108. KUFUFULIWA KWA TABITA
Petro alipiga magoti na kusali, alijigeuza juu ya mwili na kusema Tabitha, inuka.
Shabaha
Kuonyesha jinsi Petro alivyoweza kuwaponya Ainea na Thabita kwa nguvu za Roho Mtakatifu. Kufuatilia kuongoka kwa Sauli alitumia miaka mitatu Uarabuni na Dameski kabla ya kwenda Yerusalemu (Gal. 1:15-24). Alikaa Yerusalemu kwa muda mfupi akiwa na mitume wengine na kasha alikwenda katika mji wa ke Tarso, ambapo alitumia muda wake mwingi akihubiri Injili ambayo hapo mwanzo aliipinga. Na ikawa sasa Sauli, ambaye alikuwa adui yao mkubwa, akaamini mabo yale yale kama wengine ndugu wanaume na wanawake wakawa na amani katika Yudea (Matendo ya Mitume 9:31).
Matendo ya mitume 9:31-43.
PETRO ANAWATEMBELEA WAAMINI (mstari 32-35)
Kusanyiko la Bwana lilikuwa linaongezeka haraka sana. Siyo tu kwamba kusanyiko la Bwana katika Yerusalemu lilikuwa kubwa lakini pia zilianzishwa eklesia ndogo sehemu nyingine za nchi. Ilikuwa sasa ni muhimu kwa mitume kutembelea eklesia mpya na kuwaimarisha watakatifu, kama jinsi ambavyo ndugu wanaume na wanawake walivyoitwa. Wanaitwa watakatifu kwa sababu ni watakatifu nbele ya macho ya Mungu. Wametengwa na dunia kwa ajili ya kufanya mapenzi ya Mungu (Angalia somo la 2 - “Roho Mtakatifu ni nini?”). Tumesoma kwamba Petro “akawatelemkia watakatifu waliokaa Lida”. Lida ilikuwa njiani kutoka Yerusalemu kwenda Yafa Huko Petro alimkuta mtu jina lake Ainea ambaye alikuwa kitandani kwa miaka minane kwa sababu alipooza. Petro akamwambia “Ainea Yesu Kristo akuponya ondoka ujitandikie”. Mara moja Ainea akaondoka. Aliyaamini maneno ya Petro na mwili wake ukapona. Mara nyingine tena mwujiza ukatendeka katika Jina la Yesu Kristo. Kila aliyeishi Lida na mareneo ya jirani walimwona Ainea akiwa ameponywa na hivyo walimwamini Bwana Yesu Kristo.
KIFO CHA TABITHA (Dorkasi kwa Ugiriki) (mstari 36-37)
Huko Yafa mji wa jirani na pwani, aliishi mwanamke mwema aliyeitwa Tabitha, tafsiri ya jina lake kwa lugha ya Kigiriki ni Dorkasi (yaani paa). Dada huyu siyo tu aliamini ujumbe wa Injili kwa moyo wake, bali pia alijaribu kufuata mfano wa Bwana wake, Bwana Yesu Kristo kwa kuwatendea mema watu wote. Aliiamini Kweli na aliionyesha imani yake kwa vitendo, alipenda kuwasaidia watu kwa namna yoyote aliyoweza na alikuwa akijishughulisha na kushona, alitengeneza nguo kwa ajili ya maskini na wagonjwa. Hii ilikuwa ni njia ya kuonyesha jinsi alivyompenda Bwana na upendo wake na akithibitisha kuyaamini kwa vitendo mafundisho ya Bwana.Wale waliomfahmu walimpenda sana, maana popote alipokwenda alifanyika faraja na kutenda mema. Hata hivyo siku moja Tabitha aliugua na kufa, ilikuwa siku ya majonzi kwa akina kaka na dada wa Yafa.
PETRO ANAITWA KWENDA YAFA (mstari 38-43)
Yafa ilikuwa umbali yapata kama kilometa 20 kutoka Lida ambapo Petro alimponya Ainea. (Tafuta miji hii katika ramani yako na ufuatilie safari ya Petro). Habari ya mwujiza huu ilienea hadi Yafa kwa hiyo ndugu wawili walitumwa kwenda kumtafuta Petro na kumwomba waende naye Yafa. Petro hakusita, na alikwenda pamoja nao moja kwa moja katika nyumba ya Tabitha, alipofika wakampeleka juu ghorofani ambapo Tabitha sasa alilala, wajane wote walikwa pale ambao Tabitha aliwasaidia. Wakasimama karibu naye wakilia na kumwonyesha zile nguo ambazo aliwashonea wakati ule walipokuwa naye. Petro akawatoa nje wote akapiga magoti akamwomba Mungu. Baadaya akaelekea yule maiti akasema “Thabita amka mara moja”. Naye akafumbua macho yake na alipomwona Petro akajiinua akaketi. Petro akamshika mkono akamwinua hata akiisha kuwaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele yao hali yu hai huzuni yao ikageuka kuwa furaha. Mwujiza huu ulisababisha watu wengi wa Yafa kumwamini Bwana Yesu Kristo. Petro alikaa na waamini hapo Yafa kwa muda, akiishi na Simoni mtengenezaji wa ngozi na Mhubiri wa Injili kwa watu waliomsikiliza.
PETRO ANAMPA MUNGU SIFA NA KUOMBA MSAADA KATIKA SALA
Ni lazima tuwe waangalifu kwa kumwangaia Petro wakati alipomponya Ainea hakusema kwamba kuwa ni yeye mwenyewe aliyemponya. Alisema “Yesu Kristo akuponya” (Matendo ya Mitume 9:34). Na vilevile kabla hajamfufua Thabita Petro alipiga magoti na kuomba (Matendo ya Mitume 9: 40). Haikuwa kwa nguvu zake kwamba Petro aliponya. Ilikuwa ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu aliopata kwa Mungu. Petro hakupenda watu wamsifu yeye bali aliwataka wamtukuze Mungu kwa maajabu na miujiza iliyokuwa imetendeka.
FUNDISHO KWETU
Maisha ya Tabitha yanaonyesha kuwa kila mmoja ni muhimu kwa kazi ya kumtumikia Mungu. Hatuwezi kuwa wote walimu wakubwa kama mitume lakini sisi wote tunaweza kufanya kazi katika eklesia na kuonyesha upendo wa Mungu kwa watu wanaotuzunguka. Kila wakati wapo ndugu wanaume na wanawake na watoto wao wanaohitaji msaada na kuna kazi nyingi za kufanya ambazo zina mfurahisha Baba yetu wa Mbinguni. Mtume Paulo alisema sisi tumekuwa kama viungo vingi vya mwili ambapo kila kiungo kina kazi yake katika mwili (Hii ndiyo eklesia) ili kufanya kazi sawasawa (1 Korintho12:14-25).Wengine wanapaswa kufundisha, na wengine waende wawaone wagonjwa na watengeneze nguo kwa ajili ya watu maskini au kugawa mwaliko ili kusikia Neno la Mungu. Na tuwe kama Tabitha na tufanye kazi ya Mungu kila siku,siyo kwa ajili ya kusifiwa na wanadamu, bali kwa ajili ya matendo yetu Mungu atukuzwe
MAELEZO YA NYONGEZA
Sala ni jambo kubwa ambalo Mungu amempa mwanadamu, maana kwa njia ya sala tunaingia mbele za Mungu wa dunia yote. Petro alimwombea Tabitha kwa Mungu. Mungu alijibu sala zake na kumrudisha kwenye uzima. Hii inatufundisha kwamba sala ni jambo lenye nguvu la kuweza kutusaidia sisi na wenzetu. Kwa hiyo ni muhimu kujifunza kusali na kufanya kuwa tabia yetu katika maisha yetu ya kila siku. Ni lazima tumkaribie Mungu kwa heshima kwa sababu yeye ni Mfalme Mkuu. (1 Timotheo 6:15-16). Ni lazima tuwe wanyenyekevu wakati tunapozungumza na Mungu wakati wa maombi kwa sababu Mungu yuko Mbinguni na sisi tuko duniani (Mhubiri 5:2). Yeye Mungu hujua yote tunayoomba kabla hatujaomba (Mathayo 6:31-32) na tunapaswa kumshukuru Mungu kwa mambo yote anayotupatia (Wathesalonike 5:18). Zaidi ya hayo yote Mungu anatutaka kuomba hekima ili tuweze kuelewa Neno la Mungu na ndipo tunaweza kujifunza kumtukuza Mungu (Yakobo 1:5; Mathayo 6:33).
MASWALI
Majibu Mafupi
1. Ainea alikuwa na matatizo gani?
2. Petro alimwambia nini Ainea?
3. Tabitha alikuwa anaishi wapi?
4. Kwanini Tabitha alifahamika sana?
5. Ni jambo gani lililomtokea Tabitha?
6. Ni nani waliyemwomba kuja kumsaidia?
7. Petro alifanya nini kabla ya kumfufua Tabitha?
8. Ni jinsi gani Petro aliweza kuwaponya Ainea na Tabitha?
Majibu ya Kina
9. Elezea habari jinsi Petro alivyofanya kule Lida.
10. Elezea yote uyajuayo kuhusu mwanamke aliyeitwa Tabitha.
11. Tunajifunza nini kutoka katika habari ya Tabitha?
Majibu ya Nyongeza
12. Ni jambo la muhimu kujifunza kusali. Mungu alijibu maombi ya Petro kwa namna ya ajabu. Ni
jinsi gani tunavyoweza kumwomba Mungu ili aweze kutusikia?