128. KUSUDI LA MUNGU LA KUMWUMBA MTU
Mwanzo 1 inaelezea kwa upana sana kuhusu siku sita za uumbaji.
Katika Mwanzo 2 tunajifunza kuhusu njia ambayo Mungu alimwumba mwanamume na halafu alimwumba mwanamke. Na baada ya tendo hili la kuwaumba aliwaweka katika Bustani na akawapa sheria.
Tutaona katika somo hili jinsi mtu na yule mwanamke walivyoshindwa kutii sheria ya Mungu na matokeo yake, dhambi na mauti vikaingia duniani.
Mwanzo 1:24-28; 2
KUUMBWA KWA MTU (Mwanzo. 2:7)
Kama tulivyoona katika somo lililopita, tendo kubwa muhimu katika uumbaji wa Mungu lilikuwa ni la kumwumba mtu.Mungu alikusudia mtu atawale uumbaji wake wote (Mwanzo 1:26). Wanyama walikuwa “wema sana” kwa jinsi yao, lakini wangeweza kufuata silika zao tu, ambazo ziliwafundisha jinsi ambavyo wangeweza kupata chakula, na jinsi ya kujilinda na namna ya kuwalinda watoto wao. Hawakuweza kumpa Mungu utukufu kama alivyohitaji, kwa sababu hawakuwa na uwezo wa kuelewa njia za Mungu.
Katika Mwanzo 1:26 tunaambiwa, “Mungu akasema na tumfanye mtu kwa mfano wetu (yaani mwonekano wa umbile), kwa sura inayofanana na sisi (yaani uwezo wa akili wa kupokea mawazo ya Mungu na kukuza tabia kama yake).” Kwa hiyo mtu aliumbwa kwa mfano wa Mungu mwenyewe akiwa na mwonekano kama wa malaika,lakini siyo kuwa na namna ya hali ya asili waliyonayo wao, kwa sababu wao wana miili ya uzima wa milele, ni viumbe wa kiroho wasiokufa.
Tunaambiwa katika Mwanzo 2:7 ya kwamba “BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akwa nafsi hai”au kiumbe kamili. au kiumbe hai. Aliumbwa kutoka katika mavumbi, kama walivyoumbwa wanyama (Mwanzo 2:19), nao wote waliendelea kuwa hai kwa njia ile ile ya “pumzi ya uhai” (Mwanzo 7:21-22; Zaburi 104:29). Lakini mtu alikuwa tofauti na wanyama, kwa sababu alikuwa ameumbwa kwa mfano wa Mungu. Akili yake ilikuwa na uwezo wa kufahamu njia za Mungu. Hili lilimfanya aweze kumpenda Mungu na kumtii na kwa hiyo kumtukuza na kumsifu yeye ambaye ni na kuendelea kumsifu na kumtukuza Muumba wake.
HAWA ALIVYOUMBWA (Mwanzo 2:18-23)
Mungu alikuwa amemweka Adamu juu ya Uumbaji wake wote. Adamu alikuwa amewapatia majina ndege na wanyama, lakini hakuwepo yeyote kati yao aliyeweza kufanana na mtu huyo. Hawakuwa na akili sawa naye wala ufahamu. Kwa hiyo Mungu akasema, “Si vema mtu huyo awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufafanana naye (anayefaa, au anayestahili) kwa ajili yake”.
Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akachukua ubavu wake mmoja, akaufanya mwanamke. Adamu alipoamka akamwona huyo ambaye akatakuwa mke wake, ambaye angefikiri na kuhisi kama yeye alivyofanya kwa sababu alikuwa ameumbwa kutokana na sehemu ya mwili wake mwenyewe. Adamu akamwita “Mwanamke”, ambalo linamaanisha “ aliyetoka kwa mwanamume” na baadaye akampa jina la “Hawa” inayomaanisha “kuishi” (Mwanzo. 3:20). Mungu angeweza kumwuumba mwanamke moja kwa moja kutoka katika mavumbi, kama alivyomwuumba mwanamume, lakini kama angefanya hivyo haingelikuwepo huruma na mapenzi ya kweli kati yao.
Tunafahamu kwamba hivi ndivyo mwanamume na mwanamke walivyoumbwa. Mungu alimvuvia Musa kuandika kuhusu tukio hilo, na Yesu Kristo mwenyewe aliamini hilo na kulifundisha, alinukuu kutoka kitabu cha Mwanzo 1:27 na 2:24 na katika Mathayo 19:4-6 na Marko 10:6-8. Kwa hiyo hatukubaliani na watu wasemao kwamba wanaume na wanawake na wanyama wote walitokea tu kutokana na mabadiliko au kukua kwa kuongezeka kutokana na viumbe vingine vyenye umbo dogo.
Akizungumzia habari za mwanamke, Adamu akasema “Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu”, na maandiko yanaongezea- “kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja”. Kwa hiyo, ndoa ni agizo na lilianzishwa na Mungu kuwa muungano wa kudumu wa mume na mke. Kwa akili inayoweza kuongozwa katika upendo na kujiweka wakfu kwa Mungu na ufahamu na hisia kwa mahitaji ya kila mmoja kwa mwenzake, mume na mke, katika kumcha Mungu na umoja wa upendo,ili wanaweza kusaidiana katika kazi ya Mungu.
MTU KATIKA BUSTANI YA EDENI (Mwanzo. 2:8-15)
Adamu alikuwa amewekwa na Mungu katika bustani ya Edeni, ili “ailime na kuitunza”. “Edeni” maana yake “furaha” na katika bustani hii ulichipuka “kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya bustani,na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.”
Kila kitu alichokuwa Mungu amekiumba kwa maumbile kilikuwa ni “chema sana”, ikiwa ni pamoja na mwanamume na mwanamke. Adamu na Hawa kwa sababu mpaka hapo walikuwa hawajapimwa (kupewa mtihani) hawa kwa sababu mpaka hapo walikuwa hawajapimwa (kupewa mtihani) hawakuwa na tabia ya mtu. Mungu alihitaji upendo wao na utiifu na hili lingeweza kuonekana tu kwa kuona iwapo wangemtii Mungu kwa uhuru wa hiari yao wenyewe.
AMRI (Mwanzo 2:16-17)
“Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema,Matunda ya kila mti wa bustani,waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakayokula matunda ya mti huo; utakufa hakika ”.
Kama Adamu na Hawa wangetii amri hili ingekuwa kumheshimu Mungu.Na kama wangekosa kumtii, “wangekufa hakika”. Walikuwa na hiari kuchagua tendo walilotaka kutenda, na Mungu alipenda watumie hiari hiyo kwa njia sahihi ya kumtii Mungu. Lakini aliwaonya kuwa kutokutii kungeleta kifo.
Kwa hiyo ni muhimu kukumbuka kuwa kutokutii sheria ya Mungu ni dhambi.Kama tukitenda dhambi tunastahili kupewa adhabu na tunajiletea aibu na kutokumheshimu Mungu pamoja na familia zetu.
JARIBU (Mwanzo 3:1-5)
Mambo yote yalienda sawa kwa kadiri Adamu na Hawa walivyokumbuka sheria ya Mungu na kuitii. Lakini ndani ya bustani alikuwamo nyoka, mnyama mwerevu sana aliyekuwa na uwezo wa kuogea.Na ingawaje alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwituni, alikuwa ni mnyama, mwenye akili ya mnyama tu. Hakuwa na uwezo wa kuelewa kwamba kila kitu alichosema Mungu kilikuwa ni kweli. Hakuwa na uwezo wa kukuza dhamiri kama Adamu na Hawa walivyoweza na kwa hiyo hakuelewa lipi ni jema na lipi ni baya, kutii, au kutokutii.
Hatimaye alisikia amri ya Mungu, na kwa akili yake mnyama aliyokuwa nayo ilimwongoza afikirie kwamba yale yaliyoyasemwa yalikuwa ni kinyume kabisa na ukweli.
Nyoka akamwuliza mwanamke, “Je, Mungu alisema msile matunda ya miti yote ya bustani?” Hawa alijibu kama amri ya Mungu ilivyosema. Ndipo nyoka aliposema uwongo wa kwanza, “hamtakufa hakika”. Ilikuwa kinyume kabisa na jinsi Mungu alivyosema. Hata hivyo uongo ulikuwa umechanganyika na ukweli pale alipoongezea ”kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakapokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama miungu (yaani malaika), mkijua mema na mabaya”.
Pendekezo hili liliamsha tama mbaya ya kuwa kama malaika.Tunaweza kuona kuwa Hawa alidanganywa kuamini uongo (1 Timotheo. 2:14). Akachagua kutomshirikisha mume wake Adamu ili kujadiliana kuhusu uongo huo Hawa akakubali kula tunda la mti waliokatazwa.
KUTOTII (Mwanzo 3:6)
Mwanzo 3:6 inafafanua aina tatu za msingi za tamaa za mwili kama zinavyoelezwa na mtume Yohana katika 1 Waraka wa Yohana 2:16. Badala ya kukataa ushawishi wa nyoka, Hawa alisikiliza, na kutazama na akaona kwamba ule mti wafaa kwa chakula (tamaa ya mwili);wapendeza macho (tamaa ya macho), nao ni mti wakutamanika kumpa mtu maarifa (yaani kiburi cha uzima). Hawa,akala matunda yake akawa amemwasi Mungu,akampa Adamu pia, ambaye alishirikiana naye kula.
Katika kutenda kosa hili, Hawa alikuwa amekubali mawazo ya kimwili ya nyoka, kwa hiyo mwanamke alijipotosha kwa tamaa zake mwenyewe. Kitendo hiki kinafafanuliwa katika Yakobo 1:14-15, na sasa yamekuwa ndiyo mazoea ya wanadamu wote, kwani “kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti”. Kila tunapojaribiwa na dhambi inabidi tukumbuke mfano wake Kristo wa kuyashinda majaribu kila wakati tumfikirie Mungu na Neno lake (Mathayo 4:1-10; soma pia 1 Yohana 2:14)
MATOKEO YA DHAMBI (Mwanzo 3:17-19)
Macho ya mwanamume na mwanamke yakafumbuliwa, lakini siyo kwamba “waliweza kupata maarifa” kama ambavyo Hawa alitumaini. Wakawa ni wenye aibu nyingi na hofu kubwa. Wakatambua kuwa wako uchi na kujaribu kujifunika kwa kushona majani ya mtini. Hawakujiona tena kuwa pamoja na Mungu nao wakajaribu kujificha mbali na Mungu. Malaika wa Mungu aliwatafuta, naye Adamu akatubu kwa kukiri kwamba alikuwa amekula tunda la mti ambao alikatazwa. Akamlaumu Hawa kwa ajili ya tendo lake la kula tunda, naye Hawa akamlaumu nyoka. Wote,Mungu akawahukumu:
-
Nyoka – alilaaniwa kuliko wanyama wote (mstari 14);
-
Mwanamke – atatawaliwa na mwanamume. (mstari 16);
-
Mwanamume – ardhi ililaaniwa kwa ajili yake (mstari 17-18).
Hukumu ya mwisho “Kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana wewe ni mavumbi, na mavumbini utarudi”, (mstari 19). Mtu hakuwa tena kilicho “chema sana” akawa sasa ni mtu wa kufa - aliyepaswa kufa. Hukumu hii imewafikia wana wote wa Adamu tangu wakati huo hadi sasa. Na sisi kwa kuwa ni wa uzao wake tumerithi hali ya kufa. Nasi kwa vile tu wazao wake tunajikuta katika hali ya miili yetu kuwa na tabia ya kufikiri na kutenda kinyume na njia za Mungu (Warumi 5:2,12; 7:18; 8: 5-7).
Kifo ni hali halisi –ndiyo mwisho wa uhai, mawazo na matendo (Zaburi 6:5; Mhubiri 9:5; Isaya 38:18). Bado kuna watu wengi wanaofundisha na kuamini uwongo wa nyoka “hamtakufa hakika”, kwa kutamka ya kwamba mwanadamu ana roho isiyokufa, kitu kinachoendelea kuwa hai baada ya kifo. Hili siyo la kweli na wala siyo fundisho linalopatikana katika Biblia (Rejea kwenye Mwongozo wa Masomo Namba. 31 hadi 35). Biblia inafundisha kuwa roho inakufa (Ezekieli.18:4; Zaburi 89:48)
Tumeona ya kuwa, matokea ya dhambi, Adamu na Hawa walihukumiwa kifo. Wakawa watu wa kufa, na wakawa viumbe wa kufa,na wanadamu wote wanaendelea kurithi hali hiyo hiyo ya kufa. Ni kwa jinsi gani basi Mungu ataleta kusudi lake la kuijaza dunia na watu wanaoishi milele ambao wataweza kumsifu na kumtukuza Mungu.
Katika somo linalofuata tutafikiria Mwanzo 3:14-19 kwa kina zaidi, na hasa mstari wa 15. Tutaona jinsi Mungu alivyoleta njia ya ukombozi kwa wanadamu, ambayo itawaokoa kutoka katika hali yao ya kutokuwa na tuamini.
VITABU REJEA:
"Elpis Israel" (J. Thomas)—Part First—Chapters 2, 3
"Story of the Bible" (H. P. Mansfield)—Chapter 4
"The Visible Hand of God" (R. Roberts)—Chapter 4
"First Principles Bible Marking Course"—(C.S.S.S.)—Pages 16-19, 68-74., Ukurasa 16-19, 68-74
MASWALI YA
-
Fafanua jinsi mtu alivyoumbwa, na onyesha:-
-
Namna alivyokuwa kama wanyama na
-
Jinsi alivyokuwa tofauti nao.
-
Eleza jinsi mwanamke alivyoumbwa.
-
Ni uongo upi wa kwanza ambao Hawa aliambiwa? Ni jinsi gani Hawa alivyaitikia mawazo ya Nyoka?
-
Onyesha maandiko yanayothibitisha kuwa mtu ni wa kufa.
MASWALI YA INSHA
-
Fafanua kujaribiwa kwa Hawa, kuonyesha njia zote tatu ambazo majaribu yanawapata wanadamu wote.
-
Matokeo ya uasi wa Adamu na Hawa yalikuwa ni nini?