Mei 17

Swahili

Mei 17

Sura ya kwanza ya Yoshua ilifanyika siku ya mwaka mpya. Tunapata hili kwa kurudi nyuma kutoka sura ya 4:19 (linganisha 3:2, 2:22, 2:1 na 1:11). Ilikuwa mwanzo mpya na enzi mpya. Musa alikuwa ameenda na Yoshua sasa ana kiongozi. Matukio yalitokea wakati wa masika wakati mavuno ya shayiri yalikuwa yameiva tayari kwa watu wa Mungu. Ujumbe kwa Yoshua uko wazi na unarudiwa - kuwa hodari na jasiri! Msingi wa ujasiri huu ulikuwa ukweli kwamba Mungu alikuwa pamoja naye (mstari wa 5). Mara ya mwisho Israeli walipokaribia nchi, waliwaogopa majitu (Hesabu 13:32). Sasa Mungu aliwaambia kwamba hakuna mtu anayeweza kusimama mbele yao (mstari wa 5) - hata majitu. Lakini Yoshua hakulazimika tu kuwa hodari na jasiri dhidi ya adui. Ilibidi awe hodari na jasiri sana ili kushika sheria ya Mungu (mstari wa 7). Yoshua aliambiwa atafakari sheria, mchana, na usiku (mstari wa 8). Kwa maneno mengine, Yoshua ilibidi asome Biblia kila siku na kufikiria kile alichokuwa amesoma! Daudi alitupa ushauri uleule (Zaburi 1:2). Kushika amri kunahitaji ujasiri ili kufanya kile ambacho wengine huenda wasipende na wengine huenda wasifanye. Inahitaji ujasiri kuwa tofauti. Jmbo hili linatufaa nasi hivi leo. Sote tunahitaji kuwa hodari na jasiri katika kuishi kama waumini. Matukio ya Isaya 7 ni tukio lingine ambapo kiongozi wa Mungu alihitaji ujasiri. Wafalme wawili, mfalme wa Shamu na mfalme wa Israeli, waliandamana na majeshi yao dhidi ya mfalme wa Yuda. Mfalme wa Yuda, Ahazi, na watu wake waliogopa sana (mstari wa 2). Wafalme hao wawili walitaka kuchukua nafasi ya Ahazi kama mfalme. Mungu alimwambia Ahazi kupitia nabii Isaya asiogope (mstari wa 4). Ujumbe huu ulikuja mahali palepale ambapo Hezekia baadaye alihitaji ujasiri (Isaya 36:2). Mungu alikuwa tayari kumpa Ahazi ishara, ili awe na imani na Mungu. Lakini Ahazi alikuwa mfalme mwovu (2 Wafalme 16:2-3). Hakutaka sababu ya kumwamini Mungu. Mungu angefanya nini wakati mfalme alikuwa mkaidi na mwovu hivyo? Mungu alifanya kile ambacho alipaswa kufanya kila wakati. Alitabiri wakati ambapo angeingilia kati. Alizungumzia kuhusu mwana mteule ambaye angewaokoa watu wake. Hapa tuna ishara ya bikira kupata mtoto, ambayo ilikuwa utabiri wa kuja kwa Kristo mfalme (Mathayo 1:23). Ahazi alipewa ishara bila kujali kama alipenda au la. Kabla mwana hajakua na kujifunza tofauti kati ya mema na mabaya, wafalme hao wawili hawangekuwa tishio tena. Mwana aliyezaliwa huenda alikuwa mwana wa Isaya (Isaya 8:3). Hata hivyo, angeweza pia kuwa mwana wa Ahazi mwenyewe. Ahazi alimwita mwanawe ‘Hezekia,’ jina lenye maana ya ‘nguvu zangu ni Yahweh (Mungu)’. Ahazi mwenyewe hakumtumaini Mungu (alimtumaini mfalme wa Ashuru badala yake) lakini ni Hezekia ambaye alikuwa na imani katika Mungu licha ya jeshi kubwa la Ashuru (2 Mambo ya Nyakati 32:7-8). Sisi pia tunapaswa kumtumaini Mungu na si katika nguvu za mwanadamu. Haja ya kumtumaini Mungu tena inakuja kama ushauri katika 1 Wathesalonike 1 na 2. Kwa bahati mbaya, eklesia ilikuwa katika mji ambapo Wayahudi walikuwa wanapigana dhidi ya Wakristo (Matendo 17). Na hivyo, historia ya barua kwa Wathesalonike ilikuwa moja ya mateso kwa ajili ya imani yao. Mtume Paulo aliteseka zaidi, lakini pia waliteseka (1:6, 2:14). Kwa mateso kama hayo, mtu yeyote aliyedumisha imani yake alikuwa mwanafunzi mwaminifu. Walikuwa maarufu kwa imani yao (1:7). Paulo alisema kwamba Mungu huwajaribu waumini ili kujua kilicho mioyoni mwao (2:4). Wathesalonike walikuwa wamestahimili mtihani. Paulo alimshukuru Mungu kwa imani yao, tumaini na upendo (1:3) - sifa kuu za Kikristo (1 Wakorintho 13). Mfano wa Paulo ulikuwa muhimu kwa waumini kuona jinsi ya kuishi kwa imani. Paulo alikuwa mfano mzuri kwao. Hii ni tofauti na mfalme Ahazi ambaye alikuwa mfano mbaya kwa watu. Paulo anaelezea jukumu lake kama baba (2:11). Kisha anaelezea jukumu la baba ni lipi. Lazima wawatie moyo, wafariji, na kuwahimiza watoto wao kuishi maisha ya kimungu (2:12). Akina baba kila mahali wangekubali kwamba hivi ndivyo wanavyopaswa kufanya. Na watoto wanapofanya walichofundishwa, basi baba anafurahi. Paulo alifurahia Wathesalonike (2:20). Vivyo hivyo, Baba yetu wa mbinguni anafurahishwa nasi tukitenda jambo sahihi. Mawazo yetu yote yametupa ujumbe uleule, ambao tunawakumbusha tena - kuwa imara na jasiri katika kuishi kwa uaminifu mbele ya Baba yetu wa mbinguni. Sisi ambao ni viongozi lazima tuwe mfano mzuri katika hili.

Swahili Title
Mei 17
Swahili file
Literature type
Month