82. YESU ANAKATALIWA NAZARETHI
“Roho wa Bwana juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema”
Shabaha
Kuonyesha namna watu wa Nazarethi walivyo mkataa Yesu na kujaribu kumwua. Kutoka Kana Yesu aliamua kurejea Nazarethi mji wa nyumbani kwake. Kila mtu alimfahamu kule, walimfahamu kuwa ni mwana wa Yusufu yule seremala. Walikuwa wamesikia juu ya miujiza yake na yale aliyoyatenda huko Yerusalemu. Alikulia kati yao nao walimfahamu kuliko mwingine yeyote yule, walakini hili ndilo lilikuwa jambo hasa lililofanya watu wa Nazarethi kuona vigumu kuamini kuwa Yesu angeweza kuwa ndiye masihi, mwana wa Mungu. Hakuna shaka walikuwa wamempenda alipokuwa mvulana mdogo, kwani kila wakati alikuwa mtiifu na mwangalifu, sasa lakini, alirudi akiwa ni mwalimu nao hawakumsikiliza.
Luka 4:16 – 22.
YESU ANAFUNDISHA KATIKA SINAGOGI HUKO NAZARETHI:
Luka. 4:16 – 22.
Siku ya Sabato Yesu alikwenda katika sinagogi “kama ilivyokuwa desturi yake” (mstari16). Alikuwa akipenda kujifunza neno la Mungu kila wakati, tangu alipokuwa kijana mdogo. Sasa siku hiyo ya Sabato akasimama kusoma.Akapewa chuo cha nabii Isaya naye akafungua akasoma kifungu kinachosema “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuhubiri maskini habari njema, Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa” (mstari18 – 19; soma Isaya 61:1 – 2).
Akiwa imefikia nusu ya fungu alilokuwa akisoma Yesu akaacha kusoma akakikunja chuo na kukaa. Macho ya kila mmoja katika sinagogi yalikuwa kwake, wakati wakingojea kusikia alichopasiwa kusoma. Maneno aliyoyasoma yalilenga mbele kwa masihi, yeye “aliyetiwa mafuta” na Mungu. Maneno hayo aliyoyasoma yalielezea miujiza na nyakati za furaha na uhuru kutokana na maumivu na huzuni. Kila mtu alisikiliza kimyakimya, huku wakishangazwa na “maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake” (mstari 22). Alipoanza kusema nao, akawaambia “leo andiko hili limetimia masikioni mwenu” (mstari 21). Huyu alikuwa Yesu wa Nazarethi akiwaambia kuwa ndiye aliyekuwa Masihi, nao wakasemezana wao kwa wao, “Huyu siye mwana wa Yusufu?” (mstari 22).
Jinsi gani walivyokosea! Yesu kwa hakika alikuwa mwana wa Mungu. Hata hivyo kwa hawa watu wa Nazarethi, Yesu alikuwa mwana wa seremela, aliyekulia mjini mwao pamoja nao na watoto wao. Akili zao zilikuwa zimefungwa wala hawakuweza kumwamini. Kama tu wangesikiliza kwa makini maneno yaliyotoka ndani ya chuo cha Isaya, wangefahamu kuwa Masihi alikuwa ni mtu wa aina gani, kwa maana alitumwa kwa watu masikini, waliovunjika moyo, watumwa, vipofu na waliumizwa. Hawa watu wa Nazarethi hata hawakutambua kwamba walimhitaji. Wakawa na mawazo ya hisia za nguvu kinyume naye, hata ikiwa kwamba na Yesu mwenyewe akashangazwa na kutoamini kwao (Marko 6:6).
HAKUNA NABII ANAYEKUBALIKA KATIKA NCHI YAKE MWENYEWE: Luka 4:23-27
Yesu alitambua kwamba walimtazamia kufanya “ishara na maajabu” hapa kama alivyofanya huko Kapernaumu. Na wala hawakumpokea. Hawakuonyesha imani yoyote. Kwa hiyo “hakufanya miujiza mingi huko kwa sababu ya kutokuamini kwao” (Mathayo 13:58).
“Hakuna Nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe”. Yesu aliendelea kuwaambia watu wa Nazarethi walipokuwa wamekaa pale na kumkazia macho ya chuki na hasira (mstari 24). Akawakumbusha juu ya Manabii wawili wakuu katika Agano la Kale, ambao waliwapatia msaada watu waaminifu waliokuwa watu wa Mataifa , kwa sababu watu wa Israeli hawakujali maneno ya Mungu (mstari 26 – 27).
- Kulikuwa na wajane wengi katika Israeli katika siku za nabii Eliya, wakati Mungu alipofunga mbingu mvua mvua isinyeshe kwa miaka mitatu na nusu, lakini Eliya hakutumwa kwa mtu yeyote kati yao. Lakini Mungu alimpeleka Sarepta, mji ulio nje ya mipaka ya nchi ya Israeli kwa mwanamke mjane kule, aliyemwamini Mungu wa Israeli. Wanawake wa Israel walikuwa wamegeukia katika kutomwabudu Yahwe, Mungu wa kweli, Hivyo Mungu akampeleka Eliya kwa mwanamke mpagani na akamsaidia nyakati zile za njaa (soma 1 Wafalme 17:1, 8 – 16).
- Na tena, kulikuwa na wakoma wengi katika Israeli nyakati za Nabii Elisha, lakini hata mmoja waohakutakaswa ukoma wao. Isipokuwa ni kamanda wa vita wa Shamu (Syria), Naamani, aliyeponywa (soma 2 Wafalme 5).
Fundisho hapa lilikuwa wazi. Eliya na Elisha walikuwa manabii wakuu, lakini waliwapata watu sana wachache katika Israeli walioaamini maneno yao. Lakini watu wawili walio wa mataifa walionyetha imani kubwa naye Mungu aliweza kuwasaidia.
FUNDISHO KWETU
Jinsi inavyosikitisha wakati watu wanapojiona wenyewe kuwa ni wenye haki. Wana uhakika kuwa wako sahihi kabisa na wala hawahitaji kusikiliza neno la Mungu. Sisi sote tunahitaji Mungu atusaidie, lakini ni lazima tunyenyekee kiasi cha kutosha ili tuweze kusikiliza.
Ni rahisi sana kufanya sawasawa na wale wayahudi wa Nazarethi, kwa kuziba masikio yetu tunapoonywa na kukemewa. Mara nyingine tunaziba masikio yetu wakati wazazi wetu wanapoonyesha pale tulipokosea. Wanajaribu kutufundisha njia zilizo sahihi nasi tusifanye kiburi kwa kutowa kusikiliza. Maana yote ni katika kutuandaa ili tuwe watoto watiifu wa Mungu. Mungu hatatenda kamwe maishani mwetu kutuongaza sisi iwapo tunakataa kusikiliza neno lake linaposemwa na wazazi wetu na walimu wetu pia.
MAELEZO YA NYONGEZA.
Yesu aliponukuu kutoka Isaya 61:1 – 2, tunaona kwamba aliacha kuendelea kusoma alipokuwa amesoma nusu ya kifungu cha maneno. Kwa nini alifanya hivyo? Ukisoma maneno yanayofuata katika Isaya utayakuta maneno yafuatayo “na siku ya kisasi cha Mungu wetu”. Siku ile ya kisasi, ni wakati Mungu atakapowaadhibu waovu, siku hiyo ilikuwa bado inakuja. Mtume Paulo anaisema siku ile kuwa wakati Mungu atakapowatuma malaika wake wenye nguvu “kuwalipa kisasi wote wasiomjua Mungu, nao wasiotii injili ya Bwana wetu Yesu Kristo” (2 Wathesalonike 1:8; soma mstari 7–10). Itakuwa siku ya kutisha kwao waovu, lakini ni siku ya furaha iliyoje kwa waongofu, waliompenda na kumtii Mungu. Isaya anasema siku hiyo ya furaha kwenye mstari wa 3, naye Paulo anaiandika katika warumi 2:7 na 10 “Wale ambao kwa saburi katika kutenda mema wanatafuta utukufu na heshima na kutokuharibika, na uzima wa milele (Mungu atawapatia siku ile) uzima wa milele… utukufu, heshima na amani, kwa kila mtu atendaye mema, kwanza myahudi na kwa mmataifa pia”
Hivyo Yesu aliposema katika sinagogi kule Nazarethi, hiyo “siku ile ya kisasi” ilikuwa bado mbali sana. Hapohapo Mungu alikuwa “amemtia mafuta” yeye ili afanye kazi ya kuwahubiria wale ambao wangesikiliza. Watu wa aina hiyo walipata msaada na baraka kutoka kwake wakati ule alipokuwa kati yao na hao hao watu watapokea uzima wa milele katika ufalme wake.
MASWALI.
Majibu Mafupi
- Yesu alipokuwemo ndani ya sinagogi huko Nazarethi, ni sehemu gani ya Biblia
aliyosoma?
- Alipokaa, aliwaambia nini watu?
- Je, walimfikiria yeye kuwa ni nani?
- Je, kwa uhakika yeye alikuwa nani?
- Ni kwa nini hakufanya miujiza mingi huko Nazarethi?
- Manabii wakuu wawili ni nani ambao Yesu aliowataja ili kuwambusha waisraeli?
- Kwa nini Mungu aliwatuma Manabii hawa kuwasaidia watu wa mataifa?
- Ni kwa nini watu wa Nazaraethi walikasirika sana wakati Yesu alipowaambia habari
hizi?
- Ni nini watu wa Nazarethi walijaribu kumfanyia Yesu?
- Kwa nini tunaziba masikio yetu wakati fulani tunapolaumiwa?
Majibu ya Kina:
- Eliza kilichotokea ndani ya sinagogi huko Nazarethi wakati Yesu aliposimama ili
kusoma.
- Yesu aliwaeleza watu katika sinagogi kule Nazarethi kwamba “hakuna Nabii
anayekubalika katika nchi yake mwenyewe”
- Ni historia zipi mbili alizowaambia kuonyesha alilomaanisha?
- Kwa nini hili lilisababisha kukasirika?
- Alipomaliza kusema, je wayahudi walifanya nini?
Majibu ya Nyongeza
- Ni maneno gani yaliyofuata katika Isaya 61:2 ambayo Yesu hakuyanukuu?
- Ni wakati gani maneno haya yatatimia lini?