189. KUDHOOFIKA NA KUPELEKWA UTUMWANI KWA MAKABILA KUMI YA KASKAZINI
"BWANA akawaghadhabikia sana Israeli, akawahamisha mbali na uso wake"
Katika somo letu la mwisho tulitafakari kuhusu maisha ya Yona na ujumbe wake kwa watu wa Ninawi. Lilikuwa ni hili taifa la Ashuru ambalo lingewachukua Israeli kuwapeleka uhamishoni kama miaka 100 baada ya mahubiri ya Yona. Ingawa Yehu aliwaangamiza watu wamwabuduo Baari, lakini bado waliendelea katika dhambi za Yehoboamu, ambazo kwa hizo aliwakosesha Israeli kutenda dhambi kama walivyofanya wafalme wa Israeli waliomfuata baadaye nalo taifa liliendelea kufifia kiroho. Hatimaye, wakati wa kutawala kwake Hosea, Israeli ilitekwa na Ashuru na kuchukuliwa utumwani. Katika somo hili tutafuatilia kufifia huku na na kilichosababisha yatokee, ili tuweze kujifunza kutokana na kushindwa kwa Israeli.
2 Wafalme 17
KUDHOOFIKA KWA ISRAELI – 2 Wafalme 17:1-6
Kuanzishwa kwa ibada ya uongo na Yeroboamu, ulikuwa ndiyo mwanzo wa kufifia kwa Israeli. Ufalme wa Kaskazini haukuwa imara katika Kweli ya Mungu. Katika utawala wa Hoshea, mfalme wa mwisho wa Israeli inakumbukwa kwamba yeye, "akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, ila si kama wafalme wa Israeli waliomtangulia" (2 Wafalme 17:2). Hoshea alifanya jaribio hafifu tu la kutaka kuleta uamsho katika miaka 9 ya kutawala kwake. Ingawaje hakuwa mwovu kama wafalme waliotawala kabla yake, kwa wakati huu imani tu uwezo ingeweza kuzuia hali hii ya kufifia isitokee. Badala ya kutafuta msaada wa BWANA, mfalme Hoshea alitafuta ushirikiano na So, mfalme wa Misri. Alifikiri kuwa Misri ingekuwa nguvu yake na kwa hiyo akaacha kupeleka kodi kwa mfalme wa Ashuru (mstari 4). Israeli ambao walikuwa wametoka Misri siku za Musa, kwa mkono wa BWANA na sasa wakawa wamegeuka kutafuta msaada kwa wa Misri. Nabii Hosea anawalinganisha Israeli sawa na "njiwa mpumbavu; asiye kuwa na fahamu" (Hosea 7:11).
Wakati Shalmanesa, mfalme wa Ashuru, alipofahamu kuwa Israeli wamekataa kulipa kodi, jeshi lake likakwea na kuanza kuangaamiza. Na tena kwa ukatili aliteketeza miji kwa moto na kuanza kuwaangamiza watu; Hoshea akachukuliwa hadi Ninawi na kufungwa gerezani. Na hatimaye Isrtaeli walitekwa na kutawanywa.
KILICHOSABABISHA ISRAELI KUDHOOFIKA - Mistari 7-23
Katika 2 Wafalme sura 17 mstari 7-23 sababu ya kuhamishwa kwa Israeli inaelezwa waziwazi. Mungu ni mvumilivu na ni mwingi wa rehema, lakini hatawaacha waovu bila kuwaadhibu. Israeli walikuwa na nafasi tele ya kutubu, lakini walishupaza shingo zao wakakataa kuwasikiliza manabii wa Mungu. Angalia dhambi nyingi ambazo Israeli walizitenda ambazo zilisababisha BWANA kuwaacha: 2 Wafalme 17
mstari 7- walimtenda BWANA dhambi kwa kuabudu miungu mingine.
mstari 8- walifuata matendo maovu ya mataifa yaliyowazunguka.
mstari 9- kwa walijenga mahali pa juu walipotoa kafara kwa vinyango vyao.
mstari 10-walitengeneza sanamu na vichana.
mstari 11-walimkasirisha BWANA kwa kufukiza uvumba kwa miungu yao.
mstari 12-walitumikia vinyango.
mstari 13-14-hawakuwasikiliza manabii ambao BWANA aliwatuma kuonya juu ya uovu wao.
mstari 15-walidharau sheria za BWANA na agano alilolifanya na baba zao, wakawa batili au watupu kwa ajili ya kufuata mataifa yaliyowazunguka.
mstari 16-walitengeneza ndama wawili wa kuyeyusha na kuabudu jeshi la mbinguni na wakamwabudu Baari.
mstari 17-waliwatoa wana wao na binti zao kwa kuwapitisha katika moto.
BWANA hakuwa tayari kuwavumilia zaidi. Walikuwa wameinajisi nchi yake, na kwa hiyo Mungu, "akawahamisha Israeli mbali na uso wake, kama alivyokuwa amesema, kupitia kwa watumishi wake manabii". Kwa hiyo Israeli wakawa wamehamishwa kutoka katika nchi yao hadi Ashuru (mstari 23). Tena katika sura 18:12 Mungu anasisitiza sababu ya utumwa wao, "kwa sababu hawakuitii sauti ya BWANA, Mungu wao, bali waliyaharifu maagano yake ambalo Musa mtumishi wa BWANA, aliwaamuru, wasikubali kuyasikiliza wala kuyatenda".
MWANZO WA WASAMARIA - Mstari 24-41
Waisraeli wengi walipelekwa utumwani Ashuru na wakatawanywa sehemu mbalimbali katika Ashuru; na watu wa Ashuru wakaleta wageni kuja kuishi katika Israeli. Kwa njia hii kukawa na vikundi vichache vya watumwa waliotawanywa katika dola yote, ili kupunguza uwezekanao wa kutokea kwa maasi. Katika mstari 24 tunaambiwa kuwa, "Naye mfalme wa Ashuru akaleta watu kutoka Baberi, na Kutha, na Ava, na Hamathi, na Sefarvaimu, akawaweka katika miji ya Samaria badala ya wana wa Israeli". Kwa hiyo mchanganyiko wa watu kutoka katika mataifa mbalimbali wakaletwa kuishi ndani ya Isreali. Baada ya muda, BWANA akapeleka simba kati ya hao watu ambao walikuwa wageni, kwa sababu hawakumjua Mungu (mstari 25). Watu hawa walipeleka ombi lao kwa mfalme wa Ashuru, wakalalamika kwamba matatizo haya yalikuja kwa sababu walikuwa hawamwabubu Mungu wanchi ile kwa usahihi (mstari 26). Ili kutatua tatizo, ndipo Ashuru wakawarudisha baadhi ya makuhani ili kuwafundisha wageni "kuhusu Mungu wa nchi". Kumbuka aina ya watu waliofanywa kuwa makuhani (1 Wafalme 12:26-33). Kwa hiyo aina ya ibada ya uongo ilianzishwa, "wakamcha BWANA, na wakaitumikia miungu yao wenyewe" (mstari 33). Huu ulikuwa ni mchanganyiko wa ibada ya ukweli na ibada ya uongo, waka anzisha nao makao yao makuu katika Samaria kwa hiyo wakajulikuwa kuwa ni Wasamaria. Yesu alipozungumza na mwanamke Msamaria alimwambia "Ninyi mwaabudu msichokijua".
ISRAELI BADO HAWAJAKUSANYWA
Ufalme wa kaskazini ulitawanywa katika dunia yote, lakini siku inakuja ambayo mataifa yote mawili Israeli na Yuda yataungana na kuwa taifa moja na kuwa chini ya mfalme wao mmoja mwenye haki, Bwana Yesu Kristo (Ezekieli 37: 16-28). Hosea, ambaye aliandika mengi kuhusiana na matendo maovu na kurudi nyuma kwa Israeli alitabiri kuhusu wakati huo wa kukusanywa kwao akisema, "Ndipo wana wa Yuda na wana wa Israeli watakusanywa pamoja na kumteua mmoja ambaye ndiye atakuwa kiongozi wao (Bwana Yesu Kristo)", sura 1:10-11; 3:4-5; 6:1-3. Tunaona baadhi ya sehemu za unabii ukitimia ambapo Israeli wakirudi katika nchi yao, lakini unabii utatimia kwa ukamilifu wakati Yesu Kristo, kwa kumtumia Eliya, atakapowarejesha "kama siku ya kale".
FUNDISHO KWETU
Ni matukio ya hatari iliyoje ambayo tumekuwa tukiyatafakari. Tunaona kutawanywa kwa makabila kumi ya Israeli, na Mungu ambaye aliruhusu tukio hili litokee, ingawaje ndiye Mungu aliyekuwa amewaleta katika nchi na kuwastarehesha humo kwa baraka nyingi. Tukishafahamu sababu ya tukio hili la kutawanyika, tunaweza kujifunza sisi wenyewe somo muhimu katika habari hii. Kwanza, Israeli walishindwa kwa kuwa waliiharibu ibada ambayo Mungu aliianzisha kupitia kwa Musa. Tunatakiwe tuwe makini na tuendelee kudumisha mafundisho ya kweli na kumwabudu Mungu (Wagalatia 1:6-9; 2 Timotheo 3:14-17; 2 Petro 3:15-18). Israeli walianzisha vitendo viovu, na vitendo hivi walivifanya kwa njia mbili;kwa njia ya hadharani na kwa njia ya sirini, kwa kutoa dhabihu wana wao na binti zao kwa kuwapitisha katika moto na kumbadili Mungu wa Kweli kwa miungu ya mataifa. Tunatakiwa tujitenge kabisa na sanamu, kama vile, kitu chochote kinachosababisha tusimtumikie Mungu kwa moyo wote na badala yake tukawa tukatumikia kitu kingine (1 Yohana 2 :15-17; 5: 21). Israeli alikuwa na shingo ngumu, alikataa kusikiliza sauti za manabii wa BWANA, wakaifanya mioyo yao kuwa migumu kwa kutotii amri zake. Tunatiwa moyo kila wakati tufungue mioyo yetu kwa Mungu wetu, na tuwe tayari kupokea Neno lake na siyo kuasi kwa kufanya kinyume cha mapenzi yake (Isaya 57:15-17; 66 :1-2).
Kama vile wakati wa Wasamaria, siku hizi pia zimejaa mafundisho potofu na mfumo wa dini za uongo, na maneno ya Yesu ndiyo yanayotuongoza kwamba "wamwabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli" (Yohana 4:23). Na tuyaone masomo haya wazi wazi na kwa hiyo tujiweke wenyewe wakfu kwa ajili ya kumtumikia Mungu kila wakati. Ni lazima tufahamu kuwa dunia na mambo yake, starehe, maslahi na michezo siyo tu kwamba vinatuondoa kwa Mungu; bali pia vinatuzingira katika njia ambazo hatuwezi kumpendeza Mungu!
MAKTABA REJEA
Njia ya Mungu ya kutoshereza mahitaji (R.Roberts) - Sura 19,20.
Historia ya Biblia (H.P. Mansfield) - Kitbu cha 5, Namba 11 na 12, ukurasa 175-186.
Huduma za manabii (R.Roberts na C.C .Walker) - ukurasa 95-98
MASWALI YA VIFUNGU
1. Ni sababu gani iliyosababisha Israeli kuchukuliwa na Ashuru na kupelekwa utumwani?
2. Je dini ya dini ya Wasamaria ilianzishwaje?
3. Orodhesha matukio na masharti yatakayosababisha Israeli kurudi tena katika nchi yao.
MASWALI YA INSHA
1. Je, ninani aliyekuwa mfalme wa mwisho wa Israeli na baadhi ya sababu zilizosababisha kufifia na kuhamishwa kwa Israeli kwenda utumwani?
2. Je, tunaweza kujifunza nini kutokana na hali ya kuharibika kiroho kwa Israeli ambayo ilisababisha kutekwa kwao na kuchukuliwa na Ashuru utumwani?