94. MIFANO MIWILI: WANA WALI KUMI MBILI NA TALANTA
“Ninani basi yule mtumwa mwaminifu na mwenye akili”
Kuonyesha jinsi Yesu alivyofundisha kwa kumia mifano miwili ili kwamba tuwe watumishi waaminifu wakati ambapo hayupo na tuendelee kusubiri kurudi kwake. Yesu alikwisha waonyo watu kuhusu hukumu ambazo Mungu atazileta juu ya Yerusalemu na watu wake, kwa sababu hawakuzaa matunda. Kulaaniwa kwa mti wa mtini lilikuwa ni onyo kwa watu wote. Bado Yesu alikuwa anapenda watu wale waliomfuata na kusikilizamaneno yake wawe wenye busara na waweze kuyaepuka matatizo yaliyokuwa yanakuja mbele.
Na kwa hiyo aliwaeleza mifano miwili ili kuwaonyesha wao umhimu wa kuwa na bidii na uaminifu. Mifano hii ni muhimu kwetu sisi, maana tunayo hamu kubwa ya kuona kurudi kwa Bwana kutoka mbinguni. Akasema, “Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atkayokuja Bwana wenu” (Mathayo 24:42, Mathayo 25:1-31).
KUMSUBIRI BWANA ARUSI: 25:1-13
Welikuwepo wasichana vijana kumi au “mabikira”, waliokuwa wamechaguliwa ili kuhudhuria shughuli ya arusi. Walitakiwa wakeshe kwa ajili ya kusubiri kuja kwa bwana arusi na wao watoke kwenda kumlaki na taa zao, ili wammulikie bwana arusi kwenye chakula cha usiku cha arusi. Na katika tukio hili, bwana alichelewa kuliko ilivyotarajiwa na hivyo “wote wakasinzia wakalala usingizi” (mstari 5). Ghafla, wakati wa usiku wa manane, kelele zikasikika, “haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki” (mstari 6). Kwa haraka wale wanawali waliamushana na wakazichukua taa zao. Watano kati yao ndiyo walikuwa tayari. Na hata ikawa watano waliobakia, mara moja wakagundua kuwa hawana mafuta na taa zao zilikuwa zinaanza kuzimika.
MLANGO UKAFUNGWA
Wale wanawali watano wapumbavu wakasema, “Tupatieni mafuta yenu”, lakini wale wanawali wenye busara wakasema, “Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie” (mstari 9). Kwa hiyo wale wanawali wapumbavu wakaenda upesi kununua mafuta. Na wakati wale walipokuwa wameondoka bwana arusi alifika na wanawali watano wenye busara wakamlaki na wakafuatana naye kwenye chakula cha usiku cha bwana arusi. Waliingia pamoja naye “mlango ukafungwa” (mstari 10).
Na baadaye wale wanawali nao wakafika na wakakuta mlango tayari umefungwa, wakapaza sauti zao: “Bwana, Bwana, utufungulie” (mstari 11). Lakini jibu peke walipolisikia liliwafanya waaibike na kuhuzunika: “Amini, nawaambia, siwajui ninyi” (mstari 12). Walikuwa wamechelewa. Ulikuwa ni uzuri gani wa taa ambazo hazina nuru? Hazikuwa na maana yoyote kwa bwana arusi wakati huo.
MAANA YA MFANO
Yesu alianza mfano kwa kusema, “Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi...”. Inazungumzia wakati ambapo Kristo atarudi na kuuweka ufalme wake. Kristo mwenyewe “ndiye bwana arusi” (mstari 9:15). Sisi ni wanawali tunangojea kurudi kwake. Na “mafuta” katika taa zetu ni Neno la Mungu. Tunaona kutokana na mfano huu kuwa wanawali walitakiwa kuwa tayari wakiwa na mafuta mengi sana. Wote walikuwa na mafuta, lakini ni watano kati yao tu waliokuwa na mafuta ya akiba. Mfano huu unatuambia kwamba wote walisikia Neno la Mungu na kuliamini. Hata hivyo, baadhi yao hawakuweza kuongeza zaidi ya yale waliyojifunza mwanzo na kwa sababu hiyo Kweli ilikuwa haionekani tena katika maisha yao. Yesu alisema: “nuru yenu iangaze mbele za watu, ili wayaone matendo yenu mema; wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni” (mstari 5:16).
Mtume Petro anatuambia kwamba, kama tunataka kuingia katika ufalme wa milele wa Mungu ni lazima “tuongeze” katika imani yetu (2 Petro 1:5,11). Kusoma masomo ya Biblia ya kila siku inatupatia mafuta na inatusaidia kuongeza zile sifa muhimu ambazo Mungu anapenda kuziona tukiwa nazo. Na Yesu atakaporudi atatukuta tukiwa tayari kumpokea na kuwa pamoja naye katika ufalme wake. Na wale wasiokuwa tayari watatupwa katika giza la dunia. “Siwajui ninyi”, atawaambia, maana hatawahesabu kamwe kati ya rafiki zake. Maneno ya mwisho ya Yesu, alipomaliza kusema mfano huu, ni onyo kwetu wote. “Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa ambayo Mwana wa Adamu yuaja” (mstari 13).
MTU ALIYEKWENDA SAFARI YA MBALI: Mathayo 25:14-30
Yesu alisema mfano mwingine kuhusu kujitayarisha kwa ajili ya ufalme “Maana ni mfano wa mtu atakaye kusafiri kwenda nchi ya mbali, akawaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake” (mstari 14). Kutokana na safari hii alimpatia kila mtumishi wake kiasi cha fedha; akampatia mtumishi mmoja taranta tano, na akampatia mwingine taranta mbili na mwingine akampatia taranta noja. Alimjua kila mtumishi wake uwezo wake, na kwa wakati atakapokuwa mbali aliwategemea kuwa waafanya kazi kwa bidii kutokana na taranta hizo alizowapatia.
Na mara baada ya bwana yao kuondoka, yule mtu mwenye taranta tano na yule mwenye taranta mbili walianza kufanya kazi. Na wao, kila mmoja alitumia kile alichoachiwa katika uangalizi wake. Kwa hiyo walikuwa waaminifu wote wawili wakapata mara mbili ya taranta walizopewa na bwna wao. Yule aliyekuwa na taranta tano akapata tano zingine na yule aliyekuwa na mbili akapata taranta zingine mbili.
Hata hivyo, yule mtumishi aliyepewa taranta moja, hakuinyia kazi yoyote ile taranta aliyopewa. Alikwenda akachimba shimo ardhini na akaificha pale ile fedha ya bwana yake.
BWANA AKARUDI
Baada ya muda mrefu, bwana akarudi na akawaita watumishi wake ili waweze kumpatia hesabu ya jinsi walivyokuwa wanamtumikia wakati alipokuwa hayupo. Yule mtumishi aliyepewa taranta tano aliweza kumwonyesha bwana wake taranta tano nyingine ambazo alipata wakati alipokuwa hayupo. Bwana wake akafurahi. “Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi;ingia katika furaha ya bwana wako” (mstari 21).
Na alipokuja yule aliyepewa taranta mbili akamwonyesha taranta mbili zaidi alizopata, bwana kafurahi sana na akampatia thawbu sawasawa na jinsi alivyompatia yule mwenye taranta tano. Na alipokuja yule wa tatu, kwa kweli ilikuwa ni dhahiri jinsi gani alivyokuwa mvivu. Alionyesha hakumhudumia bwana wake kwa furaha kwa kila alilofanya. Yeye alimfikiria bwana wake kuwa alikuwa ni mtu mgumu aliyetegemea apate vitu vingi. Kwa hiyo ile taranta aliyopewa aitunze hakuifanyia kazi yoyote. Alikuwa ni mtumishi asiye na imani wala utii. Bwana akamkasirikia mtumishi yule “mbaya na mlegevu” (mstari 26), na akaamuru atupwe nje ya nyumba yake “katika giza la nje” (mstari 30). Mtumishi yule hakutambua jinsi bwana wake alivyokuwa mwenye haki na mzuri, lakini sasa alipata kile alichokuwa amestahili.
MAANA YA MFANO
Katika mfano huu mtu aliyesafiri nchi ya mbali ni Bwana Yesu Kristo, ambaye yuko mbinguni mkono wa kuume wa Mungu kwa zaidi ya miaka elfu moja na mia tisa. Amekuwa hayupo “kwa muda mrefu sana” (mstari 19), lakini ameahidi kurudi. Kwa wakati huo, sisi ambao ni watumishi wake, tumeambiwa tufanye bidii katika kumtumikia hadi atakporudi. Anategemea kila mmoja wetu kuwa mwaminifu na atatupatia kila mmoja wetu thawabu ya uzima wa milele katika ufalme wake, maadamu tu tuwe na bidii wakati huu ambao hajarudi.
Bwana akawapatia watumishi wake “mali zake” (mstari 14). Kwa hiyo tumepewa Biblia tusome na kuelewa. Kila mtumishi alipewa taranta tofauti. Na kwa hiyo Mungu ametupatia uwezo tofauti lakini anategemea tutumie uwezo wetu katika ubora wa uwezo wetu katika kumtumikia. Katika Biblia tunaambiwa kwamba: “Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya” (2 Wakrintho 5:10). Kwa hiyo, haijalishi ni aina gani ya taranta ambazo tumepewa na Mungu, lazima itumike kwa kumtumikia, kwa ajili ya kumtukuza yeye.
FUNDISHO KWETU
Yesu akasema, “Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake” (Mathayo 24:45) Alisema miifano hii miwili kuwaonyesha wanafunzi wake jinsi gani alivyotegemea wafanye, na akawatia moyo. Ni lazima tuzingatie maana ya mifano hii miwili, kwa maana tunafahamu kwamba Kristo Bwana wetu anakuja mapema. Mfano wa kwanza unatufundisha kuwa wenye busara na kuwa tayari kila wakati, “kwa kuwa humwijui saa ambayo Bwana wenu atakuja”.
Jinsi ilivyo rahisi kufurahia michezo na mambo ya starehe na kusahau kusoma masomo yetu ya kila siku ya Biblia. Hebu tujitahidi kujiwekea utaratibu katika maisha yetu kusoma Neno la Mungu kidogo kila siku. Ndipo hautaweza kuaibika wakati Yesu atakaporudi. Mfano wa pili unatufundisha kuwa watumishi waaminifu wakati ambapo hayupo. Hatuwezi kutegemea kupata thawabu ya uzima wa milele kama hatutajionyesha sisi wenyewe kuwa na nia na wenye bidii.Kuna njia nyingi ambazo tunaweza kuwa watumishi waaminifu. Jambo la kwanza tunalopaswa kufanya ni kuamini kuwa Mungu humaanisha kile anachosema. Na kisha ni lazima tutii amri zake.
Mtume Paulo wakati wote alifundisha: “Enyi watumwa, watiini bwana zetu”. Tukiwa watumwa wa Yesu Kristo ni lazima tufanye mapenzi ya Mungu “kutoka mioyoni” (Waefeso 6:6). “Lolote mfanyalo”, Paulo anasema, “fanyeni kwa moyo, kama vile kwa Bwana ... Mnamtumikia Bwana Kristo” (Waefeso 3:23-24).
MASWALI
Majibu Mafupi
1. Ni kwa nini wanawali alitakiwa kukesha kwa ajili ya bwana arusi?
2. Ni kwa nini wanawali wote walisinzia?
3. Ni kelele gani zilizosikika usiku wa manane?
4. Ni wanawali wangapi waliokuwa tayari waliposikia kelele?
5. Kulitokea nini wakati wale wana waliwapumbavu walipokwenda kununua Mafuta?
6. Bwana arusi alisema nini wakati wanawali wapumbavu waliporudi?
7. Ni mafuta gani tunayotakiwa kuwanayo?
8. Ni onyo gani ambalo Yesu aliwapatia alipomaliza kusema mfano huu?
9. Ni taranta ngapi jumla ambazo bwana aliwapatiawatumishi wake?
10. Je, bwana alitegemea watumishi kutokana na taranta alizowapatia?
11. Nimtumishiyupi ambaye bwana alimpatia thawabu na kwa nini?
12. Ni kwanini alimkasirikia yule mtumishi wake watatu kutokana na mfano Huu?
Majibu ya Kina
13. (a) Eleza mfano wa wanawali kumi
(b) Ni nani bwana arusi
(c) Je, mabikira ni akina nani?
(d) Tunajifunza fundisho gani kutokana na mfano huu?
14. (a) Katika mfano wataranta, ni wapi waliotumia taranta ya bwana wao alipokuwa hayupo?
(b) Tunatakiwa tuwe watumishi wa aina gani wakati Yesu anapokuwa hayupo?