129. AGANO LILIFANYIKA EDENI
Katika somo la tatu tuliona kilichotokea ikiwa ni matokeo ya kuasi sheria ya Mungu. Adamu na Hawa walihukumiwa kifo, na wazao wa Adamu wote wanarithi laana ile ile ya hali ya kufa. Lakini Mungu, kwa rehema zake, aliweka tumaini la ukombozi kutokana na laana ya dhambi na kifo, hata anapowahukumu wenye dhambi. Wakati nyoka alipopewa laana, Mungu pia alitoa ahadi ya Mkombozi ambaye angeleta wokovu.
Mwanzo 3:14-24 AGANO LENYEWE (Mwaanzo 3:15)
Katika kumlaani nyoka, Mungu alisema “nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino”.
Vipengele muhimu katika ahadi hii ni kama ifuatavyo:-
-
“Wazao” wawili au uzao wa aina mbili
-
Uadui ( hasa chuki au ugovi) kati yao;
-
Uadui kati yao,ulisababisha (1) jeraha la kudumu/ la kifo (kupondwa/ kukanyagwa kichwa chini ya nyayo) kwa “uzao wa nyoka”, na (2) Jeraha la muda (kwenye kisigino) kwa “uzao wa mwanamke”. Ni akina nani hawa wazao wawili?
Kwanza, yapasa ieleweke ya kwamba ahadi hii inaelezwa kwa lugha ya mifano. Ni lazima tuelewe maana ya “nyoka” na “mwanamke” inachowakilisha. Ndipo tutakapoelewa inamaanisha nini kusema “wazao” wa aina mbili.
“Nyoka” anawakilisha mafundisho aliyotamka (“hamtakufa hakika”), ambayo inaelezwa katika Agano Jipaya kuwa “nia ya mwili”. Ni uadui juu Mungu (Mwanzo 3:4).
Mwanamke anawakilisha kweli, au Neno la Mungu, ambalo alilisema wakati wa kwanza alipoulizwa na nyoka (Mwanzo 3:2-3).
Uzao wa nyoka ndio wale watu wanaofikiri na kutenda kwa jinsi ya namna ile ile ya nyoka. Hakuweza kuonyesha imani kwa namna yeyote (akiwa mnyama) na wala hakuwa ametawaliwa na maadili kwani hakuwa na ufahamu wa mema au mabaya. Paulo anafafanua hili kuwa ni “tabia ya mwilini”, “ubinafsi” au “nia ya mwili”. Katika Wagalatia 5:19-21 anaorodhesha“Matendo ya mwili”.
Mawazo yote na matendo ambayo yako kinyume na amri za Mungu yako katika aina hiyo hiyo. Watu wanaojipenda wenyewe katika kila wanachofanya,wanaoongozwa na nia ya mwili, nao wanaorodheshwa pamoja na kujulikana kuwa ni “uzao wa nyoka” (Warumi 8:6-8; Mathathayo 12:34; 23:33).
“Uzao wa mwanamke” ni wale watu wanaofikiri na kutenda kwa kufuata Neno la Mungu. Mfano mmoja kamili pekee wa uzao wa mwanamke ni Bwana Yesu Kristo. Ambaye ndiye pekee aliyeshinda dhambi. Kamwe hakushindwa na majaribu ambayo wote yanatukabili . Alilikubali Neno la Mungu kumwongoza katika kila wazo na tendo. Hata katika jaribu kuu mno la kuepuka kifo cha msalaba katika bustani ya Getsemane, bado aliweza pia kusema, “walakini si mapenzi yangu,bali yako yatendeke” (Luka 22:42). Kwa hiyo kupondwa kabisa kwa nia ya mwili kulionekana katika maisha ya Yesu hata akawa mtii wa kifo cha msalaba. Kwa hiyo ndiye hasa aliyekuwa “uzao wa mwanamke”- liyeipatia dhambi pigo la kifo. Kifo chake na ufufuo ulikuwa ndiyo kumponda nyoka kichwa (Waebrania 2:14).
Ili kufikia ushindi juu dhambi ilimpasa kuvumilia mateso na kifo. Alikaa kaburini muda wa siku tatu. Katika hili linaweza kuonekana kuwa utimilifu wa ''kumponda kisigino”, yaani pigo la muda. Kaburi liliweza kumshikilia muda wa siku tatu tu kwani Mungu asingeweza kumruhusu Mtakatifu wake kuona uharibifu .Mungu akampatia thawabu ya ufufuo kwa ajili ya utiifu wake na kumwinua hadi kumketisha mkono wake wa kulia (Matendo ya Mitume 2:27; Waebrania 1:3).
Sisi pia tunaweza kuwa katika kundi hili linalojulikana kama “uzao wa mwanamke” kwa kuamini na kubatizwa katika Bwana Yesu Kristo. Tutakataa kuzifuata njia za mwili ambazo huwa zinafanywa na ule “uzao wa nyoka”. Tutajibidiisha kufuata kielelezo cha Kristo. Hapo ndipo tutakapoonyesha kwamba tumo ndani ya kusanyiko la uzao wa mwanamke. Tutakapopatikana katika kusanyiko hilo wakati Kristo atakaporudi tutashiriki katika utukufu na furaha ya wale waliokombolewa.
Kusanyiko hilo litapigania kuiponda dhambi kwa bidii zote na kumtii Mungu, kama Bwana wao ambaye amekuwa mfano wao kamili.
MPANGO WA MUNGU WA UKOMBOZI (Yohana 3:14-16; 1 Petro. 2:21-24)
Agano lililofanyika katika Edeni ni ufafanuzi wa mpango wa Mungu wa ukombozi kwa ajili yetu.
Kama tungeachiwa tujiokoe wenyewe, tungekufa wote, nakurudia mavumbini na kubakia kaburini. Kwa njia ya “uzao wa mwanamke” (Yesu Kristo) tunaweza kupata msamaha wa dhambi kwa njia ya ubatizo katika Kristo, na kuutazamia uzima wa milele (Yohana 3:16).
Inatupasa kudumu katika kumtumikia Mungu na kufanya mapenzi yake kila wakati, tukifuata mfano wa Yesu, “ambaye hakutenda dhambi , wala hila haionekana kinywani mwake. (1 Petro 2:21-22). Yesu Kristo alikuwa mtiifu kabisa kwa Babaye hadi mauti. Pale sisi sote tunaposhindwa, Kristo alishinda na kushinda kila jaribu. Kwa sababu Yesu alifanikiwa hili, Mungu kwa rehema yake amefanya iwezekane kwa watu wote wanaofuata mfano wa Yesu na wao watafufuliwa siku atakaporudi na watapewa uzima wa milele.
Yesu alishinda nguvu ya dhambi ndani yake yeye mwenyewe, lakini uzao wa nyoka hautaangamizwa kabisa mpaka mwisho wa miaka elfu moja ya Utawala wa Kristo. Ndipo nia za mwili zitatoweka milele, na kifo hakitakuwepo tena.
ADAMU NA HAWA WANAVIKWA NA MUNGU-ISHARA YA UPATANISHO: (Mwanzo 3:21; 1 Petro 1:18-20)
Wakati Adamu na Eva walipotambua kuwa wako uchi, walijitengenezea mavazi kutokana na majani ya mtini. Hili lilikuwa wazo lao la kujifunika na wala kwa hakika haukuwa utaratibu wa Mungu. Badala yake Mungu aliwafunika na “mavazi ya ngozi”, ikiwa na maana ya kwamba ilitakiwa mnyama achinjwe na damu kumwagika. Katika hili Mungu alikuwa akiwafundisha somo. Kwa kuwapatia vazi la kuwafunika kwa njia hii, Mungu alikuwa akiwekea sheria kwamba “pasipo kumwaga damu, hakuna ondoleo” la dhambi (Waebrania 9:22).
Kumwagika kwa damu na kufunika uchi katika sura hii, ilielekeza mbele kwenye kifo cha Mwana wa Mungu. Kwa damu yake iliyomwagika, dhambi zetu zaweza kusamehewa. Kristo ndipo yeye anapofanyika vazi la kufunika dhambi zetu.
Bwana Yesu Kristo anakuwa ndiye kielelezo chetu. Tunaekeza akili zetu kutoka katika mawazo ya kimwili, na kuwaza kama Kristo, tunaelekeza mawazo yote katika mapenzi ya Mungu. Tunatubu dhambi zetu na kutafuta kuyatii mapenzi ya Mungu. Kwa ubatizo, baada ya kuielewa Injili, tunavaa au tunakuwa tumemvaa Kristo (Wagalatia. 3:27). Ndipo “dhambi zetu zinakuwa zimefunikwa” (Warumi 4:2)
ADAMU NA HAWA WANAFUKUZWA BUSTANINI (Mwaanzo 3:22-24)
Baada ya Mungu kutoa hukumu juu yao na kuwavika nguo, Adamu na Hawa waliondolewa katika bustani ya Edeni. Mungu akasema, “Basi huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya”. Pale kulikuwa na hatari,“asije akanyosha mkono wake, akayatwaa matunda ya mti wa uzima akala akaishi milele”. Kwa hiyo aliondolewa katika Bustani ya Edeni aende ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa. Upande wa mashariki wa bustani waliwekwa “Makerubi, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima”. Adamu na Hawa walizuiliwa kuufikia ule mti wa uzima.
Inawakilisha kwetu kama mfano wa uzima wa milele ambao wale watakaostahili watapewa wakati Kristo atakaporudi – kwa hao zawadi ya uzima wa milele itakuwa sawa na kula mti ule wa uzima.
VITABU REJEA:
"Elpis Israel" (J. Thomas)—Part First, Chapter 3
"Key to the Understanding of the Scriptures" (H. P. Mansfield)—Pages 36-54
"The Story of the Bible (H. P. Mansfield)—Chapter 4
MASWALI YA AYA
1.Eleza kwa kifupi inamaanisha nini katika Mwanzo 3:15 “Nyoka”, “Mwanamke”; “Uzao wa nyoka”, “Uzao wa mwanamke”
2.Ni jinsi gani Yesu Kristo “alivyomponda kichwa nyoka?”
3.Mungu ameweka njia gani ya “kufunika dhambi zetu?”
MASWALI YA INSHA
1. Fafanua maneno katika Mwanzo 3:15: Atakuponda kichwa, naye atamponda kisigino chake”.
2. Tunawezaje kuwa sehemu ya “Uzao wa mwanamke?”