CSSA 1-3-01 - THE KINGDOM IS ESTABLISHED

Swahili

51. UFALME WAANZISHWA

“Naye BWANA akampa Daudi kushinda kila alikokwenda”

 

Shabaha

 Ni kuonyesha jinsi Mungu alivyomwinua Daudi kuwa mfalme juu ya Israeli. Baada ya watu wa Israeli kukaa katika Nchi ya Ahadi kwa miaka mingi, wakatamani wawe na mfalme, ingawa Mungu kwa kweli ndiye aliyekuwa mfalme wao, lakini walimtaka mfalme ambaye angewaongoza kwa fahari vitani kama vile mataifa yaliyowazunguka. Sauli alikuwa mfalme wao wa kwanza, lakini alishindwa kuwa mtiifu kwa Mungu. Hivyo Mungu akamtia mafuta Daudi mtu aliyeupendeza moyo wake, kutawala watu wake.

2 Samweli 8 na 9

 

DAUDI AWA MFALME:- 2 Samweli 7: 1 – 17

Sasa Daudi alikuwa mfalme huko Yelusalemu, ilikuwa inakaribia miaka 20 tangu Mungu alipomtuma nabii Samweli kumtia mafuta yeye kuwa mfalme (1 Samweli 16: 12 – 13). Ingawaje alikuwa kijana mchungaji wa kondoo tu wakati ule, Mungu alikuwa akimfundisha jinsi ya kutawala watu wake. Kwa miaka mingi iliyofuata alikuwa amekabili matatizo mengi.Hata hivyo kila wakati alikuwa akikumbuka kwamba Mungu alikuwa naye, akimwongoza wakati huu hadi muda wenyewe hasa ambapo mwishowe angekuwa mfalme huko Yerusalemu. Kwenye masomo yetu mwaka jana tulijifunza jinsi Mungu alivyomwahidi Daudi ahadi nzuri sana ajabu, kuhusu “mzao” wake, Bwana Yesu Kristo.

 

 Ndiye angekuwa mwana ambaye ni mkuu wa Daudi ambaye angeketi katika kiti cha enzi cha Daudi milele. Wakati ajapo huyo mfalme mkuu hatatawala waisraeli tu,bali atatawaa ulimwengu mzimak (2 Samweli 7: 12 – 16)

 

DAUDI ANAWASHINDA ADUI ZAKE:- 2 Samweli 8

Wakati Mungu alipotoa ahadi yake kwa ajili ya “mzao” wa Daudi, Daudi alikuwa na hisia ya kumshukuru sana kwa ajili ya baraka za Mungu hata ikawa anataka kumjengea Mungu nyumba ili waitumie kwa ajili ya kumwabudu yeye. Mungu kwa hakika alipendezwa sana kuona jinsi Daudi alivyokuwa na shukrani, lakini akasema “wewe hatajenga nyumba kwa ajili ya jina langu, kwani umekuwa mtu wa vita, nawe umemwaga damu” (1Mambo ya Nyakati 28:3). Hekalu la Mungu ilibidi lijengwe wakati wa amani, wakati huo huo lilikuwa ni jukumu la Daudi kuwashinda adui waliokuwa wamezunguka ufalme wake kila upande.

 

Tunajifunza katika 2 Samweli 8-12 kuhusu mapigano saba ambayo Daudi aliyapigana, alipigana na ufalme wa Kaskazini, kusini, mashariki na magharibi mpaka maadui wa Israeli waliposhindwa (tazama ramani).

 

Alipotoka kwenda vitani, Mungu alimsaidia kushinda mapigano juu ya mataifa. “Naye BWANA akampa Daudi kushinda kila alikokwenda” (2 Samweli 8:6,14). Daudi hakuacha kamwe wazo la kujenga nyumba kwa ajili ya kumwabudu Mungu. Kutokana na kushinda mapigano vitani akakusanya hazina kubwa ambayo baadaye ingetumiwa na mwanaye wakati wa kujenga Hekalu Tukufu ambalo yeye mwenyewe alikuwa ametamani mno kulijenga (2 Samweli 8:10-11)

 

DAUDI AWAKUMBUKA RAFIKI ZAKE:2 Samweli 9: 1-4

 Daudi alikuwa na shughuli nyingi sana, lakini hata angekuwa na kazi nyingi namna gani, hata mara moja hakuwasahau rafiki zake. Akawatuma watumishi wake kuangalia kama kuna mtu mmoja yeyote aliyesalia katika nyumba ya Yonathani aliyekuwa hai.Daudi alisema, “Je hajasalia mtu mmoja yeyote wa nyumba ya Sauli” Daudi akasema “ili kwamba nimtendee wema wa Mungu?Katika siku ambazo alikuwa akimkimbia Sauli, Yonathani alikuwa ndiye rafiki yake mkubwa.

 

 Wote walimpenda Mungu nao walikuwa wamejaa na imani na ujasiri. Ingawa Yanathani alikuwa ndiye mwana wa kwanza wa Sauli kwa kuzaliwa, alifurahi alipofahamu kuwa Mungu alikuwa amemchangua Daudi kuwa mfalme atakayefuatia. Hao wawili walikuwa wamefanya mapatano ya urafiki wa dhati naye Daudi alikuwa ameapa kuwatendea mema familia ya Yonathani wakati atakapokuwa mfalme.Kwa hiyo sasa Daudi akamwita Siba mtumishi mmoja katika nyumba ya Sauli, ambaye alimwambia kwamba Yonathani alikuwa na mwanaye ambaye alikuwa bado hai, ambaye aliitwa Mefiboshethi.

 

DAUDI AMTUNZA MEFIBOSHETI:- 2 Samweli 9: 5 -13

 Mefiboshethi alikuwa mlemavu wakati babaye Yonathani alipokufa vitani, yaya wake akamchukua akakimbia, ikawa alipokimbia kwa haraka kutokana na hofu, akaanguka pamoja na mtoto huyo, yule akaumia sana.Na kuanzia wakati huo akawa kilema wa miguu yote na hivyo akawa hawezi kutembea sawasawa.

 

Mfalme alipomwita aingie Mefiboshethi akaingia ndani na kusujudu mbele yake, alifahamu kuwa mlemavu hakuwa na thamani yoyote kwa mfalme na kwa ajili hiyo aliogopa kidogo alipomkabili Daudi, lakini Daudi alikuwa na furaha kupata nafasi ya kumsaidia mwana wa rafiki yake. Akamrejeshea maeneo ya ardhi yote iliyokuwa mali ya Sauli, babu yake na kumkaribisha kula naye kwenye meza ya mfalme.

 

Lakini Mefiboshethi hangeweza kutunza mashamba ya familia yake, hivyo mtumishi wake Siba akateuliwa kuyashughulikia. Daudi akamleta Mefiboshethi kuishi huko Yeresalemu na kuwaambia watumishi wake “Mefiboshethi atakula mezani pangu kama mmoja wa wana wa mfalme” (mist 11) kwa njia hii Daudi akatunza ahadi yake kwa Yonathani na kumheshimu mwanaye.

 

Mefiboshethi alikuwa ni mwenye shukrani nyingi kwa ajili ya heshima aliyopewa na mfalme na kudumisha uaminifu wake kwa Daudi, kwani ni kwa njia hiyo pekee angeonyesha shukrani zake.

 

FUNDISHO KWETU

Mungu alikuwa amemchagua Daudi kuwa mfalme wakati akingali kijana mchungaji wa kondoo, alijua kwamba vitu ambayo angejifunza Daudi wakati wa kuchunga kondoo vingemfundisha jinsi ya kuwatawala watu wake kwa hekima. Mchungaji inabidi kuwa na uwezo wa kuwaongoza kondoo wake kwenye sehemu salama na kuhakikisha kuwa hawapotei na kujiumiza. Inampasa kuwalinda kutokana na maadui zao, inampasa kuwa mwema kwa kila mmoja wao, ili kwamba wajifunze kumpenda na kumwamini.

 

Daudi alikuwa namna hiyo hiyo kwa watu wa Israeli alikwenda vitani pamoja nao na kuwasaidia kupata ushindi tunaambiwa kwamba 'naye akawafanyia hukumu na haki kwa watu wake wote'(8:15)- linaloelezea kuwa alikuwa mtawala wa haki na mwenye busara, akiwaongoza kama mchungaji wa kondoo.

 

Hata mara moja hakuwa na kazi nyingi mno kushindwa kuonyesha wema kwa wahitaji, na kwa sababu hiyo walimpenda na kumwamini. Inatupasa kukua na kuwa namna hiyo hiyo kwa wenzetu- siyo tu kwa rafiki zetu, kwani hilo ni rahisi, lakini tuwe hivyo kwa wote tulio nao, wakiwa ni vijana au wazee wanaoipenda Kweli. Kwa njia hiyo kutokana na kutenda vitu vidogo vilivyo vyema na kuwaza mawazo mema, tunasaidiana na kutiana moyo katika mwenendo wetu kuelekea kwenye Ufalme.

 

MAELEZO YA ZIADA: 2 Samweli 12: 7 – 25

 Tunapenda kusoma habari za Daudi na kufuata maisha yake kadiri alivyokuwa kutoka kuwa kijana mchungaji wa kondoo hadi kuwa hodari mwenye ujasiri, ambaye imani yake kwa Mungu ilimsaidia kuua jitu kubwa Goliati. Akiwa katika kumkimbia Sauli tunapendezwa na ujasiri wake na kuanza kumpenda tunapoangalia urafiki wa upendo mwingi ukikua kati yake na Yonathani.

 

Mwishowe anakuwa askari hodari mwenye nguvu sana na mfalme mkuu, mwenye imani kwa Mungu na mwenye shukrani kwa ajili ya yote aliyopewa. Hata hivyo, habari haimalizikii hapo, kati ya vitu tulivyovizungumzia katika somo hili na utawala mtukufu wa mwanaye Selemani, kulikuwa na miaka ya matatizo, maumivu na huzuni sana.

 

 Haya yote yalitokea juu ya Daudi kwa sababu alimkosea Mungu kwa kuwa alitenda dhambi. Watu wa Israeli walikuwa vitani, wakipigana na Waamoni, Daudi ilimbidi awaongoze vitani, lakini aliamua kubaki nyumbani katika jumba la ufalme, badala ya kushughulikia kuwahami watu wake, kama mchunga kondoo mwema na mfalme mwema akawa mvivu, nayo akili yake haikuwa kwa watu wake hata kidogo.

 

Na wakati wa jioni alipokuwa akitembea juu ya dari la nyumba yake, alimwona mwanamke mmoja aitwaye Bath-sheba na kumtamani awe mkewe. Dhambi moja huongoza kutenda dhambi nyingine na hivyo ili kujaribu kuficha dhambi yake ya kwanza akafanya njama ya kumuua vitani mumewe mwenye haki na mwaminifu aliyeitwa Uria.

 

 Katika haya yote, Mungu hakuwemo katika mawazo ya Daudi lakini Mungu alijua yote haya aliyoyatenda Daudi, hakuna kitu kilichokuwa kimefichikana machoni pake. Hvyo Mungu akampeleka Nabii wake Nathani kuzungumza na Daudi, Nathani akamkumbusha Daudi yote ambayo Mungu aliyafanya katika kumleta yeye hadi kwenye kiti cha enzi cha Israeli. “Kwa nini umelidharau neno la BWANA, na kufanya mabaya machoni pake?

 

 Nathani akamwuliza “Umemwua Uria Mhiti, kwa upanga, na umemtwaa mkewe kuwa mke wako, nawe umemwua kwa upanga wa wana wa Amoni” (12:9)

 

Daudi alikuwa amerudisha uovu kwa upendo wote wa Mungu ambao alimtendea. “Nabii akaendelea kusema, “Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau mimi” (12:10) Daudi angeweza kusema nini?

 

Alielewa alikuwa amefanya kosa na Mungu angemwadhibu sana Daudi alisema, “Nimemkosea BWANA” Jibu la Nathani lilikuwa hili “Mungu naye ameondoa dhambi yako mbali nawe, hautakufa” (mstari 13)

 

Oh, jinsi zilivyokuwa kuu rehema zake Mungu kwa Daudi! Ilikuwa auawe, lakini Mungu aliona mabadiliko ndani ya moyo wake naye akamsamehe, kamwe tena hakusahau upendo wa Mungu kwake.

 

 Ila hakuruhusiwa kamwe kusahau ubaya wa habari hii katika maisha yake yote yaliyobakia. Matatizo yakajitokeza kati ya wanawe, waliomletea aibu na huzuni kubwa. Matatizo yote haya yalimfundisha Daudi kuwa mnyenyekevu sana mbele za Mungu, na hilo lilimpendeza Mungu.

 

 Oh, jinsi dhambi ilivyo na udanganyifu! Ni rahisi sa kutenda lolote tulitakalo na kujaribu kuficha dhambi zetu. Tusisahau kwamba Mungu aona na kujua mambo yote hata mawazo yaliyo mioyoni mwetu, ni Mungu wa haki naye atatuadhibu tukifanya dhambi kwake. Tunyenyekee kama Daudi alivyofanya, tukiri kuwa sisi tumekosa na kumwamini Mungu nyakati zote.

 

MASWALI

MAJIBU MFUPI

  1. Ni miaka mingapi ilipita tangu Samweli alimpaka mafuta Daudi?
  2. Ili kuonyesha shukrani kwa Mungu, Daudi alitaka kufanya nini?
  3. Kwa nini Mungu hakupenda Daudi afanye jambo hilo?
  4. Ni kazi gani Mungu sasa alitaka Daudi aifanye akiwa mfalme?
  5. Ni nani ambaye Daudi alimwahidi kumtunza?
  6. Nini kilimtokea Mefiboshethi alipokuwa mtoto mdogo?
  7. Ni mambo gani mawili ambayo Daudi alimfanyia Mefiboshethi?
  8. Ni nani aliwekwa kumtunza mashamba ya Mefiboshethi?
  9. Ni jambo gni Daudi alikuwa ametenda alipokuwa kijana lilimsaidia kuwa mfalme bora?

 

Majibu ya Kina

  1. Eleza Daudi alichofanya baada ya kuwa mfalme, ili kuonyesha upendo wake kwa Yonathani
  2. Daudi alikuwa mchunga kondoo ni kwa namna gani hilo lilismaidia kumfanya kuwa mfalme bora?
  3. Ni funddixhoo gani tunalojifunza kutokana na wema wa Daudi kwa Mefiboshethi

 

Majibu ya Ziada

  1. Daudi alikuwa amefanya dhambi kwa Mungu
    1. Eleza jinsi Mungu alivyoonyesha rehema kwa Daudi
    2. Eleza jinsi Mungu alivyomwadhibu Daudi?
    3. Ni mafundisho gani tunajifunza kutokana na dhambi ya Daudi?

 

Swahili Title
051 UFALME WAANZISHWA
English files
Swahili file
Literature type
Sub type
Sub sub type