105. STEFANO – MWAMINIFU HADI KUFA
“Tazama!, naona Mbingu zimefunguka na Mwana wa Adamu amesimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu”
Shabaha
Kumwonyesha jinsi Stefano alivyokuwa amejiandaa kupoteza uhai wake kwa ajili ya kuhubiri wokovu kwa watu. Stefano alikuwa amejaa Imani na nguvu alifanya maajabu na miujiza katika watu. Bwana aliwaonya wanafunzi wake kwamba watu wanapenda kusikia Injili ”Nanyi mtakuwa wenye kuchukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu”. Yesu alisema. “Lakini mwenye kuvumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokoka” (Mathayo10:22). Ingawaje wangeteseka, waliahidiwa thawabu ya uzima wa milele, ikiwa watamtumikia Mungu kwa uaminifu mpaka Mwisho (Matendo ya mitume 6 na 7).
NDUGU SABA WANACHAGULIWA (6:16)
Tangu siku ya Pentekoste Mitume waliendelea kuhubiri Injiri kwa Wayahudi katika Yerusalemu. Watawala wa Kiyahudi bado waliendelea kuwakataza kufundisha katika jina la Yesu. Lakini kazi iliendelea na Mungu aliibariki, na kwa hiyo eklesia ilizidi kuongeza na kuendelea kuongezeka. Iliendelea kuwa vigumu sana kwa mitume kuendelea kuhubiri na kuhudumia mahitaji ya kundi la wanawake kwa wakati mmoja. Hivyo Mitume walisema “Haitupasi sisi kuliacha Neno la Mungu, na kuhudumia meza (yaani kuwapatia chakula na pesa maskini)”. Wakaagiza kwamba ndugu saba wenye hekima na waliokuwa wameshuhudiwa kutenda mema wachaguliwe kushughulikia mahitaji ya kila siku ya kusanyiko. Mitume waliweka mikono juu yao na baada ya kuwaombea ili kwamba hao saba wabarikiwe na kupewa nguvu na wafanya kazi ambazo hao saba walitakiwa kufanya, miongoni mwao alikuwa ni Stefano.
STEFANO ANAHUBIRI INJILI (Mstari 8-10)
Tunaambiwa kwamba Stefano alikuwa “akijaa neema na uwezo” ambaye, “alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa kati ya watu”. Ni dhahiri kuwa alitumia kila nafasi aliyoipata kuhubiri Injiri kwa Wayahudi. Hawakujizuia kumsikiliza. Miujiza aliyoifanya kwa nguvu za Roho Mtakatifu iliwafanya wasiwe na mashaka kuhusu yale aliyosema kwamba ni kwa nguvu za Mungu. Lakini bado wengi hasa wale wakuu wa Wayahudi, walikuwa wakaidi na hawakuweza kuamini kwamba Yesu wa Nazareti alikuwa Masihi. Hawakuweza kupata jibu kwa maneno ya Stefano na matendo yake na walikataa kuamini. Na kwahiyo walifanya sawa sawa kama yale wakuu wa Wayahudi walivyomtendea Yesu. Waliwapata watu waovu waliokubali kusema uongo dhidi ya Stefano.
STEFANO ANATIWA HATIANI (mstari 11-15)
Watu hawa wabaya wakasema “Tumemsikia mtu huyu akinena maneno ya kumtukana Musa na Mungu” (mstari 11). Maneno yao hayakuwa ya kweli, lakini watu na wakuu wa Wayahudi walipatwa na mshangao na wakampeleka Stefano kwenye baraza, ambalo lilitwa Sanhedrini. Mashahidi wa uongo waliongeza zaidi kwa yale maneno yaliyokuwa yamesemwa. Maana “Tumemsikia akisema kwamba Yesu huyu Mnazareti atapaharibu mahali hapa; na kuzibadili desturi tulizopewa na Musa” (mstari 14). Stefano alipopewa nafasi ya kujibu maneno ya uongo yaliyotolewa na mashahidi dhidi yake, jambo la kushangaza lilitokea wale wote waliomtazama “walimwona uso wake kuwa kama uso wa Malaika”. Mungu alikuwa pamoja naye kumsaidia kusema mbele ya baraza la Wayahudi.
STEFANO ANAJITETEA MBELE YA SANHEDRIN (mstari 7:1-53)
Hatimaye Mkuu wa baraza, kuhani Mkuu aliuliza; Je, mambo haya ndivyo yalivyo? Hadi mwisho, Mkuu wa baraza Mchungaji Mkuu akasema. Stefano akajibu, “Ndugu zangu na baba zangu, sikilizeni” (sikilizeni kwa makini). Aliwakumbusha mambo mengi yaliyokuwa yamewatokea wana wa Israeli wakati uliopita. Akazungumza kuhusu Ibrahimu, Isaka na Yakobo ambao Mungu aliwaahidi Nchi ya Israeli. Aliwakumbusha habari za Musa na wana wa Israeli ambao walimwabudu Mungu jangwani miaka mingi sana kabla ya kujengwa kwa Hekalu. Na sasa Stefano alijua kwamba Mungu ataliteketeza Hekalu lile lililojengwa na Herode na watu wote waliokuwa wanalitumainia. Yeye alitaka watu hawa wajue kuwa Hekalu si kitu chochote isipokuwa jengo tu lililojengwa kwa mawe walimwabudu Mungu hata kabla ya kujengwa kwa Hekalu. Stefano alisema “Ila yeye aliye juu hakai katika nyumba zilizofanywa kwa mikono” (mstari 48). Alikuwa akinukuu katika maandiko ya manabii. Kwa wakati huo Stefano alifahamu kuwa watu hawatilii maanani maneno yake. Kama walivyofanya baba zao vile vile ambao hawakujali maonyo ya manabii na badala yake wakawaua, na watu hawa wakamwua Mwana wa Mungu. Akasema “Kama baba zenu walivyofanya, na ninyi vivyo hivyo” (mstari 51)
STEFANO ANAUAWA (Mstari 55-50)
Sanhedrini walikasirika sana waliposikia maneno ya Stefano. Walikasirika sana hata wakamsagia meno wote kwa pamoja. Lakini Stefano akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake akatazama Mbinguni akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama mkono wa kuume wa Mungu. Stefano akasema, “Tazama! Ninaona Mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu”. Mungu alipendezwa na Stefano, kwa maana aliwaambia ukweli hata watu waliokuwa wanamchukia. Kwa hiyo Mungu alimwonyesha Stefano, Bwana Yesu Kristo akiwa amesimama mkono wa kuume wa Mungu ambao ni upande wa nguvu. Wakati Sanhedrini waliposikia maneno ya Stefano wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia wakamkamata wakamtoa nje ya mji. Wakamvua nguo zake wakaziweka miguuni pa kijana (ambaye jina lake aliitwa Sauli) na kisha wakaokota mawe na kumpiga mawe Stefano.Hakuyajali hayo waliyomtendea akawaombea kwa Mungu, kama vile Bwana alivyofanya kwa hiari akiwasamehe walio msulubisha, na ndivyo hata alivyofanya Stefano mwenye imani alimwomba Mungu awasamehe watu hawa waovu. Wakati mawe yakimpiga Stefano alipiga magoti. Akalia kwa Sauti kuu, “Bwana usiwahesabie dhambi hii”, Na akiisha kusema hayo Stefano akafa.
FUNDISHO KWETU
Hatutaweza kuulizwa kufa kwa ajili ya Kweli, kama Stefano alivyofanya,lakini ni lazima tumpende Mungu sana kadri tuwezavyo kama vile alivyofanya. Jinsi alivyokuwa mtumishi mnyenyekevu wa Mungu akawaombea maadui zake ingawaje walimchukia sana na hata wakamwua kwa mawe. Hili ni fundisho alilolipata kwa Bwana Yesu na kwa hiyo na sisi tunapaswa kujifunza kuwapenda maadui zetu na kuwafanyia mema wale wote wanao tuchukia sisi. Kama kweli tunampenda Mungu hakika tutaweza kufanya hayo.
MAELEZO YA NYONGEZA
Katika majibu yake, Stefano aliwaambia Wayahudi mifano mingi ya historia yao. Alipenda kuwaonyesha hasa mambo mawili ambayo yangejibu mashtaka yao ya uongo dhidi yake. Mungu anakuwa pamoja na watu kila mara wanapomwabudu Mungu “katika roho na kweli”. Mungu alimtokea Ibrahimu – katika Uru, Mungu aka mbariki Yusufu – katika Misri; Mungu alimbariki Musa – katika Misri na katika Midiani. Lakini wana wa Israeli hawakupewa nchi ya ahadi. Kote huko hakika hapakuwa na Hekalu katika Yerusalemu katika siku hizo. Lakini watu hawa wenye imani wa zamani walimwabudu na kumtii Mungu kila mahali walipokwenda. kwa hiyo Wayahudi walipaswa kuwa na uhakika kwamba Mungu ataangamiza Hekalu na kuwafukuza katika nchi ile. Watu hawa waaminifu wa zamani ambao Stefano aliwataja kuwa walimwabudu Mungu hata kabla Musa hajapewa sheria katika mlima Sinai. Kwa hiyo Wayahudi hawakupaswa kujivunia sheria za Musa. Kwa kweli, hakuna hata mmoja aliyeishika sheria yote kama ilivyotakiwa katika maisha yao. Ni Bwana Yesu Kristo ambaye alitii sheria kikamilifu. Na baada ya kifo chake watu hawakupaswa kuzingatia tena sheria ya Musa. Mara tu Mungu alipo mfufua katika wafu watu wote wanatakiwa kumwamini yeye na kubatizwa. Na hivi ndivyo tunavyoweza kumpendeza Mungu. Hivi ndivyo Stefano alivyojaribu kuwaambia, lakini walizifanya “Shingo ngumu” na kuwa miaka michache baadaye Mungu aliwaadhibu. Wakati majeshi ya warumi walipoingia Yerusalemu mwaka 70BK (baada ya Kristo) walijifungia ndani ya Hekaru wakifikiri kuwa watakuwa salama. Hekalu la Herode liliteketezwa na kubomolewa mpaka chini na watu waliokuwamo ndani waliangamia.
MASWALI:
Majibu Mafupi.
1. Mitume walikuwa na kazi kubwa ya kuhubiri Injiri Jee ni kazi ipi nyingine waliyoifanya?
2. Je, ni ndugu wangapi waliochaguliwa kuwasaidia Mitume?
3. Stefano alikuwa mtu wa aina gani?
4. Wayahudi walikosa majibu ya kujibu maneno ya Stefano. Jee walitumia mbinu gani
kumnasa?
5. Je, watu wabaya walisema nini mwanzo dhidi ya Stefano?
6. Sura ya Stefano ilikuwa na mwonekano gani alipozungumza katika baraza?
7. Wayahudi walimfanya nini Stefano?
8. Maneno ya mwisho ya Stefano yalikuwa yapi?
Majibu ya Kina
9. Kwa kadiri eklesia ilivyokua Mitume walikuwa na kazi sana
(a) Nini kilichowafanya kuwa na kazi sana?
(b) Ni jinsi gani walivyopata msaada?
10. Eleza nini kilitokea baada ya Stefano kumaliza kusema?
11. Ni jinsi gani Stefano alivyo kielelezo cha muhimu kwetu?
Majibu ya Ziada.
12. (a) Manabii walisema nini kuhusu Mungu anapoishi?
(b) Je watu waaminifu wa zamani walimwabudu Mungu sehemu gani? Eleza baadhi ya
mifano.
13. (a) Je, kila mmoja alitii sheria za Musa kwa ukamilifu?
(b) Je, tunawezaje kumfurahisha Mungu siku hizi?
14. (a) Ni tendo gani la kutisha ambalo Wayahudi walifanya ambalo Mungu aliwaadhibu
kwa ajili ya jambo hilo?
(b) Je, Mungu aliwaadhibu namna gani?