131. NUHU – KUANGAMIA KWA DUNIA YA ZAMANI
Wazawa wa Sethi ambao walikuwa watu waliofuata njia ya Mungu, waliitwa “wana (au mabinti) wa Mungu”. Wazawa wa Kaini, ingawa walikuwa mafundi katika sanaa nyingi, walikuwa waovu, nao wakajulikana kama “wana (au mabinti) wa wanadamu”. Kwa muda mrefu makundi haya mawili waliishi wakiwa wametengana kundi moja na jingine,na kwa kadiri muda ulivyokwenda, hali ile ya kutengana ilitoweka, ndipo kila kundi lilianza kutafuta uhusiano na kundi lingine. “Wana wa Mungu” waliwaona “binti za wanadamu” kuwa ni wazuri, “nao wakajitwalia wake wowote waliowachagua”. Hii ilikawa ni kuiacha njia ya Mungu. Wana waliozaliwa kutokana na kuoana kwa makundi haya mawili; wakawazaa “majitu watu wenye sifa”. Walikuwa ni “majitu” siyo lazima kwa ukubwa wa umbile lakini majitu katika kutenda uovu. Walijulikana kuwa “watu wenye sifa”, inayomaanisha walikuwa watu hodari kwa matendo makuu, hasa katika vita. Mungu akatoa hukumu kwa waovu hao na akaweka muda ambao angewaangamiza.
Mwanzo 6,7,8
UOVU ULIONGEZEKA DUNIANI (Mwanzo 6:5-13)
Kiburi cha mwanadamu na kumwasi Mungu kiliongezeka haraka. “Mungu akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani, na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu siku zote. BWANA akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo… maana kila mwenye mwili amejiharibia njia yake duniani.
Dunia ilijaa uovu na mauji, lakini hata katika siku hizo za kutenda mabaya, mtu mmoja, Nuhu na familia yake, walikuwa waaminifu kwa Mungu (mstari 8 na 9).
Mungu akamwambia Nuhu kwamba, atawaangamiza wanadamu, lakini kwa rehema zake atawapa onyo na nafasi ya kutubu (mstari 3). Nuhu akafanyika kuwa “mhubiri wa haki” kwa watu waliomzunguka, akiwaita watubu na kuwaonya kuhusu hukumu ya Mungu ambayo ilikuwa inakuja (2 Petro 2:5).
Kutoka Mwanzo 6:3 na 1 Petro 3:20 inaonekana kwamba “uvumilivu” wa Mungu ulipongojea kwa miaka 120 wakati Nuhu akiwahubiri watu. Bahati mbaya kwao, watu hao hawakujali mahubiri ya Nuhu, nao wakaendelea katika njia zao za uovu.
SAFINA YA USALAMA (Mwanzo. 6:14-22)
Mungu alimwambia Nuhu kutengeneza safina ambayo ingewezesha kuwapatia sehemu ya usalama wakati hukumu yake itakapofika. Mungu akasema “Na tazama, ninaleta gharika ya maji juu ya nchi, nitaharibu kila kitu chenye mwili na pumzi ya uhai, kisiwepo chini ya mbingu; kila kilichoko duniani kitakufa. Lakini nitafanya agano langu nawe kuwa thabiti; nawe utaingia ndani ya safina wewe, na wanao na mkeo, na wake za wanao pamoja nao (mstari17-18).
Nuhu alipewa maelekezo jinsi ya kutengeneza safina, na akaifanya kazi hiyo kwa imani na utiifu. Vipimo vilikuwa urefu wa dhiraa (yadi) 300 kwa yadi 50 upana na yadi 30 kimo. Dhiraa moja yapata urefu wa sentimeta 45 hadi sentimeta 55, kwa hiyo ilikuwa na urefu upatao kama mita 150 kwa upana wa mita 25 na kimo chake (kwenda juu) mita 15 - kilikuwa chombo kikubwa sana. Ilikuwa na ghorofa tatu, na dirisha upande wa juu na mlango sehemu ya pembeni. Ilikuwa na chumba kwa ajili ya watu na wanyama, na vilevile kilikuwepo chumba (stoo) kwa ajili ya mahitaji ya lazima ya chakula.
Shughuli ya aina hii ingefanyika kwa muda wa miaka mingi ya kazi ngumu, kazi ilifanyika kwa imani na utii. Wakati Nuhu alipokuwa akiendelea kutengeneza safina ile, pia alikuwa akihubiri ujumbe wake wa maonyo kwa watu, ambao hawakujali maonyo. Imani yake Nuhu ilipimwa, kwa maana, kwa kadiri mwaka ulivyopita na mwaka ukafuata, ndivyo uovu ulivyozidi kuongezeka duniani; lakini hata hivyo bado hukumu ya Mungu haikufunuliwa. Hata hivyo, imani ya Nuhu haikupungua, kwa maana imeandikwa “Kwa imani Nuhu akiisha kuonywa na Mungu, katika habari za mambo yasiyoonekana bado, kwa jinsi alivyomcha Mungu, aliunda safina, apate kuokoa nyumba yake. Na hivyo akauhukumu ulimwengu makosa, akawa mrithi wa haki ipatikanayo kwa imani” (Waebrania.11:7).
Tunaweza tukatiwa moyo na imani ya Nuhu na utiifu wake kwa kukubali maagizo ya Mungu kwa kuonyesha imani na ujasiri wa kufanya mapenzi ya Mungu wakati tunapochanganyika pamoja na watu wasiomwamini Mungu huko mashuleni na maofisini. Badala ya kuvunjwa moyo tunaweza kwa furaha kuwaelezea kuhusu habari njema za kurudi kwa Kristo.
JINSI MUNGU ALIVYOWAOKOA WENYE HAKI NA KUWAADHIBU WAOVU: (Mwanzo 7;8: 1-19)
Safina ilipokuwa imeshakamilika Mungu alimwambia Nuhu “Ingia wewe na jamaa yako yote katika safina; kwa maana nimekuona wewe u mwenye haki mbele zangu katika kizazi hiki”. Huu ulikuwa mwaliko wa Mungu wa “Tokeni kati yao na mjitenge” kutoka katika ulimwengu mwovu ambao ulikuwa unakaribia kupata hukumu ya Mungu.
Kwa hiyo Nuhu na nyumba yake- watu wanane tu kati ya kusanyiko kubwa la watu wote ulimwenguni – hao peke yao ndio walioupokea wito wa wokovu wa Mungu.
Nuhu aliagizwa kuleta ndani ya safina jozi saba za kila aina ya wanyama wasafi na ya ndege, na jozi moja ya kila mnyama najisi na ya ndege (Zingatia: Biblia ambayo ni Toleo la Umoja( Union Version). Katika sura ya7:2-3 inaonyesha “saba saba”, lakini tafsiri nyingine za Biblia zinaonyesha: “jozi saba”.
Nuhu alitii maelekezo ya Mungu na kukusanya familia yake na wanyama na viumbe wengine ndani ya Safina, pamoja na vyakula vya kutosha kwa ajili yao na wanyama pia.
BWANA, Mungu “akafungiwa ndani” na baada ya siku saba mvua ilianza kunyesha na kuendelea kwa siku 40 mchana na 40 usiku, “alipoleta gharika juu ya ulimwengu wa wasiomcha Mungu” (2Petro 2:5). “Kila kilicho hai juu ya uso wa nchi kikafutiliwa mbali tangu mwanadamu hata mnyama wa kufugwa,na kitambaacho, na ndege wa angani ”. Kwa hiyo hukumu ya Mungu ikashuka juu ya wale watu waovu naye,“akabaki Nuhu tu,na hao waliokuwa pamoja naye katika safina”.
Baada ya mvua kuacha kunyesha, Nuhu na familia yake ilibidi wabakie katika safina mpaka nchi ikauke.
Maji ya ghalika yalipoendelea kupungua, Nuhu akamtoa nje Kunguru,na kisha akamtoa njiwa.Kunguru akaruka huko na huko mpaka maji yalipokauka, lakini njiwa alirudi tena katika safina, kwa maana “hapakuwepo mahali pa kutua kwa wayo wa mguu wake”.
Baada ya siku saba tena akamtoa yule njiwa katika safina na njiwa akarudi akiwa na jani bichi la mzeituni kinywani, ikionyesha kwamba maji yalikuwa yakipungua juu nchi. Baada ya siku saba nyingine tena yule njiwa alitolewa tena, na safari hii hakurudi.
Hatimaye, muda mfupi baada ya mwaka mmoja tangu walipoingia katika Safina, nchi ilikauka. Nuhu na familia yake waliambiwa na Mungu “watoke”, waliwachukua pamoja nao viumbe wote, ili “waongezeke na kuijaza nchi”.
AGANO LA MUNGU (Mwanzo 8:20-22; 9: 1-18)
Tendo la kwanza la Nuhu baada ya kutoka ndani ya Safina ilikuwa kujenga madhabahu na kumtolea BWANA sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya kumshukru kwa ukombozi wake.Hili tendo lilimpendeza Mwumbaji. Akambariki Nuhu na kumwahidi kuwa hataangamiza kila kiumbe chenye uhai kama alivyotenda. Nuhu na wanawe waliambiwa “zaeni, mkaongezeke, na kuijaza nchi”. Mungu alikuwa ameuondoa uovu duniani. Mwanzo mpya ungeanzishwa na Nuhu, mtu mwenye haki, aliyekuwa mwaminifu na familia yake.
Mungu akasema, “Na agano langu nitalithibitisha nanyi; wala kila chenye mwili hakitafutwa tena kwa maji ya gharika...Hii ndiyo ishara ya agano nifanyalo kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi; kwa vizazi vyote hata milele; Mimi nauweka upinde wangu winguni, nao utakuwa ni dalili (ishara) ya agano kati yangu na nchi ” (Mwanzo 9:11-13).
GHARIKA INACHOFUNDISHA (2 Petro 2:5-9; Mathayo 24:37-39; 1 Petro3:20-21)
Mungu atawaokoa watu wenye haki siku ya hukumu.
Kumbukumbu iliyoandikwa kuhusu tukio la gharika yanatuonyesha sisi haki na rehema ya Mungu. Katika siku za Nuhu Mungu alikuwa mvumilivu kwa ulimwengu ambao ulikuwa umejaa maovu. Hatimaye alileta hukumu juu yake na kwa wakati ule ule akamwokoa Nuhu na nyumba yake ambao walionyesha imani na utiifu. Kama ilivyokuwa kwa Nuhu, watu wale wote ambao watakuwa wametii wito “Tokeni kati yao, mkatengwe nao, msiguse kitu kilicho kichafu (2 Wakorintho 6:17) wataokolewa katika siku ambayo Mungu ataihukumu hii dunia yenye uovu (2 Petro 2:5-9)
Hali itakayokuwepo “kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu”, kabla ya kurudi kwa Kristo: Yesu Kristo alitumia “siku za Nuhu” kuonyesha hali itakayokuwepo duniani kabla ya kurudi kwake. Tunayaona mambo haya ya uovu yaliyopo siku hizi. Dunia imejaa machafuko, kizazi kiovu kinakataa nguvu za Mungu na hata husema kuwa Mungu hayupo. Maisha yao wameyakabidhi tu kwenye anasa zao wenyewe nao wanadharau maonyo yatolewayo na eklesia na hata kuwadharau watu wanaohubiri injili kwa juhudi kuhusu hukumu inayowataka kutubu. Hii ni mojawapo ya dalili zinazotuonyesha kuwa kurudi kwa Kristo kumekaribia, kwa maana Yesu alisema “kwa maana, kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu” (Mathayo. 24:37-39).
Ingawaje dunia ni yenye maovu nayo imejitenga mbali na Mungu hatutakiwi kushindwa na tabia za watu wanaotuzunguka wasiomcha Mungu, Kristo aliwafundisha wafuasi wake kuwa wangekuwa “katika ulimwenguni lakini wasishiriki ya ulimwengu)” ikitufundisha sisi kutumia muda wetu kwa hekima, tusijiingize katika mazungumzo ya kipumbavu na mwenendo wa kipuuzi-na badala yake tunatakiwa kutumia nafasi yoyote kuzungumzia kuhusu kuja kwa Ufalme wa Mungu ili kuibadilisha dunia hii ya uovu.
-
Ubatizo:
Mtume Petro, katika waraka wake wa kwanza, alisema gharika ilikuwa ni mfano wa ubatizo… “wakati uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa, ambamo ndani yake wachache, yaani watu wanane waliokoka kwa maji. Mfano wa mambo hayo ni ubatizo,unaowaokoa ninyi pia siku hizi;(siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili,bali jibu la dhamiri safi mbele za Mungu) kwa kufufuka kwake Yesu Kristo” (1Petro 3:20-21). “Dunia hapo zamani” ilitakaswa kwa gharika na maisha mapya yakaanzia kwa Nuhu na familia yake walipotoka ndani ya safina.
Yesu ndiye “Safina” ya wokovu kwa watu wote wale waaminio Injili na kutii amri ya kubatizwa kwa Jina lake (Marko 16:15-16). Katika yeye tunakuwa salama kutokana na maangamizo yatakayokuja duniani kwa ajili ya watendao maovu, iwapo tutadumu kuwa waaminifu kama alivyofanya Nuhu. Tunapogeukia upande kwa kuyachaa maovu yanayotuzunguka na kuamua kumtii Kristo katika ubatizo, ndipo sisi tunakuwa kama Nuhu.
Tendo la kwanza la Nuhu mara baada ya kutoka ndani ya safina ilikuwa ni kumtolea BWANA sadaka ya kuteketezwa, ili kuonyesha kujiweka wakfu kabisa kwake.
Na sisi pia baada ya ubatizo, inatupasa kuyatoa maisha yetu kuwa dhabihu kwa ajili ya mapenzi ya Mungu, ili kwamba “kuanzia hapo na kuendelea tusiitumikie dhambi tena” (Warumi 6:4-6).
Kwa hiyo mafundisho kuhusu gharika yanakuja nyumbani kwa kila mmoja wetu na sisi inapendeza kama tutakuwa kama Nuhu na nyumba yake tukitenda kwa pamoja ili tujiokoe wenyewe kutokana na hukumu za Mungu juu ya ulimwengu mwovu na usiosikia (Waebrania 11:7). Hata kama sisi ni vijana, bado tunaweza kujionyesha katika maisha yetu, kwamba dunia haituvutii kwa jambo lolote, bali tunangojea kwa shauku kurudi kwa Kristo.
VITABU REJEA:
"The Story Of The Bible" (H. P. Mansfield)—Chapter 6
"Elpis Israel" (J. Thomas)—Pages 118-120
"The Visible Hand Of God" (R. Roberts)—Chapter 5
MASWALI YA AYA
-
Mungu aliwaonaje watu siku za Nuhu?
-
Nuhu alifanya nini Mungu alipomwonya kwamba hukumu ingekuja juu ya dunia alimo kuwa anaishi?
-
Ni nani anayefananishwa na safina aliyoitengeneza Nuhu na nyumba yake?
-
Utiifu wa Nuhu wa kuijenga safina na kuingia ndani yake wakati wa gharika ni sawa na tendo la utiifu ambalo Mungu anahitaji kwetu. Ni tendo gani hili?
-
Ni agano gani Mungu alimpatia Nuhu?
MASWALI YA INSHA:
-
Fafanua hali iliyokuwepo duniani siku za Nuhu, na ueleze jinsi ilivyo sawa na nyakati zetu.
-
Fafanua tabia ya Nuhu, ukitoa vielelezo kutokana na maisha yake.
-
Abramu alifika pamoja na Lutu akiwa pamoja na familia yake kutoka Harani na akamjengea BWANA madhabahu (Mwanzo 12:6-7)
-
Abramu akapiga hema yake katikati ya Betheli na Ai na kisha akamjengea BWANA madhabahu (Mwanzo 12:8)
-
Abramu akasafiri, akashuka Misri ili kujiepusha na njaa kisha akarudi Betheli /Ai (Mwanzo 12:9-10; Mwanzo 13:1-4)
-
Baada ya Lutu kuondoka na kwenda mji wa Sodoma, Abramu akaelekea kusini hadi Hebroni na akamjengea BWANA madhabahu huko (Mwanzo 13:18)
-
Ibrahimu akaishi Gerari katika nchi ya Wafilisti (Mwanzo 20:1)
-
Ibrahimu akafika Beer-sheba ambapo alitoka hapo akaenda Mlima Moria ili kumtoa Isaka kuwa sadaka ya kuteketezwa (Mwanzo 21: 32-33; Mwanzo 22:2)
-
Ibrahimu akamzika Sara katika pango la Makpela karibu na Hebroni. Na baadaye Ibrahimu naye akazikwa huko (Mwanzo 23:19; Mwanzo 25:8-9)