Exploring the Bible - 14

Swahili

NYAKATI ZA WAAMUZI NA WAFALME

 

Somo la 14 Kusoma 2 Samuel 7

 

Waamuzi wa Israeli.

 

Baada ya kifo cha Joshua na wazee waliomfuata, Israeli iligeuka haraka na kuacha kuabudu Yahweh Mungu wao na kuanza kufuata tabia ya kuabudu sanamu ambayo yalikuwa nayo mataifa ya nchi (Waamuzi 2:6-13). Kwa sababu ya uovu wao Mungu aliruhusu maadui wa Israeli kuishinda ili imrudie kwa ajili ya kutaka msaada na usalama.

Katika kipindi cha miaka 400 iliyofuata Mungu aliinua msululu wa watu waaminifu waitwao Waamuzi waikomboe Israeli kutoka mkononi mwa wale waliowakandamiza na kuwatia moyo ili warudi kwa Mungu wao (Waamuzi 2:16-19) kwa kusikitisha kila Mwamuzi alipokufa watu wengi haraka waligeukia tena kuabudu sanamu na Mungu akaruhusu tena mataifa ya jirani kuwakandamiza. Watu walipochoshwa na udhalimu walimlilia Mungu tena naye alimuinua Mwamuzi mwingine. Baadhi ya Waamuzi waliotawala katika kipindi hiki walikuwa watu kama Gideoni, Samson na Jephthah, Mwamuzi wa mwisho kuitawala Israeli alikuwa Samweli. Kipindi cha Waamuzi kimeelezwa kwa maneno haya “Katika siku hizo hapakuwa na mfalme katika Israeli: kila mtu alifanya kile alichoona kuwa ni sahihi.” (Waamuzi 21:25).

 

Ruti Mmoabu

 

Kitabu hiki kidogo kinaeleza kisa kilichotokea katika siku zile Waamuzi walipokuwa wanatawala (Ruti 1:1). Ingawa kitabu cha Waamuzi kinaeleza juu ya uovu uliotapakaa katika nchi hapa tuna habari za kusisimua kuhusu imani ya Ruti, mwanamke wa kimoabu ambaye alikiri kwa mama mkwe wake Naomi, “Watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako, Mungu wangu.” (Ruti 1:16) Alizikataa sanamu za moab halafu akaenda na Naomi Bethlehemu alipokutana na mcha Mungu Boaz ambaye alimwoa. Wazao wao ni pamoja na mfalme Daudi (Ruti 4:22) na kutoka kwake, Bwana wetu Yesu Kristo (Mat. 1:5, 16).

 

Samueli Mwamuzi wa Mwisho

 

Vitabu viwili vya Samueli vinazungumzia historia ya Israeli tangu mwisho wa enzi za Waamuzi hadi uteuzi wa sauli halafu daudi kama wafalme wa Israeli. Samueli, kama Mwamuzi na nabii (Matendo 3:24) ndiye aliyeanzisha msingi wa “Ufalme wa Israeli”

 

Watu Watamani kuwa na Mfalme

 

Japo Samueli alikuwa mwaminifu akifanya kazi yake kama Mwamuzi kila wakati watu walikuwa wakiangalia mataifa yaliyowazunguka na hatimaye wakamwendea samueli na ombi la kuwa na Mfalme: “Tuwekee Mfalme wa kutuhukumu kama mataifa mengine” (1 Samueli 8:4-5) Samueli hakufurahishwa na ombi hilo hivyo alimwomba Mungu ampe jibu. Jibu la Mungu lilikuwa lenye kuelimisha sana: “Sikiliza sauti ya watu kwa yote wanayokwambia: kwa kuwa hawajakukataa bali wamenikataa mimi kwamba nisiwatawale tena” (aya ya 7). Mungu alikuwa mfalme wao lakini walikuwa hawajakiri wala kuelewa ukweli huu.

Mungu aliwakubalia ombi lao na kumchagua Sauli kuwa mfalme wao wa kwanza, mwanaume ambaye umbo lake zuri liliwapendeza. Hata hivyo sauli alishindwa kutii amri mahsusi za Mungu na hivyo akapokonywa ufalme (1 Samueli 15:22-28)

 

Daudi ateuliwa kuwa Mfalme

 

Kwa sababu ya kushindwa kwa Sauli kufuata maagizo ambayo Samueli alimpa Mungu alimwambia Samueli kuwa atampata mtu anayefaa zaidi kuwa mfalme wa Israeli. Samueli alimwambia Sauli: Bwana amemtafutia mtu anayekubalika moyoni mwake na bwaba amemuamrisha kuwa kiongozi wa watu wake” (1 Samueli 13:13-14). Daudi mwana wa Yesse kijana mchunga kondoo wa bethlehemu, ndiye aliyechaguliwa na Mungu. Paulo anamuelezea Daudi hivi: Nimempata Daudi mwana wa Yesse, mtu anayekubalika moyoni mwangu atakayetimiza matakwa yangu yote (Matendo 13:22)

 

Ukweli Kuhusu Daudi

 

Baada ya kukalia kiti cha enzi Daudi alitawala kwa muda wa miaka saba na nusu hukop Hebron akitawala Israeli yote akiwa Yerusalemu (2 Samueli 5:4-5). Aliandika mengi ya mashairi yaliyomo katika Zaburi ambayo yanatuonyesha jinsi alivyompenda Mungu. Mifano ifuatayo inaonyesha hivyo:

“Nifundishe Ee Bwana njia ya sheria zako nami nitaishika hadi mwisho” (Zaburi 119:33)

 

“Oo Jinsi niipendavyo sheria yako! Ndivyo ninavyowaza kutwa nzima” (Zaburi 119:97)

 

“Neno lako ni taa ya miguu yangu na mwanga wa njia yangu” (Zaburi 119:105)

 

  • Aliwahi kuwa mchunga kondoo mwenye bidii katika ujana wake na hivyo aliweza kuandika kwa hisia zinazofaa na uelewa: “Bwana ni mchungaji wangu sitakuwa na dhiki.” (Zaburi 23:1)

  • Bwana wetu Yesu Kristo anatambulika mahsusi kama mwana wa Daudi (Mathayo 22:41-46; 1:1; Warumi 1:1-3)

  • Mungu alimpa daudi ahadi nzito ambayo imeandikwa katika 2 Samueli 7. Ahadi hii inabashiri kuja kwa Yesu ambaye atakuwa mwana wa Daudi na wakati huo huo mwana wa Mungu.

 

Kuna mambo ya kweli na ya kupendeza kuhusu Daudi utakayoona utakaposoma habari za maisha ya Daudi.

 

Ahadi kwa Daudi (2 Samueli 7:12-16)

 

Ahadi hii ni “mojawapo kati ya ahadi muhimu katika Biblia” ihusuyo kazi ya Bwana wetu Yesu Kristo. Tunaposoma 2 Samueli 7 tunaona kwamba Daudi alitamani kumjengea Mungu nyumba. Ingawa Mungu alipendezewa na kusudio la Daudi, alikuwa na mipango mingine moyoni mwake. Badala yake ni yeye ambaye angemjengea Daudi nyumba, si nyumba ya miti na mawe bali familia ambayo msingi wake ungekuja kuwa Bwana wetu Yesu Kristo ambaye angekuwa mwana wa Daudi na mwana wa Mungu. Tusome aya ya 12-16.

 

Aya ya 12

 

“Na siku zako zitakapotimia na utakapokuwa umeisha lala kaburini na baba zako”

Ahadi hii ingetimia baada ya kufa na kuzikwa kwa Daudi.

“Nitasimamisha uzao wako baada yako” Mungu angesimamia ulimizo sahihi wa ahadi hii.

“Utakaotoka katika tumbo lako”

Aliyezungumziwa katika ahadi hii angekuwa wa nasaha iliyonyooka toka kwa Daudi. Yesu Kristo ndiye huyo anayezungumziwa . Fikiria Luka 1:30-33 na maneno ambayo Malaika Gabriel alimwambia Maria.

 

  • Maria angepata mtoto ambaye angeitwa Yesu (aya ya 31)

  • Mtoto huyu pia angekuwa mwana wa yule aliye juu kabisa ambaye ni Mungu (aya ya 32)

  • Angekalia kiti cha enzi cha Daudi, baba yake (aya ya 32)

  • Angetawala nyumba ya Yakobo (yaani Israeli) milele (aya ya 33)

 

Ahadi hii haijatimizwa. Alipokuja mara ya kwanza Wayahudi walimkana (Yesu) wa Nazareti kama mfalme wao na wakamsulubu (Yohana 19:13-16). Lakini Mungu ametuambia kuwa Yesu atarudi duniani (Mat 1:11) na kusimamisha ufalme wa Mungu utakaodumu milele (Daniel 2:44; Zaburi 72:17).

Nabii Isaiah pia alimtambua Yesu kuwa ndiye ambaye angekalia kiti cha Daudi (Isaiah 9:6-7; Luka 2:11)

Yesu mwenyewe alisema kuwa yeye ndiye mwana wa daudi aliyahidiwa (Ufunuo 22:16) na Mtume Petro alithibitisha hivyo baada ya kufufuka kwake (Matendo 2:34-36)

 

Aya ya 13

 

Atajenga nyumba kwa ajili ya jina langu”

 

Hili linatumika kiroho na kikawaida. Yesu atasimamia ujenzi wa nyumba ya ibada wakati wa Ufalme, “nyumba ya sala” kwa ajili ya mataifa yote (Isaiah 56:7; Zakariah 6:12). Yeye pia ni jiwe la msingi la nyumba ya kiroho ya Mungu, iliyojengwa kwa wanaume na wanawake wenye imani (Waefeso 2:20; Waebrania 3:6)

 

Nitaanzisha kiti cha enzi cha ufalme milele”

 

Mungu atanzisha ufalme wake na kumweka Yesu Kristo kama mfalme, kama Daudi alivyokuwa kabla yake (Yeremia 23:5-8; 33:15-16; Amos 9:11; Isaiah 9:6-7; Zaburi 132:11 linganisha na Matendo 2:30). Mji mkuu wa ufalme huu wa dunia nzima yatakuwa yerusalemu (Yeremia 3:17) kama ilivyokuwa enzi za Daudi.

 

 

Aya ya 14

 

Nitakuwa Baba yake naye atakuwa Mwanangu”

 

Mwana wa Daudi (mzao wake) pia atakuwa mwana wa Mungu. Hili kwa hakika linazungumzia Yesu Kristo kama Agano Jipya linavyofafanua (Waebrania 1:5).

Unabii huu mzito unabashiri kuwa Yesu Kristo atatwala duniani katika ufalme wa Mungu ulioanzishwa upya. Tunaweza kuelewa msisimko wa Maria Gabriel alipomwambia kuwa ni yeye aliyetokana na Daudi ambaye angemzaa mtoto ambaye angekuwa mwana wa Daudi na mwana wa Mungu” (Luka 1:35)

Katika Zaburi, Daudi pia alizungumzia kifo na ufufuo wa Yesu Kristo. Petro ananukuu Zaburi ya Daudi inayotabiri mambo haya (Matendo 2:22-36; tazama Zaburi 16:8-11; 132:11; 110:1). Alitabiri kuwa Yesu angepaa mbinguni lakini hakika angekuja tena duniani (Zaburi 110:1 linganisha na Matendo 2:34) kwa kuwa sasa hawezi kufa (Warumi 6:9) Yesu Kristo atakuwa mfalme katika ufalme wa milele. Watakaokuwa wanamsaidia ni watu wenye imani wa nyakati zote wakishiriki katika kutokufa na kutawala na kuishi naye (Ufunuo 5:10)

Isaiah anatuambia juu ya mabadiliko ya serikali za kidunia yatakayotokea wakati huo. Ufalme utakuwa umejengwa kwenye misingi ya kweli na uadilifu ili iwepo amani duniani kote Isaiah 2:2-4; 32:17) Katika Zaburi 72 Daudi anatupa picha nzuri sana ya ufalme huu pamoja na mabadiliko ya kijamii ambayo Yesu Kristo ataleta kwa kuwa yeye ni mwenye haki na mwenye huruma.

Sasa tunaweza kuelewa kwa nini Yesu alifundisha wafuasi wake kusali: “Ufalme wako uje. Itafanyika duniani kama mbinguni” (Mathayo 6:10)

 

 

MUHTASARI

 

  • Watu walikuja kwa Samweli, mwamuzi wa mwisho wa Israeli na kuomba wapewe mfalme awatawale kama mataifa yaliyowazunguka yalivyokuwa yanatawaliwa. Kwa kufanya hivyo walimkataa Mungu, mfalme wao wa kweli (1 Samueli 8:5-7)

  • Mfalme wa kwanza wa Israeli alikuwa Sauli lakini kwa kuwa alilichukulia neno la Mungu ki-mzaha Mungu alimnyang’anya ufalme (Samueli I, 15:22-23)

  • Mungu alimchagua Daudi kuchukua nafasi yake kwa sababu alikuwa mwanaume “aliyempendeza Mungu” (1 Samueli 13:14; Matendo 13:22)

  • Mungu alipendezewa na Daudi na akaahidi kuwa atapata mwana ambaye atakalia kiti chake cha enzi “milele” (2 Samueli 7:12-16) Mwana huyu atakuja kuwa Mwana wa Daudi na mwana wa Mungu wakati huo huo.

  • Ahadi hii inahusiana na Yesu Kristo aliyezaliwa katika nasaba ya Daudi na kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwa kumfunika Maria akawa pia mwana wa Mungu (Luka 1:30-33; Waebrania 1:5)

  • Yesu Kristo atakuja tena kuanzisha upya ufalme wa Mungu duniani akitawala kutoka Yerusalemu kwenye kiti cha Daudi kilichoanzishwa upya (Jeremiah 3:5-8)

 

 

SOMO LA 14 – MASWALI

 

  1. Mungu aliinua watu fulani kutawala Israeli, watu hao waliitwaje?

  2. Biblia inasema nini kuhusu enzi za Waamuzi?

  3. Ni kukiri gani kulikofanywa na Ruti wakati alipotoka Moab na kwenda Israeli na Naomi?

  4. Waisraeli walikuwa wamemkataa nani walipomwomba Samueli awape mfalme wa kuwatawala?

  5. Mfalme wa kwanza wa Israeli alikuwa nani?

  6. Kwa nini Mungu alimteua Daudi kuwa mfalme?

  7. Ni ahadi gani kuu ambayo Mungu alimpa Daudi?

  8. Ni nani “mzao” ambaye Daudi aliahidiwa?

  9. Mzao huu ungekuwa mwana wa Daudi; angekuwa pia mwana wa nani?

  10. Luka 1:30-33 anatuambia nini kuhusu ahadi hii?

  11. Ufalme huu ulioahidiwa utakuwa wapi?

  12. Utaanzishwa lini?

  13. Ufalme wa Mungu utatofautiana vipi na dunia tunayoishi?

 

Swahili Title
NYAKATI ZA WAAMUZI NA WAFALME
Swahili file
Status
Added to Internet
African text
Christadelphian Bible Mission
Translator 1
Raphael Mkeya
Literature type