, ukajazwe Roho Mtakatifu. Mara vikaanguka machoni pake vitu kama magamba, akapata kuona, akasimama, akabatizwa” (Matendo 9:17, 18).

Kuna mawazo mengi ya kupendeza katika taarifa hii. Hebu ona vile neno la kwanza kabisa analosema Anania kwa Paulo linavyokuwa; ‘Ndugu’. Huyu ni mtu ambaye alikuwa akija Dameski kuwatia nguvuni Anania na wafuasi wengine! Lakini, Anania anajua kuwa Yesu amemwita awe mfuasi, na kwa hiyo, kama mshirika katika familia ya Mungu, ni ‘ndugu’ katika Kristo kwa Anania.

Neno ‘ndugu’ kwa kawaida, kiimani, ni kwa ajili ya wale tu waliobatizwa. Hapa Anania analitumia kwa kuwa amepata ufunuo wa moja kwa moja kutoka kwa Mungu juu ya Paulo.

Inaelekea upofu wa Paulo ulipokuwa ukimwondoka, mtu wa kwanza wa kumwona alikuwa mtu huyu aliyefanya muujiza huo; Anania. Jina Anania maana yake ni, ‘Mungu amekuwa wa neema’.

Kwa hiyo, kitu cha kwanza alichokiona kilikuwa ni mtu huyu aliyekuwa akisimama badala ya ‘neema ya Mungu!’ Paulo sasa alielewa kuwa, angeweza kuokolewa kutokana na dhambi zake kwa neema hiyo tu kwa kuwa, sio kwamba alikuwa amewezeshwa kuona tena kwa macho yake tu, bali alikuwa amepata kuona mambo yalivyo kwa namna ya kiroho. Hili lilipotokea, kitu cha kwanza ilikuwa kubatizwa.

Tunaambiwa na Paulo kuwa, baada ya hapo alikuwa na matatizo alivyokuwa akisafiri kuihubiri Injili. Mojawapo ya mambo yaliyompa shida sana ilikuwa ni ugonjwa uliompata, usiotibika. Alikuwa amemuomba Mungu mara tatu amuondolee tatizo hilo, lakini jibu lake kwake lilikuwa:

“Neema yangu yakutosha, maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu” (2 Wakor. 19:9).

Inawezekana Mungu alikuwa akimtaka Paulo amkumbuke Anania, na jinsi alivyopewa kuona mambo kiroho miaka mingi nyuma. Katika mazingira yote Paulo alitakiwa kuukumbuka upendeleo asioustahili alioupata, na hili limpe nguvu ya kuweza kukabiliana na changamoto zote za kimaisha na za ufuasi. Baadaye, akiwa amefungwa, aliweza kuandika akisema:

“Zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu, ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nimpate Kristo; tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani; ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake, ili nipate kwa njia yoyote kuufikia ufufuo wa wafu” (Wafilipi 3:8-11).

Alikuwa ni mtu aliyeacha kazi yake, marafiki, mali, madaraka na afya kwa ajili ya Bwana Yesu. Anatuambia, vitu hivyo havikuwa na maana yoyote tena kwake. Tunaelewa hapa kuwa, ujasiri alioupata Paulo, kwa kuielewa neema ya Mungu, alibakia nao kwa maisha yake yote yaliyobakia. Sehemu ya maneno yake ya mwisho aliyoandika yanatuambia hili:

“Kwa maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa, nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa, tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na mwokozi wetu, ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema” (Tito 2:11-14).

Kama Anania (ambaye ni ‘Mungu amekuwa wa neema’), alivyomtokea Paulo, ndivyo ambavyo Mungu amekuwa wa neema kwetu. Tumemjua Bwana Yesu Kristo, ambaye katika yeye tumepata neema.

Tunamshukuru Mungu kwa mambo haya yanayoijaza mioyo yetu, na kutupa nguvu katika uamuzi wetu wa kumfuata Bwana Yesu, kama wafuasi wake wa kweli. Ni neema ya Mungu tuliyopewa, inayotuonesha namna ya kuishi na kusema kwa wengine, ili tuweze nasi kuwa watu wa neema katika maisha yetu (Wakolosai 4:6).

Tunajua ya kuwa mara nyingine tutashindwa, lakini tunajua pia kuwa, kama tukizikiri dhambi zetu kwa Bwana Mungu, yeye ni mwaminifu na wa haki wa kutusamehe. Hatuna nguvu au uwezo, hatuna haki iliyo ya kwetu wenyewe mbele ya Mungu. Ni neema yake inayotufundisha kugeuzia migongo maisha haya, na kumfuata Bwana Yesu Kristo tukiwa ni wanafunzi wake. Ni neema yake inayotufanya tupende kufanya lililo sahihi na ndiyo itakayotuleta kwenye Ufalme wake:

“Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, Naam, naja upesi. Amina; na uje, Bwana Yesu. Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi nyote. Amina!” (Ufunuo 22:20, 21).

Swahili Title: 
Neema ya Mungu
Swahili Word file: 
PDF file: