119. EUTIKO AKALALA USINGIZI MZITO
“Wakamleta yule kijana, yu mzima, wakafarijika faraja kubwa sana”
Shabaha
Kuonyesha namna wanafunzi walivyokusanyika siku ya kwanza ya juma huko Troa na jinsi Eutiko alivyofufuliwa. Katika safari yake ya pili Paulo alifika Troa, lakini hakukaa pale kwa sababu ya maono ya usiku ambapo Mungu alimwonyesha kwamba alihitajika huko Makedonia (Matendo ya Mitume 16:8–9; angalia somo la 15). Aliporejea Troa alikaa siku saba pamoja na eklesia aliyokuwa ameianzisha pale. Ndugu kutoka eklesia kadha waliosafiri pamoja naye wanaorodheshwa katika Matendo ya Mitume 20: 4, Luka, aliyeandika matendo ya Mitume na yeye pia alikuwa na Paulo.
Matendo ya Mitume 20: 7 -14
SIKU YA KWANZA YA JUMA HUKO TROA (mstari 7)
Ilikuwa ni desturi ya Wayahudi kuitunza siku ya saba, Sabato kwa ajili ya siku ya dini ya kuabudu. Mungu alikuwa ameiagiza amri hiyo (Kumbukumbu la Torati 5:12). Wafuasi wa Kristo walizoea kukutanika kama tunavyofanya katika siku ya kwanza ya juma, ambayo ndiyo siku ambapo Kristo alifufuka kutoka kwa wafu. (soma mstari 7:1 na Wakorintho 16:2). Tunaweza kutafakari jinsi wnafunzi wa Troa walivyosisimka kwa furaha kubwa kuwa pamoja na Paulo katika siku ya ukumbusho. Kungekuwepo na kusoma maandiko na kisha Paulo angetoa hotuba ya mausia. Wangekuwa na furaha pia kwa kuwa na wageni ambao walitoka nchi zingine, ndugu wanaume na dada ambao wote waliunganishwa na Kweli moja ambayo waliishiriki. Hivyo walikusanyika pamoja kama Yesu alivyokuwa amewafundisha wanafunzi wake kukumbuka upendo mkubwa na dhabihu aliyoitoa Bwana wao. “Maana kila mlapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo” (1 Wakorintho 11:23 –29). Kila inapowezakana wanafunzi wote wa Bwana Yesu Kristo wanakutana kila siku ya kwanza ya juma kukumbuka kifo chake na ufufuo kwa njia hii. Inawalazimu kukusanyika pamoja ili kumkumbuka Bwana Yesu na kutiana moyo kwa kuishi katika njia inayompendeza Mungu. Tumaini la ufufuo kwa uzima wa milele ni kwa ajili yao tu wanaoendelea kuwa waaminifu hadi Kristo atakapoudi. Katika siku zile za mwanzo kwa wale walioiamini Kweli ilikuwa ni desturi ya ndugu wanaume na wanawake kula chakula kwa pamoja baada ya mkutano wa kumbukumbu ya kumega mkate na kunywa divai. Na kwa wale waliokuwa watumwa, wakati mwingine waliwatumikia mabwana ambao walikuwa wakali, kuna uwezekano kuwa hiki chakula kingekuwa ndiyo chakula bora ambacho walipata kwa juma zima.
ROHO MTAKATIFU ANAGEUZA KIFO KUWA FURAHA (mstari 8-12)
Mkutano ulifanyikia katika chumba cha ghorofani, naye Paulo bila shaka alikuwa alikilinganisha matukio na Agano la Kale, wakati ndugu wanaume na wanawake wapokuwa wakisikiliza kwa makini. Alinena kwa muda mrefu, lakini hawakujali kwa kuwa alikuwa akitarajia kuondoka siku iliyokuwa inafuata na hii ilikuwa ndiyo nafasi ya pekee ya kumsikiliza. Mkutano uliondelea mpaka usiku wa manane na taa nyingi zilikuwa zikiwaka katika chumba hicho walichokuwa wamekusanyikia. Na kwa sababu ya uwingi wa watu waliokuwa chumbani, kijana mmoja aliyeitwa Eutiko alikuwa amekaa dirishani akisikiliza. Tofauti na madirisha yetu, hili lilikuwa ni uwazi uliotobolewa tu ukutani. Wakati Paulo akiendelea kunena Eutiko akazidiwa na usingizi akasinzia na polepole akalala. Ghafla kwa ajili ya usingizi akawa amepoteza uwezo wake wa mwili wa kujimudu akaanguka kutoka ghorofa ya tatu mpaka chini . Kila mmoja alifadhaika sana na kukimbia mbio kupitia ngazi mpaka chini na kumkuata Eutiko akiwa amesha fariki. Paulo bila shaka, alikuwa naye amekimbia chini pamoja nao hadi pale alipolala yule kijana alipokuwa amelala. Ndugu wanaume na wanawake, wakiwa wenye fadhaa kwa hilo lililotokea, walimwachia Paulo njia ambaye alimkumbatia Eutiko alipoanguka. Mtume alijua kuwa alikuwa amepewa nguvu za Roho Mtakatifu kufanya miujiza na sasa alitakiwa alitakiwa kumwomba Mungu ili kwamba uweza huu utumike. Mungu alisikia ombi lake na uhai wa yule kijana ukamrudia. Paulo akawageukia ndugu na dada waliokuwa wakilia na kusema, “Msifanye ghasia, maana uzima wake ungalimo ndani yake” (mstari 10). Kwa furaha kuu wote wakarudi ndani ya chumba ambacho walikuwa wamekutania, mahali ambapo Paulo alimalizia hotuba yake, nao “wakamega mkate” kwa ajili ya kumbukumbu ya kifo chake, kuzikwa na kufufuka kwa Bwana Yesu Kristo. Nitukio la kutisha na kutotazamiwa namana gani kutokea katikati ya mkutano. Hata hivyo, fikiria, furaha kuu waliyokuwa nayo wanafunzi walipoona uweza wa Mungu ukitendeka mbele ya macho yao kwa kumfufua kweli mtu huyu kutoka katika mauti! Jinsi tukio hili lilivyowatia moyo ya kuwa imani kwa Mungu. Wasingeweza kusahau kamwe mkutano ule!
PAULO ANAWAIMARISHA NDUGU WANAUME NA WANAWAKE NA KISHA ANAONDOKA (mstari 11 -13)
Baada ya mkutano ule wa kumbukumbu wanafunzi walikaa chini na kushirikiana kumega mkate kwa pamoja. Hakuna mtu yeyote aliyetaka kurudi nyumbani usiku ule ingawaje ilikuwa ni muda wa saa za alfajiri za asubuhi siku ile. Paulo akazidi kunena nao mpaka kulipopambazuka. Mtume na wenzake walipanga kuondoka siku hiyo kwenda Aso iliyokuwa umbali yapata kama kilometa 30. Paluo alikusudia kutembea, wakati wengine walikwenda kupanda meli. Akaungana nao kule Aso, nao wote wakendelea na safari yao ya kurudi Yerusalemu.
FUNDISHO KWETU
Jina Eutiko, maana yake “mwenye bahati” mambo kweli yalimwendea vyema yule kijana, lakini baraka yake kubwa kabisa ilikuwa, bila shaka kabisa, kwamba aliisikia Injili iliyohubiriwa na Mtume Paulo, na akarudishiwa uhai wake tena. Alipewa nafasi zaidi ya kumtumikia Mungu. Hakuna shaka kwamba Eutiko aliutazamia ufufuo wakati Kristo atakaporudi, kwa maana ndipo atakappewa uzima wa milele na hatakufa kabisa. Na hili ndilo tumaini letu pia, kwa maana tunafahamu kwamba Kristo atarudi upesi kama alivyoahadi.
MAELEZO YA NYONGEZA
Makusanyiko ya kumbukumbu ya eklesia za nyakati za mwanzoni ilikuwa ni yenye kufanana na makusanyiko ya leo. Tunajaribu kufuata mtindo huo huo kwa kadri inavyowezekana. Wanafunzi walikutana mahali pamoja, mara nyingi katika nyumba ya ndugu mwanamme au mwanamke (kwa mfano, Warumi 16 4-5, katika nyumba ya Akila na Prisila; Filemoni mstari 2, nyumba ya Filemoni). Kulikuwa na kusoma Maandiko na kufafanua neno ili kuwapa moyo “kwa ajili ya upendo na katika kazi nzuri” (Waebrania 10: 24). Waliomba sala na kila mmoja alipelekewa kwa zamu mkate na mvinyo ili kila mwamini aweze kula na kunywa. Wao pia waliimba nyimbo za kusifu kama vile sisi tunavyofanya. Kama tulivyojifunza katika masomo ya mwaka uliopita, Yesu aliumega mkate na kunywa divai pamoja na wanafunzi wake kwa mara ya kwanza ikiwa na maana maalumu, kabla tu ya kusulubiwa kwake. Aliwaambia kwamba iliwapasa kumkumbuka kila wakati kwa njia ya namna hii waliposhiriki mkate na mvinyo kwa pamoja. Kwa upande wa mkate akasema: “Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu, fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu”. Na kwa upande wa divai akasema: “Hiki ni kikombe cha Agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu” (Luka 22: 19 – 20). Ni kwa wale tu walio na tumaini linalofanana sawa na wanafunzi wanaweza kushiriki mkate na divai kwa njia hii. Kwa hiyo wanakumbuka yale ambayo Yesu aliyafanya kwa ajili yao pale alipokufa msalabani. Linawakumbusha pia juu ya ufufuo wake na tumaini walilonalo la ufufuo wakati atakaporudi, kwa sababu aliwaambia kwamba angekula na kunywa pamoja nao tena “katika ufalme wa Baba yangu” (Mathayo 26:29). Katika waraka wake kwa Waebrania, Paulo aliwaeleza jinsi ilivyo lazima kwa ndugu wanaume na wanawake kukutana kwa ajili ya Neno la Mungu kila mara inapowezekana, “na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadri mwonavyo siku ile (ya kuja kwa Kristo) inakaribia” (Waebrania 10: 25). Jinsi Mungu alivyo na hekima katika kutuagiza kufanya mambo haya. Yanatusaidia kutuepesha kusumbukia maisha haya ili yasi tuelemee, na kutufanya kusisahau tumaini kubwa lile tulilowekewa mbele yetu.
MASWALI
Majibu Mafupi
1. Ni katika siku gani ya juma wanafunzi walikutanika kule Troa?
2. Walikumbuka nini siku hiyo?
3. Ni nani aliyekuja kusema nao kule Troa?
4. Ni tumaini gani kuu ambalo ndugu wote walikuwa nalo?
5. Ni jambo gani lililomtokea Eutiko wakati Paulo akisema?
6. Je, Paulo alifanya nini kwa ajili ya Eutiko?
7. Ni kwa jinsi gani Paulo angeweza kumfufua Eutiko?
8. Paulo alikuwa akifanya nini mpaka kukapapambazuka?
Majibu ya Kina
- Eleza yote unayoyafahamu kuhusu mkutano wa Paulo pamoja na wanafunzi kule Troa na nini kilitokea kwa
Eutiko.
Majibu ya Nyongeza
- Eleza unavyofahamu kuhusu namna mikutaniko ya ukumbusho ilivyoendeshwa siku za mwanzoni kwenye katika eklesia
- (a) Ni kwa nini ndugu wanaume na wanawake wanakutana pamoja kila juma kumega mkate na kunywa
divai?
(b) Yesu alisema mkate na divai viliwakilisha nini?
(c) Je, Yesu alisema ni lini atamega mkate na kunywa divai tena?