Correspondance Course - Lesson 60

Somo la 60

HATUA INAYOFUATA

Somo: Matendo 2

Imekuwa ni furaha kushirikiana nawe katika kozi hii ya kujifunza Biblia. Kwa sasa tumefikia mwisho wa masomo haya, na pengine unajiuliza: Nini kinafuata, au kitu gani nifanye? Kabla hatujajaribu kukusaidia kwa maswali haya, ni muhimu kukumbuka kozi hii ni kwa ajili ya nini. Tumekuwa tukikuonesha mafundisho ya msingi ya Biblia.

Lakini ujumbe unaoupata kwenye masomo haya, haukuwa ujumbe wetu. Kila wakati ulipofunua na kuisoma Biblia yako, ulikuwa ukilisikiliza Neno la Mungu. Hivi ndivyo Mungu anavyowafundisha wanawake kwa wanaume juu yake mwenyewe, na kusudi lake na dunia hii. Ni kwa kuwa ulikuwa ukiliheshimu Neno la Mungu, ndio maana amekuwa akiongea nawe na akitegemea umwitikie.

Biblia yote ni Neno la Mungu, ni neno la pumzi yake, na lina nguvu ya kuweza kuyabadili maisha yako. Kama kwa kukuhubiria Injili kupitia katika kozi hii tumeweza kukusaidia, kwa kukufanya kuyaangalia Maandiko kwa undani mwenyewe, basi tumefanikiwa na tunashukuru.

Masomo haya yamekugusa?

Unaweza ukawa umejifunza mambo kadhaa ambayo hukuyajua kabla. Utakuwa umewafikiria ‘wakuu’ kama Ibrahimu na Daudi, na kuona vile ambavyo:

 • Injili inavyopatikana katika Agano la Kale kama ilivyo katika Agano Jipya.

 • Wayahudi walivyo mashahidi wa Mungu kati ya mataifa.

 • Bwana Yesu Kristo alivyozaliwa na kuishi ili kuwaokoa wanaume na wanawake wanaomwamini.

 • Kifo na ufufuo wa Yesu vilivyotoa uthibitisho wa mpango wa Mungu kwa nyakati zijazo.

 • Bwana Yesu Kristo atakavyorudi duniani kuusimamisha Ufalme wa Mungu.

Lakini kuyafahamu mambo haya sio kitu kinachotosha kwa chenyewe. Tunajua, wapo watu wengi tu wanaokwenda katika vyuo kujifunza dini ili kupata vyeti, au kupata ajira na kuwa wachungaji, lakini hili haliwafanyi wawe Wakristo. Jumuia yetu ya Kikristadelfia haitoi vyeti, diploma au digrii kwa kuifahamu Biblia. Tunaihubiri tu Injili kwa kuwa tunajua, Mungu anataka kuifikisha rehema yake kupitia kwa Kristo, kwa wote wale wanaotamani kuokolewa na dhambi zao.

Mungu anamwalika kila mtu anayeweza kuipokea Njia yake ya Wokovu, kuwa na sehemu katika Ufalme wake unaokuja duniani.

Kuwa Mkristo kuna maana gani?

Wakristo-wa-kweli ni watu wanaoziamini ahadi za Yesu, na ambao wamechagua wabatizwe na kuishi maisha ya kumfuata, wakijiandaa kwa huduma pamoja na Bwana atakaporudi kuwa Mfalme wa dunia.

Wakristo-wa-kweli ni watu walio tofauti na watu wengine kwa kuwa, wako katika kuitwa na kuandaliwa kwa ajili ya Ufalme wa Mungu katika dunia. Muumba anao mpango mmoja tu na dunia yake, na namna ya kuuitikia wito wake na kushiriki katika mpango huo ni moja, popote pale tunapoishi duniani.

Mungu hana kanuni fulani-fulani kwa watu walio India, na nyingine kwa nchi za Kiarabu au Afrika au Amerika au visiwa vya Pasifiki. Yupo Mwokozi mmoja tu, na namna moja ya kuweza kuokolewa: Mtume Petro alisema:

“Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hakuna jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo” (Matendo 4:12).

Kwa nini Makanisa ni mengi sana?

Unaweza ukajiuliza: “Ni kwa nini, basi, kuna makanisa mengi sana na vikundi vingi vya kidini?”

Hili ni suala linalowapa mashaka watu wengi, wanapofikiria kujiunga na jumuia yoyote ya Ukristo. Lakini ni hivi: sio Mungu aliyeyagawa makanisa katika ‘Ukristo’ kuwa Wakatoliki, Waprostanti au Walokole. Kwa sehemu kubwa ilikuwa ni tamaa za watu waliopenda kuwavuta watu wawafuate kuanzisha makundi mpya. Wengi walikuwa wajanja mno kuweza kusikiliza au kuyapokea mafundisho ya kawaida, tena ya kueleweka, yaliyopo kwenye Injili, kama yalivyofundishwa na Yesu na wanafunzi wake.

Walifanya kile alichotabiria mtume Paulo, akisema: “Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima, ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi-makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti (masikio ‘yanayowawasha’), nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo” (2 Timotheo 4:3, 4).

Mimi, Je?

Wakati wa kuitafakari KWELI unakuja tunapoanza kuelewa kuwa, sisi wote ni wadhambi mbele ya Mungu na kwamba, ni Mungu tu, kupitia kwa Yesu, anayeweza kutusaidia: “Kwa sababu, wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na Utukufu wa Mungu” (Warumi 3:23).

Lakini, Andiko linasema: “Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu” (Warumi 5:8).

‘Hatua inayofuata’ kwako itategemea haya mambo uliyojifunza kuhusiana na Neno la Mungu, kama yamekugusa kiasi gani. Sisi sote tupo katika njia ya kuutafuta wokovu, tunapokuwa tumeanza kujua ukweli unaotuhusu sisi wenyewe. Nabii Yeremia alisema:

“Ee Bwana, najua ya kuwa njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu” (Yer. 10:23).

Unajisikia hivyo, sijui? Neno la Mungu limeanza kukuvuta ufanye kitu kuhusu, kuutafuta, ‘Ufalme wa Mungu na haki yake?’ Kwa sasa au kwa baadaye, ni kila Mkristo anatakiwa aone haja ya kufanya mabadiliko katika maisha yake; mabadiliko ya kuacha kuwa mtu anayeendelea tu na dhambi; yaani, kuwa tu katika Adamu na kufa na kutokomea milele, na kuwa ‘mtakatifu’ katika Kristo, mtu mwenye tumaini la ufufuo atakaporudi Yesu na uzima wa milele katika Ufalme wake.

Wanaume fulani katika Yerusalemu, walipokuwa wameanza kuelewa ukweli ulivyo, walichomwa mioyo yao: “Wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?”

Jibu la Petro lilikuwa: “Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina la Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu” (Matendo 2: 37, 38).

Ni tumaini letu kuwa, utakuwa ukijifikiria kwa umakini. Unaweza ukawa na mashaka kidogo hapo ulipo; huhitaji mtu yeyote akusukume. Unahitaji muda kutafakari; tunalielewa hilo!

Pengine unaweza kuwa unataka tu kuendelea na kujifunza kwako Biblia kwanza, au kukutana na Wakristadelfia fulani kuongea nao kwanza juu ya mambo haya, au umeyaridhia mafundisho haya na unataka kubatizwa.

Kuna ushauri hapa wa kukusaidia

 1. Tafadhali yapitie tena masomo yote, somo la 1 mpaka la 59, ukiandika kwenye karatasi ugumu wowote unaouona na ukipigia mistari, mistari ya muhimu katika Biblia yako.

 2. Mwandikie mkufunzi wako umwambie jinsi unavyojisikia juu ya mambo uliyojifunza katika Biblia. Uliyafurahia masomo? Kulikuwa na mada zilizokuwa ngumu kwako, na ungependa kupatiwa maelezo zaidi juu ya baadhi ya mada?

 3. Umekuwa ukitumia mpango wa kusoma Biblia wa kila siku (Bible Reading Planner) na umepokea Mshirika wa Biblia (Bible Companion). Ni utaratibu wa kusoma angalau vifungu vitatu kwa siku, na utakuchukua uimalize Biblia yote kwa mwaka mmoja (Agano Jipya mara mbili). Endelea kuisoma Biblia kila siku. Sio kitabu cha kusoma na kuweka mbali na kama ukiisoma Biblia mara kwa mara, itakugusa moyo, akili na maisha yako.

 4. Utapenda uunganishwe na Wakristadelfia walioko karibu na wewe (kama wapo)? Unaweza kupenda kuwaandikia au kuwapigia simu kama unaona inafaa, au hata kuwatembelea kwa majadiliano zaidi ya Biblia. Kama wapo karibu ya kutosha, ungependa kuhudhuria baadhi ya mikutano yao?

 5. Ungependa kupata masomo zaidi kuhusiana na Biblia? Kama ni hivyo mwandikie mkufunzi wako, umwambie unataka kujifunza zaidi juu ya nini. Tunavyo vijitabu vya maana sana kuhusiana na mada nyingi.

 6. Kama unataka kuendelea mbele ubatizwe, lakini unajisikia kuhitaji muda zaidi na maelekezo, tuna kozi zingine. Mwambie mkufunzi wako.

 7. Kama unakubaliana na mada zote ulizozipitia katika kozi hii ya Biblia njia ya Posta na unafikiria kubatizwa, tuandikie utuambie.

Ninawezaje kubatizwa?

Kama ulivyojifunza katika somo la 31, ni muhimu kuwa uielewe vizuri Injili. Ubatizo ni kitu kikubwa, ni vizuri utambue na kuyakubali matokeo yanayoendana nao katika maisha yako. Ni jukumu letu kuhakikisha kuwa unaelewa hili kabla hatujakusaidia uweze kubatizwa.

Kwa hiyo kwanza tutakutumia maswali ya kujibu kwa Posta, maswali juu ya mafundisho ya msingi ya Biblia, na baadhi ya mambo ya kuzingatia kimaisha katika kuishi maisha ya Kikristo. Baada ya hili, kama utakuwa umefanya vizuri, tutapanga ili mmoja wetu au zaidi, kati ya waumini wenzetu akutembelee. Kama kweli umekuwa tayari kwa kubatizwa, hili litapangwa liwe mahali panapofaa, penye maji ya kutosha.

Kama kuna kikundi cha Kikristadelfia hapo jirani, utakuwa sehemu ya Eklesia hiyo. Kama hakuna, bado tutahakikisha kuwa unapata wakati wote machapisho mbalimbali ya kusoma na ya kuwapa rafiki zako. Tutakutumia pia makaratasi ya ‘mahubiri’ kwa ajili yako kuyatumia, katika Kumega kwako Mkate kila juma nyumbani kwako.

Kama utakuwa umeamua kubatizwa, hilo litakuwa tukio la muhimu kuliko yote katika maisha yako. Kuwa Mkristadelfia ni kuzaliwa katika familia ya Yesu Kristo, yenye ndugu duniani pote, walio na imani moja na ushirika wa hali ya juu na wewe.

Hatua yako inayofuata ni rahisi

Mwandikie tu mkufunzi wako, uambatishe kuponi iliyokamilishwa utakayoiona pamoja na somo hili.

Ukipenda, anaweza kukupatia ‘Maziwa ya Akili’; kozi nyingine ya Biblia yenye masomo 125.

 

Swahili Title: 
Hatua inayofuata
English files: 
Swahili Word file: 
PDF file: