CSSA 2-1-07 - FROM THE CALL OF ABRAM TO THE DESTRUCTION OF SODOM

Swahili

132. TANGU KUITWA KWA ABRAMU MPAKA KUANGAMIZWA KWA SODOMA

Haikuchukua muda mrefu watu wakasahau fundisho la gharika na wakaiacha imani ambayo Nuhu aliwaonyesha. Mungu alikuwa amewaagiza kwenda duniani kote na kuitawala (Mwanzo 9:1-7), lakini badala yake wakakusanyika pamoja na kujenga mji (Babeli) (Mwanzo 11:4-9). Mapema tu walianza kuabudu sanamu na Mungu mmoja wa kweli na njia zake zikasahauliwa kabisa. Katikati ya ibada ya kuabudu sanamu Mungu alimwita mtu mmoja – Abramu, ambaye baadaye alimwita Ibrahimu. Tafadhali zingatia kwamba ahadi kwa Ibrahimu zitaelezewa kwa undani zaidi katika Somo la 9.

Mwanzo 11:31-32; 12: 1-9

 

MUNGU ANAMWITA ABRAMU (Mwanzo 11:26-32; 12:1-9)

Abramu aliishi katika mji mkubwa na uliostaarabika sana, wa Uru ya Ukaldayo. Wakazi wa Uru waliabudu mungu-mwezi ambaye walimjengea hekalu la kupendeza sana. Huko Uru, Mungu alimtokea Abramu na kumwita aende katika nchi atakayo mwonyesha (Matendo ya Mitume 7:2,3). Hiki kilikuwa ni kipimo kikubwa cha imani yake na tumaini lake kwa Mungu. Kwa Abramu kuacha nyuma mafanikio yake yote na usalama wa maisha yake katika ule mji na kuhamia sehemu ambayo hakuijua, kunaonyesha imani yake ya kwamba Uru isingempatia chochote ukilinganisha na imani aliyokuwa nayo ya wito wa Mungu (Waebrania 11:8)

 

Abramu alitii na kusafiri mpaka Harani, mji ambao ulikuwa mbali upande wa kaskazini ukingoni mwa mto Frati. Alikwenda pamoja na Tera, baba yake. Nahori ndugu yake, Lutu mtoto wa ndugu yake na Sarai mkewe .

 

Akiwa huko Harani, Abramu kwa mara nyingine tena Mungu alimtokea na Mungu akamwambia, “Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako (Mwanzo 12:1). Abramu alionyeshwa wazi wazi kuwa kama alitaka kumwabudu Mungu, ilimpasa kujitenga mwenyewe kwa kuacha mambo yote aliyoyazoea, hata kama ni jamaa zake (iwapo ni muhimu) kufanya hivyo.

 

Mungu pia alimpatia Abramu ahadi nzuri sana (mstari 2-3). Aliambiwa kwamba:-

 

  1. Angekuwa taifa kubwa.

  2. Jina lake lingekuzwa naye angefanyika baraka

  3. Mungu angewabariki wambarikio na kuwalaani wamlaanio.

  4. Katika Abramu jamaa zote za dunia watabarikiwa.

 

Wakati huo Tera alifariki huko Harani naye Nahori asingeweza kushauriwa kuacha mji na kuongoza kuishi maisha ya ugeni. Hata hivyo, Abramu alimtii Mungu na kutoka Harani, akamchukua pamoja naye Sarai mkewe pamoja na Lutu mtoto wa ndugu yake.

 

Kwa hiyo akiwa na mifugo na mali na watumishi, Abramu na kundi lake wakavuka mto (Yoshua 24:2-3). Abramu akajulikana kuwa ni Mwebrania- inayomaanisha “aliyevuka ng’ambo ya mto” (Mwanzo 14:13). Alikuwa amevuka kutoka njia za ibada ya sanamu kuelekea katika njia ya Mungu mmoja wa kweli: kutoka nchi ya Babeli na kwenda Nchi ya Ahadi.

 

ABRAMU ANAPITA KATIKA NCHI YOTE (Mwanzo 12: 6; 13:1-18)

Abramu na wenzake wakasafiri wakitembea katika nchi yote, wakipitia malisho hadi malisho, huku wakichunga mifugo yao. Pale Shekemu Mungu alimtokea tena Abramu na kumwahidi “Uzao wako nitawapa nchi hii” (mstari7). Ingawaje wakati ule nchi ilikuwa ikikaliwa na Wakanaani.

 

Wakati huo kulikuwa na njaa katika nchi naye Abramu akashuka kwenda Misri kupata chakula kwa ajili ya watu wake na mifugo yake. Alipoondoka Misri alikuwa tajiri sana “kwa mifugo, kwa fedha na kwa dhahabu”(Mwanzo 13:2). Kutokana na ongezeko la makundi ya mifugo yao, ikawa vigumu kwa wachungaji wa Abramu na wa Lutu kupata mbuga za kulisha kwa pamoja nao wakawa wanagombana. “Abramu akamwambia Lutu, Basi, usiwepo ugomvi, nakusihi kati ya mimi na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wachungaji wako, maana sisi ni ndugu” (Mwanzo 13:8). Kwa hiyo Abramu akampa nafasi Lutu ili achague kwanza katika nchi yote kwa ajili ya kuchunga mifugo yake. Lutu akachagua mabonde yenye maji mengi ya Yordani na baadaye akafanya makao yake katika mji wa Sodoma.

 

Abramu mwenyewe akabakia kwenye maeneo ya miinuko na kuendelea kuishi katika mahema. Hata hivyo, Mungu akamwahidi Abramu tena nchi yote aliyoweza kuiona “Nchi hii nitakupa wewe na uzao wako milele” (mistari 14-17)

 

Hadi hivi leo, Abramu hajaipata nchi hii, lakini lile ambalo Mungu ameahidi kwa hakika atalitimiza. Abramu itabidi, afufuliwe kutoka kwa wafu wakati Yesu Kristo atakaporudi. Ndipo atakapopokea nchi aliyoahidiwa yeye na uzao wake karne nyingi zilizopita (soma Wagalatia 3:16,26-29). Abramu alijua kwamba Mungu alimwahidi nchi ile, naye akaingojea kwa subira kwa maana makusudi ya Mungu ni lazima yatatimizwa. Hakukuwa na chochote katika miji ya bondeni cha kumvutia Abramu. Alilidhika kuzunguka zunguka katika nchi, mgeni na msafiri “akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu” (Waebrania. 11:10)

 

CHAGUO BAYA LA LUTU

Lutu alipata taabu kutokana na chaguo lake la kuishi ndani ya Sodoma. Fikiria matukio yake ambayo hatimaye yalisababisha kupotea kwa mali zake na hata kukaribia kupoteza familia yake yote.

 

  • Akaliona bonde zuri sana lenye kujaa maji (Mwanzo 13:10)

  • Alichagua kuelekea bondeni akipenda zaidi kuliko sehemu za milimani (mstari 11)

  • Alisafiri kwenda upande wa mashariki (mstari 11)

  • Akajongeza hema yake mpaka Sodoma (mstari 12)

  • Alikaa huko Sodoma, katika nyumba (Mwa. 14:12)

  • Alikaa mlangoni pa Sodoma (Mwanzo 19:1)

  • Alilazimishwa kuacha kila kitu na kuokoa uhai wake(mstari 17)

 

Lutu alichagua njia iliyo rahisi ambayo ilimpendeza machoni pake. Inawezekana alifikiri ya kwamba angeweza kudumu katika kujitenga na maovu ya watu wa Sodoma lakini hatua kwa hatua yeye na familia yake wakawa wamezingirwa na maisha ya watu wasiomcha Mungu, wa mji ule wa waovu pamoja na matokeo ya kutisha ya mauti . Inatupasa kuwa waangalifu sana kutoruhusu maovu ya miji yetu kuharibu maisha yetu. Tunaweza kuathiliwa kwa urahisi na matendo yao mabaya (1 Wakorintho. 15:33; 34; 2 Timotheo 2:22)

 

Inatupasa tuwe waangalifu kufikiria yale ambayo Mungu anayohitaji na tufanye nini ili kumpendeza Mungu. Hatulazimiki kuchagua vitu rahisi na vyenye mvuto katika maisha, ambavyo havitadumu (soma 2 Petro2:6-8). Kristo alituonya jinsi itakavyo kuwa ujinga “kupata” anasa na furaha ya maisha haya na “kupoteza” uzima wetu wakati Yesu atakapokuja. Ombi lake lilikuwa“mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe ajitwike msalaba wake, anifuate” (Mathayo 16:24-26).

 

 

 

KUKUBALIWA KWA ABRAMU NA MUNGU

Abramu aliamini ahadi za Mungu na maandiko yanaeleza ya kwamba imani yake “ilihesabiwa kwake kuwa haki” (Mwanzo 15:6; Warumi 4:3). Alionyesha imani yake katika vitendo vyake: katika kuacha mahali alipozaliwa;na kuchagua kuishi katika mahema, kwa kuziamini ahadi za Mungu kuhusu nchi, kuzaliwa kwa Isaka na wingi wa uzao wake . Kwa hiyo basi ametajwa kwa haki kuitwa “rafiki wa Mungu” (Yakobo 2:23)

 

LUTU ANAOKOLEWA KUTOKA SODOMA (Mwanzo 18:19)

Tunasoma katika Mwanzo sura 18 ya kwamba malaika watatu walimtembelea Ibrahimu. Baada ya kumaliza kula chakula, waliondoka kuelekea Sodoma ili kuiteketeza.

 

Ibrahimu aliwasihi kuuokoa mji iwapo wangepatikana humo watu wenye haki katika mji (Mwanzo 18:23-32). Ibrahimu alizingatia usalama wa Lutu, lakini habari inatuonyesha jinsi watu wa Sodoma walivyokuwa watenda maovu, kwa sababu hawakuonekana hata watu kumi wenye haki ndani ya mji. Kwa kweli alikuwamo mtu mmoja tu- Lutu.

 

Nyumba yote ya Lutu pamoja na watumishi wake wote walikuwa wamezama ndani ya vitendo viovu vya mji ule. Jinsi ilivyokuwa vigumu kwake kudumisha nia ya kumwabudu Mungu katikati ya watu wengi watendao uovu namna hiyo.Tukitenda bila hekima kama Lutu alivyofanya, hapo tutaingia katika hatari mbaya ya kushindwa na dunia inayotuzunguka, na kuteseka kutokana na hukumu kuu ya Mungu kwa watu wa dunia hii watendao maovu na wasiomcha Mungu.

 

Kati ya watu wote waliokwenda pamoja naye, ni Lutu peke yake aliyeendelea kuwa mwamini tu kwa Mungu. Alikuwa mtu mwema moyoni mwake, lakini naye pia alikuwa mzito mno kusikia onyo la malaika na “akakawia-kawia”. Lakini Mungu “alimhurumia” (Mwanzo 19:16) na kumwongoza nje ya mji huo ambao unaangamizwa. Na kwa upande wake mke wa Lutu hakuweza kukubali kuondoka na kuacha mali zake zote nyuma, na familia yake aliyoipenda iliyobaki licha ya matendo yao kutokumcha Mungu.

 

Hivyo akageuka nyuma kwa hamu kuu ya Sodoma na hivyo akaunguzwa na moto wa kiberiti ulioiteketeza miji yote ya bondeni. Lutu na binti zake wawili wakakimbilia Soari na kuokoka.

 

ONYO LA KRISTO KWETU (Luka 17:28-32)

Maandiko yanatueleza ya kwamba “kama ilivyokuwa katika siku za Lutu .... ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu” (Luka 17:28-32).

 

Tunauona uovu wa Sodoma ukiwa kila sehemu zetu zote kwa namna watu wanavyoishi siku hizi,wanavyosema, wanavyotenda na kuvaa. Yesu anatuonya kwamba katika siku zetu atakuja kama mwizi usiku, kuleta hukumu ya Mungu, mithili ya moto na kiberiti ulioteketeza Sodoma na Gomora bila onyo. Hizi ni siku za mwisho na za hatari.

 

Maelezo ya Paulo kuhusu siku zetu zimeandikwa katika 2 Timotheo, sura ya 3 ni sahihi kabisa na yamejaa maonyo mengi kwa ajili yetu.

 

Kamwe tusikubali kushindwa na majaribu na kujifurahisha katika anasa za dhambi kwa kuwa zinatuelekeza kwenye dhambi zingine na maangamizo wakati hukumu ya Mungu itakapokuja katika dunia yote.

 

Inatupasa kutenda mambo yanayompendeza Mungu, kwa kuamini ahadi zake na kungojea kwa subira na uaminifu kama Ibrahimu. Hii inamaanisha kuwa, kama vile Ibrahimu inatupasa pia kuwa kama “wageni na wapitaji” katika dunia hii. Ni lazima tukae mbali na matendo mabaya ya dunia na kusubiri wakati utakapofika wa Ufalme wa Mungu.

 

Ibrahimu alibarikiwa sana kwa sababu alijitenga kabisa na kuwa na imani yake kwa Mungu ambapo Lutu aliteseka kwa ajili ya kupotea kwa familia yake na mali zake kwa sababu ya kujihusisha mno na maovu ya Sodoma.

 

Kristo anatuonya sisi kwamba inatupasa tumkumbuke mkewe Lutu. Angeliweza kuokoka lakini maonyo ya malaika na maombi ya mumewe hayakuweza kuingia katika moyo wake ambao ulikimbilia anasa na kufurahia mambo maovu yaliyomzunguka. Alitazama nyuma, akitamani maisha ya Sodoma, bila kuamini ukweli wa neno la Mungu. Njia za uovu za dunia hii hazitadumu milele. Maonyo ya hukumu za Mungu yatageuka hivi punde kuwa hali halisi ya kutisha. Na sasa tujifunze fundisho la haraka la kujitenga na maovu. Kristo alisema “mkumbukeni mkewe Lutu” (Luka 17:32)

 

VITABU REJEA:

"The Story Of The Bible" (H. P. Mansfield)—Pages 77-110

"Elpis Israel" (J. Thomas)—Part 2, chapters 1 and 2

"The Visible Hand Of God" (R. Roberts)—Chapter 7

"The Ways Of Providence" (R. Roberts)—Chapter 3

"Christadelphian Instructor" (R. Roberts)—Nos. 82-89

 

MASWALI YA AYA

  1. Ni jinsi gani Ibrahimu alivyouitikia wito wa Mungu na kuondoka Uru ya Ukaldayo?

  2. Fafanua namna Lutu alivyo mwacha Abramu na fundisho tunaloweza kujifunza kutokana na njia ya maisha ya Abramu?

  3. Ni kosa gani la Lutu la kuchagua Sodoma kama sehemu yake ya kuishi?

  4. Ni onyo gani Yesu alilitoa kutokana na siku za Lutu?

 

MASWALI YA INSHA

  1. Andika Insha kwa kulinganisha imani ya Ibrahimu na ujinga wa Lutu.

  2. Ni masomo gani tunaweza kujifunza kutoka kwa Lutu na familia yake kwa kujihusisha na mji wa Sodoma?

 

Swahili Title
132 TANGU KUITWA KWA ABRAMU MPAKA KUANGAMIZWA KWA SODOMA
English files
Swahili file
Literature type
Sub type
Sub sub type