CSSA 2-3-12 - NAAMAN THE SYRIAN

Swahili

187. NAAMANI MTU WA SHAMU

"Sasa najua kuwa kwamba hakuna Mungu mwingine ulimwenguni pote ila katika Israeli"

 

Maandiko yanasema kwamba "Kwa kuwa yote yaliyotangulia kuandikwa yaliandikwa ili kutufundisha sisi, ili kwa saburi na faraja ya maandiko tupate kuwa na tumaini" (Warumi 15: 4). Kwa hiyo kuponywa kwa Naamani ukoma ni muhimu zaidi sana kuliko habari yenyewe ambayo ni ya kufurahisha tu. Habari hii iliandikwa kama vile, kama vile zilivyoandikwa sehemu zingine za Biblia. Ili tuweze kupata fundisho la kutusaidia katika kulifahamu Neno la Mungu na kusudi lake. Habari inaonyosha yale yatakayo tokea mbele kuhusu kuwahubiri Injili watu wa Mataifa kwa sababu ya kutokuamini kwa wana wa Israeli. Na zaidi ya hayo, wakati tukianagalia kwa makini kuhusu Naamani tunaona kushindwa kwake - mawazo yake potofu na kiburi chake - mara nyingi hii ni tabia inayomzuia Mungu kutenda katika maisha ya wale wanaomtafuta Yeye. Tunaonyeshwa kuwa utii ni ufunguo wa kufungua mlango kwa ajili ya nguvu za Mungu na kuleta furaha na amani, nasi tunaelekezwa kuona kuwa utii huu ni lazima utokane na unyenyekevu na moyo uliopondeka. Kuna ma fundisho kwa ajili ya sisi wote katika habari hii rahisi lakini ni habari yenye utata.

 

2 Wafalme 5.

 

NAAMANI MGONJWA WA UKOMA ANAKWENDA SAMARIA

Naamani alikuwa mkuu wa jeshi la Shamu - mtu mwenye majivuno, skari jasiri aliyeheshimiwa na mfalme na watu. Ingawa alikuwa mtu maarufu na shujaa wa vita alikuwa na ugonjwa wa kutisha wa ukoma. Kutokana na mawazo ya wa Israeli; sheria ya Musa ilifundisha mafundisho muhimu sana ya kiroho kuhusiana na ugonjwa huu. Ugonjwa huu ulikuwa ni ishara ya dhambi na kifo, na Mwebrania yeyote aliyepigwa na ugonjwa huu alitengwa na kuwekwa nje ya kambi na alitengwa na watu wake na wala asingehudhuria katika Hema ya kukutania. Kwa hiyo ulikuwa ni ishara ya ugonjwa wa maisha! Wakati mtu alipokuwa na ukoma, mwili wake ungegeuka kuwa kusanyiko la uvimbe wa vidonda vilivyonuka na upele mkubwa unaoharibu sehemu za mwili na hatimaye kusababisha kifo. Wakati Miriamu alipopigwa kwa ukoma kwa sababu ya dhambi yake, Haruni alisema, "Na asiwe kama mmoja aliyekufa, ambaye nyama ya mwili wake nusu imelika" (Hesebu 12:12). Kama vile mtu mwenye ukoma anavyoendelea kuwa dhaifu na mwili wake ukiwa unaendelea kuoza na hatimaye anakufa, ndivyo alivyo mwanadamu ambaye huendelealivyo navyo kuzeeka huku akififia na kisha anakufa. Mungu aliupatia ugonjwa huu maana ya ishara ili kuwajulisha Israeli kwamba dhambi hakika husababisha kuoza na kifo. Hata hivyo kwa watu wa Mataifa, haikuwa na maana yeyote kiroho. Ulikuwa ni ugonjwa wenye kuhuzunisha na kwa hakika ni kuepuka kwa ajili ya matokeo yake, lakini siyo kwa ajili ya kuwa na aibu. Katika muda ambapo tukio hili lilipotokea, Israeli na Shamu hazikuwa katika vita, ingawaje vikundi vidogo vya Shamu vilikuwa vikivamia miji iliyokuwa upande wa kaskazini mwa Israeli na kuchukua nyara na mateka. Na mmojawapo kati ya mateka hao alikuwa msichana mdogo ambaye alifanywa mjakazi wa mke wa Naamani. Akifahamu kuwa Naamani na ugonjwa wa ukoma, siku moja yule mjakazi mdogo alisema, "Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake" (mstari 3). Haikuchukua muda mrefu, Ben hadaddi mfalme wa Shamu akamsikia yule mjakazi ya kuonyesha kumwamini Elisha, nabii wa Mungu aliye Israeli naye akamwandaa Naamani kuchukua barua ya utambulisho pamoja na maelezo ya ugonjwa wake kwa mfalme wa Israeli, pamoja na zawadi ya dhahabu, fedha na nguo.

 

AIBU YA YEROBOAMU - 2 Wafalme 5:6-9

Wakati Yeroboamu aliposoma barua ile alifadhaika sana kwa hofu na kwa hasira. Mfalme wa Shamu alikuwa amemwomba Yeroboamu amponye Naamani ukoma wake. Hili lilikuwa ombi la kenjeli na mzaha namna gani! Angewezaje kutibu ugonjwa wa aina ile? Akirarua nguo zake akasema, "Je, mimi ni Mungu niue na kuhuisha hata mtu huyu akanipelekea mtu nimponye mtu ukoma wake?" Fahamuni, basi nakusihini, mwone ya kuwa mtu huyu anataka kugombana nami". Yeroboamu alikuwa ni mtu asiyekuwa na imani na wala hakumjali Mungu. Bila shaka alikuwa amesahau nguvu za Mungu zilizodhihirika kupitia mkono wa Elisha mwanzo katika enzi yake wakati alipokwea kupigana na mfalme wa Moabu (2 Wafalme 3: 13-18). Pia alikuwa amesahau tukio hili muda mfupi uliokuwa umepita wakati Benhadadi alipoishambulia Israeli. Yeye alimkubali na kumwabudu Mungu ulipofika wakati mwafaka wa yeye kufanya hivyo. Yule msichana mdogo Mwisraeli aliyekuwa mateka na mjakazi katika Shamu alikuwa na imani kubwa kuliko mfalme wa taifa lake. Wakati Elisha aliposikia habari ya kufika kwa Naamani alituma ujumbe kwa mfalme kusema, "Na aje sasa kwangu mimi, naye atajua ya kuwa yuko nabii katika Israeli" (mstari 8). Kwa hiyo Naamani shujaa mkubwa wa vita akapelekwa kwenye nyumba ya nabii wa Mungu. Hadi wakati huu kila kitu kilikwenda sawasawa na jinsi alivyokuwa amepanga Naamani, lakini alikuwa anakwenda kujifunza haraka kuwa Mungu anamtendea mwanadamu kwa kufuata masharti ya Mungu mwenyewe.

 

KIBURI NA KUNYENYEKEZWA KWA NAAMANI - 2 Wafalme 5: 10-19

Hakuna shaka kuwa Naamani alikwenda kwa Elisha akiwa tayari ameshajenga mawazo kuhusu kile ambacho yeye alitakiwa kutoa. Na bila shaka katika mawazo yake alifikiria jinsi ambavyo nabii angefanya haraka kwenda kumlaki, na kumponya ugonjwa wake na halafu na yeye kwa upande wake apokee zawadi kutoka kwa mkuu wa majeshi ya Shamu. Hata hiyo kiburi chake ilishushwa wakati mtumishi alipotumwa kumpatia ujumbe uliotoka kwa nabii. Naamani alikuwa anatarajia kuwa Elisha atatoka mwenyewe na audhihirishe uweza, kwa kumwita BWANA, Mungu wake ili kumponya. Lakini alichopokea ni ujumbe, "Enenda ukaoge katika Yordani mara saba". Naamani alighadhabika. Siyo tu kwamba wazo la kuoga mara saba lilikuwa la dhihaka, lakini ukweli ni kwamba matope ya mto Yordani yangesababisha hali yake kuwa mbaya zaidi kuliko hali aliyokuwa nayo. Je, mito ya Shamu haikuwa ni bora zaidi kuliko mto Yordani? Kwa hiyo akageuka na kuondoka akiwa mwenye ghadhabu nyingi. Kama angerudi Dameski ngeendelea kuwa mgonjwa wa ukoma, kwa kuwa alikuwa amekaidi na kukataa kutii amri ya Elisha angeudumisha ukoma wake. Naamani alipaswa kujifunza na watu wote pia inatupasa tujifunze, kwamba kabla ya kupokea rehema ya Mungu, tunatakiwa tunyenyekee na tutii amri zake. Kwa bahati nzuri, katika suala la Naamani, ushauri mzuri ulishinda, na watumishi wake wakamshauri afikirie tena maneno ya Elisha. Kama angeambiwa atende jambo lililo kubwa zaidi asingesita, basi ni kwa nini alishindwa kutenda jambo dogo kama hili la kwenda kuonga Yordani mara saba. Naamani kwa bahati njema alikuwa ameandaliwa kupokea ushauri kutoka kwa washauri wake. Siyo tu kwamba hili lilihitaji atambua ujinga wa matendo yake mbele ya watumishi wake, lakini pia ilimpasa anyenyekee mbele za Mungu. Mara sita alijichovya bila mabadiliko yeyote, lakini katika mara ya saba mwili wake ukawa safi ajabu ugonjwa ule wa kutisha haukoonekana tena. Zaidi ya hayo, mawazo yake nayo pia yakawa yamebadilika. Kiburi chake na ukaidi vilitoweka naye akarudi nyumbani kwa Elisha akaseme, "Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli". Ni katika tukio hili nabii alifurahia kumpokea kama vile Bwana Yesu Kristo anavyofurahia kuwapokea wale wote wanaokwenda kwake kwa unyenyekevu na mioyo iliyopondeka kupitia maji ya ubatizo.

 

Uhusiano uliopo kati ya kusafishwa kwa Naamani mwenye ukoma na ubatizo (kusafishwa kutokana na dhambi) kwa wale wanaotafuta kumfuata Yesu Kristo ni wa muhimu na wa kusisimua sana. Ni sawa na kukubali yale aliyoyasema Elisha na kutii kwa kuoga maji ya mto Yordani ilivyokuwa muhimu sana kwa Naamani ili kuupoteza ukoma wake, ndivyo ilivyo siku hizi kuamini na kubatizwa ni muhimu sana kwa ajili ya wokovu. Yesu mwenyew alisema ,"Mtu asipozaliwa kwa maji (ubatizo) na kwa roho hawezi kuingia katika Ufalme wa Mungu, na "yeye aaminiye (Injili) na kubatizwa ataokoka, lakini yeye asiye amini atahukumiwa (Yohana 3:5; Marko 16: 15-16; soma pia matendo ya Mitume 2:28, 41, 44; 8:12-16; 10:45-48; 18:8; 19: 2,4,5; 22:16). Watu wale wanaouona ubatizo kuwa hauna umuhimu yoyote wafanana na Naamani mwenye kiburi, na roho ya ukaidi kabla hajajinyenyekeza. Wakati Naamani aliporudi kutoka nyumbani kwa Elisha baada ya kutoka mtoni Yordani akampatia Elisha zawadi nyingi kama ishara ya kuthamini kuponywa kwake. Elisha alikataa kuzipokea kwa kuwa alimpatia Mungu utukufu kwa mwujiza huu, naye akamwambia Naamani aende zake kwa furaha. Lakini, Gehazi, mtumishi wa Elisha hakukubaliana na uamuzi uliofanywa na bwana wake, naye akasema mwenyewe; "Tazama, bwana wangu amemwachilia huyu Naamani, Mshami, asivipokee mikononi mwake vile vitu alivyovilete; kama BWANA aishivyo, mimi nitamfuata mbio, nipokee kitu kwake" (mstari 20). Naamani alikuwa ameshuhudia kiburi cha Naamani na jinsi alivyonyenyekezwa na aliona uamuzi wa bwana kwa yule mkuu wa jeshi la Shamu, na yote haya yalionekana kutokuwa na maana yoyote kwake. Alikosa ufahamu wa kujua kanuni za utendaji wa Mungu - neema ya Mungu haiwezi kununuliwa kwa fedha za mwanadamu (Isaya 55: 1-3). Gehazi alikuwa ni mfano wa Israeli ambao pamoja na nguvu ya Mungu kuwepo kati yao; hawakuitambua kanuni iliyokuwa ndani ya Sheria. Na kwa hiyo, akalikimbilia gari la vita, na wakati kundi liliposimama akamwambia Naamani kuwa bwana wake alikuwa amemtuma kwa ajili ya talanta ya fedha na jozi mbili za mavazi, kwa sababu ya wana wawili kati ya wana wa manabii waliomjia. Ingawa Naamani huenda alishangaa kidogo, kwa furaha alimpa Gehazi zaidi kuliko vile alivyoomba, na akawaamrisha watumishi wake wawili kubeba vyombo hadi mahali pa siri ambapo Gehazi alitayarisha kuvificha (mstari 24 wa pembezoni).

 

Hata hivyo, Elisha alimwambia waziwazi kutokana na tendo la uongo wa Gehazi aliporudi na akamwambia kuwa ugonjwa wa ukoma aliopona Naamani ungehamishiwa kwake. Akiwa mtumishi wa nabii mkubwa wa Mungu na baada ya kushuhudia nguvu za Mungu katika matukio mengi sana kwa mkono wa Elisha, tunaweza kufikiria kuwa haiwezekani Gehazi kutenda jambo la aina hiyo. Lakini yaelekea utajiri wa dunia hii ya sasa ulikuwa wa maana zaidi kwake kuliko kitu kingine chochote. Yeye kwa uchoyo alitafuta zawadi, na ingawa alipata zawadi kubwa, kutokana na mawazo dunia, haikumpatia furaha au shangwe ya kudumu au furaha, ila badala yake alipata huzuni, maumivu na kukataliwa. Sisi sote ni watu wa kufa ni sawa na yule mkoma, "tunaugua" na tunakufa. Na sisi pia tunaweza kumtafuta Mungu wa Israeli ili tuweze kusafishwa kama alivyofanya Naamani. Kabla Naamani hajaponywa ilitakuwa kunyenyekea mbele za Mungu na kutii amri amri zake, na hivi ndivyo inavyotupasa sisi pia. Yule mfalme asiye na imani, Yehoramu alimwamini na kumtambua Mungu pale tu alipoona kuwa kwa kufanya hivyo anapota manufaa yeye. Ni lazima tuzingatie na kutenda kana kwamba Mungu yuko pamoja nasi; tusimkatae Mungu. Na turidhike na vitu tulivyonavyo na tena tusiache kazi ya Mungu kwa ajili ya kutafuta mambo ya dunia hii kama Gehazi alivyofanya.

 

MAKTABA REJEA

Historia ya Biblia (H.P.Mansfield) Kitabu cha 5 Namba 5

 

MASWALI YA VIFUNGU

1. Eleza namna ukoma unavyotumiwa na Mungu kuwakilisha dhambi.

2. Fafanua Naamani ilimpasa afanye nini ili aweze kupona. Fafanua matendo yake muhimu aliyopaswa kufanya na tabia aliyopaswa kuwa nayo.

3. Je, kunauhusiano gani kati ya kusafishwa kwa Naamani na ubatizo?

4. Fafanua uchoyo wa Gehazi na matokeo yake

 

MASWALI YA INSHA

1. Fafanua uponyaji wa Naamani na uonyeshe jinsi Naamani alivyopata kujua kuwa unyenyekevu na kumtii Mungu ilikuwa ni muhimu sana kwa ajili ya kusafishwa kwake.

2. Fafanua kuhusu uchoyo wa Gehazi na hukumu ya Mungu na ueleze kwa ufasaha tunaweza kujifunza nini kutokana na habari hili

 

Swahili Title
187 NAAMANI MTU WA SHAMU
English files
Swahili file
Literature type
Sub type
Sub sub type