87. MCHANA NA USIKU WA MIUJIZA: AKIWALISHA MAKUTANO
“Mimi ndimi chakula cha uzima; yeyote ajaye kwangu hataona njaa kamwe”
Shabaha
Kuonyesha jinsi Yesu alivyowalisha watu elfu tano na akatembea juu ya maji.
Yesu alikuwa ameshahubiri kwa miaka miwili. Miji ya Israeli ilikuwa imekwisha sikia injili ya ufalme na kuona nguvu za Mungu alipokuwa akizunguka kati yao.Na kusini mwa Yudea, yule mtu mwovu, Herode, alikuwa amemtupa Yohana gerezani. Wakati wa sherehe ya kuheshimu siku ya kuzaliwa kwake Herode alikubali Yohana akatwe kichwa. Wanafunzi wa Yohana walipokuwa wamemzika mwalimu wao waliyempenda, wakaenda na kumpasha habari Yesu. Akiwa mwenye kuhuzunishwa sana na kifo cha kikatili cha nabii huyu mwaminifu, Yesu na wanafunzi wake wakaondoka kwa mashua kwenda mahali pa faragha, ili wawe peke yao.
Yohana 6:1 – 21 Tazama pia Marko: 30 – 52; Mathayo 14:13 – 21; Luka 9:10 – 17.
WATU WANAMFUATA YESU
Yesu aliwachukuwa wanafunzi wake kuvuka ziwa la Galilaya hadi mahali pa faragha upande unao elekeana na Kapernaumu. Hata hivyo hawakuachwa wawe na amani, kwa kuwa watu wengii walikuwa wamewaona wakati wanaondoka. Taarifa ilipelekwa sehemu zote ya kuwa Yesu ameondoka, na maelfu wakakimbia kutoka miji yote ya jirani hadi wakaenda sehemu Yesu aliyokuwa na wanafunzi wake ambao walikuwa wamekaa kando ya mlima. Habari za miujiza yake zilikuwa zimeenea nao watu walikuja kuponywa. Ingawaje alijaa huzuni kwa ajili ya kifo cha Yohana, Yesu alipowaona watu hawa wote wakihitaji msaada wake, moyo wake uliwahurumia, “Kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji” (Marko 6:34). Kwa hiyo alitumia siku nzima kuhubiri habari njema za ufalme wa Mungu na kuwaponya magonjwa yao yote.
MUUJIZA WA MIKATE NA SAMAKI
Kadri siku ilivyoendelea wanafunzi wake walikuwa na wasiwasi, kwani hapo palikuwa ni jangwa na watu walianza kuona njaa. Kwa hiyo wakamshauri Yesu kwamba awaruhusu watu waende zao kununua chakula (Marko 6:36). Yesu akawageukia wanafunzi wake akawaambia, wapeni ninyi chakula (mstari 37). Walishangaa. Ni wapi wangepata hata fedha za kutosha kwenda kununua chakula kuulisha mkusanyiko mkubwa jinsi ile? Yesu akamwuliza Filipo, Twaweza kununua wapi mikate, ili watu hawa waweze kula? (Yohana 6:)
Wakati huo Yesu alikuwa anaelewa ni nini angefanya, lakini alitaka kupima imani ya wanafunzi wake. Yote ambayo Filipo aliweza kusema ni kwamba wangehitaji zaidi ya kiasi cha mikate ya thamani ya fedha zipatazo mia mbili kuwapa watu hawa wote kiasi kidogo tu cha kula. Ingemchukuwa mtu miezi mingi ya utumishi kuzipata fedha nyingi jinsi ile.
Yesu akawatuma kupepeleza kama yupo yeyote ndani ya kusanyiko hilo ambaye alikuwa ameleta chakula chochote. Andrea akampata kijana mdogo akiwa na mikate mitano ya shayiri na samaki wawili. Hiyo ndiyo yote iliyopatikana. “Lakini hiki ni nini mbele ya umati huu mkubwa wa watu?” Andrea akasema (mstari 9).Yesu akasema; Nileteeni hapa (Mathayo 14:18).
Ndipo akawaambia wanafunzi wake kuwakalisha chini watu kwenye manyasi katika vikundi vya mia na hamsini. Wakati watu wakingojea kuona litakalotokea, Yesu alichukua mikate na akatazama mbinguni akamshukuru Mungu. Kisha akamega mkate na kuendelea kumega na kuwapatia wanafunzi wake kugawa kwa watu. Akawagawa samaki kwa njia hiyohiyo, mpaka kukawa na cha kutosha kuwalisha watu wale wote elfu tano.
Filipo alijua ni kiasi gani kingaliwagharimuulisha umati huo walau kipande kidogo kiasi tu chakule cha kula, lakini Yesu aliwalisha mpaka wote wakashiba (Luka 9:17).
KISIPOTEE KIPANDE CHOCHOTE CHA MKATE.
Baada ya mlo kumalizika kulikuwa bado na chakula kilichobaki. Yesu akawaambia wanafunzi wake “kukusanya vipande vilivyobaki, ili kisipotee chochote” (Yohana 6:12). Na kwa hivyo wakachukua vikapu kila mmoja wao na kuvijaza na chakula chote kilichobakia kutokana na mikate mitano ya shayiri – wakajaza vikapu kumi na mbili. Wakawa na chakula zaidi kuliko walipoanza.
Hivyo nguvu za Mungu zilionekana kwa njia ya ajabu. Mchana kutwa Yesu alikuwa amewalisha na chakula cha kiroho, Neno la Mungu, na sasa alikuwa amewapatia chakula kumaliza njaa yao.
Hivi ndivyo hasa Yesu alivyowafundisha wanafunzi wake kule mlimani (tazama somo la 10 – Mungu anajua tunahitaji nini) “utafuteni kwanza ufalme wa Mungu, na haki yake; na vitu hivi vingine (chakula chetu cha kila siku n.k.) mtaongezewa” (Mathayo 6:33).
WATU WANATAKA KUMFANYA YESU AWE MFALME.
Watu walipatwa na mshangao. Kwa kweli kwa mwujiza huu. Uliwafanya wakumbuke maneno ya Mungu kwa Musa katika Kumbukumbu la Torati 18:18 – 19 ambapo Mungu aliahidi kwamba siku moja angewapelekea watu nabii aliye kama Musa. Atanena kwa jina langu. Mungu akasema, “... Nitatia maneno yangu kinywani mwake”. Kwa hiyo watu wakafikiri juu ya yote waliyoyaona na kuyasikia siku ile nao wakaamua kwamba Yesu ni lazima ndiye yule nabii ambaye Mungu alimuahidia. Wakaanza kuwa na mshangao wenye furaha, lakini mara Yesu alipoelewa kuwa walitaka kumfanya mfalme wao, kuanzia siku ile na palepale akawaamuru wanafunzi wake kuingia chomboni wakaondoka. Ni kweli alikuwa ndiye “nabii yule” na alikuwa amepakwa mafuta na Mungu wakati wa ubatizo wake, lakini haukuwa muda wake bado kwake kuwa mfalme wao. Hivyo akawaruhusu makutano waende majumbani kwao, ambapo yeye mwenyewe akaenda peke yake mlimani kumwomba Baba yake.
YESU ANATEMBEA JUU YA BAHARI
Wakati Yesu akiwa mlimani kusali kwa Baba yake wanafunzi wake walikuwa katika mashua yao ziwani wakipiga makasia kwa nguvu wakishindana na upepo mkali sana. Dhoruba ilikuwa imeumuka katika ziwa la Galilaya na mashua yao ilikuwa ikirushwa kwa mawimbi. Hata kwa juhudi kubwa vipi ya kupiga makasia hawakuelekea kuwa karibu na ufukwe zaidi, wakakazana kwa masaa mengi bila kupata mafanikio hata kidogo.
Katika saa za alfajiri na mapema, kuelekea saa 9 na saa 12 alfajiri “Hiyo inaitwa ni zamu ya nne, Yesu akawaona. akawaendea, akitembea juu ya bahari. Wanafunzi wake walipotazama, wakamwona akiwajia akitembea juu ya mawimbi, wakashikwa na mshangao sana. Wakiwa na hofu kubwa, sauti wakapaza, mzuka” (Mathayo 14:27). Akitambua jinsi walivyofadhaika, kwa haraka Yesu akawambia “changamkeni; ni mimi; msiogope” (mstari 27). Jinsi walivyofurahi kuisikia sauti ya Bwana wao.
Petro alikuwa wa kwanza kusema. “Bwana ikiwa ndiwe wewe, niruhusu nije kwako juu ya maji” (mstari 28). Yesu akasema, “Njoo”.
Hivyo Petro akaruka kutoka kwenye mashua na kukanyaga bahari iliyokuwa imechafuka, kwenda alipokuwapo Yesu! Watu wawili kwa hakika walitembea juu ya maji. Kisha Petro ghafla akatambua upepo mkali uliokuwa ukivuma kumzunguka, akili yake ilikuwa imelenga kwa Yesu mara alipotoka kwenye mashua, naye alikuwa amesahau dhoruba. Sasa ujasiri wake ukamtoka, kwani imani yake iliyumba na hofu ikaingia ndani yake akaanza kuzama akalia, “Bwana niokoe” (mstari 30). Mara moja Yesu akanyoosha mkono wake na kumdaka. Yesu alimwambia Petro, “Ewe mwenye imani haba, kwa nini ulitia shaka?”. Wakati wanafunzi wengine wakiangalia mara upepo ukatulia kuvuma kabisa nao mara moja wakafika Kapernaumu (Yohana 6:21). Sasa Yesu alikuwa pamoja nao, matatizo yao yote yakapotea. Kwa masaa mengi walikuwa wameshindana kwa juhudi dhidi ya upepo mkali, bila mafanikio yoyote. Ndipo Yesu alipotokea na upepo mara moja ukatulia na mashua yao ikafika salama badarini.
Si ajabu walishangazwa. Wakasema, “Hakika wewe ndiye mwana wa Mungu”. Kwa mambo yaliyotokea usiku ule, hawakubakia tena na shaka akilini mwao.
FUNDISHO KWETU
Kuna masomo mengi kiasi gani katika matukio ya siku ile na usiku ule. Yesu alihubiri na kuponya. Aliwapatia chakula waume elfu tano na wake zao na watoto wao kwa mwujiza wa ajabu. Kwa mwujiza pia alitembea juu ya maji na kutuliza dhoruba. Akiwa Mwana wa Mungu, akitumia nguvu za Mungu, aliweza kutenda haya yote siku ile, akimsaidia kila mmoja kwa kadiri walivyomhitaji. Wote aliowasaidia walimwamini. Kama tukiamini, Mungu atatulisha pia, yote mawili chakula cha mwili na kile cha kiroho kwa njia ya Neno lake. Kama tunakula chakula hiki tutaishi milele.
Petro aliamini naye akaweza kutembea juu ya maji. Alipotazama mbali kutoka kwa Kristo, imani yake ilimtoka naye akaanza kuzama. Inatufunza kuweka imani yetu kwa Mungu kila wakati, si kitu matatizo yetu ni makubwa kiasi gani.
MAELEZO YA ZIADA
Tunaendelea kufundishwa kupitia habbari hizi za maisha ya Yesu,mafundisho ya kiroho ya kutusaidia maishani mwetu kututayarisha kwa ujilio wa Bwana Yesu kutoka mbinguni.
Wakati kusanyiko lilipokuwa limelishwa na kushiba, wanafunzi walikuwa wameelekezwa kukusanya mikate iliyosazwa “ili kwamba kisipotee chochote” (Yohana 6:12). Kila mmoja wa wale wanafunzi kumi na mbili alipata kikapu kimoja kilichojaa mikate. Mikate ile ingalitumiwa kulisha watu wengine. Tunapokumbuka kwamba mikate huwakilisha Neno la Mungu, tunaweza kuona kwamba Yesu alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake kuwa imewapasa kulihubiri Neno kwa watu wengine pia. Neno la injili kwanza lilihubiriwa kwa wana wa Israeli (likiwakilishwa na orodha ya kumi na mbili makabila kumi na mawili, mitume kumi na wawili, vikapu kumi na viwili) na halafu kwa mataifa wasio kuwa wana wa Israeli.
Katika Yohana 6, tunaambiwa kwamba wale watu ambao Yesu aliwalisha mikate na samaki walirejea moja kwa moja kumtafuta. Alijaribu kuwafundisha masomo ya kiroho kutokana na mwujiza huo.
Yesu akasema, “Mimi ndimi chakula cha uzima, yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa” (mstari 35). “Mtu akila chakula hiki, ataishi milele (mstari 51) na chakula nitakachotoa ni mwili wangu” (mst 51).
Tunapoyaangalia maisha yake na kuwazia yale aliyoyasema na kuyatenda tunakula mwili wake. Tukimfuata kwa njia hii na kumuiga mfano wake, Mungu atatupatia uzima wa milele tutaishi milele. katika ufalme wake. Kwa kuwa yeye alikuwa mtii kwa ukamilifu kwa Babaye katika mawazo yake yote na maneno na matendo.
Watu waliweza kuona waziwazi ndani ya Yesu Neno la Mungu lenyewe hasa kila amri ya Mungu aliyoiandika katika Neno lake Yesu alitii. Kitu cha mwisho cha ajabu alichokifanya kutii Neno la Babaye, kilikuwa kuwaruhusu watu waovu kumwua msalabani bila kulalamika, bila kutisha,na bila kukasirika (1Petro 2;21 – 24) Kwa hiyo Yesu alikubali kwa hiari kufa msalabani. Wote wamwaminio na kubatizwa, wanakumbuka hili wanapokula mkate pamoja wakati wa mkutano wa ukumbusho kila juma.
MASWALI
Majibu Mafupi
- Yesu alikwenda wapi aliposikia kuhusu kifo cha Yohana mbatizaji
- Kwa nini Yesu alijisikia kuwasikitikia makutano waliomfuata?
- Kwa nini wanafunzi walitaka watu waruhusiwe kwenda zao?
- Kuna yeyote katika mkusanyiko aliyekuwa na chakula chochote? Kilikuwa ni kiasi
gani?
- Yesu alifanya nini kabla hajaumega mkate?
- Ni watu wangapi Yesu aliowalisha siku ile?
- Ni kiasi gani cha chakula kilibakia?
- Watu walipouona muujiza walitaka kumfanyia nini Yesu?
- Katika zamu ya nne Yesu aliwaona wanafunzi wake wakipiga makasia dhidi ya upepo
ziwani. Alifanya nini?
- Ni mwanafunzi yupi aliondoka ndani ya mashua kwenda kwa Yesu?
- Kwa nini Petro alianza kuzama?
- Ni chakula gani Mungu hutupatia sisi?
Majibu ya Kina
- Yesu aliposikia habari za kifo cha Yohana mbatizaji aliondoka kimyakimya pamoja na
wanafunzi wake. Eleza yaliyotokea siku ile
- Watu walitaka kumfanya Yesu kuwa mfalme.
(a) Alifanya nini alipotambua hilo?
(b) Aliwatuma wanafunzi wake wapi?
(c) Nini kilitokea usiku ule?
Majibu ya Nyongeza
- Mungu hutupatia mkate wa asili na wa kiroho
- Ni mkate gani wa kiroho Mungu hutupatia?
- Yesu alimaanisha nini aliposema “Mimi ni chakula cha uzima?”
- Je, mkate unaoliwa wakati wa kukumbuka meza ya Bwana hutukumbusha juu ya
nini?