CSSA 1-1-07 - THE SEPARATION OF ABRAM AND LOT

Swahili

7. KUTENGANA KWA ABRAMU NA LUTU

“Na tazama moshi wa nchi ukapanda juu kama Tanuru”

 

 

Shabaha

Kuonyesha kuwa Abramu alikuwa mwaminifu na Lutu alikuwa mpumbavu.

Abramu na Lutu walisafiri katika nchi yote ya Kanaani, lakini kwa sababu ya njaa waliendelea kuelekea kusini katika nchi ya Misri. Kule waliishi kwa muda tu (Mwanzo 12:10). Walipo kuwa wakirejea walisimika mahema yao kati ya Betheli na Hai. Wote wawili sasa walikuwa ni matajiri wa mifugo, fedha na dhahabu. Mwanzo 13;19:1-30 na 21; 2 Petro 2:6-8.

ABRAMU NA LUTU WANAAMUA KUTENGANA: Mwanzo 13:2-10

Wakati Abramu na Lutu waliporejea kutoka Misri walipatwa na matatizo halisi. Makundi ya kondoo na ng`ombe zao yaliongezeka na hivyo walihitaji malisho zaidi lakini “ile nchi haikuwatosha, ili wakae pamoja(mstari 6). Haukupita muda mrefu watumishi wa Abramu na Lutu waligombana. Abramu aliona njia pekee ya kufanya ilikuwa kutengana. Mungu alikuwa ameahidi nchi hiyo kuwa milki ya wana wa Abramu - “Uzao wako nitawapa nchi hii” (Mwanzo 12:7). Lakini asingeitumia nchi hii ya ahadi kuwa chanzo cha kuzozana kati yake na Lutu. Kwa hiyo Abramu alimpatia Lutu nafasi ya kuchagua sehemu yoyote ambayo angependa kuishi alisema “Je nchi hii yote haiko mbele yako? Basi ujitenge nami, nakusihi… na Lutu akainua macho yake, akaliona Bonde lote la Yordani, ya kwamba lote lina maji” (mistari 9-10). Mbele yake aliliona bonde zuri la nchi na akapendezwa nalo. Hivyo Lutu akafanya kuwa chaguo lake. Ilionekana dhahiri kuwa alichagua malisho ya kijani kibichi karibu na Yordani. Kwa hakika maisha yangekuwa rahisi sana kule. Alimuaga Abramu na kuondoka kuelekea upande wa mashariki.

Abramu aliridhika. Kama mgeni na mpitaji hasa akitarajia ufalme wa Mungu wenye utukufu aliridhika kwa lolote ambalo Mungu angempatia. Kila siku akaliitia “Jina la Yahwe” (mstari 4), akielewa kuwa Yeye ndiye ampatiaye mahitaji yake. Hebu tafakari tabia ya Abramu ilivyokuwa tofauti na ile ya Lutu. Lutu alitamani vitu vilivyoonekana mbele ya macho yake lakini Abramu aliweka tumaini lake kwa Mungu ambaye alimbariki sana. Bwana Yesu Kristo anatufundisha somo hili wazi wazi “Bali utafuteni kwanza ufalme wake na haki yake na hayo yote mtazidishiwa” (Mathayo 6:33).

CHAGUO LA LUTU NA KUHARIBIWA KWA SODOMA: Mwanzo 13:11-13;1:29

Lutu alichagua mwenyewe na mwishowe alikwenda kuishi katika mji wa Sodoma. “Lakini watu wa Sodoma walikuwa wabaya wenye kufanya dhambi nyingi juu ya Yahwe” (mstari 13) Ulikuwa sio uchaguzi wa busara kwenda kuishi miongoni mwa watu wabaya kama hao. Hapana shaka alidhania atajitenga nao kwa kujua kuwa siku zote alikuwa anayachukia matendo yao mabaya. (2 Petro 2:7-8) Lakini ingawa Lutu mwenyewe hakufanya yale waliyo kuwa wakifanya watu wa Sodoma hata hivyo yalikuwa ni kishawishi kibaya kwa jamaa yake. Mkewe na watoto wake hatimaye walifanya urafiki na watu wa Sodoma. Hata baadhi ya binti zake waliolewa na watu wa Sodoma. Baadaye, hata wakati ule, malaika wa Mungu walipokuja kuwatoa kabla ya Mungu kuharibu sehemu yote hakuna hata mmoja wa jamaa ya Lutu aliyetaka kuondoka. Walikuwa wameshapenda watu na jinsi walivyoishi hata wakasahau kabisa ahadi kuu za Mungu ambazo Abramu aliziamini.

Lakini Mungu aliwaadhibu watu wote waovu katika Sodoma kwa kuuharibu mji na wakazi wake kwa tetemeko la ardhi na moto. Mungu “aliinyeshea kiberiti na moto kutoka Mbinguni” na akaipindua miji “kuwa majivu” (2 Petro 2:6) Malaika wawili walimtembelea Abramu na kumwambia jambo ambalo Mungu angefanya katika Sodoma. Abramu alihofu sana kwa ajili ya Lutu na kumwombea kwa Mungu ambaye alikuwa ni mwenye rehema. Mke wa Lutu halikadhalika naye angeokolewa lakini waliambiwa wasiangalie nyuma pindi wakimbiapo kutoka Sodoma na hakutii. Aliona vigumu kuachana na mambo ya Sodoma na marafiki zake wengi aliokuwa nao na kwa hiyo alipata adhabu kwa kugeuka kuwa nguzo ya chumvi. Ni jambo la upumbavu kwa kupuuzia yale asemavyo Mungu tunayopasiwa kuyatenda. Wale wanaorahisisha Neno la Mungu daima wanaishia kuwa na huzuni, bali furaha kuu inawajia wale wanaotii.

CHAGUO LA ABRAMU: Mwanzo 13:14-17

Mungu alipendezwa na ukarimu na Imani aliyo onyesha Abramu. Sasa alimfanyia ahadi ya ajabu nyingine zaidi. Soma Mwanzo 13:14-17 “Inua sasa macho yako”, Mungu akasema, “na ukatazame kutoka hapo ulipo, upande wa kaskazini na wa kusini na wa mashariki na wa magharibi; maana nchi hii yote uionayo, nitakupa wewe na uzao wako hata milele”

Kumbuka somo letu lililopita. Tuliona kwamba Abramu hakurithi sehemu yoyote ya nchi ile katika maisha yake. Hata Hivyo ahadi ya Mungu bado ingalipo. Nchi ni ya Abramu na uzao wake kuwa milki ya milele (Warumi 4:13). Sasa Abramu ameshafariki. Bali Yesu (ambaye ni uzao wa Abramu) atarejea na atawafufua wafu na atawapo thawabu waaminifu. Wakati huo Abramu atapata Urithi wake pamoja na wale wote ambao wameonyesha uaminifu kama Abramu (Wagalatia 3:29).

MWANA WA AHADI – ISAKA: Mwanzo 17:15-23;21:15

Wakati Abramu alipopokea ahadi hii, hakuwa na mtoto yeyote. Wote, yeye na Sarai walikuwa wakiendelea  kuzeeka na kwa kuwa ilionekana kuwa Sarai asingeweza kupata mtoto yeyote alidhani Abramu angeweza kupata mtoto wa kiume kwa kumwoa Hajiri, mjakazi wake. Kwa hiyo alipewa Hajiri kuwa mke wa Abramu na hatimaye alimzaa mwana, aliyeitwa Ishmaeli. Hata hivyo asingeweza kuwa uzao wa ahadi aliyoahidiwa Abramu kwani Mungu alisema Sarai atamzalia Abramu mwana, atakayeitwa Isaka (Ikiwa na maana ya “kicheko au furaha”(mstari 19). Jina la Sarai lingebadilishwa kuwa Sara na Abramu kuwa Ibrahimu “kwa kuwa nimekufanya baba wa mataifa mengi”(mistari 5,45) Ibrahimu alikuwa na umri wa miaka 100 na Sara miaka 90, yaani miaka 10 pungufu ya miaka ya Ibrahimu hapo alipozaliwa mwana wa ahadi.

Ilipita miaka mingi tangu kuondoka Uru hadi kuzaliwa kwa mwana wa ahadi. Imani ya Ibrahimu na Sara ilifutilia mbali matatizo walivyokumbana nayo. Kwao Mungu alikuwa Kweli na kamwe hakuwakatisha tamaa kwa huyo mwana wa ahadi aliyezaliwa kwao wangetarajia hatua nyingine ingefuata ya kutimizwa tena kwa ahadi ya Mungu.

Walielewa kwamba kutoka Isaka angetokeza Mzao wa ahadi ambaye mataifa yote ya dunia yangebarikiwa (mstari 19).

FUNDISHO KWETU.

Ni ahadi ilioje aliyoiweka Mungu! Ameahidi kwamba watu wanaweza kuwa warithi pamoja na Ibrahimu katika uzima wa milele katika nchi hii. Na tutazamie mabadiliko makubwa ambayo yatatokea katika dunia wakati Bwana Yesu Kristo atakaporudi. Ndipo Ibrahimu na wale wote waliobatizwa katika Kristo na wameishi kwa uaminifu watakapo irithi dunia pamoja naye.

Tukumbukia pia makosa ya Lutu kwa kuchagua yaliyoonekana rahisi na mazuri kwake, lakini yalikuwa maovu sana na kidogo yasababisha kuangamia kwa uhai wake. Marafiki zetu wabaya hutugeuza kutoka katika njia za Mungu na kutufanya kuwa watenda maovu (soma Zaburi 119:63). Ni bora tuwe kama Ibrahimu ambaye aliamini Mungu kuwa atamlinda na kumpatia mahitaji yake yaliyo ya lazima.

MZAO WA AHADI

Fikiria ahadi kwa Abrahamu katika Mwanzo 12:1-3 na Mwanzo 13:14-17. Hakuahidiwa Ibrahimu tu bali pia kwa UZAO wake au mwana. Mungu alimwahidi Ibrahimu kuwa na uzao maalum. Kupita katika mlolongo wa vizazi tunaweza kufuatilia jamaa ya Ibrahimu mpaka Yesu Kristo miaka mingi baadaye (Mathayo 1:1). “Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake: Hasemi, Kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, kwa mzao wako yaani Kristo” (Wagalatia 3:16). Tunaweza kuwa jamaa ya Ibrahimu kwa kuunganishwa na Yesu Kristo katika ubatizo. “Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo, mmevaa Kristo… na kama ninyi ni wa Kristo, basi mmekuwa uzao wa Ibrahimu na warithi sawasawa na ahadi zake”(Wagalatia 3:27-29).

MASWALI

Majibu Mafupi

1. Kwa nini wachungaji wa mifugo wa Abramu na Lutu waligombana?

2. Lutu alichagua kwenda wapi?

3. Abramu alichagua kwenda kuishi wapi?

4. kwa nini Mungu alipendezwa na Abramu?

5. watu wa Sodoma walikua wanamna gani?

6. Mungu aliwaadhibu watu Sodoma namna gani?

7. Mungu alimwahidi Abramu nchi ya Kanaani. Ni lini Abramu ataishi milele katika nchi ya Ahadi?

8. Ni nani aliye Mzao wa ahadi kwa Ibrahimu ?

9. Jina Ibrahimu lina maana gani?

10. Ni mwana yupi  aliahidiwa Ibrahimu na Sara na jina lake lina maana gani?

Majibu ya Kina

1. Kwa nini Lutu alimwacha Abramu na kwenda kuishi sehemu nyingine ya nchi?

2. Lutu aliondoka kwenda kuishi Sodoma baada ya kutengana na Abramu. Eleza nini kilimtokeza na kwa watu wote katika mji? Tunapata mafundisho gani katika hii habari?

3. Abramu alimpendeza Mungu na kwa sababu ya imani yake, alipokea ahadi zilizo kubwa. Ni ahadi ipi Mungu aliyofanya na Abramu baada ya kutengana Lutu?

4. Ibrahimu alikuwa na wana wawili ni mwana yupi wa Ibrahimu aliyekuwa “mwana wa ahadi”, na kwa nini?

Majibu ya Nyongeza

1. Mungu alimwahidi Abramu ahadi kuu baada ya kutengana na Lutu na kwenda Sodoma. Ni ahadi zipi? Eleza namna gani na lini hili itakapotimizwa?

2. Ni jinsi gani tunavyoweza kushiriki katika ahadi zile zile alizopewa Abramu?

 

Swahili Title
007 KUTENGANA KWA ABRAMU NA LUTU
English files
Swahili file
African text
CSSA
Translator 1
Carl Hinton
Translator 2
Jonathan Nkombe
Literature type
Sub type
Sub sub type