115. MUNGU ANAWAOKOA PAULO NA SILA KULE FILIPI
“Usiku wa manane Paulo na Sila walikuwawakimwomba na kumwimbia nyimbo za kumsifu Mungu”
Shabaha
Kuonyesha jinsi kweli ya Mungu ilivyobadilisha maisha ya mlinzi wa gereza na nyumba yake yote Matendo Mitume 16:23-40:
PAULO NA SILA WANATESEKA HUKU WAKISHANGILIA (mstari 23-25)
Jinsi inavyohuzunisha kuona hali ya Paulo na Sila kwenye gereza la Filipi wakati mlinzi wa gereza alipowafunga sana miguu kwenye mkatale. Ndivyo alikuwa ameagizwa kuwatunza salama naye mlinzi wa gereza alifahamu kwamba alingepoteza uhai wake kama watu hao wangemtoroka. Wali kuwa katika giza na utisho katika chumba cha ndani, wakati huomigongo yao ilikuwaka ikiwauma sana kwa maumivu waliyopata walipopigwa bakora sana kwa ukatili. Bila shaka sisi tungenjaa manung`uniko ya uchungu baada ya kutendewa isivyo haki namna hiyo, lakini Paulo na Sila walikuwa watu wa ajabu sana. Bila kujali yote yaliyotokea, hawakumwazia Mungu kuwa ni mbaya wowote au kumwuliza kwa nini aliruhusu wao kutendewa ukatili wa namna ile. Ni lazima walikuwa katika maumivu makali sana, lakini badala ya kumkasirikia Mungu, waligeuka na wakamwelekea Baba yao wa mbinguni kwa sala na Kumwimbia nyimbo za kumsifu sana mpaka usiku wa manane. Ni jinsi gani wafungwa wengine walivyoshikwa na mshangao pale walipowasikia Paulo na Sila wakiimba mle gerezani ndani ya chumba cha gereza. Mungu alisikia sala yao na akawajibu kwa njia ya ajabu kabisa.
MLINZI WA GEREZA ANAAMINI NA KUBATIZWA (Mstari 26-34)
Ghafla, usiku wa manane, kulikuwa na tetemeko lililoitikisa gereza zima. Mara moja milango yote ya gereza ilifunguka na minyororo ya kila mmoja ikafunguka. Wafungwa walikuwa huru. Tetemeko lile lilimwamsha mlinzi wa gereza naye alipoona milango ya gereza imefunguliwa, akafikiria kuwa wafungwa wote wametoroka. Akifahamu kwamba kwa hakika tendo la kutoroka kwa wafungwa wote angeuawa ikiwa litakapogunduliwa,akaufuta upanga wake ili ajiue lakini Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu akisma: “usijidhuru kwa maana sisi sote tumo humu”. Akiwa anatetemeka yule mlinzi wa gereza akaitisha taa na kurukia ndani ya chumba na kupiga magoti mbele ya Paulo na Sila na kusema: “Bwana zangu yanipasa nifanye nini ili nipate kuokoka?”. Paulo alijibu kwa furaha kubwa sana “Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako” (mstari 31). Akiwa mwenye shukrani na familia yake wakiwasikiliza kwa makini sana Paulo na Sila walipokuwa wakiendelea kuwaambia kuhusu Injili, nao wakaamini. Kwa huruma akawaosha wanafunzi mapigo yao, na halafu alfajiri kukiwa bado giza mlinzi wa gereza na nyumba yake wakabatizwa. Akifurahi sana yeye pamoja na nyumba yake katika tumaini lao jipya aliwachukua Paulo na Sila akawapeleka nyumbani kwake kuwapatia chakula.
PAULO NA SILA WANAACHIWA HURU (mstari 35 – 40)
Mchana ulipowadia makadhi walioamrisha Paulo na SIla kupigwa walituma ujumbe kwa wakuu wa walinzi wa gereza kuwa “Waacheni watu wale waende zao”. Hivyo mkuu wa gereza akamwambia Paulo, akasema “tokeni nje, na endeni zenu kwa amani”. Paulo akaona kuwa hili halikuwa tendo nzuri la kuwatoa kwa siri. Walikuwa wamepingwa bila hata wao kuweza kupewa nafasi ya kujibu tuhuma zilizotolewa dhidi yao na hilo halikuwa sawa katika sheria za Warumi, Paulo awaambia: “Na waje wenyewe wakatutoe”. Siyo kwamba Paulo alikuwa akijivuna aliposema hivi. Alikuwa akiwafikiria wanafunzi wenzake waliokuwakatika Filipi naye alitaka kuhakikisha kwamba hawatatendewa jeuri kama vile yeye na Sila walivyotendewa. Makadhi wakatambua kwamba Paulo alikuwa sahihi na kuwa wao wenyewe wengeweza kuwa katika matatizo makubwa. Kwa woga walikuja haraka gerezani na kuwatoa ndani, wakawaachia ndugu huru; wakawasihi waondoke Filipi. Paulo na Sila wakafanya hivyo, lakini ni baada ya kutumia muda kadhaa katika nyumba ya Lidia wakiwafariji na kuwatuliza moyo wanafunzi waliokuwa wamekusanyikia katika nyumba hiyo. Hili ndilo kusanyiko lililoundwa pale Filipi la ndugu waamini waliolipenda Neno la Mungu. Siku za baadaye akiwa Rumi Paulo aliwaandikia Wafilipi, mojawapo ya barua bora mno katika Biblia yetu.
FUNDISHO KWETU
Ilikuwa ni wakati Paulo alipowaandikia ndugu waamini huko Rumi ambapo aliwatia moyo waamini ili kufurahi katika tumaini kuwa na kuvumilia mateso na kudumu katika sala (Warumi 12:12). Katika fundisho hili tumekuwa tukifikiria kwa kina ili tuweze kufahamu mfano muhimu wa mausia.Paulo aliweza kuwa na furaha na akafurahia wakati alipokuwa katika mateso kwa sababu alimtegemea Mungu kwa ajili ya kupata nguvu na wakati wote alimshukuru Mungu kwa ajili ya baraka nyingi za ajabu alizompatia. Kama kweli tutafikiria wema wa Mungu kwetu na jinsi baraka hizo zilivyo muhimu sana, mateso yanayokuja katika katika upande wetu yataonekana ni mepesi mno na hata twaweza kwa furaha kama Paulo na Sila walivyofanya.
MAELEZO YA NYONGEZA
Yule mlinzi wa gereza ni dhahiri kuwa alikuwa amekwisha msikia Paulo alipokuwa akihubiri maana hakuna mtu awezaye kujifunza usiku mmoja itoshe kumwezesha kubatizwa. Akiwa anajuwa kipigo cha kikatili walichopata, mlinzi wa gereza ni lazima alishangaa kwa kusikia sala zoa na nyimbo za sifa. Tetemeko lilipokuja wao hawakutoroka, na kwa njia hiyo waliokoa maisha yao. Aliweza kuona ya kwamba matendo yao yaliambatana kila wakati, na maneno yao. Hivyo Mungu alikuwa akitayarisha akili yake kukubali kwamba waliyofundisha yalikuwa ni ya kweli. Bila shaka alikuwa amezungumza mambo haya pamoja na nyumba yake na matukio ya usiku ule yalitosha kuwaridhisha wote kuhusu umuhimu wa kuokoka. Na sasa mlinzi wa gereza na nyumba yake walikuwa watu waliobadilika. Na kila wakati hili huwatokea watu wale wanaoupokea na kuamini Injili. Waligeuka kwa kuziacha njia zao za zamani na kumwelekea Mungu, wakijifunza njia tofauti kabisa ya kufikiri na kutenda. Ni neno lake Mungu lililofanya kazi akilini na mioyoni mwao linaloleta badiliko hili. Kwa hiyo kwa kadri tunavyojifunza Neno la Mungu, ndivyo tutakavyotenda kama mitume, na kuyaona mateso yote kuwa nii mapito tu kwa kwa ajili ya utukufu wa ufalme wa Mungu.
MASWALI
Majibu Mafupi
- Paulo na Sila walifanya nini gerezani kabla ya usiku wa manane?
- Nini kilichotokea usiku wa manane?
- Wakati mlinzi wa gereza alipotaka kujiua, Paulo alipaza sauti akisema nini?
- Wakati alipopiga magoti mbele ya Paulo na Sila, aliwaomba nini?
- Jibu la Paulo lilikuwa ni lipi?
- Ni nini kilichompata mlinzi wa gereza na nyumba yake usiku ule?
- Watawala wa Filipi walituma ujumbe wakisema “waachie watu hawa waende zao” Paulo alijibu nini?
Majibu ya Kina
- Paulo na Sila waliwekwa gerezani kule Filipi. Eleza kilichotokea usiku ule wa tukio?
Majibu ya Nyongeza
- Ni mambo gani mengine yaliyoleta badiliko kwa mlinzi wa gereza wa Filipi. Hili linatufundisha nini kuhusu
mwenendo wetu tunaopaswa kuwa nao?