83. YESU HUKO KAPERNAUMU
“Nayo sifa yake ikaenea kila mahali katika nchi iliyozunguka”
Shabaha
Kuonyesha jinsi Yesu alivyowaponya watu wengi huko Kapernaumu na sifa yake ikaenea sana hata sehemu za mbali zaidi.
Baada ya mapokezi yasiyopendeza ya kule Nazarethi, Yesu alielekea Kapernaumu kwenye ukingo wa kaskazini wa bahariya Galilaya. Akakaa huko kwa siku kadhaa, akitenda miujiza ya ajabu mingi sana. Kapernaumu ulikuwa mji wenye shughuli za uvuvi wa samaki, kwenye njia kuu itokayo Dameski kwa upande wa kaskazini na kuelekea Misri kwa upande wa kusini. Hapa pia, Yesu alimwita Mathayo kutoka kwenye ofisi yake ya kukusanya ushuru ili amfuate. Ilikuwa heshima kubwa iliyoje kwa mji huu kuwa na Mwana wa Mungu ndani yake.
Luka 4:31 – 44; Marko 1:21 – 39.
YESU AFUNDISHA KWA NGUVU: Marko 1:21 – 28.
Siku ya Sabato (siku ya saba ya juma, Jumamosi yetu) watu walizoea kukusanyika katika sinagogi kusikia usomaji wa vyuo vya sheria ya Musa na Manabii. Masinagogi yalikuwa majengo madogo tofauti kabisa na hekalu la Yerusalemu, lakini yote yalijengwa kuelekea mji mtakatifu.
Watu walifurahi sana kwa kuwa na mwalimu huyu mpya kati yao na kuna uwezekano kuwa yule mtawala ambaye mwanaye alikuwa ameponywa alikuwepo. Habari za miujiza ya Yesu zilimtangulia mbele kule. Hapa kulikuwa na hali tofauti kutokana na Sabato iliyotangulia kule Nazarethi, ambako watu “walimdharau na kumkataa” (soma Isaya 53:3). Hivyo Yesu akasimama ili kufundisha. Kwa kadiri watu walivyoyasikiliza maneno yake walishangaa sana. Kwa namna alivyokuwa tofauti na waandishi, kwa maana mtu huyu alisema kwa mamlaka (mstari29). Aliwafundisha kama mmoja ambaye alifahamu maneno aliyoyasema yalimaanisha nini. Na ndivyo alivyofanya, kwa kuwa alitumia maisha yake yote kujifunza juu ya neno lile na katika maombi kwa Baba yake. Kwa hiyo aliposema, “neno lake lilikuwa na uwezo” (Luka 4:32). Huyu hapa,alikuwa mwalimu ambaye angeweza kwa kweli kuwasaidia kuzifahamu njia za Mungu.
Watu walimsikiliza Yesu kwa makini sana , hadi hapo mkutano ulipokatizwa ghafla na sauti kubwa ya kulia iliyoseme; “tuachilie; tuna nini nawe Yesu wa Nazarethi? Je,Umekuja kutuangamiza? Nakutambua unani , Mtakatifu wa Mungu” (mstari24). Yesu alielewa kuwa huyu hakuwa tu mtu yeyote mwenye kiburi anayetaka kuharibu mkutano wao. Maskini mtu huyu asingeweza mwenyewe kujisaidia. Hakuwa na uthibiti juu ya yale aliyokuwa akiyasema. Yesu akamhurumia mtu yule maskini na kujibu maneno yake kwa kusema “Nyamaza na umtoke” (mstari25).
Kwa maneno haya Yesu alimaanisha nini? Katika siku zile, walifikiri vichaa walitawaliwa na mapepo wabaya” (au madaimoni). Hivyo Yesu akasema kana kwamba alikuwa anazungumza na “pepo wabaya” ndani ya yule mtu. Baada ya Yesu kusema, yule mtu alianguka chini, akijigaragaza kama aliyepagawa akalia wakati alipokuwa akifanya hivyo. Kisha ghafla akatulia na kusimama pasipo kuumia sehemu yoyote na akiwa katika ufahamu wake wa kawaida (Luka 4:35). Watu waliokuwa ndani ya Sinagogi walishangaa.Na kila mmoja alielewa kuwa maneno ya Yesu kwa hakika yalikuwa yamemponya yule mtu mwenye ugonjwa wa akili. Ni mtu wa aina gani huyu ambaye siyo tu alisema kwa mamlaka, lakini pia alikuwa na nguvu juu ya “mapepo wachafu!”.
Hii ilikuwa ni siku ya kukumbukwa. Wakasema,“Ni neno la aina gani hili!” Ndipo Sifa za Yesu zikaenea mbali na kila mahali.
YESU AMPONYA MAMA MKWE WA PETRO: Marko 1:29 – 31.
Walipotoka katika Sinagogi kule Kapernaumu; Yesu na wanafunzi wake walikwenda nyumbani kwa Petro. Hata hivyo,mambo hayakuwa yenye kufurahisha sana pale, kwa sababu mama mkwe wa Petro alikuwa mgonjwa sana wa homa ya kutisha. Walipomweleza Yesu na kumwomba msaada wake, mara moja aliingia ndani ili kumwona. Akiwa amesimama mbele yake “akaikemea ile homa” na akamshika mkono wake na kumwinua. Mara moja homa ikamwacha naye akaamka kutoka kitandani mwake na akaanza kutumikia familia yake na wageni wake. akiwa ni mzima kabisa. Yesu alikuwa amefanya mwujiza wa ajabu, mara hii kwa niaba yao wote walioacha vyote na kumfuata yeye. jinsi zilivyo nyingi baraka atupazo Mungu tunapomtumikia, kama Petro na hasa kwa njia hii aliweza kujifunza wakati huu kutokana na uponyaji huu.
KUPONYA WAGONJWA JIONI: Luka 4:40
Jinsi ilivyokuwa na msisimko siku ile ya Sabato huko Kapernaumu. Ingawaje alikuwa amechoka, watu hawakumpa Yesu nafasi ya kupumzika. Jioni, jua lilipokuwa likizama mwisho wa Sabato, kila mmoja kwenye wilaya hiyo alimleta ndugu yake na rafiki yake aliyekuwa mgonjwa ili aponywe. “Akaweka mikono yake juu ya kila mmoja wao, akawaponya” (Luka 4:40). Ni wema na huruma ya jinsi gani alionyesha! Kamwe hajatokea kuwapo nabii au mponyaji kama mtu huyu. Mathayo anaposimulia habari hii (soma Mathayo 8:16– 17), anakumbuka maneno ya Isaya 53:4: “Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu”. Kwa wale waliokuwa kama Mathayo, waliokuwa wamejifunza juu ya Manabii wa Agano la Kale, mambo mengi Yesu aliyoyafanya katika maisha yake yalionyesha waziwazi ya kwamba alikuwa ndiye masihi ambaye manabii walikuwa wamemtari.
YESU ANAONDOKA KAPERNAUMU: Marko1:35–39; Luka 4:42–44
Yesu hakulala muda mrefu usiku ule, ila aliamka “mapema sana alfajiri kabla ya jua kuchomoza” akaenda nje ya mji kupata mahali pa faragha, mbali na watu ambapo angemwomba Baba yake bila kubugudhiwa. Petro na wanafunzi wale wengine Andrea, Yakobo na Yohana walikwenda kumtafuta. Alikuwa amefanya mambo menngi ya ajabu siku iliyopita huko Kapernaumu, hata ikiwa kwamba kila mmoja alikwenda mapema nyumbani kwa Petro ili kumwona Yesu. Wakasema; “Watu wote wanakutafuta” (Marko 1:37). Lakini Yesu alikuwa na mipango mingine, “Imenipasa kuihubiri habari njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia” akasema, “maana kwa sababu hiyo nalitumwa” (Luka 4:43). Hivyo aliendelea kutenda kazi ya Mungu katika nchi yote ya Israeli, akifundisha kwamba masihi alikuwa amekuja kuwaletea wokovu.
FUNDISHO KWETU
Yesu kwa hakika alikuwa na nguvu za Mungu, lakini alikuwa ni mtu, kama sisi ambaye aliweza kuchoka na alihitaji kupumzika. Lakini hata hivyo ona namna alivyofanya bidii katika kazi ya Mungu, Yesu alijua alichotaka Mungu nini: “Utampenda Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili yako yote” (Luka 10:27). Alikuwa yuko tayari kufanya hivyo, kila siku.Na hivi ndivyo Mungu anavyotarajia sisi tufanye pia. Kwa njia moja alikuwa tofauti sana nasisi,kwa maana yeye hakuwa na ubinafsi kabisa.Yeye aliwafikiria wengine na kamwe hakujifiria mwenyewe. Alipowaona wagonjwa wengi, moyo wake uliwahurumia naye akawaponya. Hatuna nguvu kama hizo ili kuwasaidia wengine kama alivyofanya, lakini Mungu ametujalia sisi sote uwezo wa kuwa wema na wenye kuwafikiria na kuwatunza na kuwajali wengine. Zipo njia nyingi ambazo kwazo tunaweza kuonyesha hili.
MAELEZO YA NYONGEZA
Tutaona katika masomo yanayofuata kwamba Yesu mara nyingi aliponya watu siku ya Sabato. Viongozi wa wayahudi, ambao kazi yao ilikuwa kuwafundisha watu kutokana na maandiko, walikasirishwa sana na tendo hili la kuponya siku ya sabato. Sheria ya Musa ilisema waziwazi kwamba kazi yoyote isifanyike siku ya Sabato. “Siku sita utafanya kazi zako zote, lakini siku ya saba ni Sabato ya Yahwe Mungu wako”(Kutoka 20:8 – 11). Hivyo walifikiri kuwa Yesu alikuwa akivunja sheria. Lakini kwa hakika hii haikuwa kweli. Wakati Mungu alipoandika amri hii, alimaanisha kwamba watu waache kufanya kazi zao wenyewe (mstari 9) katika siku ya Sabato ni kukumbuka vitu Mungu alivyowatendea wao. Yesu alionyesha jinsi walivyokuwa wapumbavu.Kama mtu alikuwa na kondoo na kondoo akatumbukia shimoni siku ya Sabato, je, angemwacha humo? Asingekwenda na kumtoa? “Je, mtu ni bora kuliko kondoo mara ngapi?” Yesu akasema, “Bali ni halali kutenda mema siku ya Sabato” (Math.12: 11- 13).
MASWALI
Majibu Mafupi
- Ni kwa nini watu walikusanyika katika masinagogi siku za Sabato?
- Je,watu waliyachukuliaje maneno na mafundisho ya Yesu kwa kulinganisha na
mafundisho ya waandishi?
- Nini nini kilitokea ghafla Yesu alipokuwa akifundisha katika sinagogi huko
Kapernaumu?
- Yesu alimwambia nini mtu yule aliyepiga kelele katika sinagogi?
- Yesu na wanafunzi wake walikwenda wapi walipoondoka kutoka kwenye sinagogi?
- Ni jinsi gani Yesu alimsaidia mama mkwe wa Petro?
- Nini kilitokea jua lilipozama siku ile ya Sabato huko kapernaumu?
- Yesu alifanya nini alipoamka alfajiri mapema siku iliyofuata?
- Kwa nini Yesu hakuendelea tena kukaa kapernaumu?
Majibu ya Kina
- (a) Watu wa Kapernaumu walimfikiriaje Yesu alipowafundisha katika sinagogi?
(b) Eleza ni nini kilitokea ndani ya sinagogi
- (a) Yesu alionyesha wema na huruma kwa watu wengi wa Kapernaumu. Ni watu gani
aliowasaidia?
(b) Ni kwa jinsi gani inatubidi tumpende Mungu? (Nukuu maneno ya Yesu).
Majibu ya Nyongeza
- (a) Sheria ya Musa ilisemaje kuhusu siku ya Sabato?
(b) Je, Yesu alikuwa akivunja sheria alipoponya siku ya Sabato?
(c) Ni kwa nini Mungu alitaka watu wapumzike siku ya Sabato?