CSSA 1-1-10 - JACOB AND ESAU - THE BIRTHRIGHT AND THE BLESSING

Swahili

10. YAKOBO NA ESAU – HAKI YA MZALIWA WA KWANZA NA BARAKA ZAKE

“Isaka alimpenda Esau kwa sababu alikula mawindo yake, lakini Rebeka alimpenda Yakobo”

Shabaha

Kuonyesha ni kwa nini Mungu alimpenda Yakobo kuliko Esau. Mungu alimwahidi Ibrahimu ahadi nzuri na za ajabu na akazirudia tena kwa Isaka, mwana wa ahadi. Ilikuwa wakati Isaka alipokuwa akiishi katika nchi ya Wafilisti, Mungu alipomwambia “Nitazidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, nami nitawapa uzao wako nchi hizi zote na katika uzao wako mataifa yote ya dunia yatajibarikia” (Mwanzo 26:3 – 5). Angalia kwa makini mstari 5 unamhusu Ibrahimu kuwa ni mtu “aliyesikia sauti yangu, na akahifadhi maneno yangu na akashika amri zangu, hukumu zangu na sheria zangu. Na kuhusu Isaka akazidi kuwa mkuu na kuzidi kustawi … kwa maana alikuwa na mali nyingi ya makundi ya kondoo na makundi ya ng`ombe, alikuwa na watumwa wengi sana”.

Na mwishowe, Isaka aliishi katika Beer-sheba (Mwanzo 26:23)

(Mwanzo 25:23 – 34;27)

ESAU NA YAKOBO (Mwanzo 25:23 – 28)

Hawa walikuwa mapacha wa Isaka na Rebeka (Mwanzo 25:25 – 26). Kabla ya watoto kuzaliwa, Mungu alimwambia Rebeka kuwa, kutokana na wavulana hawa wawili yatatokea “mataifa mawili …kabila mbili za watu, kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili na mkubwa atamtumikia mdogo” (Mwanzo 23). Esau ambaye alikuwa mkubwa, alikuwa mwindaji hodari na mtu wa nyikani. Alikuwa anajiamini, mwepesi wa hasira na katika Kitabu cha Waebrania 12:16 anaelezewa kuwa ni mtu asiyemcha Mungu, ndiyo kusema ni mtu ambaye hakuwa na nia yoyote ya kumpendeza Mungu. Alikuwa amesongwa sana na anasa akiwa mwindaji kiasi cha kutojali hata kidogo walau kuweza kumfikiria Mungu. Hata hivyo, alikuwa mwana mpendwa kwa Isaka, baba yake, kwa sababu likuwa akila mawindo ambayo Esau alikuwa akimwandalia (Mwanzo 28).

Yakobo, yeye alikuwa tofauti, alikuwa mkimya na mtulivu, mtu “mcha Mungu, akiishi katika hema”. Huyu ndiye mtu aliyechaguliwa na Mungu. Alikuwa akipendwa na mama yake.

Kutokana na mtu huyu (Yakobo), walitokea watu wana wa Israeli ambao walikuja kuwa watu waliochaguliwa na Mungu. BWANA, Mungu wako amekuchagua kuwa watu wake  maalum (Kumbukumbu la Torati 7:6)

ESAU ANAUZA HAKI YAKE YA  MZALIWA WA KWANZA (MWANZO 25:29 – 34)

Esau akiwa mzaliwa wa kwanza, alikuwa mrithi mara mbili zaidi wa mali za baba yake kuliko Yakobo. Lakini, upendeleo huu maalum ambao ulijulikana kuwa ni haki urithi ya mzaliwa wa kwanza, hakuijali sana hadi kipindi cha baadae.Siku moja Esau alifika kutoka kuwinda,akiwa amechoka na alikuwa na njaa, na akamwona nduguye, Yakobo, akipika chakula. Kilikuwa ni chakula alichokuwa akikitaka; hivyo, akamwomba Yakobo bakuli moja ya chakula. Kwa haraka Yakobo akaona ni vyema wafanye mapatano ya kubadilishana “Leo hii niuzie haki ya uzaliwa wa kwanza” (mstari 31). Hivyo, Esau akabadilishana haki ya urithi wa mzaliwa wa kwanza, haki ya upendeleo wake maalumu katika familia kwa bakuli moja la chakula. Alisema “Itanifaa nini haki ya uzazi kwanza?” (Linganisha, Waebrania 12:16). Hii inaonyesha kuwa hakuwa na nia katika  zawadi ya mali za thamani ya urithi hata akaamua kumpatia mdogo wake kwa ajili ya mkate na bakuli moja la dengu (mistari 33-34).

ISAKA ANAWABARIKI WANAWE NA ANAMPA YAKOBO BARAKA ZAIDI: (Mwanzo 27:1 – 29).

Miaka mingi baadaye, Isaka akawa kipofu. Aliogopa  kuwa angekufa mapema, na hivyo alitaka kuwabariki wana  wake. Alipenda mawindo ya Esau na hivyo aliomba apewe kabla ya kumpa baraka zake mwana  wake mkubwa, “ukanifanyie chakula kitamu namna ile niipendayo”. Hivyo, Esau alichukua upinde na mishale yake ili akamwue swala kwa ajili ya baba yake (mistari 1 – 5).

Rebeka alimsikia Isaka alipokuwa akimwambia Esau, na kwa hiyo akafanya mipango ya kuhakikisha kuwa Yakobo  ndiye azichukue baraka hiyo  na wala siyo Esau ambaye atapokea baraka hiyo.

Alimwambia Yakobo achinje wana-mbuzi wawili ambao atafanya chakula kitamu. Ilikuwa Yakobo avae nguo za Esau na kuweka ngozi yenye manyoya ya mbuzi katika mikono yake na sehemu nyororo ya shingo yake kisha aende mbele ya baba yake ili Isaka amdhanie kuwa ni Esau (Kumbuka kwamba, Esau alikuwa ni “mtu ambaye nywele zake zilikuwa kama vazi la mwili wake, na Yakobo alikuwa ni mtu mwenye mwili laini”).

Kwa haraka, walikamilisha matayarisho ya chakula  kabla  Esau hajarudi mawindoni. Isaka, alishangaa kidogo kwa kutambua kwamba mawindo yake yaliandaliwa upesi sana, lakini Yakobo alimdanganya na kumhakikishia kuwa alikuwa ni Esau. Hata hivyo, Isaka alihisi sauti ilikuwa tofauti. “Sauti hii ni ya Yakobo lakini mikono ni ya Esau”.

Baada ya kuridhika kuwa alikuwa ni Esau akambariki Yakobo: “Mungu akupe ya umande wa mbingu, na ya manono ya nchi, mataifa na wakutumikie, na makabila wakusujudie, Uwe bwana wa ndugu zako, na wana wa mama yako wakusujudie atakaye kulaani  alaaniwe, na atakaye kubariki abarikiwe” Mwanzo 27:28 – 29.

Hivyo Yakobo akawa amebarikiwa, Mungu alikuwa amemwonyesha Rebeka kuwa  “mkubwa atamtumikia mdogo” (Mwanzo 25:23), lakini Rebeka hakuwa mvumilivu. Alidhani kuwa kama hataharakisha Mungu asingekamilisha ahadi yake! Na kama angevuta subira matatizo yote yaliyofuata kutokana na mipango yake ya udanganyifu yasingetokea katika familia

ESAU ANACHUKIA (Mwanzo 27:30 –16).

Ni wakati huo Yakobo alikuwa ametoka, Esau akawa amerudi kutaka baraka kwa baba yake. Kwa kiasi kikubwa alichukia alipotambua kuwa Yakobo alikuwa amemfanyia hila. Ilikuwa sahihi Yakobo kuitwa “mtu anayechukua nafasi ya mtu mwingine” kwani sasa  amechukua yote mawili, haki ya urithi ya mzaliwa wa kwanza na baraka zake. Esau aliendelea kumsihi Isaka, ili ambariki yeye pia, lakini  haikuweko baraka hata ndogo kusema kwamba “kwa upanga wako wewe utaishi, nawe utamtumikia nduguyo” (Mwanzo 27:40).

Na hapo ndipo sasa Esau akadhihirisha tabia yake. Akapanga kumwua Yakobo mara baada ya kufariki baba yake. Akiwa anahamasishwa na Rebeka, Yakobo alitambua kuwa wakati wa kuondoka nyumbani ulifika. Hata Isaka  pia aliona kuwa ilikuwa ni busara kwa Yakobo kuondoka. Kwa hiyo, alimwagiza aondoke kwenda Harani kwa watu wa mama yake, na huko akaoe mwanamke anayefaa miongoni mwao, kama Ibrahimu alivyotambua umuhimu  wa mwana wake kuoa mwanamke mcha Mungu. Esau akaoa wanawake kutoka Kanaani, kitendo ambacho kiliwakatisha tamaa na kuwatia uchungu  Isaka na Rebeka (Mwanzo 26:34 – 35).

Kabla hajaondoka, Isaka alimwombea, akambariki kwamba Mungu atampatia Yakobo  baraka ya ahadi alizomwahidi Ibrahimu (Mwanzo 28:3-4).

FUNZO KWETU

Esau alisikitika kwa kuwa hakupokea baraka. “Akapaza sauti yake akalia” (Mwanzo27:38). Lakini, alilia  nafsi yake tu, akitarajia kuwa  baba yake atabadilisha mawazo yake. Hakuwa na  nia  ya dhati moyoni mwake ya kumgeukia Mungu  na kubadilisha njia zake, mawazo yake yalikuwa kwake mwenyewe. Alikuwa amekasirika na mwenye kiburi, na tena alikuwa na moyo wa uovu - na ni moyo pekee ambao Mungu huutazama (1Samweli 16:7).

Inatupasa kuhakikisha kuwa hatufuati njia za Esau. Na  “inatupasa kunyenyekea chini ya  mkono wa  Mungu ulio hodari” (1Petro 5:6), na tulitii Neno lake na ahadi zake. Na sisi  tumejifunza kwamba haikuwa vizuri kwa Yakobo kumdanganya  baba yake na kumlaghai kama alivyofanya. Ni baada ya miaka kupita, Yakobo alitambua fundisho hili baada ya  kupatwa  na matatizo mengi katika maisha yake, naye alipodanganywa na baba mkwe wake, Labani, kama tutakavyoona katika somo linalofuata baadaye. Mungu alikuwa ameshaamua tangu zamani kwamba  Yakobo atapata baraka (Mwanzo 25:23), lakini Rebeka na Yakobo waliingilia kati. Iliwapasa kumngojea  Mungu kwa imani ili atende  katika maisha yao. Kwa hiyo, inatupasa kwa subira tumwamini Mungu, daima tufanye yaliyo haki na kweli maana hatatuacha kamwe.

MAELEZO YA ZIADA

Fikiria sasa ahadi kubwa na za  thamani  alizopewa Ibrahimu, Isaka na Yakobo na haki ya urithi ya  mzaliwa wa kwanza na baraka zilizompata Yakobo. Katika mambo haya yote, tunaona mtiririko wa mambo ya baadaye. Esau alikuja kuwa baba wa taifa la Edomu, watu wa maisha ya kinyama na wasio na utaratibu na wapenda vita ambao waliishi kwa upanga na kutokupata  kibali mbele ya macho ya Mungu. Kwa upande mwingine, Waebrania 11:17 – 20 inazungumzia imani ya Ibrahimu, Isaka na Yakobo katika maisha yao na ahadi walizopewa ambazo bado hazijatimizwa. Yakobo aliwekwa juu badala ya Esau na kupokea ahadi maalumu ya mzaliwa wa kwanza. Baadaye, wana kumi na mbili wa Yakobo wakawa taifa la Israeli na Mungu aliwapa baraka maalumu na kuwaita  mzaliwa wangu wa kwanza (Kutoka 4:22).

Katika miaka iliyofuata, wana wa  Israeli walifukuzwa kutoka katika nchi yao kama ilivyokuwa kwa Yakobo, lakini watarudi tena wakati  Yesu Kristo atakaporudi,  watakuwa kama Yakobo,  kutakuwa  na mabadiliko makubwa katika mioyo yao. Ni wakati huo ndipo watatulia na kuishi katika nchi yao kwa amani: “Yakobo (yaani Taifa la Israeli) atarudi na kustarehe na wala hakuna mtu atakaye mtia hofu” (Yeremia 30:10).

MASWALI

Majibu mafupi

1.     Ni nani walikuwa wana wawili  wa Rebeka?

2.     Yakobo alikuwa mtu wa aina gani?

3.     Esau alimpa  nini  Yakobo kama malipo ya bakuli ya chakula?

4.     Ni mwana yupi aliyepokea baraka kutoka kwa baba yake?

5.     Esau alikuwa na mipango  gani kuhusu Yakobo?

6.     Yakobo alikwenda wapi alipomkimbia Esau?

7.     Mpango wa Rebeka wa kumdanganya Isaka haukuwa wa busara. Badala yake angefanya nini?

Majibu  ya Kina
  1. Isaka na Rebeka walikuwa na watoto mapacha wa kiume. Mungu alizungumza na mama yao kabla hawajazaliwa.
  2. Mungu alimwambia nini Rebeka kuhusu wana  wake wawili?
  3. Unajua nini kuhusu Esau?
  4. Kwa nini Esau alimpa Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza?
  5. Eleza nini kilichotokea siku ambayo Isaka aliwabariki wana wake?
Majibu ya Ziada

1.     Isaka alikuwa mzee, na alitaka kutoa baraka kwa wanawe. Eleza jinsi Yakobo alivyopata baraka ambayo     alitaka kumpa Esau ?

2.     Ni baraka zipi ambazo Isaka aliwapa Yakobo na Esau?

3.     Ni lini Ibrahimu, Isaka na Yakobo watarithi ahadi ambazo Mungu aliwapa?

 

Swahili Title
010 YAKOBO NA ESAU – HAKI YA MZALIWA WA KWANZA NA BARAKA ZAKE
English files
Swahili file
African text
CSSA
Translator 1
Jonathan Nkombe
Translator 2
Jacob Haule
Literature type
Sub type
Sub sub type