135. MKE KWA AJILI YA ISAKA
Imani ya Ibrahimu katika ahadi ambazo Mungu alimpatia alikuwa amepimwa kwa njia nyingi. Isaka alizaliwa kufuatana na ahadi ya Mungu baada ya muda mrefu wa kungoja, wakati Ibrahimu na Sara wote wawili walipokuwa wazee sana. Huu ulikuwa ni mtihani juu ya imani ya Ibrahimu kwa sababu kuwa wazazi katika umri wa Ibrahimu na Sara ilikuwa haiwezekani kwa hali ya kawaida (Waebrania 11:11; Warumi 4:18-21). Mtihani mkubwa kuliko yote ulikuja wakati Ibrahimu alipoagizwa kumtoa sadaka Isaka, mwana wa ahadi, na mmoja pekee ambaye kupitia yeye ile ahadi ingeweza kutimia (Waebrania 11:17-18).
Ahadi zilikuwa zitimie kupitia kwa Ibrahimu na uzao wake. Kwa hiyo Ibrahimu alikuwa na shauku kubwa kwamba Isaka apate mke anayefaa ambaye kupitia kwake, baada ya vizazi vingi, Yesu angezaliwa akiwa uzao wake Ibrahimu.
Somo hili linaonyesha kwamba Mungu huwaongoza watumishi wake kulingana na makusudi yake, na pia kwa ajili ya umuhimu wa jambo lenyewe, machoni pa Mungu, wa ndoa katika Kweli.
IBRAHIMU ANAMWAGIZA MTUMISHI WAKE
Ibrahimu alikusudia kwamba mke wa Isaka asitoke kati ya watu wa Kanaani wasio mcha Mungu ambao walikuwa wamewazunguka pande zote. Alielewa kuwa watu hawa hawakumwabudu Mungu mmoja wa kweli aliyemwita na kumpatia ahadi hizi za thamani sana. Kumruhusu Isaka kuoa binti wa familia za nchi ile ingesababisha kupotea kwa imani ambayo aliikuza kwa uangalifu sana katika nyumba yake yote (Mwanzo 18:19). Ndoa na mwenzi asiyemwaabudu Mungu ingedhoofisha imani ile kama inavyoweza leo kudhoofishwa na ndoa kati ya aaminiye na asiyeamini.
Ibrahimu alimsisitiza mtumishi wake Eliezeri kusafiri hadi nchi alikotoka, na kule achague mke anayefaa kwa ajili ya Isaka kutoka kati ya jamaa zake. Isaka mwenyewe asingeondoka katika Nchi ya Ahadi, lakini Ibrahimu aliamini kwamba mke anayefaa kwa ajili ya Isaka angeletwa kwake (Mwanzo 24:3-4). Kwa kawaida hii ilikuwa kazi ngumu sana. Safari ndefu ilikuwa mbele. Kupata mke anayefaa na kumtia moyo kusafiri maili nyingi kuolewa na mtu ambaye hakumjua lilikuwa jambo lisilowezeka. Kwa hiyo Ibrahimu alionyesha tumaini lake kwa kusali na kumtegemea Mungu na kumruhusu yeye atawale chaguo la mke kwa ajili ya Isaka mwanaye. Ibrahimu alimhakikishia mtumishi wake Eliezeri kwamba Mungu angemfanikisha safari yake kupata mke kwa ajili ya Isaka.
NJIA MBILI ZINAKUTANA
Ibrahimu alikuwa ameifundisha nyumba yake katika kweli ya Mungu kwa hiyo mtumishi wake Eliezeri alikuwa na imani kuu katika ulinzi wa Mungu na kuwa ndiye mwenye kutomsheleza mahitaji. Alipofika Mesopotamia ambako ndipo jamaa zake Ibrahimu waliishi, imani hii na uthabiti katika sala ikaonekana. Kwa kweli, tokea mbali Mungu alikuwa ameliona hitaji la Isaka la kuoa. Mungu alikuwa amemtayarisha Rebeka tangu alipokuwa mtoto kuwa mwenzi anayefaa kwa ajili ya uzao wa ahadi, Isaka. Yeye pia alikuwa amefundishwa katika maarifa na ya kumcha BWANA. Sasa muda uliwadia wa Isaka na Rebeka wa kukutana kwa kuwa kusudi la Mungu ilikuwa lazima litimizwe: “Na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa” (Mwanzo 12:3; Gal 3:8)
MTUMISHI KATIKA MJI WA NAHORI
Yule mtumishi alimwomba Mungu kwa njia ya sala ili amwonyeshe yule mwanamke aliyemchagua Mungu. “Basi na iwe hivi, yule msichana nitakayemwambia, tua mtungi wako, nakuomba, ninywe, naye akasema,Unywe, nami nitawanyesha na ngamia zako pia, basi huyo na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka” (mstari 14). Sala hiyo ilipojibiwa, akamsifu Mungu na kutoa shukrani kwa niaba ya Ibrahimu. Zingatia kuwa hakutegemea uamuzi wake mwenyewe katika kuchagua mke kwa ajili ya Isaka, lakini alimtegemea Mungu ambaye alikuwa akiangalia yote yaliyokuwa yakitokea. Ilikuwa wazi ya kwamba Rebeka alikuwa ni chaguo la Mungu kwa jinsi alivyotimiza mahitaji yote. Alikuwa ni binti wa ndugu wa Ibrahimu (mistari 15, 24). Alikuwa bikira, hajaolewa bado (mstari 16). Huyu msichana imani yake ilikuwa kubwa. Alikuwa tayari kuacha familia ya kwao na kusafiri kwenda Nchi ya Ahadi na kuwa mke wa Isaka (mstari 58). Alikuwa mpole na mnyenyekevu na akawa mke mwema wa Isaka. Jinsi lilivyokuwa jibu la kupendeza sana la maombi ya Ibrahimu na Eliezeri!
UMUHIMU WA NDOA KATIKA KWELI
Ndoa inafanyika mbele ya Mungu, kwa hiyo uangalifu mkubwa unatakiwa ili kuhakikisha kwamba chaguo la busara linafanyika. Ni muhimu kwamba wote wawili, mume na mke wawe na imani moja. La sivyo nyumba itapata misukosuko kwa kutoelewana na pengine mambo mabaya zaidi yanaweza kutokea. Ibada ya Mungu huzuiliwa au yaweza kudharauliwa. Ndoa ya aina hiyo itakuwa batili na kweli itapungua. Kupenda starehe, kutafuta anasa za kidunia huwa ni jambo linalomvuta mtu mwenye tabia ya mwilini. Mwenzi ambaye hana hofu ya Mungu hataona kuwa ni vibaya kufuata mambo kama hayo. Kwa sababu hiyo mtume Paulo anaonya “msifungiwe nira pamoja na wasioamini” (2 Wakorintho 6:14).
Mahali penye nia moja katika Kweli pana upendo, upole na heshima kati ya wote. Jinsi gani ilivyo amri kuhusu watoto, “Watiini wazazi wenu katika Bwana” inavyotimizwa kama Mungu alivyokusudia, ikiwa mzazi mmoja anaamini Kweli na mzazi mwingine haiamini (Waefeso 6:1). Kwa hiyyo tunaweza kuona umuhimu wa maneno ya Paulo katika 2 Wakorintho 6:14 na maagizo yaliyo katika Torati (Kumbukumbu la Torati 7:3-4). Ndoa pamoja na asiye amini siyo tu kuwa si busara, bali ni kuvunja amri za Mungu (soma Wakorintho 7:39). Angalia yaliyotokea katika matukio yafuatayo kupitia ndoa za mchanganyiko na (Mwanzo 6:2; 1 Wafalme 11:1-8; Nehemia. 13:23-31).
Tutakapokuwa wakubwa na kuwa tayari kwa ajili kubatizwa na baadaye kuwa tayari kwa ndoa, tunatakiwa pia tuchague mwenzi ambaye ni mwenye hofu ya Mungu. Ni kwa njia hii tu peke yake ndoa inaweza kuwa ya furaha na watoto kulelewa katika “hofu ya Mungu na kwa maadili ya Bwana”.
Rebeka alikuwa amelelewa katika maadili na mafundisho ya YAHWEH. Kwa hiyo alifaa kuwa mwenzi wa mzao wa ahadi. Wakati ulipofika ulithibitisha kuwa yeye ndiye aliyefaa, na Rebeka akawa chanzo cha faraja kwa Isaka (Mwanzo 24:67) na nguvu za kiroho katika kuenenda kwa wote pamoja katika imani.
Ibrahimu alitambua hitaji la Isaka la kupata mke anayefaa ili kwamba ahadi ya Mungu itimie. Aliamini kwa uthabiti kwamba Mungu angemletea Isaka mke anayefaa. Ili kumsaidia Isaka kuoa katika Kweli, Ibrahimu ilimbidi kumpeleka mtumishi wake kwa ndugu wa Ibrahimu, ambao pia walimheshimu Mungu. Mungu mwenyewe alikuwa ameyalinda maisha ya Rebeka na kumtayarisha kwa ajili ya Isaka.
VITABU REJEA:
"The Story Of The Bible" (H. P. Mansfield)—Pp. 130-138
"The Ways Of Providence" (R. Roberts)—Pp. 29-33
"Christadelphian Instructor"—Questions and Answers Nos. 132-137
MASWALI YA AYA
-
Kwa nini Ibrahimu alikuwa mwangalifu sana katika kumwagiza Eliezeri ili kwenda kupata mke wa Isaka?
-
Ni kwa jinsi gani Eliezeri alimpata mke wa Isaka?
-
Ni sifa gani alizokuwa nazo Rebeka kumwezesha kuwa mke anayefaa wa Isaka?
-
Kuna umuhimu kiasi gani kwa ndugu wanaume na wanawake kuoana na wale walio ndani ya imani moja?
MASWALI YA INSHA
-
Ni kwa vipi Mungu aliongoza chaguo la mke wa Isaka?
-
Kwa nini Mungu anaamrisha waumini kuoa /kuolewa “katika Bwana tu?”