49. MFALME - DAUDI
“Ndipo kabila zote za Israeli wakamwendea Daudi…wakamtia mafuta Daudi awe mfalme juu ya Israeli”
Shabaha
Kuonyesha jinsi ahadi ya Mungu kwa Daudi kwamba atakuwa mfalme ilivyotimizwa.
Muhtasari
Kwa muda wa miaka mingi Daudi alikuwa ni mtu siye na makao,akiwindwa na Sauli katika milima na nyika.Alikuwa na marafiki wachache sana na hasa wale waliokuwa wakiwindwa kama yeye mwenyewe.Kutokana na wema aliokuwa ameutenda kwa Sauli,lakini mfalme alimrudishia mabaya. Hizi zilikuwa nyakati za huzuni sana, hata hivyo katika taabu zake zote, Daudi alijifunza kumtegemea Mungu.Katika Zaburi aliandika jijnsi imani ilivyo msaidia kumngoja Mungu kwa uvumilivu ili Mungu amwokoe(Baadhi ya Zaburi ni:34,54,57,59,63). Ni vizuri kwetu,kujifunza somo hili linalohusu imani kwa Mungu,na kwa kuzisoma Zaburi hizo itatusaidia na sisi kufanya hivyo hivyo .2Samw2:1-4;5:1-10; I Nyakati 13.
DAUDI ANAVISHWA KUWA MFALME WA WAYAHUDI:2Samweli 2:1-4.
Sauli na Yonathani walikufa wote wawili siku moja katika vita,walipokuwa wakipigana na Wafilisti katika Mlima Gilboa.Daudi akaomboleza kwa ajili ya kifo chao,lakini alijua kuwa ni muda wake wa kurudi Israeli kuwa mfalme.
Ilikuwa ni desturi ya Sauli kufuata mawazo yake mwenyewe alipokuwa mfalme,pasipo kuomba msaada wala ushauri wa Mungu,lakini Daudi alikuwa ni mtu tofauti; maana alimtegemea Mungu kabisa kwa kila jambo.Alikuwa na umri wa miaka 30 alipoanza kutawala, na alikuwa amejifunza mafunzo mengi muhimu, alipokuwa mchungaji kijana akichunga kondoo za baba yake; na baada ya hapo kama askari na kiongozi wa watu.
Ni Mungu,aliyempeleka Samweli ili amtie mafuta Daudi, kuwa mfalme miaka kumi kabla ya yeye kuwa mfalme.Na kwa hiyo, Daudi akamgekia Mungu na kumwomba ushauri:“Je niupandie mji wowote wa Yuda?” Alimwuliza Mungu, na Mungu akamwambia aende Hebroni. Na mwisho wa siku zake za kukaa uhamishoni nje ya nchi yake na vilima vya Bethlehemu, aliokuwa akiupenda kama kijana,zikawa zimekwisha.
Kwa hiyo,Daudi akafika Hebroni akiwa pamoja na familia yake, na watu wake waliokuwa waaminifu kwake miaka yote aliyokuwa amemkimbia Sauli.Kule Hebroni watu walimtia mafuta ili awe mfalme wa Yuda.
Mungu alikuwa amekwishaonyesha kuwa huyo ndiye mtu aliyekuwa amemchagua Yeye,wakati alipompeleka Samweli kumtia mafuta katika nyumba ya baba yake.Na sasa Yuda walikuwa wamempata mfalme-aliye mcha Mungu na shujaa aliyejifunza imani,uvumilivu,utu wema na mwenye uongozi wa busara wakati alipokuwa katika miaka ya taabu ya uhamisho wake.
Daudi alitawala kabila la Yuda miaka saba na miezi sita wakati makabila mengine yalipokuwa yamemkataa asiwe mfalme wao.
Na mwisho wa muda huo ndipo alipotiwa mafuta kuwa mafalme wa Israeli(2 Samw 5:1-3).Na hatimaye,kwa uvumilivu wake wa kumngoja Mungu ili kutimiza mapenzi yake uliwadia.Na haikuchukua muda Mungu akampatia Yerusalemu, kuwa mji wa ufalme wake na wenye kuheshimiwa sana machoni pa mataifa yote yaliyowazunguka.
YERUSALEMU,MJI MKUU WA MFALME DAUDI:2Samw 5:6-10
Baada ya Daudi kutiwa mafuta ili kuwa mfame wa Israeli,alikwenda kuutwaa mji wa Yerusalemu(kwa wakati huo uliitwa Yebusi)kutoka kwa Wayebusi.Walikuwa ni miongoni mwa makabila ya Wakanaani,ambao Mungu alikuwa amewaambia Waisraeli kuwa wawaangamize kabisa.Hata hivyo mji huu, ulikuwa umelinajisi jeshi la Israeli kwa miaka 400 .
Yoshua alikuwa ameshamuua mfalme wa mji huu lakini bado alikuwa hakuutwaa mji huu.Na miaka mingi kabla ya Yoshua , Melkizedeki,kuhani wa Mungu aliye juu,aliyembariki Ibrahimu ,aliishi katika mji huu;ambao ulijulikana kuwa ni Salemu kwa wakati huo (Mwanzo 14:18-19).
Daudi aliuhitaji, ili uwe mji mkuu wa ufalme wake na kwa ajili ya kulihifadhi sanduku la agano, ambalo wana wa Israeli walikuwa wakilibeba muda wao wote walipokuwa wakizungukazunguka jangwani; miaka yote kabla ya kuingia Nchi ya Ahadi.
Yerusalemu ulikuwa umejengwa juu ya kilele cha mlima, na ulilindwa kwa kuta ndefu zilizokuwa zimeuzunguka pande zote.Ndani yake,Wayebusi walijiona kuwa wako salama.Kwa hiyo walipowaona wanajeshi wa Daudi wakiwa wameuzingira mji waliwacheka na kuwadhihaki(mstari wa 6).
Naye Daudi aliahidi, kuwa mtu aliye hodari sana hata aweze kumtwalia mji huo ili uwe wake atamweka kuwa mkuu wa jeshi lake(mstari wa8). Na Yoabu mmoja wa mashujaa wa jeshi la Daudi, alijifanyia njia kwa siri ya kuuingia mji akaingia kwa kupitia chini ya mfereji uliotokea kwenye chemichemi za mto Gihoni, nje ya mji,unaoleta maji ndani ya mji. Ulikuwa ni mfereji mrefu ulioshia kwenye maporomoko membamba kama kisima,yaliyoenda moja kwa moja ndani ya ngome ya juu.Maji kisimani hapo yalichotwa kwa kutumia ndoo na kupeleka mjini. Hakika lilikuwa jambo gumu sana na la hatari lakini Yoabu alifauru na Daudi akamweka kuwa mkuu wa jeshi lake. Mungu alikuwa pamoja na Daudi, kama alivyokuwa naye hapo mwanzo; na jeshi lake likautwaa mji.Na tangu hapo na kuendelea mji ukaitwa “Mji wa Daudi”. Naye Daudi akaujenga kuwa mji mkuu wa ufalme wake hapo, na akajenga na majengo mengine.“Daudi akazidi kuwa mkuu ;kwa maana BWANA,Mungu wa Majeshi alikuwa pamoja naye”(mstari wa 10).
NI HATARI KUPUUZA NENO LA MUNGU:I Nya 13
Tangu Sanduku la Agano liliporudishwa kutoka kwa Wafilisti,halikuwa limerudishwa mahali pake ndani ya Hema. Na hivyo akapenda aliweke mahali maalumu katikati ya Waisraeli wote katika Yerusalemu.Kwa hiyo alilitengenezea pazia jipya katika Mlima Sayuni.Na kisha aliomba msaada wa kwa viongozi wote wa Israeli, ili kulileta Sanduku Sayuni(mistari ya 1,2). Gari jipya lilitengezwa kwa ajili ya kulibeba Sanduku.Na wana wa Abinadabu ,Uza na Ahio wakaliendesha gari hilo kutoka ndani ya nyumba ya baba yao wakiendelea na safari kwenda Yerusalemu. “Naye Daudi pamoja na waisraeli wote walicheza mbele zaMungu kwa nguvu zao zote,na kwa nyimbo na kwa vinumbi na kwa vinanda ;na kwa matari,na kwa matoazi,na kwa tarumbeta”(mstari wa 28).
Ghafla maksai waliokuwa wakilikokota gari, walijikwaa, na Uza akaunyoosha mkono wake ili kulitegemeza Sanduka lisianguke.Papo hapo Mungu akampiga , Uza akafa hapohapo kando ya Sanduku la Agano. Unaweza ukafikiria jinsi kuimba na kucheza kulivyositishwa ghafla na watu wakagutushwa na kuogopa kwamba yawezekana jambo hilo likatendeka hata katikati yao wakiwa katika kufurahia. Daudi akashikwa na hofu sana. Ni jambo lipi baya, lililotendeka?Mungu alimpiga Uza, “kwa sababu alinyoosha mkono wake kuligusa Sanduku la Agano”(mstari wa 10).
Kufuatana na Sheria ya Mungu hakuna mtu aliyekuwa anaruhusiwa kuligusa Sanduku isipokuwa watu wale waliokuwa wameteuliwa kufanya kazi hiyo tu-wana wa Haruni (Hes 4:15). Katika juhudi yao ya kutaka kulileta Sanduku pale Sayuni,kila mmoja alikuwa amesahau mambo yaliyo muhimu-yaani kuuliza ushauri kwa Mungu.
Hawakuwa wamesoma Kitabu cha Torati, ili kufahamu yale ambayo Mungu anataka.Maana Mungu alikuwa ameshawapatia masharti kuhusu namna ya kuvichukua vyombo hivi vitakatifu sana ambavyo ni samani za vyombo vya hemani.Sanduku lisingebebwa na gari kamwe,wala gari jipya lisingetengenezwa kwa ajili ya kulibeba Sanduku. Mungu alikuwa amekwisha waagiza, kwamba miti miwili mirefu ya Mshita iwekwe katika vile vikuku vya Sanduku na lilipaswa kubebwa kwa namna hii tu na Walawi mabegani (Kut25:15). Kifo cha Uza, kilikuwa fundisho kwa wote; ilikujua umhimu wa kujifunza na kufanya vyema mapenzi ya Mungu. Daudi alifahamu hili kama tunavyojifunza kutoka I Nya15:11-13.
Katika jaribio la pili,lililofanyika miezi mitatu baadaye; mambo yote yalienda sawasawa kwa kuwa walikuwa wamelitii Neno la Mungu.
Kwa kuwa wakati huu Walawi wana wa Kohathi walilibeba Sanduku.Na lilipofikishwa Mlima Sayuni, na kuwekwa ndani ya hema aliyoiandaa Daudi kwa ajili hiyo,Waisraeli wote walishangilia kwa kuimba na kucheza.
FUNDISHO KWETU.
Nyakati za taabu, hutufundisha jinsi tunavyomhitaji sana Mungu. Zinatufundisha kumtegemea Mungu kwa msaada na ulinzi.Na hii ndiyo maana tunaambiwa na Neno la Mungu ,ya kwamba “imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi” (Matendo 14:22).Taabu za namna hii hutufundisha “tumkabidhi BWANA njia zetu,na pia tumtumaini Yeye”,tukijua ya kwamba mwisho atatupatia mema(Zab37:5-7).
Lakini siyo kwamba tumgeukie Mungu wakati wa taabu na huzuni tu.Tunapaswa kufurahia tunapofanya hivyo,kwa sababu tunajua ya kwamba Yeye ndiye anayetusaidia wakati wote.Lakini pia Mungu anapenda tumrudie nyakati za furaha na shangwe.
Kama Daudi angeweza kuangalia Neno la Mungu mara ya kwanza,na akaweza kufahamu Mungu alitaka nini,msafara wao wa kuelekea Yerusalemu wakiwa na Sanduku ,safari yao hiyo ingekuwa yenye furaha njia yao yote.
Na tukumbuke basi kusoma Neno la Mungu,kila siku tujifunze ni yapi tunayostahili kufanya ili kumpendeza Mungu;na pia tutafute msaada kwake na nguvu na faraja.
MAELEZO YA NYONGEZA.
Daudi alisubiri miaka mingi tangu alipotiwa mafuta na hatimaye akawa Mfalme.Kwa njia hii alionyesha uvumilivu mkubwa , hata wakati maisha yake yalipokuwa hatarini mara nyingi.Alikuwa akiamini kuwa Mungu atayatimiza yale aliyoahidi,lakini kwa wakati wake Yeye mwenyewe.Uzao mkuu wa Daudi ,Yesu Kristo,naye pia anasubiri kwa muda mrefu, na kwa uvumilivu ili Mungu azitimize ahadi zake. Kabla ya kuzaliwa kwake,Mungu aliahidi kwamba angechukua kiti cha enzi cha Daudi na kutawala Israeli(Luka 1:31-33).Yeye aliishi maisha ya ukamilifu na akayavumilia mateso,hata akafa pasipo kuipokea ahadi iliyotimilifu. Yeye alimwamini Mungu, kuwa atamfufua kutoka wafu, na kisha kwa muda aliouweka Mungu atamtuma kutoka mbinguni kuja hapa duniani ili apokee ahadi na kuujenga tena ufalme wa Daudi (Matendo 3:20-21).
Daudi alifahamu kuwa Mungu alichagua Yerusalemu kuwa sehemu ya “kuweka Jina lake” (Kumb12:5). “BWANA ameichagua Sayuni,ameiitamani akae ndani yake” (Zaburi 132:13).Hii ilikuwa ndiyo sababu hasa ya Daudi, kufanya bidii kutwaa mji wa Yerusalemu kutoka mikononi mwa Wayebusi; na kulichukua Sanduku la Agano na kulistarehesha hapo. Kisha Daudi akaufanya Yerusalemu kuwa mji mkuu ,na Yesu Kristo aliutaja baadaye kuwa “mji wa mfalme mkuu”(Math 5:35).Na kutoka hapo Yerusalemu,Bwana Yesu ataitawala dunia yote. Watu wa mataifa yote duniani watakwenda Yerusalemu kuabudu na kujifunza sheria za Mungu(Isaya 2:2-4;Zaburi 48:1,2).Kurudi kwa Wayahudi katika ya Israeli na hasa Yerusalemu, inatukumbusha kwamba wakati wa kurudi kwa Kristo umekaribia sana (Luka21:24-28)
Nifuraha kubwa iliyoje tunayopaswa kuwanayo,kama kuishi katika ufalme wa Mungu hapa duniani pamoja na Bwana Yesu Kristo akiwa mfalme mwenye haki,akionyesha wema wake kwa watu wote. Zaburi ya 72,inatuelezea baraka zote za ufalme huo.Kama tutamtii Mungu sasa ,na kuliamini Neno lake;hizo zitakuwa baraka zetu-uzima wa milele hapa duniani(Ufunuo 5:9-10;Rumi 2:7)
MASWALI
Majibu Mafupi
- Daudi alisubiri kwa muda gani tangu Samweli alipompaka mafuta hadi alitawazwa kuwa mfalme wa Yuda?
- Kabla ya kwenda Hebroni Daudi alifanya nini baada ya kifo cha Sauli?
- Ni kabila lipi Daudi alikuwa mfalme wake kwanza?
- Ni kwa muda gani Daudi alikuwa mfalme wa Yuda?
- Ni mji upi gani ambao Daudi aliutwaa kutoka kwa Wayebusi?
- Ni kwa njia gani Yoabu aliweza kuuingia mji?
- Daudi alisahau kufanya nini kabla ya kuliondoa sanduku?
- Ni kwa nini Mungu alimuua Uza?
- Ni nani waliolibeba sanduku lilipofikishwa Sayuni salama?
Majibu Ya Kina
- Eleza jinsi Yerusalemu ulivyotwaliwa kutoka kwa Wayebusi
- Eleza habari ya majaribio mawili ya kubeba na kulipeleka sanduku
- Ni fundisho gani tunalupata kutokana na huzuni nzito iliyotokea wakati sanduku lilipobebwa mara ya kwanza
Majibu ya Nyongeza
4.Ni kwa nini mji wa Yerusalemu ulikuwa ni wa mhimu sana kwa Daudi?
5.Ni jinsi gani Yerusalemu utakuwa mhimu wakati Kristo atakaporudi?
6. Tufanye nini,kama tunataka kushiriki katika Ufalme pamoja na Daudi na Kristo?