86. MFANO WA MPANZI
“Tazama mpanzi alitoka kwenda kupanda”
Shabaha
Ni kuonyesha jinsi Yesu alivyofundisha mfano wa mpanzi na unamaanisha nini kwetu. Yesu alikuwa ameshuka bonde la ukingo wa ziwa a Galilaya na makundi ya watu wakakusanyika na kumzunguka ili kumsikiliza. Akakaa katika mashua karibu ya pwani na kuanza kusema nao kwa mifano. Hizi hazikuwa hadithi za kuwafurahisha watu bali habari za kuwafundisha watu na tena zenye maana iliyofichika. Alitaka watu wakumbuke aliyoyasema na kwa hiyo akaziweka hadithi zake rahisi sana. Hakika ilikuwa muhimu zaidi kwa kweli, kwa wao kufikiria kwa uangalifu juu ya yale waliyoyasikia na kutafuta ni mafundisho gani aliyokuwa anajaribu kuwafundisha. Huenda katika kukaa kwake chomboni, alimwona kwa mbali mkulima akitawanya mbegu zake, kwani alieleza mifano mingi siku ile kuhusu mbegu na mavuno na mikate. Mfano wa mpanzi ni rahisi kuukumbuka, lakini inatupasa kamwe tusisahau fundisho lake lililofichika.
Mathayo 13:1 – 23; soma pia Marko 4:1 – 20; Luka 8:4 – 15
MPANZI ALITOKA KWENDA KUPANDA
Kazi za kilimo katika siku zile za Biblia ilikuwa tofauti sana na kilimo chetu siku hizia. Katika nchi ya Israeli wakulima wengi walipanda ngano na shayiri, na ni katika mazao haya mikate ilitengenezwa. Mkulima ilibidi atifue shamba lake kwa msaada wa maksai wake. Magugu ilibidi yang’olewe, na kuondoa miamba. Na wakati mwingine asingeweza kutoa miamba mazito na mawe mengine mazito yalifichwa na udongo wa juu.
Utifuaji ulipomalizika alingojea mvua ya thamani kutoka mbinguni kulainisha udongo. Ndipo alipokuwa tayari kwenda kupanda mbegu zake. Alibeba mbegu katika mfuko au kikapu mkononi mwake na kutembea kupitia mashamba yake, akisambaza (akimwaga) mbegu kwa viganja vyake vilivyojaa kulia na kushoto kwa kadiri alivyotembea.
Na mbegu zingine zilianguka njiani, karibu na njia, ambako jembe la ng’ombe halikuvunjavunja udongo, ndege walioruka angani juu yake alipokuwa akipanda, walishuka chini na kuzichukua.
Zingine zilianguka penye mwamba, mbegu ziliota haraka hapo, lakini jua kali lilipoziwakia, zilinyauka na kufa kwa haraka vilevile, kwa sababu hapakuwa na udongo wa kutosha wa kuzilisha.
Mbegu zingine zilianguka penye miiba, na hiyo miiba ilikua kwa nguvu zaidi na upesi kuliko mbegu za thamani za mpanzi na kuzisonga.
Mbegu zingine, walakini, zilianguka penye udongo mzuri, zilikuwa na kukua, kuwa mimea yenye afya, zilizaa matunda kwa ajili ya yule mpanzi baada ya kazi yake ngumu Vishada vya nafaka au ngano vilikuwa hasa ndivyo mkulima alivyokuwa anasubiri kabisa. Na hii ilikuwa ndiyo sababu alizipanda mbegu zake.
MFANO UNAFAFANULIWA
Baada ya Yesu kumaliza kusimulia mfano huu akawaambia wale waliokuwa wakimsikiliza, yeye aliye na masikio ya kusikilia, na asikie” (Marko 4:9). Ni fundisho gani walilolipata katika mfano huu rahisi katika maisha yao ya kila siku?
Mpanzi ni Bwana Yesu Kristo. Alipanda mbegu njema, yaani Neno la Mungu, kati ya watu (Luka 8:11) “Mbegu” ilikua vyema mioyoni mwa baadhi yao, lakini ndani ya wengine ilinyauka haraka na kufa. Aina zile nne za udongo ambamo mbegu ziliangukia ni aina nne mbalimbali za watu ambao walilisikia Neno la Mungu.
(a) KANDO YA NJIA
Mioyo kadhaa ya watu ni migumu, wanaposikia neno la Mungu, hawalielewi na wala hawaweza kulielewa. Akili zao zimejaa mawazo ya uchoyo na dhambi kiasi cha kuwafanya kutokuwa na nafasi kwa ajili ya Neno la Mungu. “Mbegu haiwezi” kuota sehemu hiyo.
(b) PENYE MWAMBA
Watu wengine ni sawa na penye mwamba, ambako mbegu iliota na kukua haraka mwanzoni. wana kina kidogo sana kama vile udongo kidogo juu ya mawe. Mara wanaposikia Neno la Mungu, wanaona mara moja kwamba hii ni Kweli, nao “hulipokea kwa furaha” (Marko 4:16). Hata hivyo , mara, majaribu huja juu yao, kama yanavyokuja juu yetu sisi sote. Na kwa sababu Neno la Mungu halina mizizi ya kina mioyoni mwao wanaachana mbali na Kweli (Luka 8:13). Hawaelewi kuwa “Inatupasa kupitia mateso mengi kuingia katika Ufalme wa Mungu (Matendo 14:22).
(c) KATIKA MIIBA
Mbegu iliota pia katika miiba, lakini miiba hukua kwa haraka sana, hukua upesi kuliko ngano au mahindi. Kwa njia hiyo hiyo matatizo na anasa za dunia zinaweza kusonga akili zetu na kutotuachia muda wowote wa kumfikiria Mungu. Jinsi ilivyo rahisi kuacha masomo yetu ya Biblia na shule ya Jumapili kwa sababu tunajibidiisha mno na vitu vingine! Watu wa aina hii wanaipenda Kwelii, lakini akili zao zimejaa mno vitu vingine na kwa hiyo Neno la Mungu “linasukumiwa” nje (Mathayo 13:22). Tunaposikia Neno la Mungu inatubidi kusikiliza kwa makinina kulitendea kazi maishani mwetu. Tusiwe wasikiaji tu, bali tuwe watendaji wa Neno (Yakobo 1:22). Fikiria juu ya vitu ambavyo huenda vilisukumia nje Neno la Mungu kutoka maishani mwako juma lililopita jaribu kufanya vizuri zaidi kuanzia sasa na kuendelea!
(d) UDONGO MZURI
Kitu tunachokiona kuhusu udongo mzuri kinacholeta tofauti na aina zingine zote za udongo ni ile hali ya kuzalisha sana. Watu walio kama udongo mzuri ni wale wanaolisikia Neno la Mungu kwanza; pili wanalielewa Neno; na hatimaye wanazaa matunda ya kazi njema maishani mwao. Hawa ni watu wanaozitunza amri za Mungu.
FUNDISHO KWETU
Kulikuwa na aina nne za udongo na kila mmoja wetu ni kama mmoja wa aina hizi za udongo. Kitu muhimu kukumbuka ni kwamba tunaweza kuamua kuwa ni udongo gani tufananishwe nao? Tujaribu kuwa udongo mzuri kwa kulikaribisha Neno la Mungu kuzama kabisa mioyo mwetu. Hebu tuwe na “masikio ya kusikilizia” na akili iliyo tayari kutenda yote anayotaka Mungu tuyafanye.
MAELEZO YA NYONGEZA
(a) Baada ya Yesu kumaliza kuwaeleza watu mfano huu, wanafunzi wake kumi na mbili wakaja na kumwuliza, kwa nini unasema nao kwa mifano? (Mathayo 13:10).
Makutano waliokuwa wakimsikiliza hawakuambiwa maana yake iliyofichika. Kama wangekuwa makini kujifunza, wangefikiri juu ya habari hii na kuelewa wenyewe. Baadhi yao, Yesu alifahamu, walikuwa “wazito wa kusikia, na macho yao waliyafumba” (Mstari15). Hakutaka watu wa jinsi hii wamfuate. Ni wale tu wenye mioyo safi na yenye ukweli ambao wangekuwa tayari kuitafuta Kweli na kuzibadilisha njia zao. Wanafunzi wake kwa hakika,wao walikuwa wamechaguliwa maalumu kwani wakuwa wame mwamini. Kwao akasema, “Lakini, heri macho yenu, kwa kuwa yanaona na masikio yenu kwa kuwa yanasikia” (Mathayo 13:16). Walivyoendelea kumfuata Yesu walikuwa wakiona na kusikia vitu ambavyo Manabii wa zamani wangalipenda kuviona na kuvisikia. Hivyo wanafunzi wake iliwapasa kusikiliza kwa makini na kujifunza mengi iwezekanavyo kutoka kwa Bwana wao, kwani iliwapasa baadaye wafundishe vitu hivi kwa wengine.
(b) Katika mfano wa mpanzi, Yesu alieleza juu ya mbegu zilizoangukia njiani. “Yeyote anayesikia neno la ufalme, asilielewe, hapo huja yule mwovu, na kulinyakua lile lililopandwa mioyoni mwake” (Mathayo 13:19).
Katika Marko 4:15 tunasoma “Shetani anakuja” na katika Luka 8:12, tunasoma “Ibilisi”. Kama ukiangalia nyuma kwenye maelezo ya ziada, somo la 2, utaona kuwa maneno haya yanaeleza kwa yeyote aliye adui, au anayemtenda Mungu dhambi. Na ndivyo ilivyo katika mfano huu. Imetumika kuelezea aina ya akili iliyo ndani ya watu wale wanaowakilishwa katika mfano huu kuwa “kando ya njia”. Akili zao haziwezi hata kusikiliza Neno la Mungu.Hayupo hata mmoja kati yetu anayependa kuwa hivyo. Inatupsa tujaribu kulielewa Neno la Mungu na polepole litatubadilisha. Ndipo tutakapokuwa kama udongo mzuri unaozaaa matunda mazuri.
MASWALI
Majibu Mafupi
- Jinsi gani mpanzi alipanda mbegu zake?
- Nini kilitokea kwa mbegu zilizoangukia njiani?
- Kwa nini mbegu zilizoanguka penye mwamba zilinyauka na kufa?
- Nini kilitokea kwa mbegu zilizoangukia katika miiba?
- Ni kwa vipi udongo mzuri ulikuwa tofauti na udongo mwingine?
- Yesu ndiye aliyekuwa mpanzi, mbegu ni nini?
- Iwapo sisi ni udongo mzuri, tutazaa matunda gani?
- Ni vitu vya aina gani vinavyoweza kulisonga na kuliondoa Neno la Mungu maishani
mwako?
- Inatupasa tufanye nini ili tuwe kama udongo mzuri?
Majibu ya Kina
- (a) Simulia habari ambayo Yesu aliieleza juu ya mpanzi
(b) Ni watu gani walio kama udongo mzuri?
- (a) Ni mioyo ya aina gani waliyonayo watu wanaofanana na kando ya
njia? Ni kwa nini wako hivyo?
(b) Iwapo tupo sawa na udongo penye miiba, tutaweza kufanya nini juu ya
hilo? Je, tunaweza kubadilika?
Majibu ya Nyongeza
- (a) Ni kwa nini Yesu aliongea kwa mifano?
(b) Kwa nini alifafanua mambo waziwazi kwa wanafunzi wake?
- Watu walio kama “kando ya njia” wana mioyo migumu inamaanisha nini inaposema
kwamba “yule mwovu” anaondoa mbegu iliyopandwa mioyoni mwao?