183. UFALME ULIOGAWANYIKA - ISRAELI NA YUDA
“Nitaurarua ufalme kutoka mkononi mwa Sulemani na kukupa wewe makabila kumi”
Mfalme Sulemani alitawala muda wa miaka 40. Alikuwa ni mtu maarufu sana wa ktunga mashairi na mwerevu sana kwa kila jambo. Hata hivyo, polepole upendo wake kwa hekima ya Mungu wake ulianza kuchukua nafasi ya pili, kwani “Selemani akafan ya yaliyo mabaya`machoni pa BWANA, wala hakumfuata BWANA kwa utimilifu, kama Daudi baba yake” (1 Wafalme 11:6).
Baada ya kifo cha Selemani, Israeli iligawanyika katika mataifa mawili - Taifa la Kaskazini na Taifa la Kusini.Taifa la Kaskazini lilijukana kama Israeli na Taifa la Kusini lilijukana kama Yuda.
1 Wafalme 11 na 12
ONYO LA MUNGU KWA SELEMANI KABLA YA KIFO CHAKE - 1 Wafalme 11
Utawala bora sana wa Selemani ulielekea mwisho wake, wake zake wengi walimgeuza moyo wake akaiabudu miungu (sanamu), na akajenga madhabahu kwa ajili ya sanamu hizo. “Basi, BWANA akamghadhibikia Selemani kwa sababu moyo wake umegeuka, naye amemwacha BWANA”. Na kwa sababu hii alipokea ujumbe, “Hakika nitaurarua ufalme usiwe wako” (1 Wafalme 11:11-13). Hata hivyo kwa ajili ya Daudi baba yake isingetokea wakati wa uhai wake Selemani, bali katika siku za mwanaye. Selemani alianza kutawala wakati alipokuwa kijana mdogo (yamkini alikuwa na miaka 18 au 20; 1 Mambo ya Nyakati 29:1). Akatawala kwa muda wa miaka 40, kwa hiyo hakuyafurahia maisha marefu ambayo Mungu alimwahidi ikiwa angemtii Mungu (1 Wafalme 3:14).
MKUTANO HUKO SHEKEMU – 1 Wafalme 12:1-5
Rehoboamu ambaye mama yake alikuwa wa Taifa la Amoni, ndiye aliyepaswa kumrithi Selemani katika kitin cha Enzi (1 Wafalme 11:43; 14:21). Sikukuu ya kutawazwa kwake ilifanyika huko Shekemu, nao Israeli wote wakakusanyika kwa ajili ya tukio hilo. Hata hivyo katika Israeli kulikuwa na tatizo lililokuwa likifukuta. Watu hawakuwa wameridhishwa na kodi kubwa ambayo Mfalme Selemani alikuwa akiwatoza na kwa hiyo wakamteua Yeroboamu kuwa msemaji wao ili kueleza matatizo yao kwa Rehoboamu. Yeroboamu alikuwa mtumwa wa Selemani, na alikuwa ni mtu mwenye bidii sana (1 Wafalme 11:28). Lakini Ahiya Nabii alikuwa ametumwa na Mungu kwenda kumwambia Yeroboamu, “Tazama niurarua Ufalme, na kuuondo katika mkono wa Selemani, nami nitakupatia wewe kabila kumi” (1 Wafalme 11:29-31). Selemani alipoyasikia haya alitafuta njia ya kumwua Yeroboamu (mstari 40), lakini Yeroboamu alikimbilia Misri. Sasa baada cha kifo cha Selemani watu wa Israeli wakapeleka ujumbe kwenda kwa Yeroboamu ili atoke Misri na arudi Israeli (mstari 2-3). Bila shaka Yeroboamu alikuwa ana nia kutimiza unabii wa Ahiya, naye kwa kuwa alikuwa mtu mwerevu akaazimia kuuchukua ufalme, lakini alifahamu kuwa kulikuwa na vitu viwili vilivyowasumbua watu:-
1. Kulikuwa na wivu na upinzani kati ya yale makabila 10 ya upande wa Kaskazini na Yale makabila 2 ya upande wa Kusini
2. Watu walisikitika kwa sababu ya mzigo wa kodi uliokuwa mzito ambao ilibidi walipe wakati wa Enzi ya Selemani.
Kwa kuwa watu hawakuridhika, wakati Rehoboamu alipoanza kukalia kiti cha enzi hali tete ilikuwepo. Ndipo Yeroboamu alipotumia fursa hii ili kuendeleza malengo yake. Akaongoza ujumbe uliokwenda kwa Rehoboamu na ombi, “Baba yetu alilifanya zito kongwa letu; basi sasa utupunguzie utumwa mzito tuliotumikishwa na baba yako, na lile kongwa zito alilotutwika nasi tutakutumikia” (mstari 4). Hili lilikuwa ombi la busara na ambalo linaonyesha jinsi Yeroboamu alivyokuwa mwelevu. Yeroboamu alifahamu kuwa kama Rehoboamu atakataa ombi la kufanya kodi kuwa nyepesi zaidi angeonekana mkatili, lakini kama angekubaliana ,ndipo Yeroboamu angeonekana mtu mkuu katika macho ya watu.
UPUMBAVU WA REHOBOAMU – 1 Wafalme 12:6-15
Rehoboamu akawaambia watu waondoke kwa muda wa siku tatu na kisha baada ya siku tatu atawapatia jibu lake. Kisha Rehoboamu akataka ushauri kwa “wazee waliokuwa wakisimama mbele ya Selemani, baba yake, alipokuwa hai” (mstari 6). Watu hawa wenye busara wakamshauri Rehoboamu kuwasikiliza watu, la sivyo atapata uasi mkononi mwake “uwajibu na kuwapatia maneno mazuri” (mstari 7). Walifahamu kuwa ilikuwa ni muhimu kwa mfalme kijana kupata kibali cha watu. Ndipo wakamshauri kukubali masharti yaliyowekwa mbele yake. Lakini pia Rehoboamu alitaka ushauri wa vijana wa rika lake ambao alikua pamoja nao.Hawa vijana hawakuwa na uzoefu wowote, wanaojivuna na wenye kiburi. Kwa maoni yao ilibidi kodi iongezwe sana. Walihisi kuwa kukubali ombi la watu ingekuwa ishara ya udhaifu. Kwa hiyo Rehoboamu akakataa ushauri wa busara wa wazee na akachukua ushauri wa vijana wapumbavu. Kwa hiyo hakuwa amesikiliza au kuzingatia maneno ya baba yake, Daudi, aliyekuwa amesema; “Atawalaye wanadamu kwa haki, akitawala katika kicho cha Mungu” (2 Samweli 23:3). Baada ya siku tatu mfalme alikuja mbele za watu na kuwaambia; “Baba yangu alilifanya kongwa lenu, bali mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu aliwapiga kwa mijeredi, bali mimi nitawapiga kwa nge” (mstari 14). Alitaka watu hao wajue nguvu za cheo chake, kisha naye kwa jeuri akatangaza kuwa mateso yao yangeongezeka. Matokeo ya jambo hili ilikuwa ndiyo mwanzo wa uasi.
UFALME UNAGAWANYIKA - 1 Wafalme 12:16-24
Watu walipoona kuwa ombi lao limekataliwa wakaenda zao hemani kwa kwa moyo wa uasi. Rehoboamu akiwa ametatizwa na uasi wa watu, akamtuma Adoramu kusema na watu. Lakini hapa hatua ya upumbavu zaidi iliweza kudhihirika, kwa sababu Adoramu ndiye aliyekuwa kiongozi wa kodi. Kuonekana kwake kuliongeza zaidi hasira ya watu, wakachukua mawe na kumpiga hadi kumwua (mstari 18). Rehoboamu akakimbia kutoka Shekemu hadi Yerusalemu na kutayarisha jeshi kubwa ili kudhibiti uasi ule. Lakini Mungu akaingilia kati, na kwa kumtumia nabii Shemaya, Rehoboamu alikatazwa kwenda kwa sababu yalikuwa mapezi ya Mungu; ili jambo hili litokee (mstari 22 -24). Yeroboamu akachaguliwa kuwa mfalme wa makabila ya Kaskazini, na hivyo Israeli ikagawanyika katika mataifa mawili. Ilikuwa ufalme wote uondolewe kabisa ktoka kwa rehoboamu, kama vile ulivyoondolewa kwa Sauli, lakini Mungu alimkumbuka Daudi, mtumishi wake mwaminifu, kwa hiyo makabila mawili alipewa uzao wa Daudi. Na imeengelea kubakia katika hali hiyo mpaka Kristo atakaporudi (ambaye ni uzao wa Daudi) ambapo yale makabila kumi yataungana na yale makabila mawili (Mathayo 19:28; Luka 22 30; Ezekieli 37:22).
HOFU YA YEROBOAMU NA UASI WAKE – 1 Wafalme 12:25-33
Ingawa Yeroboamu alikuwa mfalme wa Kaskazini, akawa na hofu kwamba uwezo wake ungeweza kuchukuliwa kutoka kwake. Akifahamu kuwa sasa ufalme umegawanyika na kuwa falme mbili, watu itawapasa kwenda Yerusalemu kuabudu, kwa kuwa sheria iliwataka wanaume wote kwenda mbele ya BWANA mara tatu kwa mwaka (Kutoka 23:17). Yeye akaona kuwa hakika umaarufu wake utapungua. “Kama watu hawa wakipanda kwenda kutoa dhabihu katika nyumba ya BWANA huko Yerusalemu, ndipo mioyo ya watu itamrudia bwana wao, yaani Rehoboamu, mfalme wa Yuda (mstari 27). Kwa hiyo Yeroboamu akafikiria mpango wa uovu, kwa werevu, akawaambia watu kuwa ilikuwa mbali mno kwao kwenda Yerusalemu kuabudu, akatengeneza ndama wawili wa dhahabu; mmoja huko Betheli na mwingine huko Dani, na akasema; “Tazama, hii ndiyo miungu yenu, enyi Israeli ilyowapandisha kutoka katika nchi ya Misri”(mstari 28).
Akafanya watu wa kawaida kuwa makuhani, watu ambao hawakuwa Walawi. Maana Makuhani wa kweli hawangekuja kujishughulisha na ibada hii ya uovu. Baadaye Yeroboamu akabadilisha tarehe ya sikukuu za mahema. Sikukuu hii ilitakiwa ifanyike kila tarehe 15 ya mwezi 7, lakini sikukuu ya Yeroboamu ilikuwa ikifanyika kila tarehe 15 ya mwezi 8. Kwa hiyo watu wakatoa dhabihu kwa hao ndama wawili, akifanya ibada ionekana kana kwamba ni ileile, lakini haikuwa ya aina moja; maana alikuwa ameiharibu Kweli na kuwadanganya watu. Yeroboamu ameandikwa katika Maandiko kuwa “ni mtu aliyewakosesha Israeli, hata wakatenda dhambi” (1 Wafalme 14:16). Mungu anataka kila mtu amwabudu katika njia ambayo Yeye ameagiza, “inatupasa kumwabudu Mungu katika roho na kweli” (Yohana 4:24). Na wafalme wote 23 waliofuata baadaye, walifuata njia zake, isipokuwa yule wa mwisho. Kwa hao maneno yamejirudia rudia tena mara nyingi muda baada ya muda, “Akatembea katika njia za Yeroboamu mwana wa Nebati na katika dhambi zake ambayo kwa hiyo aliwakosesha Israeli”. Mungu alimghabikia Yeroboamu hata ikawa Mungu akasema kuwa ataiangamiza kabisa nyumba yake (1 Wafalme 14:7-16).
FUNDISHO KWETU
Rehoboamu alikuwa dhaifu na hakutambua wajibu wake wa kuwaongoza Israeli katika kumtumikia Mungu. Shauku yake na uchoyo wa kutowafikiria ndugu zake katika Israeli yalimkosesha makabila kumi ya kaskazini. Mungu ametupatia majukumu ya kuwaongoza wengine kumtumikia Yeye na kisha tuwatunze. Anatutaka sisi tuwe mfano katika mambo yote ya Mungu, kwa kujifunza mapenzi ya Mungu kutoka katika Biblia, kuwafundisha wengine kwa uaminifu na kwa kudumu kufanya hivyo siku zote (1 Timotheo 4:12-16).
Usisahau kamwe kuwa Mungu anapenda kuona tukimwomba Yeye kuhusu maamuzi ambayo ni muhimu na majukumu ya kazi (Mithali 15:8,29). Kutuona tukimtegemea. Hili lilimshida Rehoboamu kulifanya alipowageuka na kufuata ushauri wa rafiki zake vijana wapumbavu. Mahali ambapo Rehoboamu alipokuwa dhaifu, Yeroboamu alikuwa na nguvu, isipokuwa katika mambo ya ubinafsi na shauku ya kujipatia. Alijipatia umaarufu kwa “kuwaongoza Israeli katika kutenda dhambi”. Tunatakiwa kujifunza kunyenyekea, na wala siyo kwa kutafuta faida yetu wenyewe na utukufu, bali tufanye mambo yote kwa ajili ya kumheshimu na kwa ajili utukufu wa BWANA, kwa kumtumikia Mungu kama alivyoamuru katika roho na katika kweli.
MAKTABA REJEA:
1. Historia ya Biblia (H.P.Mansfield) - Kitabu cha 4, Namba 11
2. Njia za Mungu za kutosheleza (R.Roberts) - Sura ya 19
3. Mkono wa Mungu unaoonekana (R.Roberts) — Sura 25
MASWALI YA VIFUNGU:
1. Ni yapi yalikuwa maombi ya Yeroboamu na watu kwa Rehoboamu?
2. Je, Rehoboamu alitafuta ushauri kwa nani na alifuata ushauri upi?
3. Ni njia zipi ambazo Yeroboamu aliwasababisha Israeli kutenda dhambi?
MASWALI YA INSHA
1. Ni sababu gain iliyosababisha ufalme chini ya Rehoboamu kugawanyika?
2. Fafanua kwa kina jinsi Yeroboamu alivyowakosesha Israeli?