Bible Prophecy

Submitted by Editor on Tue, 08/14/2018 - 11:48
Swahili
UNABII WA BIBLIA
UTHIBITISHO KWAMBA MUNGU YUPO
Biblia ni kitabu cha ajabu kuliko vyote. Maelezo yake kuhusu chanzo cha 
uovu; taarifa yake isiyo na kasoro kuhusu mahusiano ya Mungu na taifa la Israel; 
ujumbe wake unaopenya kupitia kwa manabii wao; 'habari njema' yake 
iliyohubiriwa na Yesu Kristo na mitume wake; na juu ya yote uchambuzi wake 
sahihi uhusuo mapungufu ya silka ya mwanadamu ukilinganishwa na utakatifu, 
kweli na rehema ya Mungu, iliyodhihirishwa zaidi hasa katika Mwanawe - haya 
yote ni mambo ya kipekee yasiopatikana katika kitabu kingine chochote 
duniani. Haya yalimfanya Henry Rogers, miaka 100 iliyopita kusema: "Biblia sio 
namna ya kitabu ambacho mwanadamu angekuwa ameandika kama 
angeweza, au angeweza kuandika angeweza". Kwa maneno mengine, Mungu 
anahitajika katika kuelezea uwepo wake.

Katika kazi hii fupi tutaangalia mojawapo ya mambo yake ya ajabu: 
unabii wake. Kihalisi, unabii sio kuelezea tu mambo ya mbeleni. Nabii alikuwa ni 
mtu 'aliyesema kwa niaba' ya mwingine, msemaji; na unabii ulikuwa ni ujembe 
alioutoa nabii kwa niaba ya Mungu. Lakini kwa kuwa unabii wa Biblia unao pia 
'utabiri' mwingi wa mambo yajayo, kwa lengo hili tu tutazingatia maana hiyo 
hapa.

NANI MWENYE MAMLAKA YA UNABII?
Lakini kwanza inabidi tukubaliane juu ya swali moja la muhimu: Biblia 
inadai kwamba mamlaka ya unabii inatoka kwa Mungu tu na ni uthibitisho wa 
uweza wake?

Kwa hili lipo jibu muafaka katika unabii wa Isaya. Katika kifungu cha 41 
Mungu anazitaka sanamu na wanaoziabudu wa nyakati zile kuthibitisha kama 
wanazo nguvu za kiungu. Hivi ndivyo anavyoziambia:
"Haya leteni maneno yenu, asema BWANA; toeni hoja zenu zenye nguvu, 
asema Mfalme wa Yakobo. Wayatangaze na kutujulisha yatakayokuwa; 
watuonyeshe mambo ya zamani, ni mambo gani, tukapate kuyatia moyoni, 
tukajue mwisho wake; au wamdhihirishie yatakayotokea baadaye." (Ms. 21 - 22)

Msingi wa changamoto hii ni dhahiri: Wanaoabudu kipagani wanadai 
kuwa sanamu zao ni Miungu. Sawa; wathibitishe basi! Na uthibitisho unaotakiwa 
na Mungu mwenyewe ni kwamba sanamu zitabiri mambo yajayo na pia 
kutangaza 'yaliyopita', yaani kueleza jinsi uumbaji ulivyokuwa hapo mwanzo. 
Katika msitari unaofuata dhana hii iko wazi sana.
"Tujulisheni yatakayokuwa baadaye, nasi tutakiri ya kuwa ninyi ni miungu...." 
(Ms. 23)
Hapa Mungu mwenyewe anatujulisha kwamba kuweza kutabiri mambo 
yajayo ingekuwa uthibitisho wa uweza wa kiungu. Kwa zaidi ya mara moja 
katika sehemu hii ya unabii wa Isaya, Mungu anatangaza ya kwamba Ni yeye 
pekee aliye na uwezo huo; kwa kuwa Ni yeye pekee aliye Mungu, hakuna 
mwingine.
"Kumbukeni mambo ya zamani za kale; maana mimi ni Mungu, wala hapana 
mwingine, mimi ni Mungu, wala hapana aliye kama mimi......" (46:9)
Mungu wa Israeli hapa anatangaza kwamba hakuna kitu kinachostahili 
kuabudiwa ila yeye; na anaendelea kusemea ishara za nguvu zake kwa maneo 
haya.
"...nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo 
yasiyotendeka bado; nikisema, shauri langu litasimama, nami nitatenda 
mapenzi yangu yote." (46:10)

Lifikirie, nani awezaye kusema, "Mapenzi yangu yatasimama..." zaidi ya 
Mungu? Ni nani katika dunia nzima awezaye kusema kitu kama hicho? Kusemea 
hili inahitaji mwenye uwezo wa kujua mambo yajayo kabla hayajatokea, lakini 
awezaye kuhakikisha yanaenda alivyopanga. Kwa maneno mengine, kutoa 
unabii utakaotimia kwa vyovyote, unamhitaji Mungu. Hakuna namna nyingine 
ya kuelezea.

Agano jipya linadai hivyo hivyo. Wakati Yesu alipokuwa anakaribia 
kuwaacha wanafunzi wake, aliwaahidia msaada wa Roho Mtakatifu katika 
jukumu lao la kuihubiri injili duniani. Mojawapo ya matokeo ya karama hiyo 
ingekuwa, "na mambo yajayo atawapasha habari yake." (Yoh. 16:13); kwa 
maneno mengine wafuasi wangepewa ufahamu wa mambo yajayo. Kwa 
vyovyote inamaanisha wasingepewa karama hiyo ya kipekee wasingeweza 
kuyajua. Uweza wao kutambua yajayo ndio ungekuwa ushahidi wa nguvu ya 
kiungu waliyotunukiwa.
Tena, katika kitabu cha mwisho cha Biblia, kifungu 1, msitari 1, inaelezwa 
kwamba Mungu alimpa Yesu Kristo Ufunuo, "awaonyeshe watumishi wake 
mambo ambayo kwamba hayana budi kuwako upesi..." (Uf. 1:1). Ufahamu wa 
mambo yajayo ulitoka kwa Mungu, kupitia kwa Kristo; bila ufunuo huo watumishi 
wake wasingelijua lolote linalouhusu.
Hitimisho ni wazi: Biblia inasema kiuhakika ya kwamba uweza wa kutabiri yajayo 
ni wa Mungu pekee.

BIBLIA INATABIRI YAJAYO?
Tunaweza tu kuchunguza historia na uzoefu wetu kutambua kwamba 
wanadamu kwa jinsi walivyo, hawawezi kujua hata kidogo ya mbeleni. Kwa nini? 
Hatuwezi hata kujua litakalotupata usiku wa leo, au kesho tukienda kazini, 
achilia mbali mwaka kesho; au litakaloipata dunia katika miaka 100, hata 
tusiposemea miaka 2000! Watu wangekuwa na utambuzi kidogo tu wa mambo 
yajayo, maamuzi mengi yangebadilika kiasi gani! Ajali nyingi kiasi gani 
zingeepukwa! Maafa mengi kiasi gani yasingeliachiwa yatokee. Vita vingi kiasi 
gani visingeanzishwa! Uzoefu katika maisha yetu wenyewe, na wa historia ya 
mwanadamu unatuonyesha kuwa mwanadamu hana ufahamu wowote wa 
hakika wa litakalotokea.
Lakini chukulia kwamba mambo yajayo yameelezewa, sio mara moja, 
bali mara nyingi. Na kwa nyakati zote katika kitabu hicho hicho, Biblia na sio 
katika kingine chochote duniani! Halipaswi hilo kutufanya tukae chini na 
kuzingatia? Ndio maana tunasema kwamba unabii wa Biblia ni wa maana sana, 
na unapaswa kuchunguzwa kwa makini, kwa kuwa mambo mengi mno 
yanautegemea. Ni kiashiria ya kwamba upo katika dunia uweza mkuu na nguvu 
impitayo mwanadamu.

"NDIO, LAKINI..."
Wale wasioamini kwamba Biblia ni Neno la Mungu, hawapendi kabisa 
unabii wake. Unapokubali imetabiri kisahihi mambo kabla ya kutokea utakuwa 
umeanza kukubali uwepo wa Mungu... Kwa hiyo wanajaribu kuielezea mbali. 
"Unabii," wanasema, "haukuwa hasa utabiri wa mambo. Uliandikwa baada ya 
matukio 'unayoyabashiri.'
Sasa hii hoja inaweza kuwa na nguvu kama unaweza kuthibitisha kuwa 
yale yaliyoandikwa katika Biblia, na hasa yale ya Agano la Kale kwamba 
yaliandikwa baada ya matukio yanayodaiwa kutokea. Lazima tuseme hapa 
wazi kwamba hawana uthibitisho wa moja kwa moja juu ya hili; hitimisho lao ni 
matokeo tu ya kutafsiri mambo kujiridhisha wapendavyo. Ukweli ni kwamba, 
utafiti wote uliofanywa katika miaka 100 iliyopita unaonyesha kwamba 
yaliyoandikwa katika Biblia ni halisi; ni ya nyakati zinazodaiwa kuandikwa.
Lakini kuna njia ya mkato katika jambo hili inayoweza kutusaidia katika lengo 
letu. Hakuna anayeweza kubisha kudai kwamba maandiko ya Agano la Kale 
hayakuwepo miaka 200 kabla ya kuzaliwa Kristo, kwa kuwa yalitafsiriwa katika 
Kiyunani wakati huo, na huwezi kutafsiri kitu kisichokuwepo!

Ubishi mwingine ni kusema, "Ndio, unabii huu wa Biblia ni utabiri wa kijanja 
wa kisiasa wa watu waliokuwa wakichunguza matukio enzi zao na kuona 
mwelekeo wa matokeo yake."
Utabiri wa kijanja kisiasa! Uliotolewa karne nyingi kabla ya Kristo na 
unaoendelea kuwa kweli miaka 2000 hadi leo! Hao manabii walikuwa wachawi 
wa namna gani kuweza kufanikisha hilo bao? Kusema hivyo ni kuonyesha tu 
yasivyowezekana maelezo yake.
Lakini jibu la hakika kwa ubishi huu kama ilivyo kwa ubishi mwingine 
wowote, ni kusoma sehemu ya unabii wenyewe. Kwa hiyo tunaanza na:-

UNABII KUHUSU BABELI
Katika enzi ya manabii wa Israeli (Kama 850-560 K.K) kuliinukia dola mbili 
kuu katika maeneo yanayoizunguka mito ya Frati na Tigrisi, katika Iraki ya sasa. 
Ya kwanza ilikuwa dola ya Ashuru iliyokuwa na makao makuu Ninawi. Kwa karne 
mbili, Waashuru walivamia ardhi ya mataifa waliowazunguka: kusini 
wakawatawala Wakaldayo na makao makuu yake Babeli; Magharibi 
wakaikalia Shamu, na kuendelea chini katika pwani ya Bahari ya Kati, kupitia 
Israeli mpaka Misri. Sera yao ilikuwa ya kigaidi. Lengo lao lilikuwa kuwatisha 
wakazi wa maeneo hayo watii na kulipa kodi kwa mwaka. Kufanikisha hili 
waliiswaga miji kiuporaji na kuichoma moto, wakavibamiza vijiji, na kuua wakazi 
na kuchukua maelfu ya mateka Ashuru.
Katika nusu ya pili ya karne ya saba (K.K), nguvu ya Ashuru ilipungua na 
Babeli ikaanza kupanda. Katika mwaka 612 (K.K), Ninawi uliangushwa. 
Nebukadreza, mfalme wa Wakaldayo, haraka akaanzisha dola mpya. Mataifa 
madogo madogo Mashariki ya Kati yalipokuwa yanashangilia uhuru wao kutoka 
Ashuru, mara yakajikuta wakivamiwa na majeshi ya Babeli. Na hasa 
Nebukadreza akaivamia Israeli akaiteka Yerusalemu, akalichoma hekalu lake na 
kuchukua maelfu ya mateka Babeli. Akaendelea kusini zaidi na kuivamia Misri. 
Dola ya Babeli ilikuwa ni awamu ya pili ya utawala huu wa kijeshi. Ulikuwa katika 
eneo la Frati.
Na hasa Nebukadreza, mfalme wake mkuu kabisa aliujenga mji mkuu wa 
Babeli kuwa fahari ya dunia katika Mashariki ya Karibu. Alijenga Mahekalu 
makubwa na majumba ya kifalme, na kuzungushia jiji hilo ukuta mkubwa sana 
kuulinda. Babeli ukawa utukufu na fahari kuu kwa Nebukadreza mwenyewe na 
Wakaldayo wake.
Ni vigumu kwetu sisi kwa sasa kutambua athari za utawala kama huo wa 
kimabavu na uharibifu wa mali kwa wakazi wa mataifa madogo. Kwao dola za 
Ashuru na Babeli zitakuwa zilionekana tishio na zisizoshindwa.

MAANGUKO KAMILI
La ajabu, miaka 100 kabla Babeli haijafikia kilele cha ukuu wake, nabii 
Isaya alishatabiria kuangushwa kwake kwa maneno thabiti sana. Katika kifungu 
kilichopewa kichwa cha habari 'Mzigo wa Babeli' ni hivi alivyosema.
"...Siku ya BWANA i karibu; itanyesha kama maangamizi yatokayo 
kwa Mwenyezi Mungu...Tazama, nitawaamsha Wamedi juu yao...Na 
Babeli, huo utukufu wa falme, uzuri wa kiburi cha Wakaldayo, utakuwa 
kama Sodoma na Gomora hapo Mungu alipoiangamiza. Hautakaliwa na 
watu tena kabisa... Mwarabu hatapiga hema yake huko, wala 
wachungaji hawatalaza makundi yao huko. Lakini huko watalala 
hayawani wakali wa nyikani "(Isaya 13:6,17,19-21)
Hatima ya Babeli inaeleweka: wavamizi watakuwa Wamedi (taifa mashariki ya 
Babeli); jiji litakuwa maganjo, lisilokaliwa na mtu wala mnyama pori. Tukumbuke 
utabiri huu ulitolewa miaka 100 kabla ya Babeli kukua kufikia nguvu na utukufu 
wake.
Nabii mwingine, Yeremia, akiandika miaka 100 baadaye, wakati 
Nebukadreza alipokuwa akikaribia kuivamia Yerusalemu, aliongeza mtazamo 
juu ya anguko la Babeli.
"BWANA asema hivi, Angalia, nitaamsha juu ya Babeli upepo uharibuo... 
Babeli umeanguka na kuangamia ghafla... Wekeni mataifa tayari juu 
yake, wafalme wa Wamedi... Babeli utakuwa magofu, makao ya mbwa-
mwitu, ajabu, na mazomeo pasipo mtu kukaa huko... kuta pana za 
Babeli zitabomelewa kabisa, na malango yake marefu yatateketezwa... 
Ee BWANA, umenena habari za mji huu kwamba utakatiliwa mbali, 
usikaliwe na awaye yote, wala wanadamu wala wanyama, lakini uwe 
ukiwa hata milele..."
Na mwishowe nabii anaamriwa kufunga jiwe kwenye gombo la unabii ule na 
kulitupia ndani ya mto Frati, aseme,
"Hivyo ndivyo utakavyozama Babeli, wala hautazuka 
tena..."(Yer:51:1,8,28,37,58,62-64)
uwiano kati ya unabii wa Isaya, ulioandikwa miaka 100 kabla ya mamlaka ya 
Babeli kushamiri, na ule wa Yeremia, ulioandikwa wakati dola na jiji vilipokuwa 
katika kilele cha utukufu wake ni mtimilifu. Kwa watu wa siku zile itakuwa 
ilionekana kama ilivyo kwetu leo tuambiwe miji mikubwa kama London, New 
York au Sydney itaangamizwa ibakie magofu milele. Katika enzi hii ya silaha za 
nyuklia, jambo hilo linawezekana; lakini manabii wa Israeli walitamka hayo zaidi 
ya miaka 2500 iliyopita wakati hakuna ambaye angeweza kuota kwamba 
uharibifu kamili namna hiyo ungewezekana.

Historia inaonyesha jinsi ambavyo unabii huo wa maanguko ya Babeli 
ulivyotimizwa hatua kwa hatua. Wavunjaji wa Kwanza walikuwa Wamedi na 
Wajemi katika karne ya sita (K.K). Kuanzia wakati huo umwamba wa Babeli 
ulianza kufifia. Baadaye walikuja Wayunani chini ya Aleksanda Mkuu, 
wakifuatiwa na Warumi; baada yao makabila kadhaa yapendayo vita kama 
Wapathi, Waarabu na Watarta.

Kwa karne nyingi mahali halisi pa jiji la Kale la Babeli palikuwa mahame, 
yaliyoepukwa - wasafiri wasemavyo - na wahamaji wanaotangatanga. Ni hivi 
karibuni tu wataalamu wa kihistoria wachimbuao chini ( Archaeologists), 
walipochunguza eneo hilo katika nusu ya kwanza ya karne ya 19, na kugundua 
mabaki ya kuta kubwa, mahekalu ya nguvu na malango, na masanamu 
makubwa yaliyoonyesha ulimwengu ulioshikwa na butwaa jinsi ukuu wa Babeli 
ulivyokuwa enzi zake.
Kwa hiyo historia inatuonyesha jinsi Babeli 'Utukufu wa falme,' 
ulivyoangushwa na kuachwa, kama manabii wa Israeli walivyotabiri ingekuwa.
Sasa tunageukia mfano wa pili unaotofautiana, unaotuonyesha pia 
uhakika wa unabii wa Biblia katika:-

HATIMA YA MISRI
Misri iliwahi pia kuwa dola yenye nguvu kubwa katika Mashariki ya Kati. 
Ukubwa wake ulikuwa kama 1600 (K.K) wakati majeshi ya Mafarao wavamizi 
walipojisogeza kusini ndani ya Sudani, Magharibi kuambaa pwani ya Afrika ya 
kaskazini, kaskazini kupita ardhi ya Kaanani (baadaye Israeli), na ndani ya Syria. 
Uvumbuzi kaatika baadhi ya Mahekalu ya kale, minara na makaburi 
umedhihirisha utukufu wa Mafarao ulivyokuwa katika kilele cha kuu wao.
Lakini ilipofikia miaka ya 1400 K.K nguvu ya Misri ilianza kurudi nyuma 
kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe na kukua kwa Ashuru, na 
baadaye Babeli. Hata hivyo katika kipindi Waisraeli walipokuwa wakiikalia 
Kanaani, 1400-600 K.K, Wamisri waliingilia kati kwa nyakati mbalimbali siasa za 
Mashariki ya Kati, kwa mafanikio fulani. Waisraeli, walipokuwa wakiogopa 
uvamizi kutoka Ashuru na Babeli mara kwa mara walishawishika kutafuta 
msaada Misri badala ya kumtumainia Mungu wao.
Sasa manabii wa Israeli walikuwa na kitu maalum sana kusema juu ya 
hatima ya Misri. Nabii Ezekiel, ambaye matamko yake yalitolewa katika siku za 
Nebukadreza, mfalme wa Babeli, kuanzia kama 600 K.K, alitangaza kwamba 
kutokana na hukumu ya Mungu, Misri ingekuwa upweke kwa miaka 40. Baada 
ya hapo kungekuwa na uamsho, lakini usiofikia ukuu wa nguvu zake za awali.
"Maana Bwana MUNGU aseme hivi; Mwisho wa miaka arobaini 
nitawakusanya Wamisri, na kuwatoa katika hizo kabila za watu, ambazo 
walitawanyika kati yao; nani nitawarudisha hata nchi ya Pathrosi, hata 
nchi ya kuzaliwa kwao; na huko watakuwa ufalme duni (ufalme wa chini). 
Utakuwa duni kuliko falme zote; wala hatajiinua tena juu ya mataifa; nami 
nitawapunguza ili wasitawale tena juu ya mataifa... Bwana MUNGU 
asema hivi; Pia nitaviharibu vinyago, nami nitavikomesha vitu vya ubatili 
katika Nofu (Memphis), wala hapatakuwa na mkuu tena atokaye katika 
nchi ya Misri. Ezk. 29:13-15; 30:13
Hapa napo maana ya unabii huu inaeleweka: Misri ingekabiliwa na matatizo ya 
uvamizi na watu kuchukuliwa mateka. Ingawa hakuna kumbukumbu halisi 
zilizobakia za matukio hayo, lazima yatakuwa ni matokeo ya uvamizi wa 
Wababeli kwa Misri, kama Ezekiel mwenyewe alivyotabiri (tazama Ezek: 30:17-
20). Lakini huo usingekuwa mwisho wa Misri. Maana baada ya miaka 40, mateka 
wangerudi tena katika nchi yao wenyewe. Misri, kama ufalme 
usingeangamizwa: ungedumu lakini nguvu yake ingeshushwa sana - "Ufalme 
mdogo," usioweza kutumainia nguvu zake kukabili mataifa yanayopakana nayo 
tena.

Ufalme mdogo
Na ndivyo ilivyotokea. Tangu kama mwaka 600 K.K, Misri aliangukia chini 
ya watawala wa kivamizi, kwanza wa Wababeli katika karne ya 6 K.K; kisha 
Waajemi kati ya karne ya 6 na 4; alafu Wayunani katika karne ya 4; wakifuatiwa 
na Warumi karne ya kwanza K.K mpaka karne ya 5 B.K. Walifuatiwa na Waarabu 
na Waturuki kutoka karne ya 7 B.K na kuendelea. Hata Waingereza 
wameitawala Misri kwa kipindi katika karne ya 19. Kwa miaka 2500, Misri 
imebakia kama alivyotabiri Ezekiel kuwa ingekuwa, "Ufalme wa chini," wakati 
wote ikikaliwa na wengine. Lakini Misri na Wamisri hawakutokomea. Bado wapo, 
na wameponea uhuru kiasi miaka ya karibuni, washukuru misaada mikubwa ya 
fedha wanayopata kutoka Marekani na Saudi Arabia.

Tuweke pembeni kidogo mawazoni swala la Misri wakati tukiangalia 
mfano wa tatu wa utabiri wa Biblia wa matukio ya mbele, kwa kutazama.UNABII KUHUSU ISRAELI
Huu ndio uliojaa kuliko wote, kimaelezo ya utabiri wake, na pia katika 
wingi wa thibitisho zihusuzo ukweli wake kimatukio kihistoria. Tutazingatia tu 
mambo halisi mepesi yahusuyo hatima ya ajabu ya Waisraeli.
Agano la Kale limeandika kwa ajili yetu jinsi Mungu alivyofanya ahadi 
madhubuti kwa Ibrahim (Kama 1800 K.K), iliyokuwa imemaanisha kati ya mengi 
kwamba, uzao wake ungekuwa taifa (Israeli), ambalo lingeimiliki nchi ya 
Kanaani, iliyoitwa baadaye Palestina. Kama 1400 K.K. Waisraeli walitolewa Misri 
wakati wa 'Kutoka' chini ya Mussa, na miaka 40 baadaye walianza kurithishwa 
nchi waliyoahidiwa. Lakini kabla ya hapo, kabla hawajaingia hiyo nchi, 
walionywa sana na Mungu kupitia kwa Mussa mkosi ambao ungewapata kama 
wakimwacha Mungu wao na kuabudu sanamu, na kuiga mambo ya Wapagani 
wa Kikanaani.
Katika mlango wa 28 wa Kumbukumbu la Torati, kuna unabii wa ajabu 
sana - na ulikuwa onyo kali - juu ya balaa ambalo lingewafika Waisraeli kama 
hawakuwa watiifu. Msomaji anashauriwa kujisomea kifungu chote mwenyewe. 
Hapa tuna nafasi ndogo tu ya kuonyesha yaliyo msingi kimtazamo.
"Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya BWANA, Mungu wako, 
usiyaangalie kufanya maagizo yake yote... BWANA atakupeleka wewe, 
na mfalme wako utakayemweka juu yako kwa taifa usilolijua wewe wala 
baba zako... Nawe utakuwa ushangao, na mithali, na dharau, kati ya 
mataifa yote huko atakakokuongoza BWANA... BWANA atakutawanya 
katika mataifa yote, tokea ncha hii ya dunia hata ncha hii ya 
dunia...wala katika mataifa hayo hutapata raha iwayo yote.." Kumb. 
28:15,36-37,64-65.
Hapa napo unabii ulikuwa unaeleweka: Waisraeli wangetawanywa katika 
mataifa, kuishi huko katika mazingira ya taabu, wakibezwa na kudharauliwa. Ni 
ajabu iliyoje kuona maisha yao yalivyothibitisha uhakika wa maneno hayo! 
Mtawanyo wa Wayahudi dunia nzima ulianza katika enzi za Waashuru katika 
karne ya 8, K.K. Jambo hili liliendelea wakati wa Wababeli kwenye karne ya sita. 
Baada ya sehemu yao kurudi kutoka Babeli siku za Wafalme wa Kiajemi, jumuia 
ya Waisraeli iliishi katika ardhi yao kama 500 K.K mpaka siku za Kristo, chini ya 
tawala za kiajemi, Kiyunani na waliowafuata, na mwishowe Warumi. Katika 
mwaka 70 B.K, miaka 40 baada ya Kristo kusulubiwa msalabani, palitokea 
patashika mbaya kuliko zote. Jiji la Yerusalemu lilishambuliwa na kuporwa na 
majeshi ya Kirumi kwa sababu ya uasi; hekalu likateketezwa kwa moto na 
Wayahudi kutawanywa mateka dunia yote (ya Kirumi) - tazama kielelezo 
kwenye jalada. Wamekuwa huko tangu wakati huo, kama ilivyotokea; ncha 
moja wa dunia hata ncha nyingine!
Na wamekosa, kama ilivyoandikwa mpaka hivi karibuni 'utulivu', 
wakipata mateso na mara nyingine maangamizi. Wapogrom wa Urusi katika 
karne ya 19 na mpango wa Hitler wa uhilikishaji katika karne ya 20 ni mifano 
michache tu ya karibuni. Wayahudi wamekuwa kila mahali wakikabiliwa na 
chuki na kukataliwa, kiasi kwamba uwepo wao kama jamii ya watu, ni 
mojawapo wa maajabu ya kihistoria. Tunaona vile vile ya kwamba Unabii huu 
juu ya hatima ya Waisraeli umeendelea kuwa kweli kwa zaidi ya miaka 2500 
sasa. Nani angeweza kuliona hilo, tukizingatia mtawanyo ulivyokuwa na mateso, 
kwamba Wayahudi wangeendele kwa karne nyingi kuwa jamii kamili ya watu 
inayoendelea kutambulika hadi sasa!
Lakini ni zaidi ya hayo... 
Lakini jambo la ajabu zaidi juu ya unabii kuhusu Israeli halijasemewa, 
kwani manabii walitabiri pia wazi wazi badiliko lisilotegemewa la mafanikio kwa 
Waisraeli. Fikiria, kwa mfano, utabiri wa nabii Yeremia, uliotolewa karibu miaka 
600 K.K.
"Kwa maana, tazama, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapowarejeza 
watu wangu wa Israeli na Yuda waliofungwa... nani nitawarudisha hata 
nchi niliyowapa baba zao, nao wataimiliki (30:3)
"Basi sasa, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi...Tazama, 
nitawakusanya, na kuwatoa katika nchi zote nilikowafukuza, katika hasira 
yangu... nami nitawaleta tena hata mahali hapa, nami nitawakalisha 
salama salimini; nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu 
wao..." (32:36-38)
 "Nami nitawarudisha wafungwa wa Yuda, na wafungwa wa Israeli, na 
kuwajenga kama kwanza. Nami nitawasafisha na uovu wao wote..." 
(33:7)
Na hapa pia hakuna utata juu ya lile alilokuwa akisema nabii: Kitendo kile cha 
kutawanywa na mateso kwa Waisraeli kitageuzwa. Wayahudi watarudi tena 
katika nchi ile ile ambayo kutoka kwao walifukuzwa zaidi ya miaka 1990 iliyopita, 
na kuishi hapo kwa amani zaidi. Madondoo hayo mafupi kutoka kwa Yeremia, 
yanaweza kuzidishwa mara nyingi kwa matamko kama hayo kutoka Isaya na 
Ezekieli.
Hatuhitaji hasa kuzama sana ili kuonyesha jinsi utabiri huo wa kurudishwa 
upya Israeli ulivyotimizwa kikamilifu. Ushirika wa kisayuni ulikuwa na nguvu kati ya 
Wayahudi waliotawanywa katika nchi nyingi mwishoni mwa karne ya 19. 
Uanzishwaji wa Palestina kuwa makao ya kitaifa ya Wayahudi mwaka 1917 
ulisababisha idadi yao kukua haraka katika nchi hiyo. Hili lilipozua chuki kali kwa 
Waarabu, Wayahudi walipambana na jaribio lao la kuwakandamiza mwaka 
1948, na kuanzisha taifa lao la Kiyahudi. Nalo lilipanuliwa mwaka 1967 katika 
jaribio la pili kwenye vita vya siku sita, ambapo Israeli ilijichukulia upya sehemu 
kubwa ya ardhi yake ya kale, na Yerusalemu kuwa makao makuu ya taifa lao 
chini ya utawala wao wenyewe, kwa mara ya kwanza katika miaka 2500. Kwa 
kifupi, kuibuka kwa taifa huru la Wayahudi Mashariki ya Kati imekuwa ni kitu 
kisichotegemewa kabisa. Chini ya miaka 100 iliyopita hakuna mchunguzi wa 
kisiasa aliyedhani inawezekana.
Hatujihusishi hapa na 'siasa' za jambo hilo. Tunachoangalia hasa ni unabii 
wa Biblia. Kuna mengi mengine Biblia inayosema juu ya Wayahudi. Manabii 
wanasema, kwa mfano, kwamba kutakuwa na matatizo makubwa Mashariki ya 
Kati, na kwamba Israeli itafikishwa kwenye toba mbele ya Mungu wake. Hapo 
ndipo unabii wa mwisho wa kurudishwa upya na amani utakapotimia. Hapa 
tungependa kusisitiza tu kwamba manabii walitabiria kurudi kwa Waisraeli 
kwenye ardhi yao wenyewe, na sisi katika karne hii tumeona kwa macho yetu 
utabiri huu ukianza kutimizwa.

UNABII AINA TATU - HATIMA TATU
Baada ya kufika hapa, ni kitu cha manufaa kufanya muhtasari wa yale 
tuliyoona.
Babeli: Ile dola kuu kabisa Mashariki ya Kati, ilikuwa ipoteze mamlaka yake, na jiji 
lake kuu maridadi sana liwe mahame, likiepukwa na watu na wanyama pori. Na 
ndivyo ilivyotokea.
Misri: Nayo dola kuu nyingine, ingelibakia kuwa ufalme unaotambulika. Wamisri 
wangeendelea kukaa katika nchi yao wenyewe. Lakini mara zote 
wangetawaliwa na mamlaka zingine, wakibakia 'ufalme wa chini.' Na ndivyo 
ilivyokuwa.
Hatima ya Israeli haikuwa ya kufananishwa na yoyote kati ya hizi. Wakiwa 
wametawanywa mbali na nchi yao kwenye nchi nyingine, na kupata mateso 
makali na manyanyaso, wangerudi tena katika nchi ile ile walipotawanywa, na 
kujianzisha tena hapo.
Tuzingatie kwa makini yafuatayo:-
1.	Unabii kuhusu mataifa haya ulitolewa kama miaka 2500 iliyopita.
2.	Ukweli wake umekuwa matukio halisi ya kihistoria mpaka leo.
3.	Mifano hiyo hapo juu ilihusu mamlaka tatu tofauti, zenye hatima tatu 
tofauti kabisa. Moja ilikuwa kutoweka; ya pili kubakia, lakini kukaliwa na 
mataifa mengine; ya tatu kuangamizwa, na watu wake kufukuzwa na 
kutawanywa dunia nzima, na bado hatimaye kurudishwa katika nchi ya 
awali.
4.	Hii sio 'mitazamo ya mbeleni ya kisiasa,' ya wachunguzi wajanja wa 
kisiasa, bali ni utabiri usiokosea wa mambo.

Nani angeweza kujua?
Utabiri wa mambo wa muda mrefu hivyo unawezekanaje? Kuna jibu 
moja tu linaloridhisha; Lazima awepo aliyeyajua kabla; lakini ni nani?
Kwa hakika hakuna mtu wa miaka 2500 iliyopita au tangu hapo, 
angeweza kujua. Tukiupima utabiri wa namna hii kibinadamu tu hauelezeki. 
Lakini hata hivyo, manabii wa Agano la Kale hawakudai wanatabiri kwa uwezo 
wao. Walisema walikuwa wakisema maneno yaliyotoka kwa Mungu. " Hivi 
ndivyo asemavyo BWANA," ndivyo walivyokuwa wakianza kusema wakati wote. 
Kama Mungu alikuwa nyuma ya yale waliyosema, tunapata jibu la nani 
aliyejua.' Hakuna maelezo mengine yanayoleta maana. Unabii tuliouchunguza 
hapa ulihitaji uwepo wa Mungu kama chanzo chake. Inaleta maana.
Mifano hii mtatu tuliyoinukulu ilichaguliwa kuonyesha aina tofauti za 
unabii wa Biblia. Lakini mifano iko mingi. Tungeweza, kwa mfano, kuchunguza 
ule unaomhusu Yesu Kristo: alipaswa kuwa na mzao wa Ibrahim, na wa Daudi; 
alikuwa azaliwe Bethlehem; alikuwa akataliwe na watu wake; na bado afe kifo 
cha upatanisho kwa ajili yao; na maelezo mengi mengineyo - yote yakiwa 
yametamkwa mamia ya miaka kabla hajazaliwa, na bado yakawa hivyo hivyo 
katika kuzaliwa, kwa Yesu, utumishi, kifo na kufufuka kwake.
Lakini tutahitimisha uchunguzi wetu mfupi kwa mifano miwili zaidi 
itakayoleta mpango wa kiunabii mpaka kufikia wakati tulionao.
 
BIBLIA NA MATAIFA
Unabii wa Daniel unao mpango wa kuvutia unaohusu kukua na 
kuanguka kwa dola, na hali ya mataifa ya kile kilichokuwa kikiitwa 'Dunia 
iliyostaarabika,' yaani mataifa ya Ulaya, Mashariki ya Kati, Misri na pwani ya 
kaskazini mwa Afrika, yote yanayoizunguka Bahari ya Kati (Mediterranean sea). 
Unabii huu ulitolewa wakati Daniel alipokuwa mateka katika boma Babeli karne 
ya 6 K.K. Ukweli wake umejidhihirisha katika historia tangu siku hizo hadi sasa.
Nebukadreza, mfalme wa Babeli, akiwa amejaa kujikinai na ufahari, aliona 
katika ndoto sanamu moja kubwa sana ya mtu, yenye sehemu tano (tazama uk. 
16,17):
1.	Kichwa cha sanamu kilikuwa cha dhahabu.
2.	Kifua chake na mikono kilikuwa cha fedha.
3.	Tumbo lake na mapaja lilikuwa la shaba.
4.	Miguu yake miwili ilikuwa ya Chuma.
5.	Lakini nyayo na vidole zilikuwa mchanganyiko wa chuma na udongo wa 
mfinyanzi.
Kisha jiwe likatokeza 'lililokatwa kutoka mlimani bila kazi ya mikono.' 
Likaangukia nyayo za sanamu ile, likaiangusha yote chini, na kuzisaga sehemu 
zake kuwa unga, kiasi kwamba upepo ukaupeperushia mbali. Baada ya hapa 
lile jiwe likakua kuwa mlima mkubwa na kuijaza dunia yote.
Nebukadreza alisumbuliwa sana na hatima ya sanamu ile, kwa sababu 
hakuna kati ya watu wake wajuzi aliyeweza kumwambia ilikuwa na maana gani. 
lakini Daniel, nabii wa Israel alimwambia "kuna Mungu mbinguni afunuaye siri, 
naye amemjulisha mfalme Nebukadreza mambo yatakayokuwa siku za mwisho 
"Dal. 2:28
Kwa hiyo Daniel alielezea maana ya sanamu ile. Kichwa cha dhahabu 
kiliwakilisha utawala wa Nebukadreza mwenyewe. Ulikuwa ufuatiwe na 
mwingine, wa hali ya chini zaidi (kifua na mikono ya fedha); na baada ya huo 
wa tatu (wa shaba); alafu wa nne (miguu ya chuma) ambao ungekuwa na 
nguvu na kishindo, lakini nyayo na vidole viliwakilisha falme zilizogawanyika, nusu 
nguvu na nusu dhaifu". (Ms. 37 - 42)
Kitu kimoja ni wazi: Sanamu hii iliwakilisha makabidhiano ya falme zenye 
nguvu, na sio vigumu kuzitambua. Wa kwanza tunafahamu; ulikuwa ni dola ya 
Babeli. Katika kifungu cha 8 (Mstari wa 20 - 21) tunaambiwa afuataye 
angekuwa Mwajemi na Myunani. Dola ya nne, ' kuu na inayotisha', haikutajwa 
wazi wazi katika unabii wa Daniel. Historia inathibitisha tabiri hizi kwa wingi. Kama 
530 K.K. mamlaka ya Babeli iliangushwa na Wamedi na Waajemi, ambao 
mwishoni walianzisha dola ya kiajemi. Ilidumu miaka 200, na baadaye 
kuangushwa kama 330 K.K. na Aleksanda Mkuu (Alexander the Great) 
aliyesimamisha dola ya Kiyunani.
Ni dola gani kubwa iliyofuata falme za mrithi wa Aleksanda? Hakuna 
mashaka juu ya jibu: ilikuwa dola ya Rumi. Warumi walivamia maeneo ya 
iliyokuwa dola ya Kiyunani kuanzia karne ya 2 K.K. na kuendelea. Kwa miaka 500 
iliyofuata, Rumi ilikuwa mamlaka kuu kuliko zote duniani. Dola yake ilitanda 
kama sehemu yote ya dola zile tatu, na kuenea mbali ndani ya Ulaya, Mashariki 
ya Kati na nchi zote zinazozunguka Mediterranean. Walifanikisha uvamizi wao 
kwa ukatili mwingi kama ilivyodokezwa na maneno "nguvu kama chuma." 
Katika karne zake mbili za mwisho za kuwepo kwake, iligawanyika sehemu mbili: 
ya magharibi makao yake makuu yakiwa Rumi, na ya mashariki makao yake 
makuu yakiwa Constantinople - miguu miwili ya ile sanamu.

Mungu anayefunua siri
Lakini ni nini kilichotokea baada ya dola ya Warumi kuvunjika katika karne 
ya 5 B. K. Haikufuatiwa na dola nyingine yoyote kuu, na kwa kweli haijakuwapo 
dola ya tano ya kulinganishwa kimamlaka, pamoja na kuwepo jitihada kubwa 
za watu wenye tamaa kuunda nyingine. Maeneo ya dola ya Kirumi yalimeguka 
kutokana na uvamizi wa makabila jeuri ya Kihan, Kigoti, Kivisigoti na Kivandali, 
yaliyoanzisha tawala zao wenyewe tofauti. Mataifa ya sasa ya Ulaya 
yametokana na falme hizo. Katika kipindi chote cha historia ya miaka 1500 
mpaka sasa, mataifa hayo yamebakia katika mgawanyiko, kama ilivyoashiriwa 
na nyayo za ile sanamu - nusu chuma na nusu udongo: " nusu una nguvu, na 
nusu yake umevunjika ... hawatashikamana. "(Dan. 2:42-43)
Angewezaje Daniel kujua kuwa mamlaka ile kuu ya Nebukadreza 
ingefuatiwa na zingine tatu, ya nne ikiwa na nguvu zisizo za kawaida, ambayo 
kamwe isingelifuatiwa na ya tano? Angejuaje kuwa baada ya ile ya nne 
kuanguka, watu wake wangesambaratika kuwa nchi zilizomeguka, zisizo na 
umoja kati yake? Kwa vyovyote, kwa yeye mwenyewe asingeweza kujua kitu, 
wala yeyote mwingine. Lakini Daniel hatuachi bila maelezo:
"Yupo Mungu mbinguni afunuaye siri.. Mungu aliye mkuu amemjulisha 
mfalme mambo yatakayokuwa baadaye, na ndoto hii ni ya hakika, na 
tafsiri yake ni thabiti." (Ms. 28,45)
Unawezaje kuuelezea uwepo wa unabii wa Daniel 2, karne kadhaa K.K, 
na bado kuwa na mtizamo sahihi wa madola na mataifa mpaka hivi leo, baada 
ya zaidi ya miaka 2000? Kama kweli kuna 'Mungu mbinguni,' unaweza kuelewa. 
Kama Hayupo, hakuna maelezo yanayoridhisha.
Tutatoa maoni katika sehemu ya hitimisho, juu ya jiwe linaloigonga ile 
sanamu miguuni na kuiangusha yote chini. Kwa ajili ya mfano wetu wa mwisho 
wa kinabii tuone kwanza.

NYAKATI TULIZO NAZO
Ingawa unabii tuliouzingatia mpaka sasa umeendelea kutimia hadi hivi 
leo, ulihusu zaidi matukio ya siku nyingi za nyuma (ukiacha urudishwaji upya wa 
Waisraeli hivi karibuni katika ardhi yao ya kale). Je, kuna kinachosemwa na 
unabii wa Biblia juu ya nyakati tulizo nazo kuweza kutuongoza katika siku hizi?
Kipo hasa! Tena ni ajabu kinavyotofautiana sana na matazamio na fikra 
za kibinadamu. Karne ya 19 ilikuwa kipindi cha matumaini. Maendeleo 
makubwa yalikuwa yakipigwa. Ujuzi wa Kisayansi ulivyoongezeka ulileta 
maendeleo haraka kiufundi na uzalishaji mkubwa viwandani. Hili lilikuwa lilete 
neema (ingawa sio kwa walio maskini sana). Elimu ilipanuliwa kuwafikia wengi, 
na matumaini ya maana yalipatikana. Watu walioelimika zaidi, ilidaiwa, 
wangejishughulisha na sanaa kama fasihi, muziki na uchoraji. Maadili ya jamii 
kwa ujumla yengeboreka. Wanasiasa waliahidi kuleta mpango mpya wa kijamii 
wa haki na usawa kwa wote. Vile ambavyo watu wangetajirika, ndivyo 
ambavyo wasingeoneana kijicho. "Tokomeza umaskini, na ndivyo 
utakavyotokomeza uovu, lilikuwa ndilo bango. Wakati uwezo wa juu wa akili ya 
mwanadamu ukitumiwa, ilikuwa amani ijengeke kati ya mataifa. Viongozi wa 
kanisa nao wakatazamia kwa dhati kueneza Injili dunia nzima. Kujiendeleza 
mwanadamu na kuboresha maisha, kwa mtu binafsi na kwa jamii, vilichukuliwa 
juu juu tu. Hali ya baadaye ikaonekana nzuri. 

Amani na maendeleo?
Kinyume cha matazamio hayo, matukio ya karne ya 20 yamekuwa 
mfadhaiko. Ndoto za maendeleo na amani zimefifia. Vita viwili vibaya sana vya 
dunia, vikiwa vimechinja mamilioni na kuleta uharibifu usiosemekana wa mali na 
mateso, vimefuatiwa na uundaji wa silaha kali za maangamizi ambazo 
hazijawahi kutengenezwa. Mawazo ya utatuzi ya aina mbalimbali ya 'wenye 
busara' wa karne ya 19 yamekuwa bure. Kupanuliwa elimu hakujafuatiwa na 
maadili zaidi, badala yake na kukua kwa dhuluma, choyo, vurugu na uvunjaji 
sheria. Dini ya Kikristo, mbali na kuwabadili mataifa, imekuwa katika kurudi 
nyuma duniani pote. 
Demokrasia katika siasa haijajidhihirisha kuwa muarobaini wa maovu 
katika jamii kama ilivyotarajiwa. Mwishowe pigo baya zaidi - sayansi imethibitika 
kuwa silaha ya kutisha ya makali kuwili. Mbali na kuwa enzi ya amani, karne ya 
20, ya ustaarabu, imekuwa wakati wa migogoro na mapambano. Ndio maana 
mtizamo wa wengi umekuwa ule wa kukata tamaa. Inaonekana kama hakuna 
anayeweza kufanya kitu.

Sasa unabii wa Biblia unasemeaje hali hizi?
Biblia ina utabiri wa kueleweka kabisa juu ya siku za mwisho, 'nyakati za 
mwisho,' wakati harakati za mwanadamu katika nchi zitakapofikia hatua 
mbaya. Sio picha ya maendeleo endelevu na amani, bali ya matatizo duniani 
na hofu. Mfano wa wazi sana na unaotugusa upo katika yale Yesu 
aliyowaambia wanafunzi wake walipomuuliza nini ingekuwa ishara ya kurudi 
kwake duniani na ya 'mwisho wa dunia.' Anawaambia kwanza juu ya hatima 
ya Wayahudi.
" Wataanguka (Wayahudi) kwa ukali wa upanga, nao watatekwa nyara 
na kuchukuliwa katika mataifa yote; na Yerusalemu utakanyagwa na 
Mataifa (wasio Wayahudi), hata majira ya Mataifa yatakapotimia." (Luka 
21:24)

Sasa haya ni maelezo mafupi juu ya yale tuliyoyaangalia yahusuyo unabii 
kwa Israeli. Wayahudi wangeng'olewa kuwa mateka kati ya mataifa yote; 
Yerusalemu ingekaliwa na mamlaka za kimataifa. Gundua kwamba Yesu 
anasemea mwisho wa hili 'hata majira ya Mataifa yatakapotimia.' Tumeona 
mwanzo wa jambo hili katika wakati wetu. Yerusalemu haikaliwi tena na watu 
wa nje - unakaliwa na Israeli yenyewe.

Mashaka na hofu duniani
Kwa hiyo yale anayoendelea kusema lazima yahusiane na siku hizo - siku 
za Israeli kurudishwa katika nchi yao wenyewe. Hivi ndivyo anavyotabiri.
"Tena, kutakuwa na ishara katika jua, na mwezi, na nyota; na katika nchi 
dhiki ya Mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake; 
watu wakivunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazamia mambo 
yatakayoupata ulimwengu; kwa kuwa nguvu za mbinguni zitatikisika." 
(Ms. 25 - 26)
Hii sio picha ya amani na maendeleo. Ni dunia ya hekaheka na 
kuchanganyikiwa, hofu ikiikumba mioyo ya watu wanapofikiria mambo 
yanayotokea katika 'makao ya watu duniani' kama neno alilotumia Yesu 
linavyomaanisha.
Mtume Paulo, akiwa anaandika kama miaka 35 baada ya unabii huo wa 
Yesu, anasema hivi juu ya hali ya siku za mwisho.
"...siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa 
wenye kujipenda wenyewe, na wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, 
wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, 
wasio safi, wasiopenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, 
wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, 
wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu; wenye mfano wa utauwa, 
lakini wakikana nguvu zake;.."
Hii ni sura ya ajabu ya ustaarabu; mtu anatupilia mbali vizuizi vyote na kuzifuata 
tamaa zake mwenyewe bila kujali matokeo yake. Hakuna asiyeona uwiano wa 
hali hiyo na mambo yalivyo katika dunia yetu ya sasa.
Kwa hiyo hali ni hiyo; wakati wajuzi wa mambo miaka 100 tu iliyopita 
walitazamia kwa dhati sana, kipindi cha maendeleo na amani kwa mataifa ya 
dunia, Biblia, katika maneno ya Yesu na Paulo ilitabiria dunia ya fujo, hofu na 
kuchanganyikiwa, nyakati za migogoro, kujifanyia mtu atakacho, na chuki. 
Wanafalsafa wetu wa kibinadamu walikosea; Yesu na Paulo walikuwa sawa! 
Lakini waliongea na kuandika zaidi ya miaka 1900 iliyopita. Waliwezaje kujua? 
Sababu pekee ni kwamba hawakusema maneno yao wenyewe, bali maneno 
ya Mungu Mwenyewe. Ni Mungu aliyejua, akampa uwezo Mwanawe na 
mtume wake kutufunulia hali ya siku za mwisho.

HITIMISHO
Kuna majumuisho kadhaa muhimu tunayoweza kuyafikia kutokana na 
kuchunguza kwetu unabii wa Biblia.
Kama Biblia imejithibitisha kuwa sahihi kiasi hiki katika utabiri wake wa 
matukio katika historia ya mwanadamu - hatima ya Babeli, Misri na Israeli, na pia 
katika kukua na kuanguka dola, na hali ya dunia kwa wakati huu - itakosa kuwa 
sawa katika utabiri wake wa matukio yaliyobaki?
Chukulia yale maono katika sanamu katika Daniel, kwa mfano. 
Hatujatolea maoni bado juu ya ile hatua ya mwisho: Jiwe, " lililokatwa kutoka 
mlimani bila kazi ya mikono," liliipiga ile sanamu chini ya miguu, 
likaivunjavunja, na lenyewe "likawa mlima mkubwa, na kuijaza dunia yote 
"(Dan. 2:35).
Sasa maana ya jumla ya hili iko wazi: kitu kigeni, kisichokuwa sehemu ya 
dola za sanamu na falme, kinaziharibu na kuchukua nafasi zake duniani. Kwa 
kuwa 'bila mikono,' maana yake ni 'bila mikono ya mwanadamu', lile jiwe 
lazima litakuwa linasimama badala ya nguvu isiyokuwa ya kawaida ya 
kibinadamu.
Lakini Daniel anatuambia mwenyewe maana yake:
" Katika siku za wafalme hao, Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme 
ambao hautaangamizwa milele... utavunja falme hizi zote vipande 
vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele. " (Ms. 44)
Serikali za sasa na mamlaka za dunia zitaondolewa, katika tukio moja la aina 
yake, Mungu atakapoingilia kati na kusimamisha Serikali yake Mwenyewe. 
Kuondoa utata ieleweke kwamba, sio umati wa watu unaoangamizwa: ni 
nguvu na mamlaka za falme za kibinadamu, zitakazong'olewa na ufalme 
mpya wa Mungu.
Unabii mwingi mwingine unatueleza jinsi ufalme huo utakavyokuwa; 
maongozi yake timamu, mafundisho yake yenye kweli, na amani 
utakayoleta hatimaye duniani kwa watu wote kutokana na kumtambua 
kwao 'Mungu wa mbinguni!' Soma kwa mfano Isaya 2:1-4 kupata picha 
kamili na ya kusisimua juu ya mataifa katika enzi hiyo ijayo.
Lakini ni kwa namna gani mageuzi hayo makubwa yanaweza 
kufanikishwa duniani? Agano jipya linatupa jibu. Na hasa ni Yesu mwenyewe 
anayetuambia katika unabii ule wa nyakati za taabu na hofu kwa mataifa 
yote. Maneno yake yaliyofuata ni haya
"Hapo ndipo watakapomwona mwana wa Adamu akija katika wingu 
pamoja na nguvu na utukufu mwingi" (Luka 21:27)
Anasema atarudi tena mwenyewe. Kurudi kwa Kristo duniani ni wazo 
mojawapo kuu katika mafundisho ya Yesu na mitume katika Agano Jipya na 
linakubaliana kabisa na manabii. Soma zaburi 72 kupata kinachosemwa juu 
ya utawala wake.
Sasa, kwa hakika, hili ndilo linalopaswa kutushughulisha sana: Kama 
unabii wa Biblia kuhusu mataifa na dola umekuwa kweli kama ilivyo kwa zaidi 
ya miaka 2000, hayo mengine yaliyotabiriwa yatakosa kutimia? Sio kukosa 
busara kusema: "sawa nakubali manabii walikuwa sahihi katika utabiri wao 
katika mambo haya ya kihistoria, lakini siamini wanayosema juu ya yajayo 
kutuhusu sisi." Kwa nini? Wametoa uthibitisho kwamba hawakuwa wakitoa 
mawazo yao wenyewe, bali makusudio hasa ya Mungu. Yote yale 
wanayosema yanapaswa kutufanya tujali sana.

Kitu cha muhimu
Lakini bila shaka kuna zaidi. Unabii huu wa ajabu unapatikana katika 
Biblia, na sio mahali pengine popote duniani. Hakuna maandiko mengine, 
hakuna vitabu, hakuna matamko mengine yoyote ya mwanadamu 
yanayoweza hata kwa mbali kulinganishwa na Biblia. Lakini Biblia inatuambia 
kwamba Yesu alikuwa mwana wa Mungu; mambo aliyosema 
yamehifadhiwa kwa ajili yetu katika Injili za Agano Jipya. Pamoja na 
mafundisho ya mitume wake Petro, Yohana na Paulo, wanatufunulia ukweli 
ambao hatuwezi vinginevyo kuujua. Wanatuonya juu ya ukweli kuhusu kifo; 
wanaeleza kwa nini Injili ni 'habari njema,' 'uweza wa Mungu uuletao 
wokovu' (Warumi 1:16). Wanatutia moyo na ahadi ya uzima wa milele katika 
mpango mpya atakaouanzisha Kristo atakapokuja. Ndio maana inatupasa 
kuisoma Bilia. Inaweza kutupa utofauti wa muhimu kati ya utupu wa kifo, na 
tumaini la nguvu la maisha yasiyo na mwisho.
Usomaji wa makini wa Biblia utatuhakikishia kuwa Mungu yupo, 
anatawala, na kwamba anatuita tuwe wafuasi wa mwanawe. Biblia ipo kwa 
ajili yetu. Tunafanya vizuri kujali inachosema.FRED PEARCE


TAFSIRI - CHRISTADELPHIAN BIBLE MISSION
IFAKARA ECCLESIA (TANZANIA)


Swahili Title
Unabii wa Biblia
English files
Text file
Swahili Word file
Status
Printed
African text
Carl Hinton
Translator 1
Martin Silwani
Literature type
English only
D7 Node Id
641