CSSA 1-4-02 - JESUS IS TEMPTED IN THE WILDERNESS

Swahili

77. YESU ANAJARIBIWA JANGWANI

”Kwa maana,mtu hataishi kwa mkate tu, bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha  Mungu”

 

Kusudi

Kuonyesha jinsi Yesu alivyoshinda majaribu jangwani. Mara tu baada ya ubatizo wake katika Yordani Yesu alikwenda jangwani ambako alipata mtihani. Kama ilivyokuwa desturi yake katika miaka thelathini iliyopita,Yesu kila mara alikuwa tayari ana jibu kutoka kwenye neno la Mungu wakati akilikabili kila jaribu. Lilikuwa ni neno la Mungu ndani ya akili yake ambalo aliliamini kwa moyo wake wote lililomfanya awe mtiifu kwa mapenzi ya Baba yake.

 

Mathayo 4:1 – 11, Marko 1;12 – 13; Luka 4: 1 – 13

 

 

HUKO JANGWANI

Baada ya msisimko wa ubatizo katika Yordani, Yesu bila shaka aliona haja ya kuwa na wakati wa faragha kwa kujitenga na watu. Alihitaji muda wa kutafakari kazi ambayo Mungu aliipanga ili Yesu aifanye na muda wa kumwomba Baba yake.Yohana alikuwa amemwelezea Yesu kuwa ni masihi naye sasa ilimpasa kuanza kuwaonyesha watu njia ya wokovu. Kazi iliyombidi aifanye haingekuwa rahisi, angekabiri matatizo mengi na hatimaye kifo cha kutisha. Habari njema za ufalme ilipasa ihubiriwe kwa watu wote, lakini yeye mwenyewe angeteseka na kufa. Mambo haya yote yalikuwa mbele, lakini kwa furaha angelifanya hayo yote “kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake” (Waebrania 12:2). Kwa muda siku arobaini alifunga huko jangwani, akiwa na wanyama wa porini kama washiriki wake. Kisha, mwisho ya siku arobaini alipokuwa amechoka na mwenye njaa, yule mjaribu alimjia.

 

 

MJARIBU AKAMJIA NA MASWALI: Mathayo 4:1 – 11

Huyo mjaribu alikuwa ni nani hatujui, lakini alikuja ili kuona kama Yesu angeliweza kuthibitisha kwamba yeye ndiye aliyekuwa Mwana wa Mungu, kama vile sauti kutoka mbinguni ilivyotamka wakati wa ubatizo wake. Alikuja kumjaribu Yesu, yaani kumpa mtihani kuona ni nguvu gani kwa hakika alikuwa nazo. Kwa kweli, Yesu alikuwa na nguvu za Roho mtakatifu alizopewa na Baba yake wakati alipobatizwa. Alijua kuwa alikuwa Mwana wa Mungu, na kwamba nguvu alizopewa zitumiwe kwa utukufu wa Mungu, wala siyo kwa ajili mapenzi ya Yesu.

     

Ka hiyo mjaribu akamwambia, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate” (Mathayo 4:3). Ni jaribu lilioje kwa mtu ambaye hakula kwa siku arobaini! Alikuwa na njaa sana, lakini Mungu hakumpatia nguvu za Roho mtakatifu kwa kujifurahisha tu. Yesu alikuwa na jibu tayari akilini mwake “Imeandikwa, mtu hataishi kwa mkate tu, bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu” (mstari 4). Ni muhimu zaidi kupata chakula kutokana na Neno la Mungu kwa kusoma Biblia kuliko kujali kuhusu kuilisha miili yetu. Hivyo asingeyabadili mawe yale kuwa mkate.

 

Na kisha mjaribu akamshauri kuwa ajitupe chini kutoka kwenye mnara mrefu wa Hekalu na kumwambia, “Ukiwa wewe ni mwana wa Mungu jitupe chini” (mstari 6). Mjaribu mwenyewe alifahamu kuwa malaika wa Mungu wangemlinda Mwana wa Mungu (soma: Zaburi 91:11–12). Hata hivyo, Yesu alielewa jinsi ilivyokuwa vibaya sana kumpima Baba yake. Alifahamu kuwa Mungu alikuwa pamoja naye kila wakati. Yesu akasema, “Tena imeandikwa usimjaribu BWANA, Mungu wako (mstari. 7). Na kwa sababu hiyo, asingefanya hilo.

 

Ndipo mjaribu alimtaka Yesu atumie nguvu zake mpya kuziangusha falme zote za dunia na kuanguka chini kumsujudia mjaribu. Alitaka kushiriki nguvu na utukufu wao wote. Ni kweli Mungu aliahidi kwamba Mwanaye ilipasa kuwa mfalme juu ya ulimwengu wote, lakini kulikuwa na kazi ya kufanya kwanza. Ni lazima kwanza ateswe na kufa, kabla Mungu hajampatia utukufu na heshima na ufalme. “Nenda zako shetani” akasema Yesu akamwambia adui yake (kama vile neno “shetani linavyomaanisha”), kwa maana imeandikwa, Msujudie BWANA, Mungu wako, umwabudu yeye peke yake. (Mstari 10)

 

 

JINSI YESU ALIVYOYASHINDA MAJARIBU

Je, umeona kwamba kila wakati Yesu alipojaribiwa kutenda dhambi, alikuwa na jibu tayari kutokana na Neno la Mungu? Angalia mistari yote ambayo Yesu alichukua majibu yake katika Kumbukumbu la Torati 8:3, 6:16 na 6:13. Mistari yote iliyotumika ni kutoka katika maneno ya Musa aliyowaambia wana wa waisraeli. Katika Kum. 8;3 Musa aliyasema hayo wakati wayahudi walipolalamika na kunung’unika, kwa sababu hawakumwamini Mungu kuwa alikuwa na uwezo wa kuwapatia chakula na maji katika jangwa. Musa akawaambia kwamba mkate halisi haukuwa wa muhimu sana, bali Neno la Mungu, kwa kuwa huo ndiyo mkate wa kweli. Na Mungu kila wakati atawapatia chakula na maji wale wanaoliamini Neno lake. Kwa watu kama hao, wanaomwamini Mungu, Yeye atawapatia uzima wa milele. Ni uzuri zaidi ulioje, kwa mkate wa kweli ambao Mungu anawapatia wamwaminio!

 

FUNDISHO KWETU

Kuna njia tatu ambazo sisi sote hujaribiwa,ni kwa njia hizi hizi tatu ambazo Yesu alijaribiwa. Matamanio yetu wote ya asili yanaitwa “tamaa za mwili, tamaa za macho na kiburi cha uzima” (1Yoh. 2:16). Ikiwa tunafurahia kujipenda wenyewe, ndipo tutakapo mtenda Mungu dhambi kati ya njia moja au zaidi ya njia hizi.

 

Kila kitu ambacho kinapatikana katika dunia kinaonekana kuwa cha kuvutia sana. Hata hivyo, Biblia inatufundisha “Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili,na tamaa ya macho na kiburi cha uzima, havitokani na Baba bali ni vya dunia” (1Yoh. 2;15 – 16).

 

Bwana Yesu Kristo alijua jinsi ya kuyashinda majaribu yote, kwa sababu akili yake ilijaa Neno la Mungu. Kamwe hakuruhusu hisia zake za njaa, kiburi au matamanio ya kimwili kwa kuacha Neno la Mungu. Hivyo kwa kusoma Biblia kila siku na kufikiria maneno yaliyoandikwa katika Biblia, tutakuwa na jibu tayari kwa kila jaribu. Hivi ndivyo tunavyoweza kushinda dhambi na kumpendeza Mungu.

 

MAELEZO YA NYONGEZA

Utaona katika Mathayo 4 na Luka 4 kwamba mjaribu anaitwa “ibilisi”. Hili syio jina, lakini linatueleza jinsi mjaribu alivyokuwa, ina maana mmoja anayejiweka mpinzani wa Mungu kwa kusema uwongo, kwa mfano: - Yuda Iskariote aliitwa “ibilisi” kwa sababu alimshuhudia uwongo Yesu na kumsaliti kwa watawala wa wayahudi (Yohana 6:70 – 71). Mjaribu alikuja kwa Yesu huko jangwani alimtaka atumie nguvu kuu za Mungu kutenda vitu ambavyo havikuwa sahihi. Hata sisi pia, twaweza kuwa “Ibilisi” kila mara tunapotenda dhambi dhidi ya Mungu.

 

Yesu akamwambia mjaribu, “Nenda zako, shetani” (Math 4:10). Shetani ni neno la kiebrania lilioloingizwa moja kwa moja kwenye Biblia zetu za kiingereza. Lina maana ya mpinzani au adui. Tena, siyo jina. Yesu alimwita Petro “Shetani” aliposema bila hekima, maneno yake hayakuwa yenye kusaidia, bali yalikuwa maneno ya adui. Kwa hiyo mjaribu kule jangwani alikuwa adui wa Mungu naye Yesu alimfukuza kwa maneno ya Mungu.

 

MASWALI:

Majibu Mafupi

  1. Yesu alikwenda wapi baada ya kubatizwa?
  2. Ni kwa muda gani Yesu alikaa jangwani?
  3. Yesu alifanya nini kule jangwani?
  4. Ni nani aliyekwenda kwa Yesu mwisho wa siku zake kule jangwani?
  5. Ni nini alichotaka Yesu athibitishe?
  6. Je, Yesu alipata majibu yake kutoka kitabu kipi katika Biblia ?
  7. Kwa nini Yesu hakuwa mfalme moja kwa moja baada ya ubatizo wake?
  8. Ni wapi tunaweza kupata jibu kila wakati litakalotusaidia kumpendeza Mungu kila

             tunapojaribiwa?

 

Majibu ya Kina

  1. (a) Ni kitu gani cha kwanza ambacho mjaribu alimwambia kwa Yesu?

       (b) Yesu alimjibu namna gani?

       (c) Tunajifunza nini kutokana na somo hilli?

 

  1. (a) Ni kwa nini tunaambiwa tusiipende dunia?

       (b) Ni kwa jinsi gani Bwana Yesu Kristo aliyashinda majaribu yote?

 

Majibu ya Nyongeza:

  1. (a) Ni kwa nini mjaribu anaitwa “Ibilisi”?

       (b) Nani mwingine katika Biblia ameitwa “Ibilisi?

       (c) Neno “Shetani” lina maana gani?

 

 

Swahili Title
077 YESU ANAJARIBIWA JANGWANI
English files
Swahili file
Literature type
Sub type
Sub sub type