CSSA 2-2-20 - ISRAEL AT SINAI— A KINGDOM FORMED

Swahili

170. ISRAELI KATIKA SINAI – UFALME WAUNDWA

 

Wakati wana wa Israeli walipofika Mlima Sinai walikuwa ni mkusanyiko wa watu wakishughulikia vikundi vya familia. Ilikuwa ni muhimu kwao kujiandaa kuwa ufalme. Kupitia Musa, Mungu aliwapatia sheria ambayo iliwafundisha namna ya kuishi na Mungu na jinsi ya kuishi na wengine. Iliwafanya wawe Ufalme, ikawapatia manufaa ya haraka haraka kutokana na utii wao  wa sheria, ikiwafundisha mafundisho kuhusu kazi ya masihi wao na jinsi  ya kushiriki pamoja naye uzima wa milele.

 

Walikuwa wanaelekea kuwa ufalme wa Mungu duniani na matukio yaliyofuata  yaliwaandaa vizuri  kwa ajili ya mamlaka haya makuu.

 

 

KUTOKA 19 na 20

WALIPOFIKA MLIMA SINAI – UJUMBE WA MUNGU KWA WATU WAKE

Sasa tunawaangalia watu wa Israeli karibu miezi mitatu baada ya kuondoka kutoka Misri, wakakaribia mlima Sinai, ambapo ni mlima wa kutisha unaoinuka juu angani kwa mawe makubwa kutokea uwanda unaouzunguka.

 

Watu hao wakaweka kambi karibu na mlima na Mungu akamwita Musa kupanda mpaka juu ya mlima. Mungu akaeleza ni kwa nini aliwakomboa wana wa Israeli na yale aliyoazimia kuwafanyia. Wangekuwa “ufalme wa makuhani na taifa takatifu”(Kutoka 19:6). Hawakuwa  tena kuwa kundi la wasafiri watokao utumwani ila sasa walitakiwa kujiandaa kama watu wenye bahati sana na wenye kuheshimika. Walikuwa wawe taifa ambao  waliitwa ili kumtumikia Mungu wao katika utakatifu, ambaye alikuwa amewakomboa kwa mwujiza kutoka Misri.

 

Angalia jinsi Mungu anavyosema kwamba “Aliwachukua Israeli  juu ya mbawa za Tai” . Tai hurusha makinda wake kutoka kwenye kiota ili awawezeshe kuruka. Wanaangaliwa kwa makini sana wanapofungua mbawa zao kuelekea chini. Kabla hawajaanguka chini mama huruka na kushuka chini haraka sana  na kuwabeba wale vifaranga na kuruka nao juu angani. Hivyo watoto hujifunza kumtegemea mama yao. Kwa njia hiyo hiyo Mungu alionyesha kujali taifa hilo changa la Israeli lililokuwa limezaliwa. Alikuwa amewazaa na kuwafanya taifa kwa kuwakomboa kutoka  katika mateso Misri. Jinsi alivyowajali pale Mara, Elimu na Refidimu iliwapatia sababu nyingi za kumwamini  Mungu.

 

Baada ya Mungu kumaliza kusema na Musa, alirudi kwa watu. Akawaambia kama wataitii sauti ya Mungu na kutunza Agano lake, Mungu atawafanya kuwa watu wake, watakuwa tunu ya aina yake kwake mwenyewe kuliko watu wote nao watakuwa Ufalme wa makuhani. Kwa hiyo wangekuwa ni mashahidi wa Mungu wakiwafundisha mataifa mengine kuhusu njia za Mungu (Kumbukumbu la Torati 4:6).

 

Watu wakakubali kulitunza Agano la Mungu (Kutoka 19:7,8)

 

 

MUNGU ANANZISHA UFALME WAKE

            Musa akapeleka jibu la wana wa Israeli kwa Mungu, ambaye alimwambia kuwaandaa  hao watu kwa sababu alikuwa anakwenda kujidhihirisha mwenyewe kwao (Kutoka 19:9). Alikuwa anakwenda kuwaonyesha watu kwamba ni kweli ni BWANA ndiye aliyekuwa amesema na Musa. Mungu pia alikuwa awaambie watu hao, moja kwa moja,  misingi ya kwanza ya Agano alilokuwa analifanya nao.

 

Watu walikuwa na muda siku tatu  za kujitayarisha (Kutoka 19:10-15). Walitakiwa kuwa watakatifu katika akili zao na miili yao kwa sababu walikuwa wanakwenda kukutana na Mungu. Wakiwa watoto wake  walitakiwa kuwa watakatifu  au kujitenga kwa kuwa Mungu  ni mtakatifu na mwenye wivu. Mpaka uliwekwa kuuzunguka mlima kwa sababu palikuwa mahali patakatifu na watu wa Israeli walikatazwa kuugusa mlima la sivyo wangekufa.

 

Siku ya tatu, ukimya ghafla ulitoweka kwa sababu ya sauti ya ngurumo na radi. Nchi ikatetemeka na wingu zito likafunika kilele cha mlima. Miali ya moto ikatokeza kutoka kwenye wingu hilo. Sauti kali ya baragumu ikapasua anga, na watu wakatetemeka kwa hofu. Musa akawaleta watu hadi  chini ya mlima. Mungu akamwita Musa kupanda mlimani tena na kumwambia kuhakikisha ya kwamba asiwepo mtu atakayefika karibu na mpka  wa mlima huo.

 

Ni  kwa nini Mungu alifanya hili?

 

Watu hao walitoka Misri bila kuwa na mpango na mara nyingi wakiabudu  sanamu. Ili waweze kumhofu na kumtii  yeye, Mungu aliwapatia sheria yake akiunganisha pamoja na ishara za kutisha (Kutoka 20:18-20; Kumbukumbu la Torati 4:10-11).

 

Malaika wa  BWANA ndipo aliwaambia watu kwa  sauti kuu (Kumbukumbu la Torati 5:22).

 

WATU WANAPEWA SHERIA

  1. AMRI KUMI – AGANO LA MUNGU: Malaika aliwapa wale watu amri kumi  muhimu ambazo walitakiwa kuzitii. Amri hizi zilifanyika  msingi wa agano la Mungu pamoja nao kuwa ndio watu wa ufalme wake. Zilikuwa miongozo yao  jinsi walivyotakiwa  kuendesha maisha yao na kuwa watakatifu kwa kuwa BWANA ni mtakatifu.

 

Tulisoma amri hizi katika Kutoka 20:1-7. Zimepangilwa katika mpango maalumu. Amri Nne za kwanza zinazungumzia uhusiano wetu na Mungu- Mungu  ndiye anapaswa kuwa wa kwanza katika mapenzi yetu yote.

 

  1. Usiwe na miungu mingine  ila mimi;
  2. Usiabudu sanamu yoyote ya kuchonga;
  3. Usilitaje bureJjina la  BWANA Mungu wako;
  4. Ikumbuke siku ya sabato na uitakase.

 

Amri nyingine inayofuatia inazungumzia umuhimun wa watoto wa kuwatii wazazi wao, ambayo  umuhimu wake ndio unaofuatia kwa Mungu. Ilikuwa amri yenye baraka ya kuishi miaka mingi pamoja na familia yenye furaha katika kumtumikia Mungu katika nchi ambayo atawapatia, Paulo anasema kwamba ilikuwa ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi (Waefeso 6:2,3). Jinsi inavyopendeza kuona familia yenye upendo na umoja. Na ni jambo baya lililoje kuona familia inayoishi  kinyume na mambo hayo.

  1. Waheshimu baba yako na mama yako.

 

Amri zinazobakia zinahusu jinsi ya kuishi  na mtu mwingine. Ambapo Mungu anatajwa katika amri tano za kwanza (Kutoka 20:2-12), Hatajwi katika amri zile tano za pili (mistari 13-17).

  1. Usiue
  2. Usizini
  3. Usiibe
  4. Usimshuhudie  jirani yako uwongo
  5. Usitamani kitu chochote ambacho ni mali ya jirani yako.

 

 Tunajifunza kutoka katika mpangilio huu kwamba Mungu anataka sisi tumweke yeye  nafasi ya kwanza katika maisha yetu, na wajibu wetu kwa wazazi na familia  ziwe nafasi ya pili, na watu wengine wawe nafasi ya tatu. Angalia ya kwamba hakuna nafasi ya sisi wenyewei! Hakuna amri inayotuvutia mawazo kwa “binafsi”

 

Amri hizi zinaitwa “Agano langu” (Kutoka 19:5). Musa anasema katika Kutoka 34:28 “Naye akaandika katika hizo mbao, hayo maneno ya maagano, hizo amri kumi”.

 

 

  1. Sheria za ziada na Hukumu

Mungu alipokwisha maliza kumpatia hizo amri aliwaagiza watu warudi  katika mahema yao, Kisha akampatia Musa amri na maagizo ya ziada ambayo watu walitakiwa kuyatii katika maisha yao ya kila siku. Sheria hizi na  maagizo ziliwafundisha jinsi ya kumwabudu Mungu, namna walivyotakiwa kutendeana wao kwa wao, na jinsi walivyotakiwa kuyaona mataifa mengine ambayo wangeishi kati yao. Sheria hizi zote kwa pamoja tunaziita sheria za Musa.

 

 

  1. Watu wanafanya Agano – Kutoka 24:1-11

Musa aliandika maneno ya amri kumi katika kitabu na kuwakusanya wana wa Israeli wote pamoja. Akazisoma tena masikioni mwao nao watu wakasema, “ hayo yote aliyoyanena BWANA tutayatenda nasi tutayatii” (mstari 7). Kwa bahati mbaya katika somo linalofuata tutaona jinsi walivyosahau maneno haya upesi. Ndipo Musa alipochukua damu ya dhabihu katika bakuli na kuinyunyizia  kwenye madhabahu, kitabu na  kuwanyunyizia watu kwa damu hiyo. Kwa njia hii watu walielewa ya kwamba walikuwa wameingia katika mapatano maalumu pamoja na BWANA. Msingi wa agano la kitaifa na BWANA ulikuwa  dhabihu. Kumwagika kwa damu ya uhai kuliwaunganisha kabisa na Mungu wao. Katika kukazia jinsi lilivyokuwa la muhimu na la maana agano na sheria yake, Musa na Haruni, Nadabu na Abihu na wazee 70 wa Israeli waliruhusiwa kuona utukufu wa BWANA alipojidhihirisha katika elohim (malaika) na kula  chakula cha  ushirikiano pamoja nao.

 

 

KUSUDI LA SHERIA

Tumeona jinsi Mungu alivyowapatia Israeli sheria ili kuwaanzisha kuwa taifa watu wa pekee (Ufalme wake) ili akili zao zifikiri kama zake ili kwamba mataifa mengine yote wawahusudu kuwa kama wao (Kumbukumbu la Torati 4:6-8), watawahofu (Kumbukumbu la Torati 28:9-10) na kufuata mfano wao (Zekaria 8:23).

 

Sheria iliwasaidia wao kumfikiria Mungu kila siku katika mazingira ya aina yo yote. Ililiongoza taifa kufikiria kwa kina  maana ya  sheria zao na sadaka. Sadaka na  matokeo yalielekeza kwenye sadaka yake Kristo. Kwa hiyo wana wa Israeli waaminifu walielekezwa kuja kwa  Mwana-kondoo wa Mungu ambaye ataichukua dhambi ya ulimwengu (Yohana 1:29). Paulo katika Wagalatia 3:24 anasema kwamba “sheria ilikuwa kiongozi” kuwaleta watu kwa Kristo.

 

Wana wa Israeli hawakuweza kuishika sheria kwa ukamilifu. Kushindwa kwa waisraeli kushika sheria kuliwasababishia wao wamhitaji mkombozi. Iliwafundisha kumtazamia mtu mmoja  kuja ambaye angaliweza kuwakomboa.  Naye huyu angekuwa ni Masihi (Kristo) wao (Wagalatia 3:13,24; 4:4). Utiifu wake mkamilifu kwa mapenzi ya Baba yake, mpaka hata mautini, “ulimpendeza” Mungu zaidi kabisa kuliko dhabihu za mafahali au wana-kondoo.

 

 

MMEOKOLEWA KWA NEEMA KWA NJIA YA IMANI

Kwa Wayahudi walioamini katika Kristo, Paulo anasema, “Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu,  maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti” ( Wagalatia 3:13)

 

Torati, katika kumlaani mtu mwenye haki kwa vile tu aliangikwa juu ya mti, iliondolewa. Bwana Yesu Kristo amekamilisha kila lililo la haki katika maisha yake yote na hata katika kusulubishwa kwake akatoa uhai wake kwa utii wa mapenzi ya Babaye. Katika maisha yake yote alitamka ya kwamba njia za Mungu, zilikuwa sahihi. Dhabihu yake ilikuwa kamilifu na katika msingi  huu wa kutokuwa na dhambi yoyote katika maisha yake yote kaburi halikuweza kumshika.  Na kwa sababu hiyo hatuishi tena chini ya sheria, bali tunaishi chini ya neema ( Warumi 6:14; Waefeso 2:8). Neema ni “Upendeleo wa Mungu tusiostahili” . Tunabarikiwa kwa rehema, wema na upendeleo wake Mungu kwa sababu tuna imani katika mwanaye aliyethibitisha kwa ukamilifu mapenzi ya Baba yake na tabia.

Ili tuweze kupokea neema ya Mungu tunatakiwa:-

  • Kuamini mambo yote yahusuyo ufalme wa Mungu na Jina la Yesu Kristo – Injili (Matendo ya Mitume .8:12)
  • Kubatiza katika Yesu Kristo (Marko 16:15-16)
  • Kujitahidi  sana kufuata mafundisho na mfano wa Kristo ( Mathayo 11:28-30). “Imani itendayo kazi  kwa upendo” ( Wagalatia 5:6).

 

Kama Israeli walipokuwa chini ya Musa, wale wanaomkubali Kristo kwa imani, wakabatizwa na kutii wanahesabiwa machoni pa Mungu kuwa “ mzo mteule,ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu” (1Petro 2:9). Maneno haya ni ukumbusho wa wazi  wakati  wana wa Israeli walipoitwa ili kuwa Ufalme wa makuhani na taifa takatifu. Sisi nasi kama  Israeli tumeitwa ili tuonyesha katika maisha yetu utukufu wa Mungu ambaye ametuita  tutoke  gizani, na tuingie katika nuru ya ajabu ya ile Kweli ( soma 1Petro 2:9; Kutuka 19:6)

 

 

MAKTABA YA TEJEA:

“ Tumaini la  Israeli” (J. Thomas) –  Ukurasa 298-299

“ Mkono wa Mungu unaoonekana” (R. Roberts) – sura 16

“ Historia ya  Biblia” (H.P. Mansfield) pp. 307-312

“ Mkufunzi wa  Kristadefia” –  Maswali na  Majibu Na. 96-102

 

MASWALI YA FUNGU:

  1. Orodhesha zile Amri kumi
  2. Amri kumi zinapangwa katika utaratibu gani na tunajifunza nini kutokana na mpango huu?
  3. Je,Sheria ya Musa ilikuwa na kusudi gani?

 

MASWALI YA INSHA:

  1. Eleza jinsi sheria ya Musa ilivyowabadilisha wana wa Israeli na kuwawezesha kufaa kuwa Ufalme wa Mungu  dunia.
  2. Sheria ilikuwa “kiongozi” kuwaleta wana wa Israeli kwa Kristo. Ni kwa jinsi gani hili lilifanyika na ni kwa nini sheria iliondolewa?


 

 

 

Swahili Title
170 ISRAELI KATIKA SINAI – UFALME WAUNDWA
Translator 1
Jonathan Nkombe
Literature type
Sub type
Sub sub type