138. MITIHANI (MAJARIBU) NA USHINDI WA YUSUFU HUKO MISRI
Habari za maisha ya Yusufu ni “mfano” (aina – ni sawasawa - soma somo la 14) kuhusu Bwana Yesu Kristo na ukombozi ambao atautoa. Yusufu alikwenda Misri ili “kudumisha uhai” na kuna faida kuu katika ukilinganisha na mambo yote yaliyochomtokea na kazi ya Kristo.
Somo hili linashughulikia historia ya maisha ya Yusufu na kanuni ambazo tunaweza kujifunza kutokana na somo hili. Somo la 14 litaonyesha namna maisha ya Yusufu yalivyoelekeza mbele kwa Yesu Kristo.
Mwanzo 37-45
UKOO (FAMILIA) YA YAKOBO
Yakobo alikuwa na wana kumi na mbili na binti mmoja, Dina (Mwanzo 29:31;30:24; 35:16-18). Wanawe walikuwa:-
-
Wana wa Lea: Reubeni, Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari na Zabuloni
-
Wana wa mjakazi wa Lea (Zilpa): Gadi na Asheri
-
Wana wa Mjakazi wa Raheli (Bilha): Dani na Naftali
-
Wana wa Raheli: Yusufu na Benyamini
Kutokana na wana hawa kumi na mbili wa Mungu yaliinuka makabila kumi na mbili ya Israeli.
Walikuwa wachungaji na wakichunga kondoo za baba yao. Baadhi yao walikuwa wenye kujipenda, wapotofu. Yusufu alionewa wivu na nduguze kwa sababu baba yao alikuwa akimpenda kuliko wao. Yusufu alipopata joho yenye rangi nyingi kutoka kwa baba yake, ambayo ilionyesha kwamba alipendwa zaidi kuliko ndugu zake, wivu wao uligeuka kuwa chuki. Hata hivyo, Yusufu alikuwa amethibitisha kuwa mwenye kustahili heshima hiyo kutokana na upendo aliompa Mungu na Yakobo.
USALITI WA NDUGU ZAKE (Mwanzo 37:5-36)
Yusufu alikuwa na umri wa miaka kumi na saba, Mungu alimfunulia ndoto mbili (Mwanzo 37:5-11) ambazo zilionyesha kwamba babaye, mamaye na ndugu zake wangemsujudia hata nchi. Hili liliwafanya nduguze wakasirike na kuzidisha chuki kwake.
Chuki hii ikawa kubwa sana,wakati Yakobo alipomtuma Yusufu, kuwatembelea nduguze sehemu waliyokuwa wakichungia kondoo wao huko Shekumu, wakakusudia kumwua mistari 12-20.
Kwa ushauri wa Reubeni walimtupia shimoni. Rubeni alikuwa amepanga kumwokoa baadaye, lakini kabla hajaweza kufanya hivyo, msafara wa Waishmaeli ulipita hapo. Nduguze wengine wakamwuuza Yusufu kwao kwa vipande ishirini vya fedha. Nao Waishmaeli kwa upande wao wakamwuza kama mtumwa nchini Misri. Nduguze kisha wakafanya mpango wa kumdanganya baba yao. Wakachovya kanzu ya Yusufu katika damu na ili Yakobo afikirie mwanae mdogo kuwa alikuwa ameuawa na wanyama wa porini. Yakobo akaendelea kumlilia mwanaye mpenzi na akakataa kutulizwa. Wanawe hawakumpunguzia majonzi yake kwa kukiri uovu wao wa uongo. Walikuwa na mioyo- migumu nao wakamwacha Yakobo asikitike akiamini kuwa kweli mwanaye alikufa.
Mfikirie Yusufu, akiwa na umri wa miaka kumi na saba tu, ghafla anajikuta mtumwa huko Misri. Lakini hata katika upweke wake na kazi magumu hakukata tamaa. Chini ya maisha ya kazi ngumu mno na bila shaka mara nyingi akijihisi mpweke aliyechukuliwa kutoka kwa baba na ndugu zake, Yusufu aliweka imani yake katika Mungu na katika kutimiza ndoto zake.
NCHINI MISRI – MAJARIBU (Mwanzo 39:40; 41: 1-36)
-
Anauzwa kwa Potifa – Mwanzo 39:1-20
Potifa, akida (afisa) wa Farao, alimnunua Yusufu. Alimwona kuwa mtu mwenye busara, mwaminifu na mwenye bidii- hivyo akampandisha cheo kuwa na madaraka ya Mkuu wa nyumba yake. Yusufu akapendwa na mke wa Potifa ambaye hakuwa mwadilifu na akajaribu kumtaka kimapenzi. Yusufu alikataa kushindwa na dhambi na mwishowe ilimbidi akimbie akitoka mbele ya Yule mwanamke ili kumwempuka. Huyu mke mwovu akamzushia Yusufu mashitaka ya uongo kwa bwana (mwajiri) wake ambaye alimtupa gerezani.
-
Ndoto za Mnyweshaji na Mwokaji wa mikate- Mwanzo 39:21-23;40
Yusufu angeweza kufikiria kuwa ametendewa vibaya lakini hakujionyesha. Mara moja mkuu gereza akamtambua kuwa ni mtu mwaminifu na mcheshi. “BWANA alikuwa naye Yusufu”. Ndipo akawekwa kuwa mkuu wa wafungwa wote. Kwa njia hii akakutana na mnyweshaji wa Farao na mwokaji wa mikate ambao walikuwa wametupwa gerezani. Uaminifu wa Yusufu katika kipindi hiki kirefu cha mateso ulimtayarisha kwa ajili ya madaraka ambayo Mungu alikuwa amemwekea. Kwa msaada wa Mungu aliweza kutafsiri ndoto za yule mnyweshaji na yule mwokaji wa mikate. Maneno yake baadaye yakatimia kikamilifu. Yule mwoka mikate aliuawa lakini mnyweshaji akarudishwa tena katika kazi nyumbani mwa Farao. Akielewa kuwa haya yangetokea Yusufu akamsihi yule mnyweshaji kumkumbuka, lakini yule mnyweshaji akamsahau Yusufu, akimwacha Yusufu kutumia miaka mingine miwili gerezani.
-
NDOTO ZA FARAO (Mwanzo 41:1-36)
Ilikuwa wakati Farao alipopata ndoto mbili za ajabu na za kutisha sana, ndipo yule mnyweshaji alipomkumbuka Yusufu. Aliitwa haraka kutoka gerezani na kunyolewa nywele na kuvaa nguo nzuri, Yusufu akapelekwa mbele ya Farao. Yusufu alieleza waziwazi kwamba aliweza kutafsiri ndoto kutokana na nguvu za Mungu. Yusufu akamjulisha Farao maana ya ndoto zile. Kutakuwa na miaka saba ya wingi wa mavuno ikifuatiwa na miaka saba ya njaa. Kupitia kwa Yusufu, Mungu alimwonya Farao aweze kuweka akiba ya chakula ambacho kingetumika wakatia wa miaka saba ya njaa.
-
HUKO MISRI- ANASHINDA (Mwanzo 41:37 mpaka sura 45)
Mtawala huko Misri –Mwanzo 41:37-52
Yusufu kwa msaada wa Mungu akawa na hekima sana hata Farao alimweka kuwa kiongozi mkuui wa pili katika nchi. Alikuwa ndiye Waziri Mkuu wa Misri. Alipewa kazi ya kuwa mwangalizi wa ukusanyaji wa chakula cha akiba kwa ajili ya njaa ambayo ilikuwa inakuja .
Akaonyesha uaminifu wake na bidii yake vile vile kama alivyoonyesha nyumbani kwa Potifa na gerezani. Hakuruhusu cheo cha juu kudhoofisha imani yake kwa Mungu, lakini akakumbuka wakati wote kwamba Mungu alikuwa na kusudi katika kumleta yeye nchini Misri.
Kutokea muda ambao Yusufu aliuzwa utumwani akiwa na umri wa miaka kumi na saba (Mwanzo 37:2) mpaka wakati aliposimama mbele ya Farao (Mwanzo 41:46) miaka kumi na tatu ilikuwa imepita. Sasa alikuwa tayari kwa kazi kubwa ambayo Mungu alikuwa amemwandalia. Katika miaka yote hiyo wakati kijana Yusufu alipokuwa akiteseka kwa maumivu ya moyo na kufadhaika kwa mawazo aliweka kabisa imani yake kwa Mungu wake. Jinsi alivyo mfano bora kwetu sisi wote katika ujana wetu! Nasi tudumishe imani yetu katika Mungu tunapokabiliana na vikwazo vyovyote katika maisha
.
-
Anatembelewa na ndugu zake –Mwanzo 42.
Miaka ile ya wingi wa mavuno ikaja na kupita. Njaa ikaanza na kuenea juu ya nchi zote za mashariki ya kati. Watu wakaja kutoka mbali kununua nafaka. Huko Kanaani Yakobo aliwaagiza wanawe wakubwa kumi waende Misri kununua nafaka. Akambakiza Benyamini nyumbani akihofia kwamba chochote kingaliweza kutokea kumwondolea uhusiano wa mwisho na Raheli (ambaye alikuwa ndiye mama yake Yusufu na alikuwa amekufa wakati akimzaa Benyamini).
Hivyo siku moja ndugu zake Yusufu wakatokea mbele yake na kumwinamia hadi nchi, bila kumtambua Yusufu. Ndipo Yusufu sasa alitambua ni kwa nini Mungu alikuwa amemwinua. Baada ya miaka yote hiyo, hapa walikuwa wakitimiza bila kuelewa masharti ya ndoto walizozichukia mno! Yusufu akakusudia kuwapima ndugu zake na kuwafundisha somo.
Akawatuhumu, kupitia kwa mtafasiri, kuwa wao walikwa wapelelezi na kuwaweka mahabusu kwa muda wa siku tatu. Kisha akaamrisha kuwa mmoja wao afungwe na bakie gerezani na wengine warudi kwao.
Simeoni aliyefungwa angefunguliwa ikiwa safari inayofuata watamleta Benyamini. Fikiria mshituko wao, wakati, wakiwa njiani kurudi, wakagundua kuwa fedha zao zilikuwa zimerejeshwa kwenye mifuko (magunia) yao! Yakobo alikasirika sana kwa sababu walimweleza “mtawala” wa Misri kumhusu- Benyamini. Alikataa kuwaruhusu kumchukua Benyamini isijemtokea hatari naye pia, kama alivyoamini ile hatari iliyomtokea Yusufu.
-
Safari ya Pili – Mwanzo 43; 44:1-13
Ukosefu wa chakula ulilazimisha uamuzi juu ya Yakobo. Yuda,ambaye kabla alikuwa mbele mbele katika kumwuza Yusufu utumwani, sasa alimhakikishia kuwa Benyamini atarudi salama na akaonyesha wema kwa baba yake.
Kwa hiyo wakaondoka kwenda Misri wakiwa pamoja na Benyamini, na wakiwa na fedha mara mbili na sala ya Yakobo: “Mungu Mwanyezi na awape rehema mbele usoni pa mtu yule” (Mwanzo 43:11-14). Katika Misri matukio ya ajabu yaliwangojea,hawakutakiwa kufikiria kuhusu kurudisha fedha walizokuwa wamewekewa. Walifadhiliwa kwa wema , wakatayarishiwa tafrija (sherehe), wakati ambapo Benyamini alipewa mara tano zaidi kuliko ndugu mwingine, nao wakaketishwa kufuatana na umri wa miaka yao. Wakishangazwa na heshima kuu waliyopewa, wakajaziwa mifuko yao ya nafaka na wakaondoka pamoja na Simeoni ambaye aliachiwa.
Fikiria hisia zao zilikuwaje wakati mtumisuhi wa Yusufu alipowafikia na kuwatuhumu kuiba kikombe cha kunywea divai mtawala! Walikuwa wanaonja sehemu kidogo ya maisha magumu na maumivu ya moyo ambayo walikuwa wamewapatia Yusufu na Yakobo. Kikombe kilipatikana, mahali pa siri alipokificha yule mtumishi katika mfuko wa Benyamini! Benyamini akakamatwa na kwa mshituko na kushangazwa kabisa ndugu wote wakalazimika kurudi na kuikabili hasira ya wazi ya yule mtawala.
-
YUSUFU ANAJITAMBULISHA MWENYEWE -Mwanzo 44:13-sura 45
Akijibu hukumu ya Benyamini, kwa kosa lake, kuwa ilimbidi afanyike mtumwa wake, Yuda alimwomba amwachilie Benyamini (Mwanzo 44:18-34). Kwa namna Yuda alivyoeleza kuhusu upendo wa mzazi ambao uliwaunganisha wana familia pamoja na hasa hasa pendo ambalo Yakobo alikuwa nalo juu ya mwanaye wa mwisho, Benyamini, moyo wa Yusufu ulilipuka kwa hisia juu ya ndugu zake. Hakuweza kuvumilia kuficha hisia zake zaidi. Aliwaondoa Wamisri wote, wakatoka nje, akalia kwa sauti kuu, “Mimi ni Yusufu…” Nduguze wakatishika na kudhani angelipa kisasi juu yao. Yusufu akawahakikishia usalama, na akawatia moyo kurejea nyumbani upesi na kumleta baba yao na familia yote kuja Misri.
KUSUDI LA MUNGU LAFUNULIWA – Mwanzo 45:4-13
Hatimaye upeo wa juu kabisa wa matukio ya maisha ya Yusufu ulikuwa umefika. Akawaeleza kwa uangalifu ndugu zake kwamba ilikuwa ni wingi wa rehema ya Mungu na kutoshereza kwake mahitaji kwa watu aliyeongoza matendo yao na matendo yake. Kupitia katika orodha kubwa ya matukio yaliyokuwa yakifuatana kwa mfululizo Mungu alikuwa ameleta mkombozi kutoka katika kifo, mgawaji wa chakula wakati wa shida; mwenye kuhifadhi uzao wa Ibrahimu. Katika matukio hayo Mungu alikuwa amebadilisha tabia zao ili waweze kustahili heshima kubwa ili Mungu awafanye wao kuwa taifa (Mwanzo 45:7).
Aliposikia habari hizi, Yakobo alijawa na furaha kubwa mno. ingawaje alikuwa mzee na dhaifu, alijitia nguvu katika Mungu wake ili aweze kuungana na Yusufu. Alipofika Misri, Yusufu alimtambulisha Yakobo kwa Farao ambaye kwa ukarimu alimpa nchi ya Goshemi ili aishi huko. Yakobo alikuwa amepata uzoefu wa kutosha kuhusu ukweli wa msemo ya Paulo aliyesema kwamba Mungu “anaweza kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo” (Waefeso. 3:20- linganisha Yuda 24,25)
MAKTABA YA REJEA
“Tumaini la Israeli” (J. Thomas) – Ukurasa 277-278
“Njia ya Mungu ya kutosheleza mahitaji” (R. Roberts) – Sura 8
“Yusufu na Ndugu zake” (P. pickering) –C.S.S.S. Maelezo ya kujifunza.
“Historia Biblia” (H.P. Mansfield) pp. 141-150
MASWALI YA VIFUNGU
-
Eleza jinsi ndugu wa Yusufu walivyomkamata na kumuuza utumwani.
-
Onyesha jinsi Mungu alivyomsaidia Yusufu alipokuwa mtumwa nchini Misri.
-
Ni lipi lilikuwa kusudi la Mungu katika kulinda uhai wa Yusufu huko Misri?
MASWALI YA INSHA
-
Eleza namna Mungu alivyokuwa na Yusufu, na kwa nini.
-
Eleza ndoto mbili za Yusufu na ufafanue jinsi zilivyotimia. Ni lini ndoto yake ya pili itatimia kabisa?
YUSUFU ANAUZWA HUKO MISRI
-
Yakobo anamtuma Yusufu kwenda kuwaona ndugu zake waliokuwa wakichunga kundi la kondoo kule Shekemu (Mwanzo 37:12-14
-
Yusufu alipofika Shekemu, akaambiwa kuwa ndugu zake wako Dothani (Mwanzo 37:15-17)
-
Kwa ajili ya chuki, Yusufu anavuliwa kanzu na zake na wanamtupa shimoni (Mwanzo 37:18-24)
-
Yusufu anauzwa kuwa mtumwa kwa Waishmaeli wafanya biashara waliokuwa wanatoka Gileadi, ambao walimpeleka Misri (Mwanzo 37:25-28)
-
Ndugu zake wakarudi kwa Yakobo wakiwa na kanzu ya Yusufu, ikiwa na damu nyingi, wakamdanganya Yakobo kuwa ameliwa na wanyama mwitu.