85. YESU ANAWAFUNDISHA WANAFUNZI WAKE JINSI YA KUSALI
“Usali mbele ya Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakukupa thawabu wazi wazi”
Shabaha
Ni kuonyesha jinsi Yesu alivyowafundisha wanafunzi wake kusali.
Alipokuwa mlimani pamoja na wanafunzi wake, Yesu aliwafundisha masomo mengi kwa ajili ya maisha ya kila siku. Ni lazima wawe tofauti na watu wengine, ili kuonyesha kwamba walimpenda Mungu na kumtii yeye. Na Yesu mwenyewe alikuwa ameonyesha mfano. Maisha yake yote alijifunza Neno la Mungu, na kila siku alimwomba Baba yake wa Mbinguni. Hili lilimpa nguvu kuyakabili matatizo yaliyojitokeza wakati alipokuwa akienda kuwahubiri watu. Kwa jinsi tunavyofuatilia maisha yake tutaona namna alivyosali mara kwa mara kwa Baba yake kwa ajili ya msaada na namna alivyohitaji sana kuzungumza na Mungu kwa njia ya sala. Naye pia ndipo wakati huu alipowafundisha wanafunzi wake jinsi ya kusali. Kwa kufuata mfano wake wangekaribia kwa Baba yao wa Mbinguni.
Mathayo 6:1 – 15.
MSIWE KAMA WANAFIKI:
Yesu alikuwa ameshawaonyesha wanafunzi wake kwamba wasiige mfano wa waandishi na mafarisayo (Mathayo 5:20). Maaa wao kila jambo walilolifanya ilikuwa kwa ajili ya kujionyesha kwa watu. Walitumaini watu wangeona jinsi walivyokuwa wenye haki na kuwasifia. Yesu akasema, “Wamekwisha kupata thawabu yao” (Mathayo. 6:2,5). Na hata walipokuwa wanawasaidia maskini walihakikisha kila mmoja anawaona. Na waliposali walifanya hivyo kwenye kona za barabara ambako kila mtu angeweza kuwaona! Zawadi zao ingawa ziliwasaidia maskini, lakini Mungu hakupendezwa nazo. Hata ingawa watu waliyyasikia maombii yao,lakini Mungu hakuyasikia maombi yao.Wasingeweza kupata thawabu kutoka kwa Mungu.
Yesu aliwaita “wanafiki”. Walijifanya kuwa wakarimu kwa maskini, lakini kwa kweli walitaka sifa ya watu. Walijifanya kusali kwa Mungu, lakini katika mioyo yao walikuwa wakiwafikiria watu wale waliokuwa wakiwaangalia na kuwasikiliza.Kwa hiyo Yesu hakutaka wanafunzi wake wawe kama hao. Ilikuwa ni bora zaidi kwamba walipowasaidia maskini ni Mungu peke yake aliyestahili kujua hilo. Na waliposali, walitakiwa waende faraghani ambako watu wasingewaona na kusali kwa Mungu sirini. Mungu amewasikia na kuwapatia thawabu wazi wazi. Ni thawabu kuu iliyoje, wakati Kristo atakaporudi na wanafunzi wa kweli watakapopewa uzima wa milele katika ufalme wa Mungu.
BASI NINYI MTASALI HIVI: Mathayo 6:9
Wakati Waandishi na Mafarisayo waliposali waliendelea kwa muda mrefu.Yesu akasema; “Maana wao hudhani kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi” (mstari 7). Yesu mwenyewe mara nyingi alisali “Usiku kucha” (Luka 6:12), lakini kuna tofauti yake ilikuwa nini! Wao walikuwa wakisema maneno na vifungu vile vile na kurudia rudia hayo hayo mara nyingi kwani hawakufahamu maneno mengine zaidi ya hayo na hata hivyo hayo waliyoyasema hayakuwemo ndani ya mioyo yao. Yesu, kwa upande wake, alimjua Baba yake vyema. Kwa hiyo alijua jinsi ya kusema naye, alikuwa ni kweli Baba wa mbingu mwenye upendo, aliyestahili heshima yote na sifa ambaye alipendelea kusikiliza sala zao wote waliompenda,na hasa hasa sara za Mwanaye.
Yesu alitambua kwamba wanafunzi wake walihitaji ushauri wa pekee kuhusu jinsi ya kusali. Ni kweli kwamba Mungu, yeye anajua mioyo yetu na anafahamu tunahitaji nini hata kabla hatujamwomba, lakini wakati tunaposali ni lazima tuonyesha kuwa tunampenda na tunahitaji msaada wake.
Basi,akawaelekeza njia ya kumsogelea Mungu katika sala, akasema, “Basi, ninyi salini hivi”.
“BABA YETU ULIYE MBINGUNI”: Mathayo 6:9.
Yesu aliwaambia wanafunzi wake wamfikiria Mungu kuwa ni “Baba” yao. Tunaelewa kwamba baba zetu wanatujali na kututafutia mahitaji yetu ya kila siku. Ni wazuri na wapole, lakini wanatutazamia kuwa watoto watiifu na wenye upendo. Mungu yu namna hiyo hiyo- Baba wa Mbinguni anayewajali wana wake wote.
Anatuongoza sisi, ikiwa tutalikiliza Neno lake ambalo limeandikwa katika Biblia (Mithali 3:5 – 6). Anatulinda, ikiwa tuta mwamini (Zaburi 18:1-2; 34:7); Anaturudi (kutusahihisha) sisi, tunapokosa utii (Mithali 3:11-12); Anatusikia sisi kila wakati tunapomlilia Yeye (Zaburi 116:1-2; Mathayo 7:7 – 12).
Mara nyingi alipokuwa mlimani akiwa na wanafunzi wake, Yesu aliwafundisha kumwazia Mungu kuwa ni Baba yao wa Mbinguni. Aliwaambia “Mtukuzeni Baba yenu aliye mbinguni” (Mathayo 5:16). “Wapendeni adui zenu… ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni” (Mathayo5:44–45, 48); “Je, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao” (Mathayo 7:11).
Paulo anatufundisha kuwa “Mungu ni mmoja tu, aliye Baba,ambaye vitu vyote vimetoka kwake nasi tunaishi kwake” (1 Wakoritho 8:6). Kwa hiyo, kila mwanafunzi yampasa kwenda mbele za Mungu kwa heshima na unyenyekevu unaostahili kwa Baba wa jinsi hiyo, ambaye ni Muumbaji wa vitu vyote.
“JINA LAKO LITUKUZWE”: Mathayo 6:9
“Litukuzwe” siyo neno la kawaida siku hizi, lakini lina maana ya “Utakatifu”. Jina la Mungu Yahwe (BWANA), linapaswa kuwa ni takatifu sana kwetu. Kamwe lisitumiwe juujuu. Watu leo wanamkufuru Mungu katika maongezi yao ya kila siku na wala hawawazii lolote lile kuhusu jina lake. Hata hivyo Mungu anajua, naye punde atamleta Bwana Yesu Kristo kuadhibu ulimwengu huu wa waovu. Ndipo kila mmoja atajifunza kulitukuza jina la Mungu na kumtii Yeye (Zaburi 72:17 – 19)
“UFALME WAKO UJE”: Mathayo 6:10
Na hii ndiyo imekuwa sala ya wana wa Mungu wote kwa miaka elfu nyingi. Na hili ndilo tumaini letu, Mungu alimwahidi Daudi kwamba mwanaye (Bwana Yesu Kristo) ataketi katika kiti chake cha enzi Yerusalemu naye Daudi atakuwepo na kuliona hili (2 Samweli 7:12 – 16). Kitu cha kwanza ambacho Kristo atakachokitenda atakaporudi ni kuwafufua waliokufa waungane na walio hai na achague wenye haki wote na wana wa Mungu waaminifu ili watawale pamoja naye katika ufalme wake. Danieli akasema, “Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme, ambao hautaangamizwa milele” (Danieli 2:44). Yesu aliwaahidi wanafunzi wake kwamba wataketi katika viti kumi na mbili wakihukumu kabila kumi na mbili za Israeli (Mathayo 19:28). Sisi pia, tutakuwemo ndani ya ufalme wake, iwapo tutampenda na kumtii yeye sasa (Mathayo 25:34).
MAPENZI YAKO YATIMIZWE DUNIANI KAMA ILIVYO MBINGUNI: Mathayo 6:10
Malaika wa Mungu, wanaoishi huko mbinguni, ndiyo wajumbe wake.Wanazitimiza . kwa ukamilifu amri zote za Mungu (Zaburi 103:20). Ni watu wachache sana duniani wanaofahamu amri za Mungu na hakuna hata mmoja wetu anayezitii wakati wote. Hata hivyo, siku inakuja, wakati Mungu atakapowapatia watakatifu wake uzima wa milele nao watakuwa kama malaika (Luka 20:35 – 36). Ndipo watakapo tawala pamoja na Kristo wakiwa wafalme na makuhani duniani (Ufunuo 5:10) na wataanza kufundisha sheria za Mungu duniani pote. Itachukua miaka elfu moja kuubadilisha ulimwengu wote ili uwe sehemu ya utukufu tena, ambapo wanaume na wanawake wote watatenda mapenzi ya Mungu na kumpatia utukufu.
UTUPE LEO MKATE WETU WA KILA SIKU: Mathayo 6:11
Chakula ni cha muhimu sana kila siku. Siku ya tatu ya uumbaji Mungu aliumba “kila mti wenye kuzaa mbegu na mti wa matunda unaozaa matunda” (Mwanzo 1:11,29), kuwa chakula kuhifadhi miili yetu. Katika jangwa, ambako hakuna miti yoyote ya matunda inayoota, Mungu aliwapatia Waisraeli “Manna” kila siku (Kutoka 16:14 – 15) hadi walipoingia Nchi ya Ahadi (Yoshua 5:12). Waisraeli waliichoka manna na kunung’unika. Hawakuwa na shukrani kwa haraka wakasahau kuwa bila hiyo mana wangekufa. Mungu anatupatia kila kitu ambacho ni muhimu kwetu kila siku chakula chetu, mavazi yetu, malazi yetu. Hivyo kila wakati tukumbuke kumshukuru kwa wema wake wote na kuthamini yale anayotutendea (soma mistari 25 -34).
UTUSAMEHE MADENI YETU KAMA TUNAVYOWASAMEHE WADENI WETU: Mathayo 6:12.
Maana ya fungu hili inapatikana katika mistari 14-15. “Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao (yaani, mambo au maneno yaliyowaumiza ambayo mmetendewa na watu ), basi Baba yenu wa mbinguni pia atawasamehe ninyi makosa yenu”. Mara nyingi watu hufanya vitu vinavyotuudhi au kutukasirisha na wakati mwingine tukahisi kuwa tungehitaji kulipiza kisasi. Mungu hapendei kabisa hali ya aina hiyo. Anatutaka tulipe mema kwa mabaya tunayotendewa (Mathayo 5:44) na kuwasamehe maadui zetu. Tukijifunza hilo sasa, ndipo tutakapozidi kukua tutatambua kwamba sisi pia ni wenye dhambi kwa Mungu nasi tunahitaji msamaha wake. Msamaha wa dhambi zetu ndiyo baraka ya ajabu Mungu anayotupatia tunapobatizwa. Na iwapo hatujifunzi kuwasamehe wengine, basi kamwe tusitazamie Mungu kutusamehe dhambi zetu.
USITUTIE MAJARIBUNI, BALI UTUOKOE MAOVUNI: Mathayo. 6 :13
Yesu aliwafundisha wanafunzi wake kumwomba Mungu kuwaongoza wakati wa mchana, ili kwamba wasije wakanaswa katika njia za uovu za dunia. Ikiwa tunajaribu kumtii Mungu na kuomba uongozi wake, hapo itatubidi kuwa waangalifu kwamba hatutafuti ushirikiano na marafiki waovu na wasiomcha Mungu, au kwenda mahali ambapo wafuasi wa Yesu hawangekwenda. Hatuwezi kumtazamia Mungu “Kutuokoa na maovu” iwapo tutakuwa wapumbavu hivyo. Paulo alipoandika barua kwa mwanafunzi mchanga Timotheo, alimshauri “kuukimbia” ubaya na kuwa na shirika na wale wampendao Mungu (2Tim. 2:22). Kwa njia hii tutachukua tahadhari dhidi ya maovu na kukaa mbali nayo.
“KWA KUWA UFALME NI WAKO NA NGUVU, NA UTUKUFU, MILELE, AMINA”: Mathayo 6:13.
Yesu alimalizia sala yake kwa kumtukuza Mungu. Ni Mungu aliye hai, anayetawala sasa juu ya ufalme wa wanadamu, ingawaje wanadamu hawajui hilo. Hivi punde ataonyesha nguvu zake kuu wakati Kristo atakaporudi. Ndipo watu wote watainama mbele yake na kulisifu jina lake (Isaya 45:22-23). Kama tutajinyenyekeze sasa mbele yake, atatupatia mahali pa heshima katika Ufalme wake.
FUNDISHO KWETU
Tunaona kwamba kuna mafundisho mengi kwa ajili yetu ndani ya sala hii ya ajabu ambayo Bwana Yesu aliwafundisha wanafunzi wake. Jaribu kuishika katika moyo sala hii, siyo kwa sababu tu ya kuirudiarudia kama sala kwa Mungu, lakini hasa ili uweze kufikiria kila sehemu yake na ujifunze mafundisho ambayo hii sala inafundisha. Kumbuka kwamba Mungu ni Baba mwenye upendo anayekujali nawe umpe yeye heshima anayostahili kwa jina lake takatifu. Hivi punde sala hii itajibiwa kikamilifu wakati Yesu Kristo atakaporudi kuanzisha Ufalme wa Mungu. Tutaona mapenzi yake yakitimizwa hapa duniani kama yanavyotimizwa hapa duniani, wakati “dunia itakapojazwa na maarifa ya utufukufu wa BWANA, kama maji yaifunikavyo bahari” (Habakuki 2:14).
MASWALI
Majibu Mafupi
- Kwa nini Yesu aliwaambia wanafunzi wake wasiwaige Waandishi na Mafarisayo?
- Ni nani inayepaswa kujua tunaposali kwa Mungu?
- Mungu anafahamu tunachotaka kabla hatujamwomba. Ni kwa nini basi tuombe?
- Tunaposali kwa Mungu, inatupasa tumwiteje?
5. “Jina lako litukuzwe” hili lina maana gani?
6. Ni nani anayetenda mapenzi ya Mungu huko mbinguni?
7. Ni lini mapenzi ya Mungu yatatendeka hapa duniani?
8. Tujihisi vipi wakati watu wanapotuumiza?
9. Ni lini Mungu anapotupatia baraka za ajabu za msamaha wa dhambi zetu zote?
10. Ni lini sala hii, ambayo Yesu aliwafundisha wanafunzi wake itatimia?
Majibu ya Kina
11. (a) Ni jinsi gani Waandishi na Mafarisayo walivyotenda wakati waliposali na wakati
walipowasaidia maskini?
(b) Ni thawabu gani waliyopata?
(c) Inatubidi tufanye vipi katika mambo kama haya?
(d) Ni thawabu gani tunayotarajia kupata?
- Yesu aliwafundisha wanafunzi wake kusali: “Baba yetu uliye mbinguni”
- Ni kwa vipi Mungu ni sawa na Baba kwetu?
- Kama Mungu ni Baba yetu inatupasa tuwe na mwenendo gani kwake?
13. Yesu aliwafundisha wanafunzi wake kusali: “ufalme wako uje”
- Ni thawabu gani Mungu aliwapatia katika ufalme?
- Ni zawadi gani Mungu anatupatia sisi?
- Ni kwa namna gani mapenzi ya Mungu yatatimia duniani wakati wa ufalme?