CSSA — Somo 096: Yesu Anasalitiwa na Kukamatwa

Swahili

SOMO 096 • YESU ANASALITIWA NA KUKAMATWA

“Si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.” — Mathayo 26:39

Mathayo 26:36–56; Marko 14:32–50; Luka 22:39–53; Yohana 18:1–12

SHABAHA

Kuonyesha utii wa Yesu kwa Baba yake katika Gethsemane, jinsi Yuda alivyomsaliti, na jinsi Yesu alivyojikabidhi bila kupigana ili Maandiko yatimizwe.

KATIKA BUSTANI YA GETHSEMANE

Baada ya chakula cha mwisho, Yesu alienda pamoja na wanafunzi wake hadi Gethsemane katika Mlima wa Mizeituni. Akawaambia wengi wao wakae, kisha akawachukua Petro, Yakobo na Yohana mbele kidogo. Yesu alihuzunika sana kwa sababu alijua mateso na kifo vilikuwa karibu.

Akaanguka kifudifudi na kuomba: “Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.” Yesu alikuwa na mapenzi ya kibinadamu na alihisi uzito wa majaribu, lakini kwa hiari alichagua kumtii Mungu.

KESHI NA KUOMBA

Yesu aliporudi kwa wale watatu aliwakuta wamelala. Akawaambia: “Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu” (Mathayo 26:41). Wanafunzi walimpenda lakini nguvu zao zilikuwa dhaifu.

Yesu akaomba tena, akijisalimisha kwa mapenzi ya Baba yake. Luka anaeleza kwamba malaika kutoka mbinguni alimtia nguvu. Hapa tunaona tofauti kati ya Mungu na Mwana wake: Yesu alimwomba Baba, naye Mungu akamtia nguvu.

YUDA ANAONGOZA WALIOMKAMATA

Yuda alijua mahali pale kwa sababu Yesu alikuwa amekwenda huko mara nyingi pamoja na wanafunzi. Akafika akiwa ameongoza kundi la watu waliotumwa na viongozi wa hekalu, wakiwa na taa na silaha.

Yesu akawatokea mbele na kuwauliza walimtafuta nani. Waliposema, “Yesu Mnazareti,” akajibu, “Ni mimi.” Yohana anaeleza kwamba walirudi nyuma na kuanguka chini. Yesu hakujaribu kujificha wala kukimbia.

BUSU LA USALITI

Yuda alikuwa amewapa ishara: yule atakayembusu ndiye Yesu. Akamkaribia na kusema, “Rabi,” kisha akambusu. Hivyo akamsaliti kwa ishara ambayo kwa kawaida ilikuwa ya urafiki.

Wakati watu walipomkamata Yesu, wanafunzi wakauliza kama wapigane. Petro akachomoa upanga na kukata sikio la mtumishi wa Kuhani Mkuu. Yesu akamzuia na, kama Luka anavyosema, akamponya mtu huyo. Akamwambia Petro aurudishe upanga wake.

YESU ANAJIKABIDHI

Yesu angeweza kuomba msaada mkubwa kutoka kwa Baba yake, lakini alijua Maandiko yalipaswa kutimia. Alikuwa amekuja kufanya mapenzi ya Mungu, na sasa akajikabidhi kwa wale waliomkamata.

Aliwaambia waache wanafunzi waende zao. Wanafunzi wote wakamwacha na kukimbia. Yesu akafungwa na kupelekwa kwanza kwa Anasi, kisha katika mashitaka yaliyofuata.

FUNDISHO KWETU

Gethsemane inatufundisha kwamba utii unaweza kuwa mgumu sana. Yesu hakutenda dhambi hata alipokuwa chini ya shinikizo kubwa. Alitafuta nguvu kwa sala na akasema, “Mapenzi yako yatimizwe.”

Tunapojaribiwa, tusitegemee nia nzuri peke yake. Tunahitaji Neno la Mungu, sala na unyenyekevu. Petro alijaribu kutatua tatizo kwa upanga, lakini Yesu alionyesha njia ya utii na kujitoa kwa Mungu.

MASWALI

Majibu Mafupi

1. Yesu na wanafunzi walienda wapi baada ya chakula?

2. Ni wanafunzi gani watatu aliowachukua mbele zaidi?

3. Yesu aliomba nini kuhusu “kikombe”?

4. Aliwakuta wanafunzi wakifanya nini?

5. Aliwaambia wafanye nini ili wasianguke katika majaribu?

6. Ni nani aliyemtia nguvu Yesu?

7. Ni nani aliyeongoza kundi lililokuja kumkamata?

8. Yuda alitumia ishara gani?

9. Petro alifanya nini?

10. Yesu alimwambia Petro afanye nini?

11. Wanafunzi walifanya nini Yesu alipokamatwa?

Majibu ya Kina

12. Eleza maombi ya Yesu katika Gethsemane na jinsi yanavyoonyesha utii wake.

13. Eleza kukamatwa kwa Yesu tangu Yuda alipofika hadi wanafunzi walipokimbia.

14. Kwa nini Yesu hakuruhusu wanafunzi wake kupigana?

Majibu ya Nyongeza

15. Tukio la Gethsemane linaonyeshaje kwamba Yesu si Mungu Baba mwenyewe?

16. Tunajifunza nini kutokana na maneno, “roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu”?

Swahili Title
096 YESU ANASALITIWA NA KUKAMATWA
African text
CSSA
Translator 1
Veslin
Literature type
Sub type
Sub sub type