CSSA 1-5-03 - THE HEALING OF THE LAME MAN

Swahili

103. KUPONYA KWA KIWETE

“Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende”

 

Madhumuni

Kuonyesha jinsi Mitume walivyotumia nguvu za Mungu kwa kumponya kiwete kumhubiri Injili. Watu wengi katika Yerusalemu walianza kuamini kwamba Yesu Kristo amefufuka kutoka kwa wafu. Hii ilikuwa ni sehemu ya kwanza ya habari njema ambayo Mitume waliyoifundisha.Iliwapatia watu tumaini la kujiokoa wao wenyewe katika wafu. Miujiza waliyoifanya Mitume kwa jina la Yesu Kristo iliwafanya watu wengi kufurahi, lakini hata hivyo baadhi yao walikataa kuamini.

 

PENYE MLANGO MZURI

Siku moja mchana, yapata saa 9, au kwa muda wa Wayahudi saaa tisa, Petro na Yohana wakiwa njiani kwenda Hekaluni.Muda huu ulikuwa ni muda wa saa za kusali. Lilikuwa ni Hekalu zuri sana lililojengwa na Herode miaka mingi iliyokuwa imepita, na njia ya kuingilia ili kuingia ndani ilikuwa ni kupita mlango ulioitwa Mlango Mzuri. Katika mlango huu watu ambao walikuwa ombaomba waliketi kila siku, wakitarajia kupata fedha kutoka kwa watu waliokuwa wakiingia kusali. Na Mitume wawili walipofika hapa penye Mlango Mzuri wa Hekalu walimwona kiwete ambaye alikuwa akiwaomba watu wamsaidie. Mtu huyu alikuwa mlemavu tangu kuzaliwa na sasa alikuwa na miaka arobaini (4:22) Alishindwa kutoka na kwenda kufanya kazi ya kumpatia riziki yake, alikuwa akibebwa kila siku na nduguze au marafiki zake na kumweka hapo penye mlango aombe msaada, Alilala hapo kwa miaka mingi na hata wageni waliokuwa wanakuja kuabudu mara kwa mara walimfahamu. Alipowaona Petro na Yohana wakiwa wanaingia katika Hekalu aliwaomba msaada. Petro alitambua kuwa sasa ni wakati wa kumponya na kuonyesha nguvu za Mungu na kumhubiri Injili. Petro alimwambia, “utazame sisi”, akimkazia macho yule mtu. Yule kiwete akamwangalia Petro akitarajia kwamba atapewa fedha, hakujua kuwa atapata baraka iliyokubwa zaidi. Petro aliendelea na kusema “sina fedha na dhahabu lakini nilichonacho ndicho nitakupa, kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti simama uende”. Petro akamshika mkono na kumsaidia kusimama, ghafla, mifupa ya miguu ilipata nguvu na kuanza kuchechemea, akasimama na kutembea! Ni furaha iliyoje aliyokuwa nayo mtu huyu, alipotembea pamoja nao huku akirukaruka hadi ndani ya Hekalu na akamsifu Mungu kila alipokuwa akienda zake. Tunaweza kufikiri ni jinsi gani watu waliokuwa wanamfahamu walivyostaajabu kwa furaha walipomwona yule mtu ambaye aliwahi kuwa kiwete alipokuwa akitembea ndani ya Hekalu. Kila mtu alimkimbilia ili kumwona mtu huyu na kusikia mwujiza mkubwa ambao ameupata.

 

PETRO ANAELEZEA MWUJIZA (Mstari 12-18)

Perto alipowaona watu wanakusanyika aliwauliza “Mbona mnastaajabia haya? Au mbona mnatukazia macho sisi, kana kwamba tumemfanya huyu aende kwa nguvu zetu sisi?” Petro aliendelea kuwaambia watu kuwa mtu huyu aliyekuwa kiwete ameponywa kwa imani katika jina la Yesu Kristo wa Nazareti. Ndiye huyo wayahudi walimwua juma chache kabla. Wengi waliomsikiliza Petro ndiyo hao ambao muda kidigo uliopita, wakati wa mashitaka ya Yesu, walipiga kelele, “Msulubishe” lakini Mungu amemfufua katika wafu na sasa wameshuhudia mwujiza mkubwa uliofanyika kwa jina lake.

 

KUTUBU NA KUMRUDIA (Mstari 19-21)

Kumbuka jinsi Petro alivyowaambia watu siku ya Pentekoste kuwa “Watubu na kubatizwa”. Hapa tena Petro aliwafundisha Wayahudi kwamba Mungu atawasamehe (ikiwa ni maana ya “kutubu”). Petro aliwataka Wayahudi waone aibu kwa ajili ya kumwua Yesu Kristo na kubadilisha mioyo na mawazo yao watu waliuona mwujiza huu wa ajabu kwa macho yao wenyewe, ilikuwa ni jukumu lao kuamua kulingana na ujumbe ambao Petro aliusema.

 

WATAWALA WANAKASIRIKA (4:1-4)

Wakati Petro alipokuwa akizungumza, makuhani na wakuu wa Wayahudi walifika. Walikasirishwa na mitume ambao walikuwa wakifundisha kwa jina la Yesu. Hivyo Petro na Yohana walikamatwa na kutiwa ndani usiku mzima. Lakini wengi wa watu walioona mwujiza na walikuwa wakisikiliza, waliamini.

 

MITUME WANAACHIWA (Mistari 5-10, 15-22)

Siku ya pili, Kuhani Mkuu na watawala wa Wayahudi waliwachukua Petro na Yohana kwa mahojiano, wakawauliza; “Kwa nguvu gani au ni kwa jina la nani ninyi manafanya haya?” Mitume walikuwa na furaha sana kwa kusema tena mtu huyu aliyekuwa Kiwete ameponywa “kwa Jina la Yesu Kristo wa Nazareti” (mstari 10). Wakuu wa Wayahudi waliosikiliza haya walikuwa na matatizo. Walijua kuwa ni kweli Kiwete ameponywa. Wasingeweza kulipinga hili. Lakini walikataa kumwamini Bwana Yesu Kristo kwa hiyo waliwakataza Petro na Yohana “Wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu”. Lakini Petro na Yohana waliona ni bora kumtii Mungu kuliko wanadamu, kwa hiyo walijibu: “Maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia. Kwamba ni haki mbele ya Mungu kuwasiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe” (mstari 19-20). Hili liliwafanya Wayahudi kukasirika zaidi, lakini hawakuwa na jinsi ya kuwafanya ila kuwaachia waende. Na watu wote walimtukuza Mungu kwa ajili ya Mwujiza ule wa kumponya Yule Kiwete.

 

FUNDISHO KWETU

Kama ilivyokuwa kwa Petro na Yohana, tunapaswa tutumie kila nafasi kuwaambia watu Neno la Mungu. Wakati mwingine watu hawataki kusikia ujumbe wa Mungu na wanakasirika kama watawala wa Wayahudi walivyofanya. Basi haya yanapotokea nilazima tukumbuke Mungu atawabariki wale wanaolihubiri Neno la Mungu bila hofu.

 

MAELEZO YA NYONGEZA

Viongozi wa Wayahudi waliokuja pamoja na Makuhani kuwakamata Petro na Yohana walikuwa Masadukayo. Hawakuamini kuhusu ufufuo wa wafu. Kwa hiyo hawakutaka mitume wawaeleze watu kuwa Yesu waliye msulubisha alikuwa amefufuka. mitume waliwaeleza kuonyesha waziwazi katika maandiko ya Agano la Kale kwamba Yesu ndiye Masihi aliyeahidiwa. Na kwamba watu wataokolewa kwa njia ya Yesu Kristo.

 

“Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote maana hapana jina jingine chini ya Mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo” (Matendo ya Mitume 4:12)

 

Lakini wakuu hawa wa Wayahudi walikuwa wakaidi. Walitaka watu wawasikilize wao tu kama walivyokuwa wakifanya siku zote.

 

MASWALI

Majibu Mafupi

1.    Ni nani ambaye siku zote angekutwa katika ngazi za Mlango wa Mzuri?

2.    Je, Yule Kiwete alitegemea kuwa Petro na Yohana watampatia nini?

3.    Ni maneno gani mazuri ya Petro aliyomwambia yule mtu Kiwete?

4.    Petro alisema ni jinsi gani Kiwete alivyoponywa?

5.    Petro aliwaambia Wayahudi wafanyeje iwapo kweli waliona aibu ya kumwua Yesu Kristo?

6.    Makuhani na wakuu waliwafanya nini Petro na Yohana?

 

Majibu ya Kina

7.    Elezea ni jinsi gani Kiwete aliyekuwa penye Mlango Mzuri alivyoponywa.

8.    (a) Ni kwanini Makuhani na wakuu wa Wayahudi waliwakasirikia Petro na Yohana?

(b) Wakuu wa Wayahudi waliwakataza Petro na Yohana wasifanye nini?

(c) Petro na Yohana waliwajibu nini wakuu wa Wayahudi?

 

Majibu ya Nyongeza

9.    Petro aliwaambia Wayahudi, waliomwona Kiwete aliyeponywa “Tubuni na mrejee”.

      Alimaanisha nini?

10.  Mwujiza wa kumponya Kiwete uliwaletea tatizo viongozi wa Wayahudi. Tatizo lilikuwa ni lipi?

11.  Wakati Petro na Yohana walipotishwa na watawala wa Wayahudi

       (a)  Walijibu nini; na

       (b) Tunajifunza nini katika hili?

 

 

Swahili Title
103 KUPONYA KWA KIWETE
English files
Swahili file
PDF file
Literature type
Sub type
Sub sub type