Exploring the Bible - 15

Swahili

UFALME WAGAWANYIKA – ISRAELI NA YUDEA

SOMO LA 15                                                                          Soma 1 Wafalme 11 na 12

Solomoni ajenga Hekalu Yerusalemu

Mfalme Daudi alitawala kwa muda wa miaka 40. Makao yake makuu yalikuwa Yerusalemu lakini tabernakulo yake ilikuwa Gibeoni na pale ndipo alipokuwa anatekelezea mambo yake ya ukuhani, akitoa sadaka na kuiongoza Israeli katika ibada.

Kama tulivyoona katika somo lililopita yalikuwa mapenzi ya Daudi kumjengea Mungu nyumba ili aweze kuishi katikati ya Israeli. Walakini Mungu alikuwa amemkatalia ombi lake, akisema badala yake yeye ndiye angemjengea Daudi nyumba (2 Samueli 7:11-16). Aliahidi kumpa mwana ambaye hatimaye angetawala kwenye kiti cha Daudi milele. Huyu mwana ndiye angejenga nyumba ya ibada kwa ajili ya mataifa yote ya ulimwengu. Unabii huu ulielekeza kwa kazi ya Yesu Kristo ya baadaye.

Hata hivyo Mungu alimwambia Daudi kwamba Solomon mwanawe ambaye angetawala baada yake angejenga hekalu au jumba Yerusalemu ambamo Israeli ingemwabudia Mungu. Mahali pale bado alama yake inajulikana kwa wale waliokwishaona picha za Yerusalemu. Ni ile sehemu tambarare iliyoinuka mashariki mwa Yerusalemu inayoukabili Mlima wa Mizeituni. Leo hii “Jengo la nusu duara lililoko kwenye mwamba” ambapo ni mahala patakatifu pa Waislamu ndilo lililosimama pale na ni la tatu kwa utakatifu katika ulimwengu wa Waislamu. Waislamu wanaamini kwamba Muhammadi, Nabii wao alidhuru sehemu hii. Pia ni mahala patakatifu pa kale pa Wayahudi, na tunaweza kuelewa kwa nini kuna ugomvi na uchungu kati ya Waarabu na Wayahudi kuhusu mahala hapo padogo. Kwa kuongezea dini kubwa za Kikristo zinaamini kuwa nazo zina haki ya kumiliki sehemu hiyo kwa sababu ya viwanja vyake vitakatifu ambavyo vinahusishwa na maisha ya Yesu.

Kuwapo kwa imani mbalimbali za kidini zenye kupingana  ambazo zote zinadai kuwa zina haki ya ki-Mungu za kumiliki Yerusalemu kunatusaidia kuelewa kwa nini suala hilo limekuwa lenye kubishaniwa kisiasa. Hivi ndivyo Mungu alivyotabiri zamani:- Yerusalemu ingekuwa “mwamba mzito kwa watu wote” (Zekaria 12:1-3)

Mungu alimwambia Daudi kuwa Solomoni angejenga hekalu Yerusalemu. Kwa hiyo katika miaka ya mwisho za maisha yake, Daudi alimpa Solomoni jukumu kali: Bwana amekuteua wewe kujenga nyumba ya makao yake: Jipe nguvu na ufanye hivyo (1 Mambo ya Nyakati 28 na 29). Baada ya kifo cha Daudi Solomoni alianza kuifanya kazi hii kuu na yenye utukufu. Hekalu, japo halikuwa kubwa sana, lilikuwa lenye kupendeza sana. Maelezo yake yanapatikana katika 2 Mambo ya Nyakati 2-7. Hekalu hilo hapo Yerusalemu pamoja na ukuhani uliokuwapo lilikuja kuwa kituo cha ibada na mafundisho cha taifa katika utumishi wake kwa Mungu.

Ufalme Unagawanyika (1 Wafalme 11-12)

Katika miaka yake ya baadaye Solomoni aligeuka na kuacha kumfuata Mungu. Alioa wake wa mataifa au makabila mengine na kukumbatia ibada zao za kipaganikwa kuwajengea mahekalu ndani ya Israeli. Maelezo ya kusikitisha ya kuanguka kwake yanapatikana katika 1 Wafalme 11. Kwa sababu ya dhambi ya Solomoni, Mungu alimpelekea Nabii kumwambia kuwa baada ya kufa kwake ufalme wake ungegawanyika. Makabila mawili yangefungamana na nyumba ya Daudi ambapo mengine kumi yangejitenga na kuanzisha utawala wao wenyewe.

Baada ya kifo cha Solomoni, Rehoboam mwanaye alikalia kiti chake  cha enzi. Alitishia kupandisha kodi ambazo tayari zilikuwa kubwa mno, na kitendo hiki cha kipumbavu kilisababisha kuasi kwa makabila kumi ya kaskazini yaliyoongozwa na Jeroboam (1 Wafalme 12)


Kuanzia wakati huo na kuendelea taifa liligawanyika katika falme mbili

    • Ufalme wa Yudah:  Huu uliundwa na makabila mawili yaani kabila la Yuda na lile la Benjamini na makao yake makuu yalikuwa Yerusalemu. Wafalme walioitawala Yuda walikuwa wa uzao wa Daudi wa moja kwa moja. Ibada kwa Mungu iliendelea hekaluni Yerusalemu na iliendeshwa na Makuhani na walawi waliochaguliwa na Mungu.
    • Ufalme wa Israeli: Makabila mengine kumi, kwanza yaliungana chini ya Jeroboamu, mji wao mkuu ulikuwa Samaria. Hapakuwa na ukoo mmoja wa kifalme uliotawala kaskazini na hivyo kulikuwa na ugomvi na mauaji ya mara kwa mara kwa kuwa kila mmoja wa wagomvi hao alikuwa akidai kuwa ana haki ya kutawala. Hakuna hata mmoja wa Wafalme hawa aliyekuwa mwaminifu kwa Mungu.

Historia ya Falme hizi mbili imeelezwa katika vitabu vya Wafalme na 2 Mambo ya Nyakati pia kinaeleza habari za Wafalme wa Judah.

Mwisho wa Ufalme wa Israeli.

Ufalme wa Israeli kaskazini ulijengwa juu ya uasi-imani (yaani ule ambao umedondoka kutoka kwenye dini ya kweli au uliopotoka) na huu ulienea katika Betheli na Dani (1 Wafalme 12:26-33). Hili pamoja na uchu wa madaraka ya kisiasa lilikuwa chanzo cha shida na matatizo kwa watu.

Hata hivyo Mungu hakuwatupa mkono japo walikuwa wamezipa amri zake mgongo. Kwa huruma yake aliwapelekea Manabii kama Elijah na Elisha ambao waliwabembeleza kumrudia Mungu lakini ni wachache tu waliosikiliza. Baadhi ya vitabu vya Manabii hasa cha Hosea na cha Amos ni kumbukumbu la ujumbe wa Mungu kwa ufalme huu wa kaskazini.
Mwisho kabisa Mungu alishusha nguvu kuu ya Assyria juu yao. Walipinduliwa mwaka 720 kabla ya Kristo na kutawanyika katika himaya ya Assyria (2 Wafalme 17).
Baada ya hapo Waassyria walileta watu kutoka katika nyingine walizoteka na kuwakalisha katika Israeli. Watu hawa walikuja na ibada za uongo wakazichanganya na ibada ya kweli ya Mungu wa Israeli “Walimwogopa Bwana na kutumikia miungu wao” (2 Wafalme 17:33) Ibada hii ya kutatanisha nay a uongo iliendelea kuwapo hadi siku za Yesu. Watu hawa walijulikana kama wasamaria (angalia Yohana 4)

Ufalme wa Yuda

Japo yale makabila mawili ya kusini yaliendelea na ibada ya hekaluni Yerusalemu na japo Wafalme wake walikuwa wa uzao wa Daudi wao pia mwishowe walipotoka katika ibada ya kweli ya Mungu na kuwa waabudu sanamu. Wengi wa Wafalme waliotawala hawakuwa wacha Mungu na ni wachache ndio waliokuwa na imani sawa na Daudi Babu yao. Wakati mwingine hata Kuhani Mkuu alikataa kufuata njia ya kuabudu iliyoamuriwa na Mungu.
Mungu aliwapelekea Manabii kuwaambia  kwamba wasipomsikiliza atawapelekea Wababyloni kuharibu hekalu na mji wao sawia na kuwachukuwa wakiwa watumwa na kuwapeleka mbali na kwao.  Maonyo yake yalipuuzwa na ufalme ukapinduliwa na Babylon, miaka 130 tu baada ya Israeli kaskazini kupinduliwa na Assyria.


Unabii maarufu wa “miaka 70” wa Yeremiah.

Nabii Yeremiah aliishi Yerusalemu katika miaka hii mwisho ya ufalme wa Yuda  na aliwasihi watu wake  kukiri dhambi zao na kumrudia Mungu. Kushindwa kwao kupokea ujumbe wake kwa dhati kungesababisha Mungu amtume Nebukadineza mfalme wa Babyloni apambane nao. Angevunja ufalme wao na Yuda na kuwachukua mateka hadi Babyloni kwa muda wa miaka 70 na baada ya hapo kurudi kwenye mji wao (yeremiah 25: 8-12; 29:10-14).

Mashambulizi ya kwanza ya Nebukadnezza katika Yuda na usafirishaji wa mateka kwenda Babylon yalifanyika mwaka 606 kabla ya Kristo. Mnamo mwaka 536 kabla ya Kristo ikiwa ni miaka 70 bara bara baadaye ndipo Sairas mfalme wa Himaya ya Wamede-Ajemi ambao walirithi Babyloni alipotoa amri ya Wayahudi kurudi Yerusalemu (2 Mambo ya Nyakati 36:19-23).

Katika mwaka 586 kabla ya Kristo Nebukadnezza alifanya shambulio lake la mwisho Yerusalemu na kuharibu hekalu; akavunja kuta za jiji na kuchukuwa mateka wengi hadi Babyloni. Katika mwaka 516 kabla ya Kristo, miaka 70 baadaye Wayahudi walilijenga upya hekalu Yerusalemu (Ezra 6:15). Hivyo unabii huu ulihimizwa kikamilifu kama historia ilivyothibitisha.

Unabii wa Mungu kwa mfalme wa mwisho wa Yuda (Ezekieli 21:25-27)

Mfalme wa mwisho kukalia kiti cha enzi cha Daudi katika Israeli alikuwa Zedekiah. Alikuwa mfalme mwovu ambaye Ezekieli alimwita “Mwana mwovu na kafiri wa mfalme” (aya ya 25). Alikataa kwa kiburi tu kusikiliza maonyo ya Manabii, akachukuliwa mateka mwaka 586 kabla ya Kristo, Nebukadnezza alipoiharibu Yerusalemu.

Aya ya 26
                  “Ondoa kilemba na uvue taji”
Kama mchezo Zedekiah anaambiwa kuwa utawala wake umefikia kikomo cha ghafla na mkamilifu

Aya ya 27
                 “Nitaupindua, nitaupindua, nitaupindua.” Nabii asisitiza uharibifu mkubwa wa ufalme, kwa kurudia mara tatu neno “Kupindua”
 “Mpaka atakapokuja yule ambaye ni haki yake” Hapatakuwa na mfalme katika kiti cha Enzi cha Daudi tena mpaka Yesu Kristo atakapokuja kuchukua nafasi yake ya haki ambayo Mungu alimuahidi (tazama 2 Samweli 7:12-16; Luka 1:31-33)

“Nitampa”
Hapa Mungu anatoa garantii kuwa atafanya hivyo (Linganisha na Isaya 9:6-7; Luka 1:32; Mat. 3:20)


Ufalme Uliorudishwa, chini ya Kristo.

Yeremiah, aliyeishi wakati mmoja na Zedekiah mfalme wa mwisho wa Yuda pia alizungumzia kuja kwa Yesu Kristo kutawala kwenye kiti cha Enzi cha Daudi, katika utawala uliorudishwa wa Israeli (Jeremiah 23:5-8; 33:15-16)
Ili hizi ahadi zitimizwe Israeli haina budi kukusanywa na kuelimishwa upya ukweli kuhusu kazi ya Bwana, Yesu Kristo kama mkombozi na mfalme wao (Yeremiah 30:10-11; 46:27-28; Ezekieli 11:17-20; 37:21-28)

Unabii kuhusu kukusanywa upya kwa Israeli.

Kwa mwanafunzi wa Biblia unabii wa Mungu kuhusu Israeli ni garantii ya kushangaza kuwa tunaweza kuamini Biblia. Mungu mwenyewe amesema kuwa Israeli ni shahidi wake duniani.
“Wewe ni shahidi wangu, asema Bwana, kwamba mimi ni Mungu (Isaya 43:1, 10-13)
Kwa kifupi zinagatia baadhi ya nabii hizi:-

    • Kabla hawajaingia katika nchi ya Israeli wakati walipokuwa bado jangwani, Musa alitabiri mtawanyiko miongoni mwa mataifa kwa sababu ya utovu wa utii (kumbukumbu 28:63-68). Ni kwa usahihi kiasi gani unabii huu umetimizwa historia ya Wayahudi tangu mwaka wa 70 baada ya Kristo hadi sasa inaeleza.
    • Pia Musa alitabiri kujikusanya kwao tena kutoka miongoni mwa mataifa (kumbukumbu 30:1-5)
    • Nabii Yeremiah alieleza wazi wazi kutawanyika na kujikusanya upya (Yeremiah 30:10-11; 31:10)
    • Yesu vilevile alitabiri kutawanyika kwa Wayahudi kama matokeo ya matukio ya kutisha ya mwaka 70 baada ya Kristo. Tangu wakati huo Yerusalemu imekuwa chini ya watu wa mataifa. Wayahudi wakitawanyika katika kila nchi hapa duniani. Ni katika kipindi takribani miaka miaka mia moja tu iliyopita ndipo Wayahudi walipoanza kurudi katika nchi ya baba zao.Yerusalemu yenyewe hatimaye ilichukuliwa tena na Wayahudi mwaka 1967 baada ya karibu miaka 2000 ya mtawanyiko.
    • Zekariah (Nabii) alitabiri kuwa Wayahudi wangerudi katika nchi yao na kuidhibiti Yerusalemu kabla Yesu hajarudi (Zekariah 12:1-11)
    • Alitabiri kuwa Yerusalemu ingekuwa mikononi mwa Wayahudi lakini itakuwa chanzo cha mvutano wa mataifa na mataifa yote yataelekea mashariki ya kati kwa vita kabla Yesu Kristo hajajionyesha kwa Wayahudi (Zekariah 12:2-3; 9-10; 14:1-4)
    • Nabii Ezekieli alitabiri vita hii kuu katika mashariki ya kati katika “siku za baadaye zaidi” Wayahudi watakapokuwa wameikalia tena nchi ya Israeli (Ezekieli 38:8, 12). Tulishuhudia kuundwa kwa taifa la Israeli mwaka 1948.
    • Israeli itarudi katika nchi pasipo kuamini kuwa Yesu ni masiah. Watakiri ukweli huu pale atakapokuwa ametambulishwa kwao, na kuona  makovu ya majeraha yake katika viganja vyake (Zekariah 12:10, 13:6)
    • Mtume Paulo alizungumzia wakati ambao Wayahudi watakuwa wametolewa utando kwenye macho yao na hapo kutambua kuwa Yesu alikuwa Mkombozi wao (Warumi 11:25-27; linganisha na Isaya 59: 20-21)


UFUPISHO

    • Kwa kuwa Solomoni aliacha njia ya Mungu, ufalme uligawanyika baada ya kifo chake (1 Wafalme 11:11-13) mwanae Rehoboam alitawala juu ya makabila mawili akiwa Yerusalemu na Jeroboam alitawala juu ya makabila kumi yaliyobaki kaskazini.
    • Makabila mawili ya kusini yalijulikana kama ufalme wa Yuda na yale kumi ya kaskazini kama ufalme wa Israeli.
    • Mgawanyiko ulitokea mwaka 970 kabla ya Kristo (k.k) na ufalme wa kaskazini uliendelea hadi mwaka 720 k.k. ulipochukuliwa mateka na Assyria na kutawanyika (2 Wafalme 17:6, 18, 23)
    • Utawala wa kusini uliendelea kuwepo hadi 586 k.k. wakati Yerusalemu na hekalu vilipoteketezwa na Yuda kutekwa na Babyloni (2 Mambo ya Nyakati 36:17-20)
    • Walibakia Babyloni kwa miaka 70 kama Yeremiah alivyotabiri halafu wakarudi kujenga hekalu na yerusalemu upya (2 Mambo ya Nyakati 36:21-23)
    • Mungu alimwambia Zedekiah mfalme wa mwisho kuwa hapatakuwa na mfalme kwenye kiti cha enzi cha daudi mpaka yesu kristo atakapokuja kuanzisha upya Ufalme na kukaa kwenye kiti cha Daudi (Ezekieli 21:25-27)

MASWALI – SOMO LA 15.

    1) Ni mwana yupi wa Daudi aliyetawala Israeli baada ya kufa kwake?
    2) Alijenga nini kama mahali pa kuabudia pa Israeli
    3) Ufalme uligawanyika baada ya Solomoni. Taja majina ya falme mbili na idadi ya makabila ya katika kila ufalme.
    4) Utawala wa kaskazini ulipinduliwa lini na nani aliupindua?
    5) Ni utawala gani ulioipindua Yuda na kuteka watu wake?
    6) Mungu alimpelekea ujumbe gani mfalme wa Yuda? Na ni nani pekee ana haki ya kukalia kiti cha enzi cha Daudi?
    7) Yeremiah alitabiri muda ambao Yuda angekuwa utumwani, ulikuwa muda wa miaka mingapi?
    8) Kwa kupitia manabii wake Mungu alitoa unabii wa kushangaza kuhusu kujikusanya upya kwa Waisraeli. Toa mifano mitatu ya nabii hizi ukieleza jinsi zilivyotimizwa.


 

Swahili Title
UFALME WAGAWANYIKA
Swahili file
Status
Added to Internet
African text
Christadelphian Bible Mission
Translator 1
Raphael Mkeya
Literature type