CSSA 1-3-05 - THE KINGDOM IS DIVIDED

Swahili

55. UFALME UNAGAWANYIKA

“Kwa hakika nitaurarua ufalme kutoka kwako, nami nitampa mtumishi wako”

 

Shabaha

Kuonyesha jinsi ufalme wa Israeli ulivyogawanyika. Mungu alikuwa amembariki Sulemani kwa yote ambayo mtu angeweza kuyatamani. Mali, amani, na furaha ya ufalme wake iliyafanya maisha kuwa mazuri sana, lakini jinsi muda ulivyoendelea akamsahau Mungu kuwa ndiye aliyempatia hayo yote. Mungu hakuwamo katika mawazo yake yote, naye mawazo yake yakageukia kuelekea mengine – mambo hasa ambavyo Mungu alikuwa amemkataza. Katika hasira yake Mungu alisema: “Kwa hakika nitaurarua ufalme kutoka kwako, nami nitampa mtumishi wako” (1Wafalme 11:11)

1 Wafalme 12

 

SULEMANI ANASAHAU KUWA NI MWENYE HEKIMA:

1 Wafalme 10:26-28;11:1-13

Baada ya Sulemani kumaliza ujenzi wa hekalu Mungu alimtokea mara ya pili na kusema, “Na wewe ukienda mbele zangu kama alivyokwenda Daudi, baba yako... ndipo nitakapokifanya imara kiti cha ufalme wako juu ya Israeli milele” (1 Wafalme 9:4-5). Walakini, muda ulivyoendelea alisahau yale ambayo baba yake Daudi alikuwa amemfundisha, “Nawe, Sulemani mwanangu…mtumikie Mungu kwa moyo mkamilifu na kwa nia ya kumkubali... kama ukimtafuta, ataonekana nawe ukimwacha, atakutupa milele” (1 Mambo ya Nyakati 28:9)

Muda mrefu kabla hakujakuwapo mfalme katika Israeli, Mungu alikuwa amewapatia masharti ya kuzingatia kwa ajili ya wafalme wa siku zijazo.

 

 Maelekezo haya yanapatikana katika Kumbu kumbu la Torati 17:14 – 20. Kulikuwa na mambo matatu ambayo Mungu alikuwa amewaonya wafalme wasiyafanye. Na Katika mambo haya matatu Sulemani alishindwa.

 

  • Asifanye farasi wake kuwa wengi,wala asiwarudishe watu Misri,ili kusudi apate kufanya farasi kuwa wengi (mstari16; linganisha na 1 Wafalme 10: 28 -29
  • Wala asijizidishie wake ili moyo wake usikengeuke (mstari17 linganisha na 1 Wafalme 11: 1-2
  • Wala asifanye fedha zake na dhabahu kuwa nyingi mno (mist17 linganisha na 1Wafalme 10:27)

 

Katika mambo haya yote moyo wake Sulemani uligeukia mbali na Mungu. Kati ya mambo haya matatu, jambo ambalo hatimaye lilikuja kumpotosha kutoka kwenye ibada ya kweli lilikuwa ni kuoa wake wengi kutoka nchi za kigeni, ambao walileta ibada zao za miungu katika Israeli.Wanawake hawa wa kigeni kamwe hawakujifunza kumwabudu BWANA, bali walimfundisha Sulemani kuwaiabudu miungu yao, “Hata ikawa,Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakaugeuza moyo wake, afuate miungu mingine” (11:4).

 

Sulemani akazijenga madhabahu kwa ajli ya wake zake wa kigeni ili waitolee miungu yao dhabihu kwenymadhabahu hizo hata na yeye mwenyewe akaungana na wake zake katika kuiabudu miungu. “Moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA, Mungu wake, kama ulivyokuwa moyo wa Daudi, baba yake” (11:4) naye Mungu akamgadhibikia (11:9-10). Kwa hiyo Mungu akamwambia Sulemani kwamba ufalme utaondolewa kutoka kwa mwana wako. Lakini kwa ajili ya Daudi, hatauondoa ufalme wake wote kabisa.

 

Yuda na Benyamini, ambazo mipaka yake hufika hadi Yerusalemu, zingebakia kuwa ufalme ambao wazawa wa Daudi wangetawala. Makabilia yale mengine kumi yangeraruliwa na kupewa mtu mwingine (11:43 – 36). Hekima ya Sulemani ilileta amani na furaha kwa Israeli. Dhambi zake za kipumbavu zingeleta huzuni kuu na mateso kwa watu wa Mungu.

 

REHOBOAMU ANAKUWA MFALME: 1 Wafalme 12:1 -15

Hivyo Sulemani akafariki, baada ya kutawala Israeli kwa muda wa miaka 40 (1 Wafalme 11:42-43) naye Rehoboamu mwanawe akatawala mahali yake. Watu wakakusanyika pamoja huko Shekemu kumtia mafuta ili awe mfalme juu ya Israeli.

 

Kwa wakati huo watu wengi katika Israeli hawakuridhika kwa kuwa Sulemani aliwawekea kodi kubwa ili kupata fedha kulipia ujenzi wa majumba aliyoyajenga wakati wa utawala wake. Kodi hiyo ilikuwa ni mzigo mzito sana kwa watu, nao waliturajia kwamba huyu mfalme mpya angeweza kufanya mambo yawe rahisi kwao. Wakamchagua mtu aliyeitwa Yeroboamu kwenda kwa Rehoboamu kuwasemea badala yao. Yeroboamu akamwambia “Baba yako alilifanya zito kongwa letu; sasa basi utupunguzie utumwa mzito tuliotumikishwa na baba yako, na lile kongwa zito alilotutwika, nasi tutakutumikia ” (mstari 4)

 

Kwa hiyo mfalme Rehoboamu akawaambia hao watu kuwa wampatie siku tatu kufikiria juu ya hilo na ndipo angewapatia jibu lake. Kwanza Mfalme Rehoboamu akataka ushauri wa wazee ambao walikuwa washauri wa baba yake, “Mwanipa ushauri gani ili ni wajibu hawa watu?” Wazee walimshauri kwamba ingekuwa busara kwa Rehoboamu kufanya kama watu walivyomwomba.

 

Wazee walimwambia “Ukikubali kuwapa maneno mazuri watu hawa, ndipo watakuwa watumishi wako milele” (mstari 7).

 

Rehoboamu hakuukubali ushauri huu. Kwa sababu hii, alifahamu kuwa Yeroboamu alikuwa akimchukia baba yake Sulemani, naye hakutaka kabisa akubaliane na ombi lake. Hivyo akawageukia vijana waliokuwa pamoja naye na kuwataka ushauri wao, na vijana hao kama Rehoboamu, walikuwa wamelelewa katika maisha ya anasa na maisha ya kuishi ikulu. Hawakuwa na wazo juu ya yaliyo mema kwa watu, hivyo wakamshauri mfalme kutokukubali matakwa ya watu hata kidogo, bali kutishia kufanya mambo kuwa magumu zaidi.

 

Hekima haikuwemo katika ushauri huu, ila ulikuwa ni ushauri wa kumpendeza mfalme huyu kijana mwenye kiburi. Watu waliporudi baada ya siku tatu, aliwajibu kwa ukali. “Baba yangu alilifanya zito kongwa lenu; bali mimi nitaliongeza kongwa lenu” (mstari 14). Alitaka wamwone kuwa alikuwa mfalme imara na ya kuwa ingewapasa kukubaliana na matakwa yake, katika haya yote Rehoboamu hakufikiria kumgekia Mungu ili apate ushauri wake.

 

UFALME ANAGAWANYIKA: 1 Wafalme 12:16-24

Watu waliposikia jibu lake na kuona kwamba maisha yangekuwa magumu zaidi kwao, wakachukia. Basi wale watu wakasema kwa hasira, “Haya/nendeni zenu hemani kwenu, enyi Israeli”. Waliyatamka maneno haya Mfalme, “Sasa itunze nyumba yako, Ee Daudi” (mstari16).

 

Hivyo wakaasi na kukataa Rehoboamu kutawala juu yao. Badala yake wakamgeukia Yeroboamu kuwa kiongozi wao na kumtawaza kuwa mfalme huko Shekemu. Rehoboamu alipotambua kuwa ni maneno yake ya kipumbavu yaliyowafanya watu wamchukie akakimbilia Yerusalemu kuokoa uhai wake. Ni Yuda na Benyamini pekee walibaki waaminifu kwake kama Mungu alivyokuwa amemwambia Sulemani (11:13)

 

Lakini Rehoboamu hakupenda kuachia kiurahisi namna hiyo. Ndipo akawakusanya watu wa vita katika Yuda na Benjamini na kujitayarisha kwenda vitani ili kupigana na ndugu zake waliopo upande wa kaskazini. Alifikia kuwa kama atachukua hatua mara moja alitarajia kuwa ataweza kuyarudisha yale makabila kumi kwake na kuumaliza uasi.

 

Wakati akiwa katika kujiandaa kwa ajili ya hiyo vita, Mungu akampelekea nabii kumuzuia. Nabii akasema BWANA, asema “Hamtakwenda, wala hamtapigana na ndugu zanu wana wa Israeli, Rudini kila mtu nyumbani kwake, kwa kuwa jambo hili limetoka kwangu”.

 

Huu ndiyo uliokuwa mwanzo wa huzuni nyingi kwa watu wa Mungu, utawala wa enzi ya utukufu ya Sulemani ilikuwa imekwisha, kwani kwa dhambi yake alikuwa amegeuza utukufu wake na nguvu kuwa aibu na masikitiko. Makabila yale kumi ya kaskazini yakaja kujulikana kama ufalme wa ISRAELI ambapo yale ya kusini ukajulikna kuwa ni ufalme wa YUDA.

 

DHAMBI YA YEROBOAMU- 1 Wafalme 12:25 33

Sasa kwa vile watu walikuwa wamemfanya Yeroboamu kuwa mfalme juu ya Israeli wote, akaazimia kuhakikisha kwamba watu hawairudii tena “nyumba ya Daudi”. Maana alifahamu kwamba watu kwa haraka wangetaka kwenda Yerusalemu kumwabudu BWANA katika hekalu naye akaogopa kuwa wajimtambua kuwa walitenda kosa kumkataa mfalme. Na hata wangeweza kumtaka Rehoboamu kuwa mfalme wao tena na kumwua yeye. Hivyo akafikiria mpango mwovu sana. Akatengeneza ndama wa dhahabu wawili na kuwaambia watu, “Ni vigumu kwenu kwenda Yerusalemu, tazama miungu wenu, enyi Israeli iliyowpandisha kutoka katika nchi ya Misri” (mstari 28).

 

Akamweka mmoja katika Betheli, kusini mwa ufalme wake, na wa pili akamweka katika Dani, upande wa kaskazini kabisa. Kwa upumbavu huu, watu walimwamini na kuabudu mbele ya kila sanamu hizi. Akaweka siku ya sherehe na kujenga nyumba kwa ajili ya miungu hii na kuteua makuhani ambao walikuwa watu duni kabisa katika Israeli. Mambo yote yalionekana kuwa madogo kabisa sawa na dhambi zingine ambazo walizitenda kabla - lakini mambo yote hayo yalikuwa ni uovu kabisa; hakuna hata moja kati ya mambo hayo ambalo Mungu alikuwa ameliagiza. Ilikuwa ni ibada ya sanamu, jambo ambalo Mungu huchukia. Kwa hiyo Yeroboamu anajulikana katika historia nzima ya Israeli kuwa ndiye mtu aliyewakosesha Israeli; wakafanya dhambi (1 Wafalme 14:16, 15:34 nk)

 

Fundisho kwetu

Ni lazima tuwe waangalifu na kufuate maagizo ambayo Mungu aliyaandka katika kitabu kuhusu wafalme. Mambo ambayo Mungu alikuwa akiwaonya wafalme wasitende, ilihusu anasa za dunia. Sulemani aliruhusu anasa za dunia kuchukua nafasi ya Mungu katika moyo wake.

 

 Mungu anatuambia, “msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia, mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo moyoni mwake” (1 Yohano 2:15 -16). “Basi, kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu” (Yakobo 4:4), Kwa hiyo inatupasa kumpenda Mungu na njia zake, tukifanya yote tuwezayo ili kumpendeza Mungu. Anatueleza katika Kumbukumbu la Torati 17:18 -20 jinsi mfalme angeweza kufanya hilo.Ilimpasa kuandika nakala ya torati ya Mungu na kusoma ndani yake siku zote za maisha yake. Sisi kila mmoja anayo Biblia na inampasa kuisoma kila siku, ili kwamba tuweze kujifunza kuwa waaminifu kwa Mungu siku zote za maisha yetu.

 

MAELEZO YA ZIADA

Yeroboamu alikuwa nani? Alikuwa ni afisa mwenye bidii sana katika siku za Sulemani. Mfalme alimpenda kwa bidii yake na kumweka juu ya kazi zilizofanya na familia ya kabila la Yusufu. Bila shaka alikuwa mtu mpenda maendeleo na cheo, na kuonekana kuwa mtu aliye kiongozi kati ya watu.

 

Siku moja alipokuwa ameondoka kutoka Yerusalemu, nabii Ahija alimkuta naye shambani, hapakuwepo na mtu mwingine yeyote pale, Ahija alikuwa akivaa koti jipya, akavua koti lake na kulichana katika vipande kumi na viwili. Vipande kumi kati ya hivyo ukampa mkononi Yeroboamu na kusema “chukua vipande hivi kumi kwani ndivyo asemavyo BWANA, Mungu wa Israeli, tazama nitaurarua ufalme, na kuuondoa katika mkonono wa Sulemani, nami nitakupa wewe kabila kumi (1 wafalme 11:31). Akaendelea kumweleza Yeroboamu kwamba Mungu asingempa yale makabila mawili mengine lakini atayatunza kwa ajili ya nyumba ya Daudi, “ili Daudi mtumishi wangu aweza daima kuwa na taa siku zote mbele zangu katika Yerusalemu” (mistari 36). Kama angemtii Mungu na kuahidi kuzishika amri za Mungu (mistari 38), ndipo Mungu angeuimarisha, kwa uhakika ufamle wake.

 

Mungu alikuwa amemfunuliaa Sulemani uamuzi wake wa kuugawa ufamle (mstari 11-13). Sasa Mungu alimtaja mtu aliyemchagua kuchukuwa sehemu ya ufalme kutoka kwenye nyumba ya Daudi. Inaonyesha kwamba Yeroboamu alifurahia sana kusikia unabii huu wa kushangaza, na yaelekea aliwaambia watu wengine kuhusu jambo hili, kwaana habari hizi zilifika masikioni mwa mfalme Sulemani mapema sana. Mfalme alikasirika na alijaribu kumwua Yeroboamu, lakini alikimbilia Misri na kukaa huko hadi Sulemani alipofariki.

 

MASWALI

Majibu Mafupi

1. Ni nani waliogeuza moyo wa Sulemani akaacha kumwabudu Mungu?

2. Ni kwa miaka mingapi Sulemani alitawala juu ya Israeli?

3. Ni wapi watu walikusanyika kumfanya Rehoboamu kuwa mfalme?

4. Watu walitaka Rehoboamu afanye nini?

5. Wazee walimwambia Rehoboamu afanye nini?

6. Vijana walimwambia Rehoboamu aseme nini?

7. Watu walihisi vipi Rehoboamu alipowapa jibu lake?

8. Je, Rehoboamu ingempasa apokee ushauri kwa nani?

9. Ni makabila gani mawili yalibakia na Rehoboamu?

10. Ni makabila mangapi yalimchangua Yeroboamu kuwa mfalme wao?

11. Ufalme wa Kaskazini jina lipi?

12. Ufalme wa Kusini uliitwa jina gani?

 

Majibu ya Kina

13. a) Ni mambo gani matatu ambayo Mungu aliwaonya wafalme wasiyafanye?

 b) Ni jambo lipi moja ambalo Mungu alisema kila mfalme juu ya Israeli lazima alifanye?

 c) Ni fundisho gani tunalojifunza kutokana na hili?

14. Eleza jambo gani la uovu Yeroboamu alitenda na akasababisha watu wakamfuata kwa kuwa alikuwa mfalme wao

15. a) Eleza nini kilitokea baada ya Rehoboamu kuwapatia watu jibu lake

      b) Ni jinsi gani Mungu alimkataza Rehoboamu kupigana na makabila yale mengine kumi?

Majibu ya Nyongeza

16. Eleza namna Mungu alivyomfunulia Yeroboamu kuwa atakuwa mfalme juu ya Israeli

 

Swahili Title
055 UFALME UNAGAWANYIKA
English files
Swahili file
Literature type
Sub type
Sub sub type