CSSA 2-3-05 - THE TEMPLE OF SOLOMON

180. HEKALU LA SULEMANI

“Nyumba ninayojenga ni kuu, kwani ni Mkuu Mungu wetu kupita miungu yote”

Daudi mfalme wa Israeli mkuu (kuliko wote), alikuwa ametamani kujenga Hekalu kwa jina la Yahwe. Lakini Mungu hakumruhusu Daudi; na hiyo ikawa ni heshima ya Sulemani, ambaye jina lake linamaanisha amani na ambaye enzi ya ufalme wake ilijulikana kwa amani, ili ajenge jumba lile tukufu ambalxdwake. Na mara amani ilipopatikana akaanza kazi ya maandalizi ya kujenga Hekalu.

1 Wafalme 4-8; 2 Mambo ya Nyakati 2- 7.

MUNGU ANAIBARIKI ISRAELI CHINI YA SULEMANI – 1 Wafalme 4.
Sulemani akitumia hekima aliyopewa na Mungu, aliunda serikali nzuri na imara ambayo ilileta fulaha na yenye kuwaridhisha watu wote. Ufalme wa Sulemani ulienea kutoka mto Frati ukafika hata mpaka wa Misri. Sulemani alikuwa na amani pande zote kwani tunasoma ya kwamba “Yuda na Israeli wakakaa salama, kila mtu chini ya mdhabibu wake na chini ya mtini wake” (1 Wafalme 4: 25). Linganisha na maneno ya Mika (Mika 4:1-5) ambapo anatumia maneno haya haya kuelezea ufalme ambao Yesu Kristo atausimamisha.

HEKIMA YA SULEMANI IMEANDIKWA KWA AJILI YETU – 1 Wafalme 4: 29-34.
Hekima ya Sulemani siyo tu ilimpatia ufahamu wa kuzizua njia za Mungu, bali pia ilimpatia ufahamu wa kuvijua viumbe ambavyo Mungu aliviumba Maana alizungumzia habari za miti, akanena habari za wanyama, za na vitambaavyo, na za ndege na samaki “Akanena mifano 3, 000 na nyimbo zake zilikuwa 1005” (mstari 32). Kati ya maneno yake mengi ialiyosema yameandikwa kwa ajili yetu kwenye vitabu vya Mithali na Mhubiri na Wimbo ulio Bora. Maneno yake hayaaliyoyasema yaliandikwa ili kwamba “sisi tupokee maneno yake na kuheshimu (kizishika) Amri za Mungu ili tuelekeze masikio yetu tusikie hekima na kuuelekeza mioyo yetu tupate ufahamu” (Mithali 2: 1-2).

SULEMANI ANAANDAA VIFAA KWA UJENZI  -  1Wafalme 5:2; Mambo ya Nyakati 2.
Sulemani alibarikiwa sana, kwani hazina na vyombo vingi vya kutumia katika Hekalu vilikuwa vimekwisha kukusanywa na Daudi miaka mingi kabla (angalia 1 Mambo ya Nyakati 22: 14-16). Daudi pia aliwajibika kwa baraka nyingine ambayo ilikuwa ya thamani kubwa sana kwa Sulemani katika ujenzi. Tunajifunza kutoka 1 Wafalme 5: 1 kuwa Hiramu, mfalme wa Tiro “daima alikuwa anampenda Daudi”, hivyo tunaona kwamba alikuwa na furaha wakati Sulemani alipoomba miti ya mierezi kutoka Lebanoni. Patano la amani likafanyika kati ya Hiramu na Sulemani, na kwa hiyo ombi lake kupewa mbao ulikubaliwa. Sulemani angechangia kutoa watumishi na kundi la watu 30,000 lilitayalishwa kwa kusudi hili, Ili kuhakikisha kwamba watu hao watakuwa na furaha katika kazi yao, Sulemani aliwaweka katika vikosi vya watu 10, 000 kila kipindi ambao walitumika kwa mwezi mmoja huko Lebanoni – na miezi miwili nyumbani kabla ya zamu yao iliyofuata. Zaidi ya watu hao 30,000 wengine 70,000 walihusika katika kubeba mizigo mbali mbali na wengine 89,000 walitumika katika kuchonga (kukata) mawe kwenye milima iliyo karibu na Yerusalemu. Hawa wau 50,000 walichukuliwa kati ya wageni walioishi katika taifa la Israeli, na ukijumuisha pamoja na watumishi wa Tiro, watu wengi sana wa mataifa (wapagani) walihusishwa katika kujenga Hekalu la Mungu wa Israeli (tazama 2 Mambo ya Nyakati 2: 17). Waangalizi 3,000 walikuwa ni maakida (viongozi) wa mfalme mwenyewe (1 Wafalme 5:16). Hivyo jumla ya kutisha ya watu 183,300 waliajiriwa kwenye kazi hii ya kujenga nyumba kwa ajili ya utukufu wa Jina la BWANA.

UJENZI WA HEKALU NA MAELEZO YAKE – 1 Wafalme 6: 7; 2 Mambo ya Nyakati 3:4.
Eneo lililochaguliwa kwa ajili ya Hekalu ilikuwa ni Mlima Moria mahali ambapo BWANA alimtokea Daudi. Ujenzi ulianza katika mwezi wa pili wa mwaka wa nne wa enzi ya Sulemani na ukamalizika katika mwezi wa nane wa mwaka wa kumi na moja wa enzi yake kwa hiyo miaka saba na nusu ilitumika katika kujenga. Hekalu halikuwa kubwa kulinganisha na majengo ya mataifa yaliyoizunguka, lakini matumizi makubwa sana ya dhahabu iliyowekwa kwa mistari kuzunguka ndani kwnye kuta, na hazina nyingine zenye thamani zilizowekwa ndani, zililipatia Hekalu utukufu mkuu wa uzuri usio kifani. Sawa na Hema la Kukutania kabla yake, muundo wa Hekalu, na samani zake, na kazi ya ukuhani zilifundisha masomo yale yale ya kiroho tuliyojifunza kutoka masomo yetu yaliyotangulia juu ya Hema la Kukutania. Katika vipimo vyake Hekalu lilifanana na Hema la Kukutania, likiwa na vipimo vikubwa zaidi na vyenye mapambo yenye thamani na utajiri zaidi wa mapambo. Jengo lilikuwa na chumba cha mbele chenye urefu wa mikono ishirini na Upana wa mikono kumi. Mahali patakatifu urefu wa mikono arobaini na upana wa mikono ishirini, na Patakatifu pa Patakatifu tena palikuwa mikono ishirini mraba. Kwenye behewa la nje (1) madhabahu ya shaba, ambayo juu yake zilitolewa dhabihu, (2) Bahali ya Kusubu iliyotegemezwa iliyotegemezwa (kubebwa) na ng'ombemaksai kumi na mbili, iliyotumiwa na makuhani kwa ajili ya kujiosha, (3) mabirika kumi ya shaba, iliyotuniwa kuosha dhabihu (matoleo ya kafara). Mbele ya mahali patakatifu palisimamishwa nguzo mbili za shaba, moja ikiitwa “Yakini” (“Mungu atathibisha”), na nyingine ikiitwa “Boazi” (“Imo nguvu”). Hizi nguzo mbili zilimwakilisha mwanadamu ambaye ametiwa nguvu kwa msukumo wa kiroho utokao kwenye Neno la Mungu. Katika mahali patakatifu palisimama, (1) vinara kumi vya taa vya dhahabu, vitano kila upande, (2) meza za dhahabu kumi, tano kila upande, kwa ajili ya mikate ya wonyesho, (3) madhabahu ya dhahabu ya kufukiza uvumba ambayo kwa yakini iliwekwa mbele ya pazia karibu na Patakatifu Pa Patakatifu. Pazia, lilitenganisha mahali Patakatifu na Patakatifu Pa Patakatifu, liliwakilisha ukombozi uliofikiwa na Mungu katika Kristo, na pazia hilo lilikuwa na rangi ya bluu, hudhurungi, na nyekundu, lililotengenezwa kwa kitani safi na kuzungushiwa mapambo ya Makerubi. Ndani ya Patakatifu Pa Patakatifu, ambapo palisimamia ukamilifu, mlikuwemo makerubi ya dhahabu mawili ambayo yalielekeza uso kwenye pazia na ambayo mbawa zao zilikuwa zimekunjuliwa hadi zikagusana na kugusa kuta za upande mwingine. Wakati wakuingia ndani ya Patakatifu Pa Patakatifu, kuhani mkuu ilimbidi awatazame makerubi wakiwa wametandaza mabawa yao katika chumba chote upande wa kulia. Chini ya mabawa hayo ya makerubi yaliyokunjuliwa paliwekwa sanduku la Agano, likiwa na zile mbao mbili za mawe yenye amri kumi. Zaidi ya Hekalu na thamani zake, vyombo vingine mbalimbali vilitengenezwa kama vile vyungu, makoleo, vishikio, vinusio, mabeseni, na vijiko. Vitu hivi vilitengenezwa na Hiramu wa Tiro, ambaye alikuwa mtaalamu katika shaba. Mwongozo maalumu wa Biblia umetayaliswa. Kinaonyesha namna tatu za mwonekana wa Hekalu la Sulemani, na andiko lililoambatanishwa linaelezea mfano wa umbile la kiroho kuhusu muundo wake wa jengo na vifaa vya thamani vilivyokuwemo. Kila msomi inampasa kupata nakala.

HEKALU LAFUNGULIWA – 1 Wafalme 8:2; Mambo ya Nyakati 5
Sasa baada ya miaka saba na nusu ya ujenzi, Hekalu lilikuwa tayari kufunguliwa. Sulemani na wazee wote wa Israeli wakakusanyika kushuhudia tukio la kushangaza la Sanduku la Agano kuletwa hadi mahali pake pa kukaa ndani ya Hekalu. Ilikuwa katika mwezi wa saba kwenye siku kuu ya vibanda wakati makuhani walipo lipeleka sanduku pamoja na vyombo vyote vitakatifu ambavyo vilikuwamo ndani ya Hema na kuvileta katika Hekalu. Sulemani na watu walitoa dhabihu kondoo na mafahari kwa wingi sana. Kisha sanduku liliwekwa ndani ya Patakatifu Pa Patakatifu, ambapo liliwekwa chini ya mabawa za makerubi. Na ndani yake zilikuwemo zile “mbao mbili za mawe alizoziweka Musa alipokuwa huko mlima Horebu” (1 Wafalme 8:9). Ndipo waimbaji wote na wana muziki wenye matoazi, vinanda na vinubi na pamoja na makuhani 120 wenye tarumbeta wakamsifu BWANA wakisema “Msifuni BWANA kwa kuwa ni mwema kwa maana rehema zake ni za milele” (2 Mambo ya Nyakati 5:12-13). Ndipo Hekalu lote likajawa na wingu moshi, hata makuhani hawakuweza kuona kwa sababu ya lile wingu “kwa kuwa nyumba ya Mungu imejaa utukufu wa BWANA” (mstari 14).
 
SALA YA SULEMANI WAKATI WA KULITAKASA HEKALU – 1 Wafalme 8:2; Mambo ya Nyakati 6
Moyo wa Sulemani ulijaa furaha wakati alipoomba sala ya utakaso. Alipiga magoti kwa unyenyekevu na kuinyosha mikono yake kuelekea mbinguni na kusema; “Ee BWANA Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe mbinguni, wala duniani ushikaye maagano na rehema kwa watumishi wako” (2 Mambo ya Nyakati 6:14). Sulemani akaendelea kusema kwamba Mungu kwa rehema zake amewaruhusu wana wa Israeli kujenga Hekalu hili kubwa. Alifahamu kwamba Mungu hawezi kukaa katika nyumba ndogo (mstari 18), Lakini alimwomba Mungu kila wakati kuiiangalia nyumba ambayo imejengwa kwa ajili ya jina lake (mstari19 – 12). Akamwomba Mungu kusikia sala za watu wake wakati watakapokuwa katika mafanikiwa na wakati watakapokuwa katika dhiki. Sulemani alihofia kwamba siku moja watu wangemwasi BWANA kama walivyokuwa wamefanya hapo zamani, hivyo alimwomba msamaha kwa ajili ya mazingira haya. Ni jambo la maana sana kwamba Sulemani katika sala yake alitamka ombi maalumu kwa ajili ya mgeni atakayependa kumwabudu Mungu wa Israeli (mstari 31-33). Alikuwa na shauku ya kuwa ulimwengu wote ungejifunza kumjua BWANA na kumwabudu Mungu katika Kweli. Na mwisho alimwomba Mungu kusikia sala zote zinazotolewa mahali pale na kuilinda enzi ya ufalme wa Daudi (mstari 40- 42). Kwake Sulemani kulitasa Hekalu ilikuwa tu ni ishara itayokuwa ya siku ya utukufu mkuu zaidi wakati dunia yote itakapojawa na utukufu wa BWANA na watakatifu wake wakitawala kwa amani.

MUNGU ANAIKUBALI SALA YA SULEMANI NA KUJIWEKA WAKFU KWA WATU - 2 Mambo ya Nyakati 7:1-11.
Wakati Sulemani alipomaliza maombi, moto ulishuka kutoka mbinguni na kuziteketeza sadaka za kuteketezwa Mungu alikuwa akimwonyesha Sulemani na watu kwamba, sala yake ilikuwa imekubaliwa. Watu wote wakasujudi kifulifuli hata chini wakamwabudu na wakamshukuru BWANA, wakasema, “kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele” (mstari 3). Ulikuwa ni wakati wa sikukuu ya Hema la kukutania ambapo Hekalu lilipofunguliwa. Idadi kubwa ya watu walihudhuria ili kushuhudia sherehe ya uzinduzi wa nyumba ya sala. Idadi ya sadaka nyingi zilitolewa na Sulemani na watu. Sulemani peke yake alitoa ng'ombe 2,000 na kondoo 120,000. Watu walifurahi sana na kuchangamka moyoni naye Sulemani, “akawaruhusu watu waende hemani kwao, wakifurahi na kuchangamka shangilia mioyoni kwa wema wote ambao, BWANA aliomfanyia Daudi na Sulemani na kwa Israeli watu wake”(mstari 10).

ONYO LA DHATI LA MUNGU KWA SULEMANI – 1 Wafalme 9: 1-9; 2 Mambo ya Nyakati 7:12 – 22.
Mungu alikuwa amedhihirisha kukubali sala ya Sulemani kwa kushusha moto kutoka mbinguni. Baadaye Mungu alimtokea Sulemani katika ndoto ya usiku kwa maneno ya faraja na yenye maonyo. Alithibitisha tena ahadi yake ya kuwabariki wana wa Israeli iwapo wangemrudia Mungu katika Kweli. Mungu aliahidi kwamba macho yake yangekuwa wazi na ataelekeza masikio yake kusikiliza maombi yao. Na kama Sulemani atatembea mbele ya Mungu kama alivyofanya Daudi, babaye ndipo Mungu kwa hakika angekuwa pamoja naye “Ndipo nitakapokifanya imara kiti cha enzi cha ufalme wako juu ya Israeli milele kama nilivyomwahidi Daudi baba yako, aliposema, “Hutakosa kuwa na mtu wa kukaa katika kiti cha enzi cha Israeli” (1 Wafalme. 9: 5). Na kwa upande mwingine, iwapo Sulemani atajitenga kutoka kwa BWANA na kuziacha sheria zake na amri zake, wakawatumikia miungu mingine na kuiabudu, hapo ndipo siyo Hekalu lenye utukufu tu litakalo kuwa ukiwa, bali pia Israeli watafukuzwa watoke katika nchi na kuwa “mithali na neno la tusi katika mataifa yote” (mstari 7-9) (linganisha Kumbukumbu la Torati 28:36;37). Lakini licha ya onyo hili, Sulemani katika miaka yake ya baadaye aliziacha njia za BWANA.
 
FUNDISHO KWETU:
Ni dhahiri kuwa Hekalu la Sulemani lilikuwa jengo lililotukuka. Lakini hili lilikuwa halina maana ikiwa moyo wa Sulemani pamoja na Israeli mioyo yao haikuwa sawasawa machoni pa Mungu. Sisi pia, tukiwa watoto wachanga wa Mungu, ni lazima tutambue matendo yetu kuwa ndiyo ya muhimu machoni pa Mungu. Kuna hatari ya kuyathamini mambo yanayoonekana nakuvutia kwa macho, ambapo yeye Mungu huangalia moyo. “Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele ambaye jina lake ni Mtakatifu; Asema hivi; Mimi nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliyenaroho iliyotubu na kunyenyekea.” (Isaya 57:15).

REJEA KATIKA MAKTABA:
 “Historia ya Biblia” (H.P. Mansfield) - Kitabu cha 4 Namba 8.
 “Sheria na Neema” (W.F.Barling) - Sura 5.
 “Sheria na Neema” (R. Roberts) – ukurasa 95-154.

MASWALI YA FUNGU
1. Wakati Sanduku lilipoletwa pale mahali pa kukaa Hekaluni ni kwa jinsi gani Mungu alionyesha uwepo wake?
2. Ni kwa namna gani Mungu alimwonyesha Sulemani kwamba alilikubali ombi lake?
3. Ni onyo gani la mhimu BWANAalimpatia Mfalme Sulemani na kwetu leo?

MASWALI YA ISHA (UTUNGAJI):
1. Fafanua Hekalu la Sulemani na samani zake eleza jinsi migawanyo mitatu ya Hekalu na samani zake zinavyotufundisha jinsi tunavyoweza kukubali kumkaribia Mungu.
 2. Fafanua sherehe ya uzinduzi wa Hekalu la Sulemani.
 

Swahili Title: 
HEKALU LA SULEMANI
English files: 
Swahili Word file: