Exploring the Bible - 12

Swahili

ISRAELI AKIWA MISRI

SOMO LA 12 Kutoka 3 – 12

 

Jina la Yakobo limebadilishwa kuwa Israeli (mwanzo 32)

 

Jina la taifa la Israeli limetokana na jina ambalo Mungu alimpa yakobo. Yakobo alikuwa amerejea katika nchi ya kanaani kutoka Padan-Avam ambako alikuwa ameoa wake zake wawili, Leah na Rahel, wakati huo alikuwa na watoto wa kiume kumi na mmoja (11) na makundi makubwa ya ng’ombe na kondoo. Akiwa njiani alikutana na malaika wa Mungu. Malaika alimwambia Yakobo: “Hutaitwa tena Yakobo bali Israeli kwa kuwa kama mwana wa mfalme unao uwezo kwa Mungu na kwa wanadamu na umeshinda” (mwanzo 32:28) neon hili lilirudiwa tena punde kidogo alipofika Betheli (mwanzo 35:9-12) Neno Israeli maana yake ni “Mwana wa mfalme na Mungu”.

Kwa hiyo Yakobo alirudi na kukaa katika nchi ya kanaani kwa mara nyingine tena. Masimulizi ya matukio yahusuyo maisha ya Yakobo yanapatikana katika mwanzo 25-49. kadiri tunavyosoma katika sura hizi tunaona ukuaji wa kuamini kwake na imani kwa Mungu. Katika miaka iliyotangulia alikuwa mara nyingi amepanga na kukusudia kufanikisha mradi wake lakini hatimaye aligundua kuwa kumwamini Mungu kikamilifu pekee ndilo lililokuwa jibu kwa majaribu yote ya maisha. Kwa sababu hii tunaliona jina lake limeorodheshwa miongoni mwa watu waaminifu katika Waebrania 11(21).

 

Wazao wako watakuwa wageni katika nchi isiyokuwa yao.”

 

Tunayakumbuka haya maneno makubwa ya unabii ambayo Mungu alisema kwa Abraham (mwanzo 15:13-16) Mungu alibashiri kwamba uzao wa Abraham wangekwenda Misri lakini katika kizazi cha nne wangerudi Kanaani. Tunaposoma maisha ya Yakobo na Yusufu tunaona jinsi maneno haya yalivyotimizwa bila hitilafu.

 

Yusufu Mkombozi wa Israeli (mwanzo 37-50)

 

Maelezo ya maisha ya Yusufu na jinsi Mungu alivyomtumia kusababisha kuokolewa kwa ukoo wake (mwanzo 45:4-11) ni habari ya kusisimua sana ambayo utafurahia kusoma. Kwa kuongezea tunafurahishwa na imani na maisha ya kiMungu ya Yusufu alipokutana na majaribu na vishawishi.

Imani ya Yusufu iliyokamilishwa kutokana na majaribu ya maisha, inaonekana wazi alipokaribia kufa huko Misri. Aliwaapisha wana wa Israeli kwamba Mungu atakapowatembelea watu wake ili awakomboe kama alivyoahidi, wachukue mifupa yake waende nayo na kuzika katika nchi ya Ahadi (mwanzo 50:24-26 linganisha na Waebrania 11:22). Japo hakusema aliamini yale Mungu aliyomwambia Abrahamu kuwa wazao wake watakuwa wageni katika nchi isiyokuwa yao (Misri) na kwamba baada ya miaka mingi ya utumwa Mungu atawakomboa na kuwarudisha katika nchi aliyowaahidi (mwanzo 15:13-16).

Je nasi tunayo imani hiyo katika ahadi ambayo Mungu alimpa Abrahamu? Je tunaamini kwamba ahadi ya Mungu kwa Abrahamu itatimizwa Yesu Kristo atakaporudi?

Kama tunaamini tunahitaji kuonyesha imani yetu kwa ubatizo (Wagalatia 3:26-29), na halafu tuendelee kujitahidi kuishi maisha ya ki-Mungu katika enzi hizi za uovu.

 

Kukombolewa kwa Israeli Misri (kutoka 1-4)

 

Maelezo ya utumwa mgumu ambao Israeli ilivumilia huko Misri yanapatikana katika kitabu cha kutoka sura 1 na 2. Hata hivyo ndani yake kuna mfano mzuri wa imani ya wazazi wa Musa. Mungu alibariki imani yao na Musa akaokolewa kutoka kwenye kifo ili aweze kuwatoa waisraeli Misri (Waebrania 11:23-28; Matendo 7:17-36). Mafundisho ya wazazi wake kuhusu Mungu na makusudio yake katika miaka ya mapema ndiyo yaliyokuwa msingi wa imani ya Musa. Yeye kama alivyokuwa Yusufu aliamini kuwa Mungu angeikomboa Israeli katika utumwa Misri kama alivyomuahidi Abrahamu (mwanzo 15:13-16).

Katika kutoka 2 tunasoma kuhusu kuzaliwa kwa Musa na visa vilivyosababisha amkimbie Farao ili kuokoa maisha yake na kwenda katika pori la midiani karibu na Mlima Sinai na mlima Horeb.

 

Mungu atambulisha kusudi lake na jina lake kwa Musa (kutoka 3)

 

Sura hii inaanza na muujiza wa kufurahisha uliomfanya Musa ageuke ili autazame moto uliokuwa unawake ndani ya kichaka ambacho cha kushangaza kilikuwa hakiteketei (aya ya 1-6). Aliyeongea na Musa alikuwa “malaika wa Bwana” (aya ya 2) ingawa malaika huyu anatajwa kana kwamba ni Bwana mwenyewe(aya ya 4), na kisha anasema: “mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo” (aya ya 6). Kutoka hapo tunaona kwamba katika Biblia yote, malaika ambao ni wajumbe wa Mungu wanazungumza kana kwamba ni Mungu mwenyewe, kwa sababu wanamwakilisha, wakiongea kwa mamlaka na wakifanya miujiza kwa uwezo aliowapa (Zaburi 103:20-21; 104:4; Waebrania 1:14). Hivyo, ingawa twasoma kwamba “Bwana” au Mungu angekwenda na Musa kuwakomboa Waisraeli, sasa tunatambua kuwa alikuwa ni malaika aliyetumwa na Mungu kufanya kazi hii (Matendo 7:30-35; Kutoka 3:7-10). Malaika na watumishi wake ambao hutenda kulingana na matakwa yake (Zaburi 103:20-21) kwa kuwa “hakuna mtu ambaye amemwona au awezaye kumwona Mungu” (Timoteo 6:16) malaika wanamwakilisha au wanamwonyesha kwa binadamu.

Tunaona kanuni hii katika maisha na kazi ya Yesu Kristo Bwana kwamba alikuja kudhihirisha tabia na kazi ya Mungu kwa binadamu. Kwa kweli alipewa jina “Emanueli” ambalo maana yake ni “Mungu yu nasi” (mathayo 1:23) ingawa alikuwa mwana wa Mungu, alikana kuwa alikuwa Mungu, bali alionyesha kuwa alikuwa anatekeleza matakwa na kazi ya Mungu (linganisha na yohana 5:19,30,43). Philipo alipomwambia Yesu “Tuonyeshe Baba yako”, Yesu alijibu :”Nimekuwa na wewe Philipo muda wote huu nab ado hujanifahamu?” (Yohana 14:8-9). Yesu alimwambia Philipo kuwa jinsi alivyokuwa anafanya kazi za Mungu na kusema maneno yaliyotoka kwa Mungu alikuwa akimdhihirisha Mungu kwao.

Kama malaika walivyomdhihirisha Mungu kwa wale ambao malaika wale walijionyesha, vivyo hivyo ndivyo yesu alivyofanya. Yesu aliweza kusema “nimelifunua jina lako kwa wale ulionipa” (Yohana 12:6), aliweza pia kusema “mimi na Baba yangu ni kitu kimoja” (Yohana 10:30) kwa kuwa walikuwa wamoja katika tabia na kusudi, japo tofauti kama nafsi huru.

 

 

YAHWEH – Jina la Mungu

 

Musa alisikiliza malaika alipomweleza kuwa Mungu alikusudia kuikomboa Israel katika utumwa Misri. Mungu alikuwa amemteua Musa kutenda kazi hii kwa niaba yake kwa msaada wa malaika (kutoka 3:7-12). Musa alikuwa mtu mnyenyekevu sana (Hesabu 12:3) na alijisikia kama mdogo mno kwa kazi hii kubwa. Alitambua kuwa Waisraeli wangeuliza, “Jina lake nani?” (aya 13) Israel ilikuwa imeshazoea majina mengi ya Miungu wa Misri ambao majina yao yalihusishwa na kazi walizodhaniwa wanafanya na vyeo vyao. Musa alijuwa kuwa watamuuliza jina Mungu ambaye angewakomboa.

Jina walilopewa lilkuwa lenye mafunzo kweli kweli nijibu linaloeleza kwa “neon moja” nia au kusudi la Mungu kwa binadamu Neno hilo ni jina la Mungu anayeishi.

 

Aya ya 14

 

“Mimi niko vile nilivyo”

Kiebrania ni Ehyeh Asher Ehyeh. Japo maneno haya yametafsiriwa “Niko Yule Niliye” neon Ehyeh linaashiria wakati ujao na kwa hiyo jina linatakiwa litafsiriwe “Nitakuwa” kama lilivyo katika aya ya 12. Kwa hiyo maneno haya yanasomeka “Nitakuwa Yule Nitakavyokuwa” na hasa yanaeleza kusudio la Mungu kwa njia rahisi sana. “Mimi (Mungu) Nitakuwa Yule Nitakayekuwa” Mungu amepanga kudhihirishwa si kwa njia ya malaika tu bali kwa njia ya wanaume na wanawake.

 

Mungu ni Baba wa familia “mbinguni na duniani” ambayo ina jina lake (Waefeso 3:14-15). Tumeshaona kuwa Mungu hujidhihirisha kwa njia ya malaika ambao wanasema na kutenda kwa niaba yake.

 

Amejionyesha pia kwa njia ya mwanaye Yesu Kristo ambaye kwa usahihi kabisa alionyesha tabia (au utukufu wa kimaadili) ya Mungu kwa ajili ya watu wote kujionea wenyewe (Yohana 1:14) alifanya kila kitu alichoambiwa na Baba yake kufanya, hata kutii matakwa yake kwa jinsi ya kifo chake, na hivyo kutengeneza njia ambayo kwayo dhambi za watu zingesamehewa na wao kupatanishwa na Mungu.

 

Kazi hii ya kukusanya pamoja wale wote wanaomwamini Mungu kuwa kitu kimoja kwa njia ya Mwanae inaelewa wazi katika maneno ya Yesu yafuatayo:

 

“ Wala siwaombei hawa peke yao bali pia watakaoniamini kwa neno lao; ili nao wawe kitu kimoja kama wewe Baba ulivyo ndani yangu na mimi ndani yako, kwamba na wao pia wawe ndani yetu: ili dunia ipate kuamini kuwa wewe ndiwe uliyenituma. Na utukufu ulionipa nimewapa; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo: mimi ndani yao na wewe ndani yangu, ili waweze kufanywa wakamilifu kwa pamoja na ili ulimwengu uweze kufahamu kuwa wewe ndiye uliyenituma na kwamba umewapenda kama ulivyonipenda mimi” (Yohana 17:20-23).

 

Kusudi la Mungu ni kuwaunganisha pamoja kuwa kitu kimoja na yeye wale wote wanojitahidi kuendeleza tabia yake ya utukufu, kwanza kwa kujifunza kufikiri kama Yeye, halafu kwa kuishi maisha yanayopatana na njia zake. Kwa hiyo matamko kama yaliyomo katika matendo 15:14 “ Mungu, kwa mara ya kwanza aliwaangalia watu wa mataifa ili achaguwe miongoni mwao kabila moja kwa ajili ya Jina lake” yanazungumzia kusudi lake la kujikusanyia watu ili kwamba waonyeshe tabia yao katika maisha yao si kwa wakati huu tu bali kwamba hatimaye washiriki katika umilele wake baadaye (2 Petro 1:4).

 

Kusudi la Mungu “Kweli kama ninavyoishi dunia nzima itajaa utukufu wangu” ( Hesabu 14:21) litatimizwa wakati dunia itakapokuwa inakaliwa na watu wafuasi waaminifu wa Mungu na Yesu Kristo watakaoishi milele.

 

YAHWEH - “Yeye Yule Atakayekuwa”

 

Mungu alijitaja Mwenyewe “Nitakuwa Yule Nitakayekuwa” ambayo kwa Kiebrania ni Ehyeh Asher Ehyeh (Kutoka 3:14). Walakini Musa alipowaambia watu kuhusu Mungu, alisema “atakuwa” kwa Kiebrania, Yahweh. Kwa hiyo YAHWEH ndilo jina ambalo Mungu amejichagulia kwa ukumbusho wa kusudi lake.(Hosea 12:5). Neno hili la Kiebrania Yahweh, katika Biblia zilizo nyingi limeandikwa BWANA au MUNGU. Wafasili kwa njia hii wamejaribu kuonyesha neno hili la Kiebrania linapopatikana.

 

Mungu anawafurahia wale wanaoheshimu jina lake na kusudi tukufu liliomo ndani yake, na anaahidi kuwatumikia siku ile utukufu wake utakapoonekana duniani (Malachi 3:16-17).

 

Yahweh aikomboa Israeli kutoka Misri (kutoka 4-13).

 

Yahweh alimtuma Musa kwa Faraoh kupeleka ujumbe huu: hivi ndivyo asemavyo BWANA (Kiebrania Yahweh). Israeli ni Mwanangu, kifungua minba wangu; nami nakwambia, mwachilie mwanangu aende ili anitumikie, na ukikataa kumruhusu aende angalia nitamuua mwanao hata yule wa kwanza kuzaliwa (kutoka 4:22-23).

 

Farao alikataa kusikiliza matakwa ya Musa na akakaidi agizo la Mungu. Kwa hiyo kwa mkono wa Musa. Mungu akaishushia Misri mapigo kumi ya kutisha.

Mapigo hayo yalikuwa:-

  1. Maji yaligeuka kuwa damu.

  2. Vyura

  3. Chawa

  4. Mainzi

  5. Ugonjwa wa wanyama

  6. Majipu

  7. Mvua ya mawe

  8. Nzige

  9. Giza

  10. Vifo vya wazaliwa wa kwanza.

 

 

PASAKA (Kutoka 12).

 

Pigo la mwisho na lenye kukumbukwa sana ni lile linaitwa Pasaka ya BWANA (aya 11). Onyesho hili la mwisho la uharibifu dhidi ya Misri lilisababisha ukombozi wa Israeli kutoka katika kifungo ambacho walikuwa nacho, katika kutimiza maneno ya Mungu kwa Abraham kuhusu uzao wake (mwanzo 15:13-16).

 

Masimulizi ya Pasaka yameandikwa katika kutoka 12. kila familia au kikundi cha familia kiliagizwa kuchagua mwanakondoo asiyekuwana na doa na kumuua katika wakati uliopangwa (aya 5-6). Halafu kukushia damu yake kwenye vizingiti vya milango na vizimba vya nyumba zao (aya 7) Jioni ile walitakiwa wakae ndani ya nyumba zao na kula nyama ya kondoo iliyobanikwa (aya 8-10). Kila kitu kiliwekwa tayari kwa kuondoka (aya ya 11).

 

Wakati Israeli ikifanya hayo malaika wa Yahweh alikuwa akipita katika nchi nzima ya Misri. Damu kwenye kizingiti cha mlango ilikuwa ishara ya kuonyesha kwamba familia ya nyumba hiyo ilikuwa imeua mwanakondoo (aya 12-13) malaika aliyetumwa kuua mzaliwa wa kwanza alipoona damu alipita. Nyumba za Misri ambazo hazikuwa na damu mlangoni zilikumbwa na adhabu ya kutisha ya kuuawa kwa mzaliwa wao wa kwanza.

 

Hivyo Israeli ilikombolewa kwa njia ya damu ya mwanakondoo. Ilikujakuwa kumbukumbu kwao tangu siku hiyo na kuendelea (aya 14).

 

Kristo Pasaka yetu (1 Wakorinto 5: 7-8)

 

Mafundisho ya Pasaka yanatuelekeza mbele hadi kwenye kazi ya ukombozi ya Bwana wetu Yesu Kristo, “mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za duniani” (Yohana 1: 29, 36). Ni Kwa njia ya kumwagika kwa damu yake kwamba tumekombolewa (1 Petro1:18-19).

 

Mtume Paulo azungumzia “Kristu Pasaka yetu aliyetolewa sadaka kwa ajili yetu” (1 Wakorinto 5:6-8) kwa sababu kwa njia ya damu tumekombolewa katika utumwa wa dhambi na mauti kama Israeli walivyokombolewa katika utumwa Misri (Waebrania 2:15).

 

Kama Israeli ilivyokumbuka ule usiku wa kutisha kwa kuzingatia sikukuu ya Pasaka kila mwaka hivyo hivyo Yesu alivyowataka wale wote ambao wameishakombolewa kutoka katika utumwa wa dhambi kwa njia ya damu yake kumkumbuka yeye.

 

Katika mlo wa mwisho na wafuasi wake aliwapa mkate na divai mara kwa mara kwa kukumbuka alivyotolewa sadaka (Luka 22: 19-20, 1 Wakorintho 11:23-26).

 

Kuvuka Bahari ya sham ( Kutoka 14-15).

 

Msiba wa ghafla wa kuuwawa kwa wazaliwa wa kwanza wa Misri uliwapa Waisraeli nafasi ya kuondoka Misri kundi kubwa lililokisiwa kufikia watu milioni mbili waliondoka Misri ( Kutoka 12: 37-38). Walakini haukupita Muda mrefu kabla Farao hajawazia kuwaua na kuwakamata tena (Kutoka 14) Njia pekee iliyowaponyesha Waisraeli ilitolewa na Mungu katika muujiza wa ajabu wa kufunguka kwa Bahari ya Sham ili wavuke kwa usalama, lakini Wamisri walipojaribu kuwafuata maji yalirudi na kuwafunika na kuwateketeza wote (aya ya 30-31).

 

Ishara ya ubatizo.

 

Mtume Paulo aliona ishara ya ubatizo katika ukombozi wa Wana wa Israeli walipokuwa wakitembea kati ya kuta za maji ya Bahari ya Sham kwenda kwenye usalama upande mwingine, ( Wakorinto 10: 1-2). Mfano huu unafaa kiasi gani! Tunapobatizwa tunaacha maisha yetu ya zamani (Misri) nyuma na kuinukia maisha mapya “(Kueleka nchi ya Ahadi )” kufuata mfano wa Yesu Kristo (Warumi 6:3-7).

 

Majaribu jangwani- safari kuelekea mlima Sinai (kutoka 16-19).

 

Kama mchezo, Mungu alikuwa ameishakomboa Israeli kutoka Misri. Sasa alitaka kuwajaribu aone kama walikuwa na imani ya kutosha; alitaka kuona kama wangeamini ahadi yake kwamba angewarudisha katika nchi ya baba zao (Mwanzo 15: 13-16).

 

Walikosa chakula na kunung’unika dhidi ya Musa. Mungu akawapa chakula kwa kila siku kilichoitwa “manna” ili kiwasetiri (kutoka 16) Hivyo manna ilikuwa mfano wa Yesu Kristo na “mkate wa Uhai” (Yohaba 6: 27-63) Walikosa maji, wakanung’unika tena. Tena Mungu akawapa maji ya kutoka kwenye mwamba (kutoka 17) mwamba huo ulimwashiria yesu (1 Wakorinto 10:3-4) ambaye maneno yake yanaleta uzima (Yohana 4: 10-14; 6:63). Mungu alikuwa anawaweka katika majaribu kwa matumaini kwamba wangejifunza kumwanimi kwa kiasi kikubwa Israeli ilishindwa kuthibitisha ile imani inayomfurahisha Mungu ( Kumbukumbu la Torati 8: 1-6: Waebrania 11:6).

 

Kuna mafungo na ishara nyingi kwetu katika kutangatanga kwa Israeli jangwani (1 Wakorinto 10”1-13). Je ? tunayo imani kwa Mungu na tunaamini kwamba atatupatia kile ambacho ni cha lazima katika kutusetiri katika safari yetu ya kwenda kwenye Ufalme wake? (Mathayo 6: 25-34).

 

MUHTASARI.

 

  • Yakobo alibadilishwa na jina na Mungu kuwa “Israeli” (Mwanzo 32: 28).

  • Yusufu ndiye aliyeteuliwa na Mungu kulinda na kuwakomboa ndugu zake walipokwenda Misri. Mwishoni kabisa mwa maisha yake aliamini kwa dhati kabisa kuwa Mungu angewakomboa Waisraeli kutoka Misri na hivyo aliwataka waahidi kuwa wangebeba mifupa yake wakati wa kuondoka (Mwanzo 50:24-26).

  • Musa alilelewa ili awaongoze Waisraeli kutoka Misri ( Kutoka 1-2).

  • Kwa kupitia malaika wake, Mungu alionekana kwa Musa katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto karibu na mlima Sinai. Pale mungu alitambulisha jina lake kwa Musa- “ Nitakuwa Yule Nitakayekuwa” au “Yahweh” ( Kutoka 3: 12-15). Jina hili linaeleza makusudi ya Mungu kupitia mwanae kuwakusanya kuwa kitu kimoja wale wote wanaojitahidi kutangaza jina lake katika maisha yao kwa utii, imani na upendo kwake (Yohana 17: 20-23). Mungu bado anateua miongoni mwa mataifa “jamii ya watu” kwa ajili ya jina lake (Matendo 15:14).

  • Mwanakondoo wa Pasaka, ambaye alichinjwa kwa ajili ya kuwatoa Waisraeli katika Misri anaashiria ukombozi kutoka kwenye dhambi unapopatikana kutokana na damu ya Yesu Kristo ( 1 Petro 1: 18-19; 1 Wakorinto 5: 7-8).

  • Kuvuka bahari ya Sham kuna maana halisi inayoashiria ubatizo ( 1 Wakorinto 10:1-12)

 

Somo la 12- maswali.

 

  • Mungu alibadilisha jina la Yakobo. Jina hilo lilibadilishwa kuwa nani na maana yake ni nini?

  • Yusufu aliwafanya Waisraeli waape kwamba wangefanua jambo Fulani. Je ni jambo gani?

  • Ni nani aliyechaguliwa na Mungu kuwaongoza Waisraeli kutoka Misri?

  • Musa alimuuliza Mungu jina lake. Ni jina gani ambalo Mungu alimfunulia Musa?

  • Neno “Yahweh” lina maana gani?

  • Nia ya Mungu ni kuwakusanya watu wote wenye kuamini kuwa kitu kimoja kwa njia ya Yesu Kristu. Yesu Kristu alidokeza juu ya hili katika sala. Ni sala gani hiyo?

  • Ni mapigo mangapi ambayo Mungu aliishushia Misri kuitisha ili aweze kuwaokoa Waisraeli kutoka Misri?

  • Mwanakondoo wa Pasaka alitakiwa asiwe na doa. Mwanakondoo huyu alimwashiria nani?

  • Ni kwa jinsi gani kuvuka Bahari ya Sham kunakuwa Ishara ya Ubatizo?

 

 

 

Swahili Title
ISRAELI AKIWA MISRI
Swahili file
Status
Added to Internet
African text
Christadelphian Bible Mission
Translator 1
Raphael Mkeya
Literature type