130. KAINI NA HABILI - USHINDI WA IMANI
Matokeo yaa uasi, Adamu na Hawa walifukuzwa katika Bustani ya Edeni waishi maisha shida na yenye mateso hadi walipokufa. Mungu alikuwa amemwambia Adamu “ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako;michongoma na miiba itakuzalia …kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi,ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi” (Mwanzo 3:17-19). Walipohukumiwa kifo, wazao wao wote wakawa ni wa kufa au viumbe wasiodumu. Katika watoto wao wa kwanza wawili zinaonekana hisia za “uzao wa mwanamke” na “uzao wa nyoka”. Tutaliona hili kama fundisho letu wenyewe, uamuzi wa Mungu kwa tabia na mwenendo wa hawa wana wawili.
Mwanzo 4
KAINI NA HABILI (Mwanzo 4:1-2)
Muda ulivyoendelea, Hawa alizaa mtoto wa kwanza wa kiume ambaye alimwita“Kaini”, maana yake “amepatikana”au“aliyepatikana”. Kama ilivyotokea, jina la Kaini lililingana na tabia yake akionyesha akili iliopendelea zaidi vitu kuliko mambo ya Mungu. Hawa akazaa mtoto wa kiume mwingine, aliyemwita Habili iliyomaanisha “ubatili”. Abeli alionyesha tabia iliyoona vitu vyote vya maisha ya dunia, kuwa ni ubatili kwake , au visivyo na thamani. Tabia yake ilikuwa ya imani iliyoheshimu mapenzi ya Mungu katika mambo yote.
Kaini akawa mkulima, akipanda nafaka na mazao mengine ya ardhi, naye Habili akawa mchunga Kondoo.
MUNGU ANAPEWA SADAKA (Mwanzo 4:3-5)
Wana wote wawili wa Adamu na Hawa walikuwa wanamwabudu Mungu na wakati ulipowadia wa kutoa sadaka. Kaini alitoa “mazao ya ardhi”, naye Habili alitoa “wazao wa kwanza wa mifugo yake”- mwana kondoo au mwana mbuzi
Imewekwa katika kumbukumbu kwamba, “Mungu alipendezwa na sadaka ya Habili”, lakini siyo sadaka ile ya Kaini, sadaka ya Habili ilikubaliwa na ile ya Kaini haikukubaliwa.
Kwa nini?
Ni jambo lililo dhahiri kabisa kuwa sadaka ya Habili ndiyo ambayo Mungu alihitaji,ingawa sadaka nyingine ilikuwa ni ile ambayo Kaini alifikiria kuwa ndiyo inayofaa. Ndugu hawa wawili bila shaka walielewa ni sadaka ipi Mungu alihitaji. Adamu bila shaka alikuwa amewaeleza kuhusu ile sadaka ya kwanza iliyotolewa ili kuifunika dhambi kwa ajili ya yeye mwenyewe na Eva. Kwa njia hii walikuwa wamefundishwa ya kwamba ilikuwa muhimu sana kumwagika kwa damu ili kupata msamaha wa dhambi. Fikiria mambo muhimu yafuatayo:
Habili alionyesha uelewa wake kuhusu sadaka kwa ajili ya ondoleo la dhambi kwa kutoa mzaliwa wa kwanza wa mifugo yake kwa ajili ya sadaka (Waebrania 11:4). Kaini, kwa upande mwingine akaleta matunda ambayo yalitokana na kazi yake bila kujali Mungu alihitaji sadaka ipi katika mambo ya ibada. Alifuate njia “iliyokuwa sawa sawa machoni pake mwenyewe”, na hili lilikuwa ni “nia ya mwili”. Waebrania 11:4 inatuambia kuwa Habili alitenda kwa imani alipotoa sadaka yake. Kwa kuwa “imani chazo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo” (Warumi 10:17), tunaweza kufikiria kuwa mahitaji ya muhimu ya kuabudu yalitolewa na Mungu kwa wote Habili na Kaini.
Katika tendo hili la kuheshimu Neno la Mungu, Habili alikuwa mwenye kuonyesha kuwa alikuwa mfano wa “uzao wa mwanamke” ambapo Kaini, kwa kukosa kwake heshima alionyesha kuwa alikuwa mfano wa “uzao wa nyoka”.
KAINI MWENYE WIVU (Mwanzo 4:5-7)
Badala ya kukubali kwamba Mungu anatakiwa akaribiwe kwa njia iliyo sahihi, Kaini alikasirika sana na kumwonea wivu ndugu yake. Lakini Mungu alimwambia kuwa angekubaliwa kama atapeleka sadaka iliyo sahihi. Kaini, akiwa kaka mkubwa angeendelea kuwa kwenye nafasi ya kwanza mbele ya Habili. Kwa hiyo Mungu alimjalia rehema Kaini na kumpatia nafasi ya kutubu.
MAUAJI YA KWANZA (Mwanzo 4:8-10)
Kaini alikuwa ni “uzao halisi wa nyoka”. Aliongozwa na mawazo yake ya ubinafsi. Mungu alitaka Kaini anyenyekee na kukubali kwamba Mungu alikuwa sahihi na mwenye haki katika kumtaka kuweka pembeni tamaa zake binafsi, na kufanya sawa jinsi Mungu apendavyo. Lakini chuki na hasira ya Kaini ikaongezeka juu ya Habili na Kaini akayaweka kando asifikirie akilini mwake maneno ya Mungu. Akiwa ni mwenye kughadhibika na uso wake ukiwa umekunjamana akamwua Habili uwandani.
“Naye alimwua kwa sababu gani? Ni kwa sababu matendo yake yalikuwa mabaya, na ya nduguye yalikuwa ya haki” (1 Yohana 3:12)
Kaini alidhani kuwa alikuwa ameficha kosa lake, na alipoulizwa na Mungu, “Yuko wapi Habili ndugu yako?” Kwa ghadhabu akasema “Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” Lakini Mungu anajua yote, na akamwambia Kaini, “damu ya nduguyo inanililia kutoka katika ardhi”.
ADHABU YA KAINI (Mwanzo 4:11-16)
Kutokana na tendo lake ovu Kaini alilaaniwa na Mungu. Ardhi ingetoa mavuno machache kama matokeo ya jasho la mikono yake, naye atakuwa mtoro na asiye na makao duniani. Kwa maneno mengine atatumia maisha yake kukimbiakimbia kutoka kwenye haki na kwenda mahali mahali,kila wakati akihofia kwamba mtu mmoja angemwua kwa kulipa kisasi kwa mauaji ya nduguye.
Kaini alitambua kwamba alikuwa amefukuzwa kutoka mbele ya uso wa Mungu na kuwa maisha yake yangekuwa hatarini daima. Akalalamika, “Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki”. Jibu la Mungu lilikuwa kwamba atakayemwua Kaini ataadhibiwa. Naye akamweka alama usoni, “ili yeyote amwonaye asimwue”.
Hivyo Kaini akafukuzwa akaelekea nchi ya ''Nodi'' ambayo inamaanisha “uhamishoni” au “kuzunguka zunguka”au anayetangatanga. Mwisho wa kutisha wa kudharau mapenzi ya Mungu, wivu mkali na uuaji ukiwa na maana kwamba Kaini asingeweza kufurahia tena ushirika wa Mungu.
IBADA INAYOKUBALIKA (Yohana 4:24)
Uadui kati ya Kaini na Habili ulianzia wakati mmoja wao alipomwabudu Mungu kwa usahihi na yule mwingine hakumwabudu Mungu kwa usahihi. Katika Yohana 4:24, Yesu alisema, “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli”. Haitoshi tu kwamba mtu anatamani kumwabudu Mungu; Yesu anatuambia kwamba inampasa mtu kutafuta njia sahihi ya kumwabudu Mungu.
Kaini hakufanya hivyo.
Alifikiria Mungu angependezwa na chaguo lake la sadaka yake, naye hakutambua umhimu wa kumkaribia Mungu katika njia inayofaa. Habili alionyesha tabia ya unyenyekevu ya mtu anayeabudu “katika roho na kweli”, yaani katika njia anayoikubali Mungu.
Kwa sababu ya imani yake na utii, Habili alifanyika kuwa mfano wa Bwana Yesu Kristo, “uzao wa mwanamke” (Waebrania 12:24).
Kaini alikuwa “wa yule mwovu, akamwua ndugu yake”- (1Yohana 3:12). Alijionyesha yeye mwenyewe kuwa ni “uzao wa nyoka”.
Wale wanaofuata njia zake Mungu na wale wanaojipendeza wao binafsi , kamwe hakuna amani kati yao. Kuna “uadui” kati ya hao wawili. Kaini alikwenda zake kwa njia yake mwenyewe, kwa sababu ya kufuata nia ya mwili, na hili lilimwongoza kwenye adhabu na kifo bila tumaini.
Habili alikufa kifo cha ukatili mkononi mwa nduguye mwenye wivu. Alikuwa mtu mwenye imani na utii, na kwa hiyo atafufuliwa kutoka kwa wafu siku Kristo atakaporudi. Atazawadiwa pamoja na waaminifu wengine ambao wametajwa katika Waebrania 11. Fundisho kwetu ni kwamba iwapo tunataka kumwabudu Mungu anavyotaka na kuwa na tumaini la uzima wa milele, inatupasa kufuata Biblia na kuelewa Mungu anayotaka sisi tuyafanye, na kufuata amri zake.
Kama vile Kaini, watu wa dunia wanadharau kabisa njia iliyowekwa na Mungu ili kumwabudu. Na tuwe kama Habili mwaminifu na kwa unyenyekevu tutafute kumwabudu Mungu pamoja na wengine wenye imani moja ya kweli.
UZAO MWINGINE BADALA YA HABILI (Mwanzo 4:25)
Mungu alimpatia Hawa mwana mwingine badala ya Habili yule mwenye haki, naye akamwita jina “Sethi” likiwa na maana “aliyeteuliwa”.
“Kwa maana Mungu” Hawa akasema, “ameniwekea uzao mwingine mahali pa Habili; kwa sababu Kaini alimwua”.
Sethi alimwabudu Mungu katika kweli na wazao wake wote, ambao pia walimwabudu kwa uaminifu kabisa, nao wakaitwa “wana wa Mungu”. Wazao wa Kaini walikuwa waovu, nao waliitwa“wana wa wanadamu” (Mwaanzo 6:1-2). Kwa jinsi hii, “uzao wa aina mbili au aina ya watu ilianzishwa”. Walikuwepo waabuduo wa kweli wa Mungu, wanaowakilisha “uzao wa mwanamke” na waabuduo kwa makosa wanaojifanyia watakavyo, ambao huwakilisha “uzao wa Nyoka”.
Wazao wa Sethi wameorodheshwa katika Mwanzo sura ya 5, na hutuonyesha jinsi “uzao wa mwanamke” ulivyoanzishwa hadi ukafikia jumuia kubwa ya watu (soma Mwaanzo 4 kwa maana ya jumuia iliyotoka kwa Kaini).
“Uzao wa mwanamke”wa mwisho kabla ya gharika alikuwa Nuhu na wanawe watatu.
VITABU REJEA:
"Elpis Israel" (J. Thomas)—Pages 115-120
"The Story Of The Bible" (H. P. Mansfield)—Chapter 5
MASWALI YA AYA
-
Kwa nini Mungu aliikubali ibada ya Habili?
-
Eleza jinsi Kaini alivyojisikia kuhusiana na ndugu yake, na namna hili lilivyosababisha kuanguka kwa Kaini.
-
Ni nini ilikuwa adhabu ya Mungu kwa Kaini?
MASWALI YA INSHA
-
Ni kwa nini Mungu aliikubali sadaka ya Habili na akaikataa sadaka Kaini?
-
Jinsi gani tunavyoweza kumwabudu Mungu ili kwamba atupokee?
-
Fafanua namna “uzao wa aina mbili”au makundi ya watu yaliyotoka kwa Kaini na Habili na vizazi vyao. Ni maneno gani yanatumiwa katika Mwanzo 6 kubainisha hizo aina mbili za wazao?