5. HISTORIA YA GHARIKA
“Kwa imani Nuhu alitengeneza safina kuokoa nyumba yake”
Shabaha
Kuonyesha jinsi Mungu alivyowaadhibu waovu na kumwokoa Nuhu kutoka katika gharika. Kwa miaka mingi vizazi vya Seti (walioitwa “wana wa Mungu” (Mwanzo 6:2) waliendelea kuwa mbali kabisa na uzao wa Kaini na kutokea mwanzo walitenda mambo yaliyokuwa yanampendeza Mungu.
Waliishi maisha ya kujitenga wakiwaepuka watu waovu waliokuwa wamewazunguka. Wazao wa Kaini ingawa walikuwa na ujuzi na werevu lakini walikuwa watenda mabaya, mara kwa mara walimwasi Mungu. Lakini baadaye “wana wa Mungu” walipotoshwa wakatoka katika kumcha Mungu wao kama walivyokuwa wanafahamika mwanzo, na kugeukia kutenda matendo yale yale maovu yaliyokuwa yakitendwa na kizazi cha Kaini. Dunia ikawa mahala pa watenda maovu. Mungu akaona kuwa “kila kusudi analowaza mwanadamu moyoni mwake ni baya tu siku zote”. (Mwanzo 6:5; Mwanzo 6,7,8; Waebrania 11: 7).
UOVU UKAJAA DUNIANI: Mwanzo 6:1-13
Watu walioishi katika nchi wakati ule walikuwa waovu sana na Mungu akatazama maovu haya na kuhuzunika Moyoni mwake hatimaye alisema, “nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi” (mstari wa 7). Hata hivyo alikuwako mtu mmoja aliyempendeza Mungu. Jina lake aliitwa Nuhu, na alikuwa na haki au mtu mwenye haki na mnyoofu mtu aliyekuwa akimwamini Mungu na alitembea na Mungu (mstari wa 9) ameandikwa katika waraka wa 2 wa Petro sura ya 2:5 kuwa ni “mjumbe wa haki” aliambiwa na Mungu kuwahubiri watu na kuwaonya kwamba kama hawatatubu, Mungu angewaharibu. “Nitawaharibu pamoja na dunia ” Mungu alisema (mstari wa 13). Nuhu hakusita kutekeleza aliyokuwa ameambiwa na Mungu, alianza kuhubiri na aliendelea kwa miaka 120, na wakati wote akitarajia kuwa baadhi yao wangeacha uovu wao na kuokolewa.
MUNGU ANAMWAGIZA NUHU KUTENGENEZA SAFINA: Mwanzo 4-16
Nuhu aliagizwavkutengeneza safina na alipewa vipimo kwa kubiti. Kubiti moja ni sawa na kati ya mm 500 – 600. Hii inaonyesha kwamba safina ilikuwa na urefu wa kati ya m 160 na 180, upana wa kati ya m 27 na 30 na kimo cha kati ya m 16 na 18. Ilijengwa kwa mti aina ya mpodo, ikiwa imepakwa lami ndani na nje na urefu kwenda juu kama ghorofa tatu. Ilikua na mlango na dirisha kwa chombo kikubwa kama hicho ingechukua miaka mingi kukitengeneza. Kwanza mali ghafi ilibidi kutayarishwa kisha kazi kubwa ya kukiunda ingefuata. Wakati wote Nuhu ilibidi awe mwangalifu kufuata maelekezo aliyopewa na Mungu. Aliendelea kuwa mwaniminifu kuunda na kuhubiri, akiwaonya watu kuhusu kuhukumu inayokuja kwa watenda maovu. Watu walimcheka Nuhu. Hawakuweza kufikiria kitu chochote ila kitu cha mzaha kama kile cha mtu kuunda safina katikati ya nchi mbali sana na bahari. Vicheko vyao havikumtia mashaka kwani alikuwa mtu mtiifu. Kwa uvumilivu aliendelea na kazi aliyokuwa amepewa na Mungu.
SAFINA YA USALAMA IKAKAMILIKA – GHALIKA IKAIFUNIKA DUNIA: Mwanzo 7
Kwa sababu Nuhu alimpenda Mungu, alikaribishwa kuingia katika safina. “Ingia wewe na jamaa yako yote katika safina, kwa maana nimekuona wewe u mwenye haki mbele zangu katika kizazi hiki” (mtari wa 1). Watu wanane, Nuhu na mke wake, wanawe watatu, Shemu, Hamu na Yafethi na wake zao waliingia katika safina kungojea na kuokolewa kutoka katika adhabu ya kutisha ambayo ingekuja kuwapata watu wote waovu. Wanyama na ndege pia waliingizwa katika safina kama Mungu alivyoagiza jozi saba za wanyama waliosafi na jozi moja ya wanyama wasio safi, jozi saba ya ndege wote (“warukao angani”). Mungu hatimaye alifunga mlango. Kisha siku saba baadaye, mvua ilianza kunyesha na iliendelea kunyesha kila siku, mchana siku 40 na usiku siku 40 (msatari wa 12). Maji yalijaa hadi kuifunika kabisa milima yote mirefu. “Wakafa wote wenye mwili waendao juu ya nchi, na ndege, na wanyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu, na kila kitambaacho chenye kutambaa juu ya nchi, na kila mwanadamu” (mstari 21).
Baada ya mvua kuacha kunyesha ilimbidi Nuhu kubakia katika safina mpaka kila kitu kilipokuwa salama na nchi ilipokuwa kavu tena. Wakati huo maji yalikuwa yameifunika nchi yote na safina ilikuwa ikielea kwa usalama juu ya maji. Ilikuwa yapata kama miezi minane baadaye, Nuhu alifungua dirisha la safina aliwatoa nje na kuwatuma kunguru na kisha njiwa. Kunguru hakurudi lakini njiwa alirudi, kwa sababu “ hakuona mahali pa kutua kwa wayo wa mguu wake”.
Siku saba baadaye njiwa alitumwa tena, safari hii alirudi na jani la mzeituni kinywani mwake kwa hiyo, Nuhu alijua kuwa maji yalianza kupungua polepole kwani vilele vya juu vya miti vilianza kuonekana. Mwishowe, baada ya siku saba njiwa alitumwa tena, safari hii hakurudi. Nuhu na jamaa yake walikuwa wamekaa ndani ya safina zaidi ya mwaka hadi wakati Mungu alipomwambia Nuhu, “Toka katika safina” (Mwanzo 8:15-16). Kwa hiyo walitoka ndani ya Safina na wakawatoa nje wanyama na ndege pia wakatoa kila kitambaacho juu ya nchi wakaenda “wajae katika ,wawe na uzazi, wakaongeze katika nchi” (msatari wa 17).
NUHU ANATOA SHUKRANI KWA MUNGU – AHADI YA MUNGU: Mwanzo 8:20-22
Jambo la kwanza alilolifanya Nuhu ni kujenga madhabahu na kumtolea Mungu sadaka. Jambo hili lilimpendeza Mungu na hivyo akambariki Nuhu na kufanya agano naye Agano ni mapatano maalumu kati ya watu wawili au Mungu na mtu (au Taifa) ikiwa ni ishara kwamba Mungu atatimiza ahadi yake. Ahadi za Mungu kamwe hazishindwi. Upinde wa mvua katika anga unaoonekana siku hizi wakati wa majira ya mvua ukawa ndiyo ishara ya kuwa kamwe gharika haitatokea tena kuharibu viumbe vyote katika nchi kama Mungu alivyosema, “Wala, sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai, kama nilivyofanya” (mistari 21-22).
Tangu kuumbwa kwa Adamu mpaka gharika ilikuwa kama miaka 1,656. Gharika ilifunika nchi yapata kama 2348 KK. Kutoka Shemu, Hamu na Yafethi, baada ya gharika ndipo wakawepo watu wote waliopo duniani. Viumbe hai vyote walikufa katika gharika na hivyo huu ndiyo ulikuwa ndiyo mwanzo mpya.
FUNDISHO KWETU
Kama tulivyoona katika somo hili, wakati duniani ilipojazwa na watenda maovu na maasi, Mungu aliwaadhibu wakazi wa nchi kwa kuwaharibu kwa gharika. Yesu aliwaonya wanafunzi wake kwamba maasi yataongezeka duniani katika siku hizo kabla ya kurudi kwake duniani (Mathayo 24:37-39) “Kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu”. Alisema watu wataendelea kuishi katika maisha ya dhambi. Bila kujali maonyo yake au kutarajia kurejea kwake kamwe. Hatuna budi kumshukuru Mungu maana ametufundisha kuwa kurudi kwa Yesu Kristo kumekaribia kwa hiyo tujiandae tayari kwa siku hiyo, kwa kujifunza njia za Mungu katika Biblia na kumtii Yeye. Ni wenye haki tu watakaookolewa na kupewa uzima wa milele ili kutawala pamoja na Yesu Kristo katika Ufalme wake. Watenda maovu wote na wasiotii wataangamizwa.
Ni watu wapenda haki tu ndiyo wataokolewa na dhamana ya kuishi ni kutawala milele pamoja na Kristo katika ufalme. Wote ambao ni waharifu na wasio mtii wataharibiwa.
Masomo ya Nyongeza
Tunatakiwa tukumbuke kwamba Yesu Kristo ni safina ya usalama wetu na ni budi tuingie kwa kupitia mlangoni kwa njia ya ubatizo (Wagalatia 3:27). Safina ya ubatizo ni mahali pa usalama na wokovu. Mungu atawaokoa wote ambao watabatizwa katika Yesu Kristo na ambao wanatunza amri zake na tumepewa mwaliko twende kwa BWANA kwa njia hii (Matendo 16:3; Warumi 10:9).
Gharika ilikuwa ni ishara ya ubatizo. Ilisafisha dhambi zote za dunia ya zamani ili kwamba yaanze maisha mapya “Watu wanane waliokolewa ndani ya maji,mambo haya ni sawa na ubatizo unaotuokoa sisi siku hizi” (1 Petro 3:20-21; Matendo4:12; Marko 16:16).
MASWALI
Majibu Mafupi
1. Je uzao wa Kaini uliku wa namna gani?
2. Je uzao wa Sethi uliku wa namna gani?
3. Baada ya uzao wa Sethi kuoana na uzao wa Kaini watu hao walikuwa wa namna gani?
4. Mungu aliamua kuwafanya nini watenda mabaya?
5. Je walikuwepo watu watendao mazuri katika nchi wakati huo?
6. Baada ya Mungu kuona uovu umezidi sana katika nchi mambo ni mambo gani mawili Nuhu aliyoambiwa ayafanye?
7. Baada ya safina kukamilika ni nani walioingia ndani?
8. Je, ni wakati gani mvua ilipoanza kunyesha?
9. Je, mvua ilinyesha kwa muda gani?
10. Ni kwa muda gani Nuhu alisubiri akiwa ndani ya safina?
11. Mungu alimwonyesha nini Nuhu kuwa kamwe hatawaangamiza tena watu wote kwa gharika?
Majibu ya Kina
12. Kwa nini Mungu alituma gharika katika nchi wakati wa Nuhu?
13. Mungu alimwokoaje Nuhu katika gharika?
14. Kwa nini Mungu aliweka upinde wa mvua katika anga baada ya gharika na ulikuwa na maana gani kwa Nuhu?
15. Nini maana ya agano?
16. Nuhu na wanaye walipaswa wafanye nini baada ya gharika?
17. Ni onyo gani Yesu alilowapatia wanafunzi wake kutokana na fundisho la gharika?
Majibu ya Ziada
18. Eleza historia ya Nuhu na jinsi alivyoingia ndani ya safina
19. Je, tutaingiaje katika safina ya salama?
20. Malizia usemi huu - “Kama vile ilivyokuwa katika siku za
Nuhu…” Usemi huu una maana gani?
Maktaba rejea ya Mwalimu
"The Visible Hand of God" - R. Roberts, chapter 5
"Ur of the Chaldees" - C. Leonard Woolley, chapter 1