140. MUNGU AMLETA MKOMBOZI KWA AJILI YA ISRAELI
Yakobo, alikuwa na furaha kuu kumpata Yusufu akiwa hai, alikaa na familia yake katika Nchi ya Gosheni. Wamisri waliendelea kuteseka kwa ajili ya njaa kwa sababu walilazimishwa kumwuzia Yusufu mashamba yao, ili waweze kununua chakula. Baada ya kifo cha Yakobo na Yusufu familia ya Israeli ilifanyiwa ukatili mkubwa na Wamisri.
Katikati ya mateso yao makubwa na kuvunjika moyo, nafasi ilikuwa inaandaliwa kwa ajili ya Musa, mkombozi wao.
KUTOKA 2
UTANGULIZI
Muda mfupi kabla ya Isaka kuzaliwa, Mungu alikuwa amempatia Ibrahimu unabii kuhusu Israeli kuishi katika nchi ya kigeni na kutumikishwa kwa mateso. (Mwanzo 15:13, 14). Hata hivyo Mungu alikuwa amepanga muda, ambao angewatoa katika nchi ile. Hawangekuwa familia tu ya watu sabini walioingia Misri, bali watakuwa taifa ambalo Mungu angelitamka mwenyewe na kumtukuza kati ya wanadamu wote (Mwanzo 46:3)
YAKOBO ANAWABARIKI WANA WA YUSUFU (Mwanzo 48)
Wakati ulipokaribia wa Yakobo kufariki (Mwanzo 47:29) Yusufu aliwaleta kwake wanawe wawili Manase na Efraimu ili wabarikiwe. Yakobo alifanya chaguo la kushangaza kwa kumbariki Efraimu kuliko Manase kwa kuwa Manase ndiye aliyekuwa mkubwa (mstari 14). Yakobo alikuwa anaongozwa na Mungu katika jambo hili na kwa mara nyingine tena alionyesha jinsi Mungu anavyowachagua watu kwa ajili ya mapenzi yake mwenyewe, ili katika jambo hili “mkubwa” atamtumikia mdogo.
Baraka ya Yakobo (mstari 15,16,19,20) ilikuwa ombi la dhati sana kwa Mungu ambaye alikuwa amemhifadhi kwa uaminifu kutokana na uovu. Wakati tunapotafakari maneno haya kuhusu matukio ya kutisha katika maisha ya Yakobo, imani yake kwa Mungu inathibitika.
VIFO VYA YAKOBO NA YUSUFU (Mwa. 49; 50:22-26)
Yakobo alikuwa amekaa Misri kwa muda wa miaka kumi na saba (Mwanzo. 47:27,28) wakati muda ulipofika ili akusanywe pamoja na babaze kwa kufariki. Kabla Yakobo hajafariki, aliwabariki wanawe, akiwafunulia mambo ambayo yangeotokea katika “siku za mwisho” (Mwanzo 49).
Yakobo alikufa huko Misri ingawa Mungu alikuwa amemwahidi nchi ya Kanaani kuwa urithi wake wa milele. Sawasawa na ahadi walizoahidiwa Ibrahimu na Isaka, ahadi hii ya Mungu bado haijatimizwa. Mungu alimwambia Yakobo asiogope kwenda Misri kwa kuwa Mungu “angemrudisha tena” (Mwanzo 46:4). Ingawa ahadi hili ilihusiana hasa na ukombozi wa taifa la Israeli, ilikuwa pia ikimhusu Yakobo binafsi.
Ombi lake Yakobo asizikwe Misri, bali arudishwe Kanaani (Mwanzo 47:29-30). Alikuwa ameishi katika imani ya kuirithi nchi ile ya ahadi wakati Mungu atakapoanzisha Ufalme na ufufuo wa uzao mwaniminifu wa Ibrahimu. Hata alipokuwa amekaribia kufa nchi ile ilikuwa katika akili yake. Ni wazi tumaini lake lilikuwa katika ukombozi kutoka Misri na katika ufufuo kuelekea urithi wa milele katika nchi ambayo aliahidiwa yeye. Kama waraka kwa Waebrania unavyosema, naye pia “alikufa katika imani, asijazipokea zile ahadi, lakini aliziona tokea mbali” (Waebrania 11:13).
Wakati Yusufu alipokufa. Maneno yake ya mwisho kwa ndugu zake yalionyesha imani katika maagano waliyopewa Ibrahimu, Isaka na Yakobo (Mwanzo 50:24; Waebrania. 11:22). Aliwakumbusha watu wake kuwa Mungu hatawacha waendelee kukaa katika nchi ya Misri lakini bila shaka atawajilia ili kuwarudisha katika Nchi ya Ahadi.
Yusufu aliomba waichukue mifupa yake wakati watakapokuwa wanatoka ili waizike katika nchi ambayo aliahidiwa baba yao Ibrahimu. Mifupa hii ilifanyika kama kitu cha kudumu kwa kuwakumbusha maneno ya Yusufu, “Mungu atawajilia ninyi bila shaka, atawapandisha kutoka nchi hii” (Mwanzo 50:24,25). Kwa maana, wao waliwakilisha imani iliyo hai ya mtu aliyekufa!
UTUMWA WA ISRAELI (Mwanzo 1:8-14)
Kadiri miaka ilivyopita, wazao wa Yakobo waliongezeka na kufanyika watu wenye nguvu (Kutoka 1:7). Ndipo jambo la kutisha likafika. “Akainuka mfalme kutawala Misri asiyemjua Yusufu” (mstari 8). Hakujali mambo mema ambayo Yusufu alikuwa ameitendea nchi ya Misri. Akiogopa idadi kubwa ya Waebrania na kuhofia hatari ya Misri kama wataungana na maadui wa Misri, aliwatesa na akawafanya watumwa (mstari 10). Maana utumwa haukuwazuia kuongezeka idadi yao. Wamisri wakaamua “kuwatumikisha kwa ukali na wakayafanya maisha yao kuwa uchungu kwa kazi ngumu ya utumwa”. Hatua za ukatili sana na ukatili kupita kiasi uliongezeka, hadi Farao akaangiza kwamba kila mtoto mwanamume anapozaliwa auawe (mstari 22). Na sasa tunaweza tu kutafakari mshituko na hatari iliyokuwepo katika maisha ya familia ya Waebrania.
Kukawa na uchungu mkubwa wa moyo katika nchi ya Gosheni ambako Waisraeli waliishi. Wakiwa katika mateso ya utumwa, watoto wao walipokuwa wanauawa, wana wa Israeli waliishi katika hatari ya kifo bila msaada uonekanao au tumaini. Lakini Mungu alikuwa akifahamu vizuri mateso yao na alikuwa akiwaandalia mkombozi kama alivyoahidi.
Ilikuwa ni wakati wa mateso haya ambapo Musa alizaliwa.
KUZALIWA KWA MUSA (Mwa. 2:1-10)
Musa alikuwa mtoto wa tatu wa Amramu na Yokebedi wa kabila la Lawi (Kutoka 6:20). Haruni alikuwa kaka yake Musa na Miriamu alikuwa ndiye dada yake.
Musa alizaliwa katika kipindi cha giza kuu kwa Israeli. Ilihitajika imani ya nguvu kwa upande wa wazazi wake kudharau amri ya Farao (Waebrania 11:23). Wazazi wake walitambua kwamba alikuwa “mtoto mzuri” na kwamba alikuwa “ mwenye haki wa Mungu” (Matendo ya Mitume 7:20 angalia pembezoni).
Paulo katika waraka kwa Warumi 10:17 anasema “imani huja kwa kusikia neno la Mungu”. Kwa hiyo, wakati Waebrania sura ya 11 inawaelezea wazazi wa Musa kutenda kwa imani tunaweza kuwa na uhakika kabisa kuwa Amramu na Yokebedi walikuwa wamepewa ujumbe maalumu uliomhusu Musa, ukiwaelezea ya kwamba angewaokoa Israeli kutokana na utumwa wa Misri. Kwa hiyo walichukua hatua ya uangalifu sana kumweka salama.
Ilipofikia hali ya kutoweza tena kumficha huyo mvulana, kwa makusudi aliwekwa ndani ya safina ya matete. Akaelea mahali pale pale sehemu iliyokuwa rahisi kuonekana ambapo binti Farao alikuwa akioga. Siyo kwamba walikuwa wamemkataa Musa, bali walimweka makusudi katika sehemu ile. Wakamwandaa Miriamu atakavyomwambia Binti mfalme. Kwa imani walimruhusu Mungu kutenda kusudi lake juu ya Musa.
Binti Farao alipofika na kuiona ile Safina alitoa amri mmoja wao amletee ile safina. Alipoifungua ile safina mtoto alilia. Hisia zake akiwa mama ziliamshwa, akaamua kumchukuwa mtoto awe wake. Kwa kichocheo kutoka kwa Miriamu, Musa alipelekwa kwa mama yake mwenyewe ambaye alimlea hadi alipokuwa mkubwa. Ni jibu la kushangaza kiasi gani kwa matumaini na matarajio yaliyoonyeshwa na wazazi wa Musa. Imani yao iliimarishwa kwa njia ya ajabu kwa kuwa kutokana na hiyo Musa akapewa na mama yake elimu kubwa katika ahadi ambazo walipewa mababa!
Binti Farao alimwita jina Musa kwani alikuwa “amemtoa kutoka majini”. Farao alikuwa amejaribu kuangamiza nguvu ya wana wa Israeli kwa kuwatosa watoto wao wa kiume mtoni. Binti yake mwenyewe alimwopoa mmoja kutoka mtoni aliyefanyika njia ya mkono wa Mungu ya kumwangamiza Farao na kuwakomboa watu wa Mungu. Ni kinyume cha ajabu iliyoje kwa mipango miovu ya Farao.
Musa alifundishwa “hekima yote ya Wamisri” na akawa na cheo cha juu sana katika utawala wa Farao.Akawa “hodari wa maneno na matendo” (Matendo ya Mitume 7:22). Hata hivyo Musa kamwe hakusahau maagizo ya kiroho aliyopewa na mamaye wakati alipokuwa mdogo. Alifahamu kuwa alikuwa Mwebrania na kungojea wakati na fursa ya kuwakomboa watu wake wawe huru. Alielewa kuwa lilikuwa kusudi la Mungu ili kwa mikono yake mwenyewe Israeli waweze kukombolewa (Matendo ya Mitume 7:25)
Wakati Musa alipokuwa mkubwa katika ufalme (Ikulu) alikabiliwa na chaguo gumu sana. Angeweza kutumia cheo chake kufurahia raha na anasa za baraza la Farao, au yeye mwenyewe ajikane ili kuacha tamaa za mwili, na kujitayarisha kwa kazi ya kuwaongoza watu wake watoke Misri kwenda katika nchi ya ahadi. Alichagua kujikana mwenyewe kwa sababu aliamini kwamba Mungu angetimiza ahadi yake. Alifahamu kwamba njia ya Mungu ilikuwa bora zaidi kuliko maisha mazuri ya Misri (Waebrania 11:24-26)
Musa anafanyika mfano wa maana sana kwetu, kwani tunaishi katikati ya anasa na wingi wa vitu vizuri. Inatakiwa tukatae kabisa katika kutafuta mali za ulimwengu huu na badala yake tutumie muda wetu na nguvu zetu katika kazi ya Mungu.
Tunaweza kupata thawabu kubwa sana ya kuingia kwenye Ufalme tukiwa na ujasiri wa kusimama sasa kwa ajili ya njia ya Mungu (Mathayo 6:19-21; 2 Wakorintho 4:17-18)
KUKIMBIA KUTOKA MISRI (Kut. 2:11-22)
Akiwa na umri wa miaka arobaini Musa alikusudia kuwaondoa Israeli kutoka Misri (Matendo ya Mitume 7:23-25). Lakini Waisraeli walikuwa wameshakata tamaa na hawakuwa tayari kwa ajili ya kuja kwa mwokozi. Kwa kweli wengi wao walikuwa wamefurahiaa kukumbatia ibada ya sanamu ya Misri na kumwacha BWANA.
Musa aliwaonea huruma ndugu zake. Walikuwa watumwa tu katika hali iliyoelekea kuwa yenye kukatisha tamaa. Akawatembelea ndugu zake, naye alipomwona Mmisri anampiga Mwebrania, akaingilia ugomvi huo. Akamwua yule Mmisri na kumficha mchangani. Siku iliyofuata alipojaribu kuwapatanisha Waebrania wawili waliokuwa wakigombana ikawa wazi ya kwamba siri ile ilikuwa imejulikana (Kutoka 2:11-14). Musa alifahamu kwamba Farao atafahamu kuhusu tendo hilo na angetafuta kumwua. Kwa hiyo Musa akakimbia kutoka Misri na kupata hifadhi huko Midiani karibu na mlima Sinai (Kutoka 2:15-22).
Wamidiani walikuwa wazawa wa Ibrahimu wa familia ya mke wa Ibrahimu, Ketura (Mwanzo 25:2). Kwenye kisiwa, Musa alikutana na mabinti saba wa Yethro, kuhani wa Midiani. Alikaribishwa kwa ukarimu nyumbani mwake, akamwoa Sipora, mmojawapo wa mabinti wa Yethro na akachunga kondoo wake miaka arobaini (Matendo ya Mitume 7:29,30). Katika ukimya wa mazingira ya Sinai, mbali na utukufu wa Misri, Musa alichunga kondoo wapole wasio na madhara, na kujifunza kujishusha na kuwatunza kondoo waliokuwa dhaifu. Hii ni tabia mhimu sana ya kiongozi wa kweli, na hasa wa watu wa Mungu. Kujiamini kuliondolewa na badala yake ikawa ni kumtegemea Mungu. Aliporudi Misri tabia yake ilikuwa imekua. Sasa alikuwa mchungaji ambaye Mungu angemtumia kuwaongoza “kondoo” zake kutoka Misri (Zab. 78:52; 77:20)
MATUKIO YA MUSA YANAYOFANA NA MATUKIO YA YESU –KATIKA SOMO HILI
|
Na. |
MUSA |
No. |
YESU |
|
1 |
Farao aliua watoto wa kiume |
1 |
Herode aliua watoto wote wa Bethlehemu |
|
2 |
Musa aliokoka kutoka kifo. |
2 |
Yusufu na Mariamu walionywa na wakakimbilia Misri. |
|
3 |
Mkombozi, mtoa sheria, mpatanishi |
3 |
Mkombozi, mtoa sheria, mpatanishi. |
|
4 |
Kuja kwake mara ya kwanza alikataliwa – “Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu na mwamzi juu yetu?” |
4 |
Kuja kwake mara ya kwanza alikataliwa- “tuambie unatenda mambo haya kwa mamlaka gani tena ni nani aliyekupa mamlaka hii?” |
|
5 |
Musa alikimbilia nchi ya mbali. |
5 |
Yesu alipaa kwenda mbinguni. Rejea mfano katika Luka 19:10-15. |
|
6 |
Musa alirudi kuwakomboa. |
6 |
Yesu atarudi ataleta ukombozi mkuu kwa watu wale wanaomtazamia. |
MUHTASARI
-
Yakobo na Yusufu walionyesha imani katika ahadi za Mungu katika maagizo waliyosema wakati wa kufa kwao.
-
Utumwa na mauaji ya watoto wao wachanga yaliwafanya Israeli kumlilia Mungu, aliyesikia na kuwaandalia mkombozi.
-
Musa alitunzwa kwa nguvu za Mungu na kuelimishwa kwa ajili ya kazi yake kubwa. Aliikataa Misri na anasa zake na akachagua maisha ya mateso pamoja na watu wa Mungu.
-
Akiwa mchungaji alijifunza masomo yaliyomwezesha afanikiwe, chini ya Mungu, kuwaongoza watu wake-unyenyekevu, uvumilivu, upole.
-
Alikuwa nabii kama Masihi anavyotakiwa kuwa.
VITABU REJEA:
"The Story Of The Bible" (H. P. Mansfield)—Pp. 208-237
"Ways Of Providence" (R. Roberts)—Chapter 9
"The Visible Hand Of God" (R. Roberts)—Chapter 9
"Elpis Israel" (J. Thomas)—Part 2, chap. 4, pp. 286-289
"Moses my Servant" (H. Tennant)—Chapt 1
MASWALI YA VIFUNGU
-
Wakati Yakobo alipofikia mwisho wa maisha yake ni jinsi gani alionyesha imani yake?
-
Ni agizo gani Yusufu aliwapatia kuhusiana na mifupa yake na kwa nini?
-
Ni kwa nini wazazi wa Musa walimficha?
-
Eleza elimu ya Musa tangu alipokuwa mtoto hadi alipokuwa na umri wa miaka 40.
MASWALI YA INSHA
-
Elezea matukio yaliyowapata wana wa Israeli baada ya kifo cha Yusufu na hadi Musa kukimbilia nchi nyingine.
-
Musa alikuwa wa namna gani alipokuwa kijana kule Misri na alipokuwa mchunga kondoo huko Midiani aliandaliwaje kwa ajili ya kazi ya ukombozi wa wana wa Israeli?
-
Kwa upande wa Musa imesemwa kwamba, “akaona ni afadhari kupata mateso pamoja na watu wa Mungu, kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo tu” (Waebrania. 11:25). Hili linatuhusuje sisi leo?