UASI WA BINADAMU
Nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa porini walioumbwa na Mwenyezi-Mungu. Basi, nyoka akamwambia huyo mwanamke, "Ati Mungu alisema msile matunda ya mti wowote bustanini?" Mwanamke akamjibu huyo nyoka, "Twaweza kula matunda ya mti wowote bustanini; lakini Mungu alisema, 'Msile matunda ya mti ulio katikati ya bustani, wala msiuguse, msije mkafa.' " Nyoka akamwambia mwanamke, "Hamtakufa! Basi, mwanamke alipoona kuwa mti huo ni mzuri kwa chakula, wavutia macho, na kwamba wafaa kwa kupata hekima, akachuma tunda lake, akala, akampa na mumwe, naye pia akala. Mara macho yao yakafumbuliwa, wakatambua kwamba wako uchi; hivyo wakajishonea majani ya mtini, wakajifanyia mavazi ya kiunoni, nao wakajificha kati ya miti ya bustani, Mwenyezi-Mungu asipate kuwaona. Lakini Mwenyezi-Mungu akamwita huyo mwanamume, "Uko wapi?" "Nani aliyekuambia kwamba uko uchi? Je, umekula tunda la mti nililokuamuru usile?" Huyo mwanamume akajibu, "Mwanamke uliyenipa akae pamoja nami ndiye aliyenipa tunda la mti huo, nami nikala." Hapo Mwenyezi-Mungu akamwuliza huyo mwanamke, "Umefanya nini wewe?" Mwanamke akamjibu, "Nyoka alinidanganya, nami nikala."