133. IBRAHIMU NA ISAKA: UZAO WA AHADI
Imani ya Ibrahimu ilichukua miaka mingi kuongezeka lakini ikiwa ni pamoja na mafunuo machache ya Mungu. Mungu alikuwa amemwahidi kwamba angemfanya kuwa “taifa kubwa” (Mwanzo 12:3). Waakati wake wa mwanzo wa kuishi katika hiyo nchi, Abramu alifikiria ni jinsi gani uzao wake ungepatikana kwa kuwa mke wake Sarai hakuwa na uwezo wa kuzaa watoto.
Akafikiria iwapo ahadi hii ya uzao ingeweza kutokana na mmoja wa watoto wa mtumishi wake Eliezeri (Mwa. 15:2-3). Mungu akamwambia na kusema ya kwamba uzao huo ungetoka katika viuno vya Ibrahimu mwenyewe (mstari 4), nao ungeongezeka hadi kuwa wengi kama nyota (mstari 5).
Pamoja na matatizo haya yote Ibrahimu alimwamini Mungu (mstari 6), yaani aliamini kwa sababu Mungu alikuwa amesema, na kwa hiyo angetimiza Neno lake (Waebrania 11:6). Kuhusu Abramu, aliamini kuwa Mungu yupo hakika. Alimwamini Mungu kwa ukamilifu, na kwa hiyo Mungu alimhesabia kuwa mwenye haki (mstari 6).
Mwanzo 21:13-22
ASILI YA AHADI YA UZAO (Mwa. 15-17)
Baada ya ushujaa wa Abramu kumwokoa Lutu, aliyekuwa mwana wa ndugu yake kutoka vitani kama ilivyoainishwa katika Mwanzo sura 14, Mungu alimwambia, “usiogope Abramu’. “Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana” (sura 15:1). Abramu mara moja akachukua nafasi ya kumwuliza Mungu jinsi ahadi ya uzao itakavyoweza kupatikana kwa kuwa hakuwa na mtoto. Je, inawezekana mzao huo azaliwe na mmoja wa watumishi wake? Hapana, jibu lilikuwa kwamba mzao huo angekuwa mtoto wake mwenyewe na alipoonyeshwa nyota za mbinguni aliambiwa, “ndivyo utakavyokuwa uzao wako” (mstari 5). Akiangalia uwingi wa nyota mbinguni na jinsi nyota zisivyoweza kuhesabika Abramu “akamwamini BWANA” naye Mungu akamhesabia jambo hili kuwa mtu mwenye haki. Jinsi imani hiyo na uthabiti ulivyo wa muhimu katika neno la Mungu, kwa wakati ambapo Abramu alifahamu wazi kabisa ya kwamba asingaliweza kwa njia ya kawaida ya asili kupata watoto wake mwenyewe.
Ili kuonyesha jinsi Mungu alivyokuwa na uhakika na Ahadi yake kwa Abramu, Mungu alifanya agano naye. Kama kwa mfano, Mungu alimwonyesha Abramu jinsi agano hilo litakavyothibitishwa kwa kutayarisha sadaka (sura 15:9-10). Sura hii inaonyesha kuwa mambo haya yangetimizwa baada ya kifo cha Abramu (mst 12). Mungu alimpatia Abramu unabii kwamba uzao wake watakuwa watumwa huko Misri na akaongeza maelezo ya kina kwa kuweka mipaka ya nchi ya ahadi (mstari 13-18).
Mwanzo 16 imeandikwa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Ishmaeli mwana wa Hajiri, mjakazi wa Sara. Hili lilikuwa jaribio la Sara la kutatua tatizo la ahadi ya uzao (Wagalatia 4:29). Abramu akaweka moyo wake kwa Ishmaeli akifikiri kuwa ndiye aliye uzao wa ahadi, lakini yeye ambaye ni uzao maalumu wa ahadi alikuwa azaliwe kwa mwujiza wa nguvu za Mungu, naye angekuwa mwana siyo wa Abramu pekee tu, bali wa Sarai pia, ambaye wakati huo asingeweza kuzaa watoto tena.
Miaka kumi na tatu ilipita kabla Mungu hajamtokea tena Abramu. Mungu akasisitiza tena uhakika wa agano na kwamba angeuzidisha uzao wake (sura 17:1,2). Jina lake likabadilishwa kuwa Ibrahimu, ili kuonyesha kwamba atakuwa baba wa mataifa mengi (mstari 4-8).
Kubadilika kwa jina lake kulifuatiwa na agano la tohara ambalo lingekuwa ishara ya agano. Kutahiliwa tu peke yake hakuna maana yoyote. Ilitumiwa na Mungu kuonyesha kwamba Ibrahimu alikuwa ni mtu aliyemwamini Mungu zaidi kuliko mambo yale yote ambayo mwili uliyahitaji, na hata katika nia ya kuwa na watoto (soma Warumi 4:11). Mtume Paulo amesema kwamba mtu amwaminiye Mungu na siyo nia ya mwili “yeye tohara yake ni ya rohoni” (linganisha na Warumi 2:28-29). Ibrahimu, kwa hakika aliyaacha mawazo ya asili ya kimwili, na kufuata mafundisho ya Neno la Mungu.
Hatimaye baada ya muda mrefu wakati uliwadia sasa wa kuzaliwa uzao wa ahadi, na Mungu akamwambia Ibrahimu ya kwamba Sara angezaa mwana, “Isaka” lenye maana ya “kicheko” au “furaha” (Mwanzo 17:15-22). Ibrahimu alikuwa na umri wa miaka 100 (naye Sara miaka kumi tu pungufu ya miaka ya Ibrahimu) wakati ambapo alimzaa mwana wa ahadi. Sara naye pia alionyesha imani katika Mungu naye akapata nguvu ya kuzaa mwana wa ahadi (Waebrania 11:11). Imani yao kubwa ilishinda lile linaloonekana kuwa haliwezekani kwa wanadamu (Warumi 4:17-22).
KATIKA ISAKA UZAO WAKO UTAITWA (Mwanza 21)
Nyumba ya Ibrahimu walikuwa “washiriki katika Agano” pamoja naye na walifurahi pamoja naye kwa ajili ya kuzaliwa kwa Isaka. Tunaweza kutafakari namna Ibrahimu na Sara walivyofurahishwa na baraka ya kupata huyu mwana maalumu wa ahadi. Lakini walikuwepo watu wawili ambao hawakufurahi: Hajiri na Ishmaeli (Mwanzo 21:9).
Wakati Sara alipofanya sherehe ya kumwachisha Isaka kunyonya,akamwona Ishmaeli akimdhihaki. Mungu akamwambia Ibrahimu kumwondoa Ishmaeli,''kwa maana'' Mungu alisema,“katika Isaka uzao wako utaitwa”(mstari 12).
MUNGU ANAMPIMA IBRAHIMU (Mwanzo 22:1-9)
Isaka akawa ndiye kiini cha upendo wa Ibrahimu na mrithi wa zile ahadi. Maisha ya Ibrahimu yalizingirwa na maisha ya mwanaye. Isaka alikuwa ni furaha ya wazazi wake, akaendelea kukua akiwa mwana mwaminifu na mtiifu. Siyo vigumu kufikiria matokeo ya maneno ya Mungu kwa Ibrahimu, “mchukue mwanao wa pekee Isaka … ukamtoe sadaka ya kuteketezwa” (mstari 2). Kumtoa mwana wa ahadi! Isaka mwanaye mpendwa lazima afe!
Mungu alikuwa akimtaka Ibrahimu kutii amri yake kwa gharama ya hisia zake za asili kwa mwanaye mpendwa. Jinsi ulivyo mtihani mkubwa! Kwa imani ya kushangaza aliamini neno la Mungu kuzidi hata aina yoyote ya upinzani wa asili wa mwanadamu. Akaamini kwamba hata kama Isaka angekufa, hapo Mungu, kwa ajili ya ahadi, angemfufua ili aishi tena. Imani kuu ya Ibrahimu ilikuwa sawa na wajibu wake. Jinsi ilivyokuwa ya kushangaza imani yake na jinsi alivyomwamini Mungu kwa ahadi zake!
Ibrahimu hakusita. Yeye na Isaka walisafiri hadi wakafika mlima Moria. Ibrahimu alikuwa na uhakika kwamba Isaka angefufuliwa tena. Alidhihirisha hilo kwa kuwambia watumishi wake, “mimi na kijana tutakwenda kule,tukabudu na kuwarudia tena” (Mwanzo 22:5) Ibrahimu na Isaka kwa matendo yao walikuwa ni mfano kwa kile ambacho Yesu na Babaye walifanya katika miaka ya baadaye. Tuone jinsi tendo la kumtoa Isaka sadaka linavyofanana na sadaka ya Mungu ya kumtoa Mwana wake mpendwa.
-
Mstari 2 – “Mwana wako wa peke umpendaye, Isaka.” (Yesu alikuwa ni Mwana peke wa Mungu –Mathayo 3:17)
-
Mstari 6 –Aliweka kuni juu ya Isaka (Yesu aliubeba msalaba wake –Yohana 19:17)
-
“Wakaenda wote wawili pamoja”(Yesu kwa hiari alishirikiana na Babaye Yohana 12:27-28; Waeb. 10:5-7)
-
Mistari 9 na 10-Isaka alijitolea mwenyewe kufanyika dhabihu kama vile Yesu alivyokubali kuwa sadakaa. Ingawaje Ibrahimu alizuiliwa asimchinje Isaka, hata hivyo Isaka alikuwa sawa na mtu aliyekufa katika ufahamu wa Ibrahimu. Mungu aliikubali nia ile sawa na tendo. Paulo anasema ya kwamba imani ya Ibrahimu ilikuwa katika uwezo wa Mungu wa kumfufua Isaka kutoka kuzimu “akampata tena toka huko kwa mfano”(Waebrania 11:19). Yesu aliwaambia Wayahudi kuhusu “kuinuliwa” (kusulibishwa) kwake (Yohana 8:23-28) alisema “Ibrahimu alishangilia kwa vile atakavyoiona siku yangu; naye akaiona akafurahi”(Yohana 8:6).
Kwa sababu ya imani yake kubwa na utiifu, Ibrahimu aliahidiwa ya kwamba Mungu angefanya yafuatayo:-
-
Angembariki
-
Angempatia uzao ambao atauzidisha;
-
Angefanya uzao wake kuwashinda adui zake;
-
Katika uzao wake mataifa yote ya dunia watajibarikia
Hii ahadi kubwa, Mungu aliithibitisha kwa kiapo, ikimaanisha kuja kwa Mwana Mkuu wa Ibrahimu atakayetawala akiwa mfalme wa dunia (linganisha na Wagalatia 3:16)
IMANI YA ABRAHAMU: FUNDISHO KWETU SISI.
Hiari ya Ibrahimu ya kumtii Mungu inaonyesha tabia ya imani ya Ibrahimu. Alijiweka tayari kumtii Mungu kwa mambo yote, hata kama ikibidi kwa kumchinja mwanaye,” “Maandiko yale yakatimizwa yaliyosema, Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa ni haki, naye aliitwa rafiki wa Mungu” (Yakobo 2:23).
Tunapolinganisha Mwanzo 15 na sura ya 22 tunaweza kuona namna imani ya Ibrahimu ilivyokua.Katika hatua za mwanzo alionyesha imani na tumaini katika ahadi ya Mungu ya kuhusu uzao (Angalia Warumi 4:3). Na hapa, katika Mwanzo sura ya 22 tunaweza kuona imani ya Ibrahimu inavyokomaa na kuwa kamilifu. Yakobo anasema kuwa twaweza kuona “kwamba imani ilitenda kazi pamoja na matendo yake, na kwamba imani ile ilikamilishwa kwa njia ya matendo”. (Yakobo 2:21-24). Imani yetu pia, inapaswa iwe zaidi kuliko kuamini tu pekee yake kwamba kuna Mungu mmoja.
Tunatakiwa kuonyesha kwa njia ya matendo katika maisha yetu ya kwamba tunamwamini Mungu na kumtegemea kila siku katika maisha yetu. Kwa kuwa Bwana Yesu Kristo alitawala, au aliongoza mawazo yake mwenyewe na matendo ili kwamba atii kwa ukamilifu mapenzi ya Babaye, ameahidi ya kwamba “utamiliki milango ya adui zake” Nasi inabidi kuongoza hivyo hivyo mawazo na matendo yetu. Tunaishi kati ya watu kule shuleni wanaoonyesha tabia ya utovu wa nidhamu na uasi. Kama tutamtii Mungu inatupasa kwa njia yoyote tuonyesha kwanza kuwa na kiasi.
Paulo anasema,na sisi pia, kama Ibrahimu, inatupasa kuendelea “toka imani hadi imani”- kukua katika imani hatua kwa hatua (Warumi 1:17). Na sisi pia tunaweza kuwa rafiki wa Mungu. Ufunguo ni kumfanya Mungu awe dhahiri katika maisha yetu. Inatupasa tumwone kana kwamba Mungu yupo karibu nasi kwa kila jambo tunalolitenda, tukiutafuta uongozi wake kwa uangalifu kutoka katika Neno la Mungu,kwa kumtegemea na kumtii yeye. Ni lazima “tutahiri mioyo yetu” kwa kuondoa tamaa za mwili na kuonyesha kufuata njia ya kweli kwa hiari kwa kubatizwa katika Yesu Kristo. Ndipo tutakapokuwa uzao wa Ibrahimu na warithi sawa sawa na ahadi (Wagalatia 3:29). Na kama tukitenda namna hii tutarithi pamoja na Ibrahimu mwenye imani, ahadi ya utukufu ya urithi wa milele katika nchi.
VITABU REJEA:
"The Story Of The Bible" (H. P. Mansfield)—Pages 96-127
"Elpis Israel" (J. Thomas)—Part 2, chapter 2
"The Visible Hand Of God" (R. Roberts)—Pages 64-67
"The Ways Of Providence" (R. Roberts)—Chapter 3 "Letter To The Hebrews" (J. Carter)—Pages 139-146
MASWALI YA AYA:
-
(a) Ibrahimu alihangaishwa na kuzaliwa kwa uzao wa ahadi: Je, alikuwa azaliwe na mmoja wa watumishi wake?
-
Onyesha jinsi imani ya Ibrahimu ilivyokuwa kubwa katika ahadi za Mungu wakati alipoonyeshwa nyota za mbinguni.
-
Kwa nini jina la Abramu lilibadilishwa na kuwa Ibrahimu?
-
Wakati Mungu alipomwambia Ibrahimu kumtoa sadaka Isaka, mwitikio wa Ibrahimu ulikuwa upi?
-
Ni kwa jinsi gani tendo la Ibrahimu la kumtoa sadaka Isaka lilikuwa
sawa na tendo la Mungu kumtoa sadaka Mwana wake?
-
Ni baraka gani kubwa ambazo Mungu alimwahidi Ibrahimu baada ya
kuitikia kwa hiari kumchinja Isaka?
MASWALI YA INSHA:
-
Ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Onyesha namna Imani ya Ibrahimu katika ahadi hizi ilivyoweza kupimwa kwa miaka mingi kabla ya Isaka kuzaliwa.
-
Fafanua ni nini kilitokea na eleza maana ya tendo la Ibrahimu la kumtoa Isaka sadaka.