137. YAKOBO ANAKWENDA UHAMISHONI NA KURUDI
Esau hakunyenyekeshwa na tendo lile alilotenda bali akatishia kumwua Yakobo wakati Isaka atakapokufa. Rebeka aliambiwa kuhusu mpango wa Esau. Akifuata ushauri wa mama yake, Yakobo akakimbilia upande wa kaskazini huko Padan-aramu ambako angepatiwa hifadhi na ndugu wa mama yake.
Katika somo hili tunajifunza namna Mungu alivyo mwandaa Yakobo kuwa baba wa mataifa mengi.
Mwanzo 28-32
ISAKA ANAMBARIKI YAKOBO
Kabla hajamruhusu kuondoka,Isaka alimpa Yakobo ukamilifu wote wa ahadi ya Ibrahimu (Mwanzo 28:3-4). Ahadi hii ni pamoja na:-
-
Mungu ambariki na amwongeze na kumzidisha
-
Uzao wake uwe mkutano wa makabila;
-
Airithi nchi ya kusafiri kwake, “ambayo Mungu alimpatia Ibrahimu”.
Kama vile baba zake, Yakobo alikufa pasipo kuzipokea ahadi kamilifu. Lakini Mungu atakuwa mwaminifu katika Neno lake. Atawafufua kutoka kwa wafu na kuwastarehesha katika nchi ya ahadi, katika nchi ambayo wao walikuwa wageni (Luka 13:28).
NDOTO KATIKA BETHELI (Mwanzo 28:12-22)
Ingawa Yakobo alitenganishwa na mamaye na kujihisi mpweke mno katika safari, Lakini Mungu alikuwa pamoja naye. Alipolala usiku ule pale Betheli, alipata ndoto ya maana sana. Lilikuwa ndilo tukio la kwanza ambapo Yakobo aliisikia sauti ya Mungu.
Mungu kupitia kwa malaika wake alimhakikishia Yakobo ya kwamba atakuwa naye na pamoja na uzao wake.
-
Kutimiza ahadi alizompa Isaka na Ibrahimu na
-
Kumrudisha tena katika myumba ya Baba yake.
Yakobo alifurahi sana. Akapaita mahali pale “Betheli” maana yake “Nyumba ya Mungu” na kutamka nia yake ya kumtumikia Mungu kwa uaminifu katika maisha yake yote (mstari 18-22).
YAKOBO AKIWA UHAMISHONI (Mwanzo 29,30)
Yakobo hatimaye alifika Harani na kukaa katika nyumba ya Labani, kaka wa mama yake. Yakobo akampenda Raheli, binti mdogo wa Labani na akakubali kumtumikia Labani muda wa miaka saba kama mahari ya kumwoa awe mke wake.
Baada ya kutumika muda wa miaka saba kwa ajili ya Raheli, Yakobo alidanganywa na Labani akapewa binti yake mkubwa Lea, ili amwoe. Bila shaka hili lilimkumbusha Yakobo kwa upande wake jinsi alivyomdanganya baba yake, Isaka. Yakobo ilimpasa ajifunze jinsi uongo wake ulivyokuwa mbaya kwa kweli. Kwa majaribu haya na matatizo Mungu alitaka tabia yake ipate mtihani na kukuzwa ili kwa moyo wake wote amtegemea Mungu. Kama alivyomdanganya Isaka, ndivyo pia Labani alivyomdanya yeye katika matukio mengi.
Siku saba baadaye, aliruhusiwa kumwoa Raheli kwa sharti la kumtumikia Labani tena miaka saba zaidi. Inatupasa kuzingatia kuwa Yakobo alikaa kule Harani jumla ya miaka 40 (sura 31mstari 38-miaka 20 pamoja na Labani akiwa rafiki yake: sura 31 mstari 41- miaka 20 akitumika kwa ajili ya mshahara). Muda huu wa miaka 40 unapatana na vipindi vingine vya historia ya Israeli.
Ndipo Yakobo alipotulia kujenga jamii yake na mifugo. Ni wazi kutokana na matukio ya baadaye kwamba akili yote ya Yakobo ilijikita katika ahadi za Mungu. Mawazo yake yaliendelea kufiria siku ambayo angerudi katika nchi yake, sura ya Mwanzo 31:36-42 inamfunua Yakobo kuwa mfano kwetu sisi sote kwamba alikuwa mtu aliyefanya kazi kwa bidii mchana na usiku naye alikuwa mwaminifu “hata kwa mabwana (au waajiri) wabaya”.
YAKOBO ANARUDI KWAO (Mwanzo 31:22-55)
Moyo wa Yakobo ulikuwa katika nchi ambayo Mungu alimwahidi, naye alitamani sana kurudi. Labani alimsihi Yakobo abaki na amtumikie kwa ujira (malipo au mshahara), lakini baada ya miaka sita ya kkutumika, Yakobo akaazimia kuondoka (Mwanzo 31:3-5). Mara mbili Mungu alimtokea na kumshauri aondoke. Lakini Yakobo alielewa kwamba Labani angekasirika kwani alikuwa mtu mchoyo.
Siku moja wakati Labani akiwa mbali na kondoo zake, Yakobo aliondoka. Yakobo alikuwa ashamefika mbali mbali kabla ya Labani kutambua kwamba Yakobo na wake zake na wanawe walishaondoka. Labani kwa haraka akawafuata, lakini wakati akimfuata Mungu alimtahadharisha asimdhuru Yakobo au asijaribu kumdanganya tena. Hatimaye alipowafikia, watu hawa wawili walifanya agano la amani na kujenga mnara wa mawe wa ukumbusho kuwa ushahidi kwa mapatano yao.
Labani akarudi nyumbani, na Yakobo akageuka tena kuelekea Kanaani, na akiwa na hofu nyingine rohoni mwake: utisho wa kumwogopa Esau.
YAKOBO ANAJIANDAA KUKUTANA NA ESAU (Mwa. 32:1-23)
Mungu alimpa Yakobo sababu ya kutegemea ulinzi wake kwani alipeleka kikundi cha malaika ili kukutana na Yakobo. Lakini fundisho hilo liliondoka mara moja akilini mwa Yakobo. Alifadhaika kabisa alipofahamu kwamba Esau alikuwa anakuja kuonana naye pamoja akiwa na watu 400!
Angefanya nini? Yakobo, kwa shinikizo alionyesha hofu na akawa katika dhiki akiandaa njia ambayo ni suluhisho la kumtuliza nduguye mwenye hasira, huku akimwomba Mungu kukumbuka ahadi zake alizomwahidi. Akagawanya mifugo yake akapeleka baadhi mbele yake ziwe zawadi kwa Esau. Kisha akamwomba Mungu kwa bidii kwa ajili ya wokovu ambao alifahamu ni Mungu pekee angaliyeweza kumpatia (mstari 7-12).
Kisha naye alifuata mwishoni pamoja na familia yake (mstari 22) naye alipokuwa karibu kuwafuatia ng`ambo ya mto Yaboki usiku ule , alikutana na “mtu” (mstari 24)
YAKOBO ANASHINDANA MWELEKA NA MALAIKA (Mwanzo 32:24-32)
Usiku kucha yule malaika alitafuta jinsi ya kujiondoa kutoka mikononi mwa Yakobo ambaye alikuwa amemshikilia. Kwa nguvu zote Yakobo alimng’ang’ania: Alielewa kwamba kuendelea mbele bila msaada wa malaika isingefaa chochote. Malaika akaonyesha uwezo mkuu ambao unazidi nguvu za mwilii wa mtu kwa kugusa sehemu ya nyonga na “kuitengua”. Hata hivyo Yakobo aling’ang’ania: “sitakuachia uende mpaka unibariki”. Yakobo alikuwa peke yake na hakuwa na uwezo wa kukimbia kutokana na kuguswa na malaika. Katika huo udhaifu wake na wasiwasi kwa ajili ya baraka za Mungu kupitia kwa malaika, Yakobo akaonyesha imani iliyotakaswa kutokana na mateso. Nabii Hosea anasema kuwa ndio wakati Yakobo alipokuwa na nguvu. Mungu alimwita mwenye nguvu kwa vile imani yake sasa ilijikita ndani ya Mungu tu basi. Alifikia uamuzi wa kumtegeemea Mungu na siyo werevu wake (Hos. 12:3,4).
Yakobo akatambua kwamba Mungu alikuwa amemtokea kupitia kwa malaika yule na hivyo akapaita mahali pale Penueli, “uso wa Mungu”. Lakini hata hivyo ilimpasa kuonana na Esau pamoja na watu wake 400. Akaweka familia wake nyuma yake kwa usalama wao na kuinama mpaka nchi mbele ya Esau mara saba. Kwa mshangao wake mkuu Esau akamkimbilia na kumkumbatia na kumbusu nduguye. Wote wawili wakalia kwa furaha. Esau pia alikuwa tajiri sana wala hakuhutaji zawadi zilizopelekwa na Yakobo; lakini akazipokea kwa neema nao wakafanya amani kati yao. Tatizo lilikuwa limekwisha, Yakobo akaendelea mbele na akafika Shekemu kwa “amani”. Zingatia kwamba Mwanzo 33:18 inasema “Shekemu” maana yake “amani” na itafsiriwe hivyo katika mstari huu.
Kwa hiyo Mungu alitimiza kiapo alichomwapia; Yakobo naye akawa “Mungu wake”. (soma Mwanzo 28:16-22). Kwa kuangalia nyuma juu ya matukio haya, Yakobo aliweza baadaye kusema, “Mungu, ambaye baba zangu Ibrahimu, na Isaka walienenda mbele zake, yeye Mungu aliyenilisha maisha yangu yote, hata siku hii ya leo, naye Malaika aliyeniokoa na maovu yote...” (Mwa. 48:15,16)
FUNDISHO KWA AJILI YETU
-
Habari hii inaonyesha upendo wa Mungu na ulinzi wake kwa Yakobo na familia yake. Ulinzi huo huo upo kwetu sisi pia. Mkono wa uongozi wa Mungu, ingawa hauonekani, unayaongoza maisha yetu, kama vile ulivyofanya kwa watu wa Mungu siku zilizopita. Badala yake tuonyeshe upendo na tumaini letu kwa ajili ya shukrani yetu.
-
Tabia ya Yakobo ya uaminifu alipokuwa uhamishoni ilimletea baraka yeye mwenyewe na kwa Labani. Akaja kumtegemea Mungu kwa wokovu kutokana na maovu yaliyomkabili. Kukua kwake na kumtegemea Mungu kwa moyo wake wote ilionyeshwa wakati imani yake iliposhinda wakati wa kushindana mweleka na malaika. Baada ya kukiri kwamba asingeweza kujiokoa mwenyewe kutokana na tatizo lililomkabili, Yakobo kwa bidii kuu alihitaji msaada wa Mungu. Na sisi pia tunahitaji kuacha mipango na mbinu zetu wenyewe na bora zaidi kutafuta njia zake Mungu ziwe mwongozo wetu maishani.
VITABU REJEA:
"The Story Of The Bible" (H. P. Mansfield)—Pp. 151-176
"Ways Of Providence" (R. Roberts)—Chapters 5-7
"Elpis Israel" (J. Thomas)—Pp. 270-274
"Christadelphian Instructor"—Questions and Answers Nos. 139-145
MASWALI YA AYA
-
Ni kiapo gani Mungu alimwapia Yakobo kule Betheli? Je, kilitimizwaje?
-
Je, ni fundisho gani alilojifunza Yakobo kutokana na mateso yake, taabu na udanganyifu wake mkononi mwa Labani?
-
(a) Kwa nini Yakobo alishindana mweleka na malaika?
(b) Tukio hili linafunua nini kuhusu tabia ya Yakobo kwa Mungu?
MASWALI YA INSHA
-
Eleza jinsi Yakobo alivyojifunza kumtegemea Mungu.
-
Yakobo alidanganywaje na Labani? Ni mafundisho gani tunayojinza kutokana na uzoefu wa Yakobo?
-
Elezea, Yakobo alivyoshindana na Malaika na uonyeshe ni kwa nini jina lake lilibadilishwa kuwa Israeli