CSSA 1-1-09 - CHOOSING A WIFE FOR ISAAC

Swahili

9. KUCHAGUA MKE WA ISAKA

“Isaka akamtwaa Rebeka na kuwa mke wake naye akampenda Rebeka”

Shabaha

Kuonyesha kwamba ni lazima tuomba msaada wa Mungu katika kuchagua mwenzi wa maisha ya muda mrefu.

Sasa Ibrahimu alikuwa mzee. Sara mke wake alikwisha fariki akiwa na umri wa miaka 127.Ahadi zilikuwa kwa Ibrahimu na kwa uzao wake. Zilikuwa ni zipitie kwa Isaka na halafu kupitia kwa watoto wake na kuendelea hadi kufikia wakati wa Yesu atakapozaliwa, ambaye ni uzao wa Ibrahimu (Mathayo 1:1;Wagalatia 3:16) kwa sababu hii Ibrahimu alikuwa na hamu ya kumwona Isaka anakuwa na mke ambaye ni mwaminifu. Katika siku hizo za Ibrahimu, Ilikuwa ni desturi ya wazazi kufanya mipango ya ndoa ya watoto wao na kwa kawaida wachumba hawakuweza kukutana mpaka siku ya arusi ilipofanyika. Ilikuwa ni muhimu kwamba mke wa Isaka amwabudu Mungu wa Ibrahimu ili kumsaidia katika maisha yake watakapokuwa pamoja. Watu wa Kanaani walikuwa watenda maovu kwa hiyo Ibrahimu hakutaka aoae mwanamke wa Kanaani. Hatimaye aliwakumbuka watu wa kwao walioishi Harani na aliamua kwamba angemtafuta mchumba mzuri wa Isaka kutoka kule.

Mwanzo 24:4

ELIEZERI ANATUMWA KUMTAFUTIA ISAKA MKE: Mwanzo 24:1-7

Ibrahimu alikuwa na mtumishi mwaminifu, Eliezeri ambaye alikuwa “mtawala wa mambo yote aliyokuwa nayo”. Aliitwa na kuingia katika hema ya Ibrahimu na kupewa kazi ya kumtafutia Isaka mchumba.

Ilimpasa kumwapisha. “Kwamba hutamtwalia mwanangu mke katika binti za Wakanaani ambao nakaa kati yao” (mstari 3). Ilikuwa ni kazi ngumu sana. Safari ndefu ilikuwa mbele yake, ambayo pamoja na kumpata mke anayefaa na kumtia nguvu kusafiri  safari ndefu ya kwenda kuolewa na mtu ambaye hakumfahamu, ni jambo ambalo huenda lisingewezekana. Ingekuwaje kama asingeongozana na Eliezeri? Je ange mrejesha Isaka Harani alikotoka? Hapana. Ibrahimu alikuwa thabiti juu ya jambo hili kwanza “ujihadhari usimrudishe mwanangu huko tena. Alimkumbusha mtumishi wake kuhusu ahadi ya Mungu kwamba.” Uzao wake utairithi nchi hii na mwanaye sharti akae na kuishi katika nchi ile (mstari 7)

ELIEZERI AKUTANA NA REBEKA: Mwanzo 24:7-24

Mtumishi mwaminifu alianza safari, alikumbuka tamko la ahadi kwa Ibrahimu kumleta mke wa Isaka kwa sababu familia yake ni lazima wabakie katika nchi ile. Katika safari ndefu aliongozana na watumishi wakiwa wamepanda ngamia kumi, wakiwa wamechukua mapambo ya thamani ya dhahabu na fedha ikiwa ni zawadi na nguo, kama ilivyokuwa desturi kwa mtu tajiri sana kama Ibrahimu kupeleka zawadi kwa familia ya mchumba.

Ibrahimu alimtia moyo Eliezeri kwa kumwambia kwamba Mungu atamsaidia katika shughuli yake “Yeye atampeleka malaika wake mbele yako, nawe utamtwalia mwanangu mke kutokea huko (kutoka katika sehemu hiyo)”.

Wakati wa jioni ya siku ile ya mwisho wa safari yake alipumzika karibu na kisima nje ya mji wa Harani akawachunguza wasichana wa mji waliokuja kuchota maji. Alimwomba Mungu kwamba kama itawezekana apewe ishara ya msichana anayefaa. Alikuwa akisubiri ni binti yupi atakayempatia maji ya kunywa hali kadhalika awanyweshe maji ngamia wake pia (mstari 14).

Ilikuwa kabla hajamaliza kuomba, Rebeka alitokea na watumishi walipomwomba maji ya kunywa aliwapatia na hata kuwanywesha ngamia pia. Ilionekana kama vile Mungu alikwisha jibu maombi yake mara moja. Baada ya Rebeka kumaliza kazi yake akampatia zawadi zenye thamani alizokuwa nazo na kumwuliza “U binti wa nani wewe?” (mstari 23) alikuwa na furaha ilioje alipotambua kuwa akuwa ametoka katika jamaa ileile aliyokuwa anaitafuta. Huyu mbele yake ndiye mchumba wa Isaka. Ni hakika kuwa Eliezeri alimshukuru Mungu na kwa ajili ya Imani yake alipewa thawabu.

ELIEZERI ANAFANYA MPANGO WA ARUSI: Mwanzo 24:24-51

Rebeka alimpeleka mtumishi wa Ibrahimu nyumbani kwao alikozaliwa na kwa kaka yake, Labani. Jioni ile walikuwa na mazungumzo marefu na mtumishi alikuwa na hamu ya kuzungumza kwa nini amekuja hata kabla ya kula chakula chochote. “Sitakula mpaka hapo nitakapokuwa nimesema maneno yangu” (mstari 33). Alizungumza kuhusu bwana wake, Ibrahimu, na kuhusu ukuu wake wa mali zake nyingi wa “makundi ya kondoo, ng’ombe, fedha na dhahabu” na jinsi alivyoongozwa na Mungu kwa Rebeka. Labani na familia yake walikubali kwamba ange kwenda na mtumishi. “Na awe mke wa mwana wa bwana wako kama BWANA alivyosema” (mstari  51).

REBEKA ANAKUTANA NA ISAKA: Mwanzo 24: 63 – 67

Rebeka alikuwa tayari kurudi Kanaani na Eliezeri. Kwa imani na uaminifu aliondoka na wasaidizi wake na mjakazi wake, Debora kwenda safari ndefu katika nchi asiyoijua, kuolewa na Isaka ambaye hakuwahi kumwona. Rebeka alitengana na familia yake na kuvuka mto akawa “Mwebrania” Alifuata nyayo za Ibrahimu kuungana na Isaka kuwa bibi arusi wake na mwenza wake mwaminifu. Walipoukaribia kambi, Rebeka alimwona Isaka akitembea nyikani na haraka alifunika uso wake. Hii ilikuwa ni desturi ya wakati huo kuonyesha kuwa alikuwa mkamilifu na kwamba angekua mke mwajibikaji.

Mara moja Isaka na Rebeka walioana na kulikuwa na shangwe kubwa katika familia ya Ibrahimu.

FUNDISHO KWETU

Ndoa inaweza kuwa safari ndefu isiyofikirika kwa vijana, lakini inachukua muda mrefu kuelewa umuhimu wa kuchagua mume au mke anayefaa. Ni neno la Mungu tu ndilo linalotuwezesha kufanya uchaguzi unaofaa. Soma Biblia na familia yako, kila siku kutafuta namana gani Mungu anataka wewe uweze kukua. Na hatimaye utajua jinsi ya kuchagua marafiki wanaokufaa wewe.

Daima chagua rafiki zako kwa uangalifu – kamwe usichangamana na wale watakokuongoza wewe kinyume na njia za Mungu, bali chagua rafiki wanampenda Mungu na wanaojitahidi kujifunza Neno lake na wanaomtii Yeye pia

MAELEZO YA ZIADA

1. Ujumbe wa Eliezeri – Mtumishi wa Ibrahimu alijidhihirisha kuwa mtu wa Imani, kwake kumwomba Mungu ilikuwa sehemu ya kazi yake na kungojea mwongozo wa Mungu (Mwanzo 24:12-14).Hakumchagua Rebeka kwa sababu ya uzuri wake (mstari 16) bali kwa sababu Mungu alimpatia ishara kwamba Yeye ndiye aliye mchagua kwa ajili ya kuolewa na Isaka (mistari 15-20). Mungu alipojibu maombi yake “aliinamisha kichwa chake na kumwabudu BWANA” (mistari:26-52).

2. Umuhimu wa ndoa yenye hekima – ndoa ni mkataba wa muda mrefu na hivyo hatuna budi kuwa waangalifu kwamba tunafanya uchaguzi ulio bora, tumwomba Mungu atasaidia kutuongoza katika jambo hili. Mambo muhimu ya kukumbuka ni haya:-

a. Mume na mke sharti wawe na Imani ya aina moja kusudi nyumba isigawanyike na kwamba watashiriki pamoja furaha kubwa katika kumwabudu Mungu. Soma Mithali 18:22: “Apataye mke apata kitu chema; Naye atajipata kibali kwa BWANA”.

b. Uzuri wa kweli ni ule wa moyoni. Unaoonekana kwa   njia ya kumtii Mungu na kwa kuwawazia mazuri wengine.

MASWALI

Majibu Mafupi

1. Nani alitumwa na Ibrahimu akiwa na ujumbe muhimu?

2. Ibrahimu alimtuma wapi mtumishi wake kumtafutia Isaka mke?

3. Eliezeri alichukua nini katika safari yake?

4. Mtumishi alimwomba nani msaada ili kumchagua mke mzuri wa mwana wa bwana wake?

5. Ni ishara gani Eliezeri aliyoomba ili  iwe ndiyo ya kumwonyesha  mke mzuri wa Isaka?

6. Rebeka alikwenda kuishi wapi?

7. Rebeka alimwona wapi Isaka kwa mara ya kwanza?

Majibu ya Kina

1. Kwa nini ilikuwa lazima kusafiri hadi kufikia hatua ya kutafuta mke anayefaa kwa ajili ya Isaka?

2. Ni somo gani muhimu tunalojifunza kutokana na simulizi la kumchagulia Isaka mke?

Maswali ya Nyongeza

1. Mtumishi wa Ibrahimu alihitaji msaada wa kumchagulia Isaka mke.

a. Alifanya nini?

b. Namna gani aliweza kujua ni msichana yupi anayefaa?

2. Ni mafundisho gani tunayo jifunza kutokana na habari hii ya kuhusu kuchagua marafiki  na hasa kuhusu kuchagua mume au mke?

Swahili Title
009 KUCHAGUA MKE WA ISAKA
English files
Swahili file
African text
CSSA
Translator 1
Jonathan Nkombe
Translator 2
Carl Hinton
Literature type
Sub type
Sub sub type