104. ANANIA NA SAFIRA
“Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu”
Shabaha
Kuonyesha kwamba Mungu anajua mambo yote yaliyo ndani ya mioyo yetu, na hivyo hatuwezi kumdanganya kamwe.
EKLESIA KATIKA YERUSALEMU (2:41-42)
Tumekwisha jifunza kwamba kazi ambayo Bwana Yesu Kristo aliwapa Petro na mitume wengine ilikuwa ni kuhubiri Injiri. Kazi yao ilianzia Yerusalemu wakati watu Elfu tatu walipobatizwa siku ya Pentekoste. Hawa walikutana mara kwa mara kujifunza kutoka kwa mitume, na kumega mkate, kama jinsi ndugu (wanaume na wanawake) wanavyofanya siku hizi. Waliitwa “eklesi” ya Mungu. Neno la Kigiriki likiwa na maana ya “kusanyiko (au mkutano) la watu walioitwa kutoka nje”. Mtu yeyote aaminiye na kubatizwa katika Kristo ni kweli ametii wito wa Mungu wa kumtumikia Mungu. Mtu wa aina hii ambaye anakuwa amejitenga na uovu wa dunia na kujiunga na familia ya Mungu au eklesia.
EKLESIA INAONGEZEKA KILA SIKU (4:31-37)
Ndugu, wanaume na wanawake walifurahi sana kwa kuwa Mungu amewasamehe dhambi zao na kuwapa matumaini ya uzima wa milele hivyo upendo kati yao uliongezeka.Waliuza mali zao kwa furaha na kwa pamoja waka washirikisha mali zao ndugu waliokuwa maskini ambao ni wanaume na wanawake. Kama ndugu yeyote alikuwa na ardhi au nyumba aliuza na kile ambacho hakikuwa muhimu sana kwake na kwa hiyari yake akaleta fedha kwa Mitume kwa ajili ya kazi ya kuihubiri Kweli.Kulikuwa na familia ya kweli waliopendana.
DHAMBI YA ANANIA NA SAFIRA (5:1-2)
Lakini siyo kila mtu aliyepeleka sadaka kuwa alikuwa na moyo wa uaminifu. Kulikuwa na ndugu na mkewe walioitwa Anania na Safira ambao waliuza mali zao. Walikuwa wameona ndugu wengi wanaume na wanawake ambao waliuza mali zao na kuwapaia fedha MitumeHakuna shaka kuwa walipewa shukrani na kusifiwa kwa ajili ya wema wao.Anania na Safira walipenda na wao ndugu zao wawashukuru pia. Lakini hawakutaka kutoa fedha yote ya mauzo ya mali yao. Kwa hiyo waliamua kuficha kiasi cha fedha na kuwapa Mitume fedha iliyobaki. Baya zaidi ni kwamba walitaka Mitume waamini kwamba kiasi walichotoa kuwa kilikuwa ni kiasi cha fedha yote waliyopata. Huu haukuwa uaminifu. Wangeweza kumdanganya mwanadamu, lakini wasingeweza kamwe kumdanganya Mungu. Ni dhambi ya aina gani, na upumbavu waliokuwanao. Huu ni uovu ulioje na ni jinsi gani walivyokuwa wapumbavu. Hakuna hata mtu mmoja aliyewaomba wao watoe fedha zao. Wangeweza kuzitunza fedha zao zote. Lakini walipenda kusifiwa na wanadamu.
ANANIA NA SAFIRA WANAADHIBIWA (mstari 3-11)
Kwa majivuno Anania alikwenda katika nyumba ambamo Petro na Mitume walikuwa wamekusanyika pamoja. Hapo akatoa zawadi yake. Kwa kweli hakuna hata mtu mmoja ambaye angejua ni jinsi gani alivyokuwa mchoyo hakika. Hata hivyo Petro alifahamu. Hakuweza kudanganywa. Mungu alimwezesha kwa nguvu za Roho Mtakatifu kuona mawazo yote yaliyojificha katika moyo wa mwanadamu kwa hiyo Petro alijua kuwa Anania alikuwa anadanganya. Petro alimwambia “Hukumwambia uongo mwanadamu bali Mungu,” Anania badala ya kusifiwa alipata aibu, na bila shaka aliogopa wakati Petro alipofichua yalikuwa moyoni mwake. Alikuwa na sababu nzuri ya kuogopa kwa busara Petro, kwa hekima yake, aliweza kuona kwamba eklesia ni lazima ijifunze kutokana na somo hilo. Ghafla Anania alianguka chini akafa. Mungu alimwadhibu mara moja na vijana wakamchukua nje kwenda kumzika. Hata muda wa saa tatu baadaye Safira naye akaingia akiwa hana habari ya mambo yaliyompata mme wake. Petro akamwuliza “Niambie mlikiuza kiwanja kwa kiasi hiki?” Safira akajibu ndiyo kwa kiasi hicho.Kama Anania, Safira na kwa makusudi alisema uongo. Adhabu yake ilikuwa sawa kama Anania alivyoadhibiwa. Petro kwa ukali alisema, Safira pia alianguka chini na kufa akapelekwa nje wakamzika karibu na alipozikwa mme wake. Ni jambo la kutisha namna gani kutokea ndani ya eklesia siku ya Bwana walikuwa wenye furaha walipobatizwa na dhambi zao zilikuwa zimesamehewa. Walikuwa na mshangao mkubwa wa furaha kwa kuona nguvu za Mungu zikiponya, lakini sasa nguvu zake kubwa zilitumika kuua.
FUNDISHO KWETU:
“Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu” (2 Kor.9:7), lakini “Huchukizwa na mwongo” (Mithali 12:22). Anania na Safira walijaribu kudanganya kwa sababu walitaka sifa. Hawakumpendeza Mungu hata kidogo. Kama kweli tunampenda Mungu itaonekana katika ukweli wa maneno na matendo, na kwa wema wa kweli na upendo kwa ndugu waamini wanaume na wanawake na watoto wao.
MAELEZO YA NYONGEZA
Wakati Petro alipomkemea alisema “Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako?” katika Yeremia 17:9 tunaambiwa “moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, na una ugonjwa wa kufisha”. Yesu aliwaambia Wayahudi wengi waliosikiliza “Watu hawa wananiheshimu kwa midomo yao, lakini mioyo yao iko mbali nami” (Mathayo 15:8). Walikuwa wanafiki. Kama Anania na Safira walijifanya kutenda mema lakini mioyo yao ilikuwa ya uovu. Mungu alisema “Mpende BWANA Mungu wako kwa moyo wako”. (Mathayo 22:37). Tunapaswa kuwa waangalifu kiasi gani na kuwa na moyo mweupe na moyo wa uaminifu, kwa kuwa Mungu huangalia Moyo.
MASWALI
Majibu Mafupi:
1. Neno “eklesia” lina maana gani?
2. Je, ndugu wanaume na wanawake walionyesha upendo jinsi gani kwa wenzao?
3. Anania na Safira walipeleka nini kwa Mitume?
4. Je, Petro alijuaje kuwa walikuwa wanadanganya?
5. Kulitokea nini kwa Anania na Safira?
6. Kwa nini ilikuwa ni lazima Anania na Sarafina wafe?
7. Ni fundisho gani muhimu tunalojifunza katika habari ya Anania na Safira?
Majibu ya Kina:
8. Anania na Safira walifikiri kuwa wangeweza kumdanganya Mungu
(a) Anania na Safira walifanya kitu gani ambacho ni kibaya?
(b) Eleza jinsi Anania na Safira walivyo adhibiwa.
(c) Mungu hapendi tuwe kama Anania na Safira, je ni mfano gani mzuri ambao yatupasa
tuuonyeshe?
Majibu ya Nyongeza
9. Anania na Safira walikuwa wanafiki:
(a) Hii ina maana gani?
(b) Ni jinsi gani tunavyoweza kuwa tofauti?