144.WANATUNZWA NA MUNGU KATIKA JANGWA
Wana wa Israeli walikuwa katika msisimko mkubwa. Walikuwa njiani wakirudi kwenda nchi ya baba zao! Lakini hawakuwa wamejiandaa vizuri sana, na walitakiwa wafanye juhudi kubwa kwa ajili kuwa katika makundi ya familia. Safari ilikuwa ndefu na ngumu nayo iliijaribu imani yao. Kama Israeli wa zamani, tunaelekea kujihurumia wenyewe mambo yanapokwenda tofauti na jinsi tulivyotarajia katika mambo yetu au inapoonekana kuwa ngumu. Ingawa wana wa Israeli walinung’unika kwa uchungu wakati fulani, Upendo wa BWANA haukuwaacha kamwe. Aliwapa Manna ya kutosha kwa ajili kula, akawalinda kutokana na maadui zao na kuwaleta kwake kule mlima Sinai.
Kutoka 15-17
MAJI YA KUNYWA (Kutoka 15:22-27)
Wakiwa huru sasa kutoka katika utumwa wa Misri, watu hao wakaongozwa na Musa kuelekea kusini kwenda Mlima Sinai. Walitakiwa wapite jangwa la Shuri ambalo lilikuwa eneo linalochokesha sana, jangwa ambalo ni kame lenye miinuko mirefu ya vilima vya mchanga. Walitakiwa “wathibitishwe” ili kujua yaliyokuwa ndani ya “mioyo yao”, kwa ajili ya “kuwanyenyekeza” ili wajifunze kumtegemea kabisa Mungu na Neno lake. Hilo ndilo lilikuwa kusudi la kuzungukazunguka jangwani (Kumbukumbu la Torati 8:2). Kwa muda wa siku tatu walitembea mwendo mrefu na wa kuchosha bila ya kupata maji hata kidogo. Hatimaye wakafika Mara ambapo palikuwa na chemchemi.
Lakini Mara maana yake ni “uchungu” na hiyo ndiyo ilikuwa hali ya maji yale- yasiyoweza kunyweka! Watu wakakasirika na kumnung`unikia Musa wakasema, “Tutakunywa nini?”
BWANA akawapatia watu ishara ya kushangaza ya kuwalinda watu wake kwa ajili yao aliposababisha maji yale kunyweka wakati tawi la mti lilipotumbukizwa ndani ya maji hayo. Huu ni “mfano” wa Kristo ambaye aliuawa ( aliposulibiwa) alifanya uchungu wa dhambi ya mwanadamu kuwa mtamu kwa kuwapatia/ tumaini la wokovu. Mungu angeweza na aliweza kuwatunza watu wake katika majaribu yao yote. Zaidi ya yote ni kwamba aliwaahidi baraka ikiwa watatii Neno lake. Aliwaahidi uhuru kutokana na magonjwa ya Misri iwap:-
-
Watamsikiliza Mungu
-
Watafanya yaliyo sawa machoni pake.
-
Watazifuata Amri zake na kutunza sheria zake (mstari 26)
Kisha watu hao wakaendelea na safiri wakafika Elimu ambako waliburudishwa na hali ya kupendeza ya sehemu hiyo maana palikuwa na visima 12 vya maji matamu yakizungukwa na miti ya mitende 70. Hili linawakilisha Ufalme wakati mataifa yote (mitende 70) yatapokusanyika kuzunguka makabila kumi na mbili ya Israeli.
NYAMA ZA KULA (Kutoka 16)
Kusanyiko hilo kubwa la Waisraeli sasa liliingia jangwa la Sinai. Tabia ya nchi ilibadilika. Milima mikubwa ya mawe makubwa yaliyochongoka kwenda juu, na watu wakalazimika kupitia kwenye makorongo mengi yenye kupindapinda. Huko walitembea kwa taabu sana na mawasiliano yalikuwa ya shida na chakula chao kilikuwa kinaendele kupungua. Licha ya kuwepo ile nguzo ya wingu juu yao, iliyokuwa ishara ya uwepo wa Mungu, hata hivyo walijihisi kuwa wamepotea na wakafadhaika.
Wakaanza kunung’unika. Wakatamani vyungu vyenye nyama na wingi wa mikate walivyokula katika Misri, wakasahau kabisa maumivu ya uchungu mkubwa wa utumwa wao. Angalia “mmetutoa huko” katika mstari 3. Wakawalaumu Musa na Haruni kuwa ndio waliosababisha hayo matatizo yao. Mungu akasema kupitia kwa Musa kwamba ni yeye aliyewaleta kule na sasa angewaonyesha tena nguvu zake kubwa na ulinzi wake. Mungu angewapatia nyama na mikate ili wale.
Jioni ile watu hao wakaona mwujiza. Makundi mengi ya kwale wakaja kambini na watu waliweza kuwakusanya kwa ajili mlo.
Asubuhi iliyofuata baada ya jua kuchomoza na umande ulipokuwa umekauka, ardhi ilijaa kitu cheupe, kidogo na cha mviringo. Watu wakasema, “Hiki ni nini?” (yaani “mana”) tazama pembezoni mst.15).
Musa aliwaambia kwamba hicho ndicho Mungu alichowapatia kwa ajili ya mahitaji yao. Walitakiwa wakusanye cha kuwatosha kwa ajili ya familia zao kila siku na kutumia chote. Hakingekaa kikibakia. Kujaribu kufanya hivyo baadhi waliona kuwa kiliibua minyoo na kunuka. Wakakiri katika siku ya sita waliruhusiwa kukusanya mara mbili na kukitunza kwa usiku huo kwa kuwa mana isingekuwepo siku ya Sabato.
Haruni aliagizwa kuweka baadhi ya mana katika kopo la dhahabu na kuliweka ndani ya sanduku la Agano. Mana hiyo haikuoza, ingawaje baadaye sanduku lenyewe lilipotea (linganisha na Ufunuo 2:17). Mana hii isiyooza ilimwakilisha Kristo aliyefufuka ambaye sasa anaishi milele.
Wakati wote wa kuzungukazunguka kwao jangwani Mungu aliwalisha kwa manna ambayo ilisitishwa tu wana wa Iisraeli walipoingia katika nchi ya ahadi (Yoshua 5:12).
KUSHABIHIANA NA YESU KRISTO (Yohana 6:31-38)
Israeli walikula mana ili kuyaokoa maisha yao ya asili kutokana na njaa. Pia ilitayarishwa kuwafundisha masomo ya kiroho. Musa aliwafundisha kuwa “mtu hataishi kwa mkate tu, bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha BWANA” (Kumbukumbu la Torati. 8:3). Kwa hiyo walitakiwa,kulitafuta Neno la Mungu kama vile wakivyokuwa wakitafuta chakula chao cha cha asili kila siku (linganisha Mathayo 5:6) – kila siku kwa bidii.
Yesu baadaye alitamka ya kwamba alikuwa ndiye “mkate wa kweli”, maana mtu yeyote anayekula mkate anaopewa na Yesu ataishi milele. “Mkate” huu ni mfano aliouomyesha kwa kumpenda Mungu na kufanya mapenzi yake wakati wote. Tunatakiwa tuwe na “radha” ya Neno la Mungu. Kula na kutafuna mkate huu unatosheleza sana kuliko kula kipande kikubwa cha mkate wa asili (Isaya 55:1-3; Yohana 6:56-57). Kwa huo mkate anaotupatia Yesu tunaweza kuendelea kuishi kiroho na kuongezeka nguvu.
Waisraeli walitakiwa kukusanya mana kila siku, na kwa hiyo tunatikwa na sisi kusoma neno la Mungu kila siku.Mana iliwaweka hai muda wote walipokuwa katika kuzunguka zunguka jangwani na neno la Mungu litaweza kutuimarisha “utu wetu wa ndani” na kutupatia sisi uzima wa milele katika Ufalme wa Mungu. Waisraeli waliokula mana ni marehemu sasa, lakini Yesu alisema kwamba watakaokula ule “mkate wa kweli ushukao kutoka mbinguni” wataishi milele (Yohana 6:33,40,49).
Tunaweza kuutunza utu wetu wa ndani kwa kula chakula cha asili. Ili tuweze kuufikia ufalme wa Mungu tunahitaji kula kila siku chakula ambacho Mungu anatupatia –Neno la Mungu.
MAJI KUTOKA KWENYE MWAMBA (Kutoka 17:1-7)
Lile wingu liliendelea kwenda mbele nao watu wakalifuata mpaka walipofika Refidimu mahali lilipotulia – lakini sehemu hiyo hapakuwa na maji! Kwa mara nyingine tena Musa alipata malalamiko yao, naye kwa mara nyingine tena akayapeleka kwa Mungu kwa njia ya sala. Mungu akamwagiza Musa kwenda kwenye mwamba maalumu na kuupiga fimbo mbele ya Israeli wote. Musa akafanya hivyo na kwa mwujiza maji yakabubujika, nao wakanywa na kumaliza kiu yao.
Paulo anasema kwamba mwamba huu ulielekeza mbele kwa Kristo (1 Wakorintho 10:4). Yesu kwa kule kufa kwake ni kwamba “alipigwa” na Mungu. Lakini Mungu alimfufua, na matokeo yake, ni “maji” ya uzima yakatoka ndani yake yakibubujikia kwenda kwa mataifa yote (katika Injili). Wale wanaokunywa maji ya “kijito” hiki wataburudika kwa kuwa hawatakuwa na kiu tena na kuimarika katika safari yao ya jangwani (Yohana 4:14)
SHAMBULIO LA WAAMALEKI – NGUVU YA SALA (Kutoka 17:8-16)
Ghafla Israeli walikabiliana na hatari mpya. Pale Refidimu walishambuliwa kutokea nyuma yao na Waamaleki waoga (Kumbukumbu la Torati 25:17-18)
Musa akamteua Yoshua kuwa Mkuu wa jeshi ambalo alilipeleka kupigana na adui. Waisraeli hawakuwa na ujuzi wa vita na kwa kweli kama Mungu asingewasaidia wangeshindwa. Musa akamchukua Haruni na Huri hadi kwenye sehemu ya mwinuko ambapo waliweza kuona mbali na akainua mikono yake juu ili kumwomba Mungu aliye juu.
Mara moja sura ya vita iligeuka nao Israeli walishinda lakini mara mikono ya Musa iliposhuka kutokana na kuchoka kwa kuinyosha mikono yake, Waamaleki wakaanza kushinda. Hivyo Haruni na Huri wakamketisha Musa juu ya jiwe na kuishikilia mikono yake mpaka Israeli walipopata ushindi juu ya Waamaleki. Kwa ajili ya shambulio lao kwa watu wake, Mungu akatamka chuki ya daima dhidi ya Amaleki na dhidi ya watu ambao kama wao wangetafuta fursa ya kuwashambulia Waisraeli (Kutoka 17:14-16). Tendo la Samweli kwa Agagi, mfalme wa Waamaleki wote inathibitisha hukumu ya Mungu juu ya Taifa hili (1 Samweli 15:2, 3)
Fundisho kwa ajili yetu kutoka Refidimu ni kwamba maombi yana nguvu sana.Tunaweza kupata nguvu kutoka kwa BWANA tukiomba msaada kutoka kwake.
Hata sasa, Yesu ameketi mkono wa kuume wa Mungu ili kuwasaidia wale watakaoweka imani yao kwake, wanaamini Neno lake na wanamwomba Mungu ili wapate nguvu (Yakobo 5:16; 1:5-6; Luka 18:1). Mungu atawaokoa wanaomtegemea na kuwapatia ushindi mkuu juu ya dhambi na mauti (2 Wakorintho 10:4-5; Wafilipi 4:13).
Kuna wakati unakuja, pia, ambapo Kristo na watakatifu wake wakiwa kama majemadari wote wenye nguvu wote wa Israeli watayashinda mataifa kuyaweka chini ya utawala wa Kristo (Isaya 55:4; Zekaria 9:13,14).
MUHTASARI
-
Kutokana na tukio lile lilitokea pale Mara tunajifunza kwamba kwa kutii amri za Mungu tutaweza kupata afya ya kiroho na utamu katika safari yetu ya jangwani.
-
“Mtu hataishi kwa mkate tu bali kwa kila neno la BWANA” Mungu ametupatia sisi chakula ambacho, tutakula chakula hiki kila siku, kitatufikisha katika Ufalme wake. Manna ni ishara ya Neno la Mungu.
-
Yesu alijifananisha na “Mkate wa kweli”. Kwa kula mkate huu wa kweli utatupatia uzima wa milele. Hili linatendeka tunaposoma Neno lake na kulitii, hii inakuza tabia za Yesu Kristo katika maisha yetu.
-
Musa alitoa maji ndani ya mwamba uliopigwa ambao ni mfano wa Bwana Yesu Kristo. Maji ya uzima (Injili) yametirirka kwenda kwa mataifa yote kwa yao ili wanywe na wapone.
-
Kuwashinda Waamaleki kunaelekeza wakati ambapo Kristo hatimaye ataushinda uovu wote na kuanzisha Israeli ambao watakuwa kiini cha ule Ufalme.
-
Yatupasa tutambue tegemeo letu kwa Mungu na kuomba bila kukoma kwa ajili ya uongozi wake.
VITABU REJEA:
"Elpis Israel" (J. Thomas)—Pages 294, 295
"The Visible Hand Of God" (R. Roberts)—Chapter 15
"The Story Of The Bible" (H. P. Mansfield)—Pp. 279-306
"The Wilderness Of Life" (J. Martin)—C.S.S.S. Notes
MASWALI YA VIFUNGU
-
(a) Ni kwa jinsi gani maji ya Mara yalivyoweza kuponywa?
(b) Ni fundisho gani walifundishwa Waisraeli kutokana na tendo hili?
-
Mana ilikuwa nini na ni kwa njia gani mana jangwani ilikuwa mfano wa Kristo?
-
Je, umuhimu wa kupigwa mwamba kule Refidimu kulikuwa ni upi?
-
Ni kwa jinsi gani Israeli waliweza kuwashinda Amaleki?
MASWALI YA ISHA:
-
Ni mafundisho gani tunayojifunza kutokana na kupewa Mana na maji katika jangwa?
-
Ni kwa jinsi gani Waamaleki walishindwa kule Refidimu na ni mafundisho gani tunajifunzo kutokana na tukio hili?