CSSA — Somo 083: Yesu Huko Kapernaumu

Swahili

SOMO 083 • YESU HUKO KAPERNAUMU

“Na habari zake zikaenea kila mahali katika nchi iliyozunguka.” — Luka 4:37

Luka 4:31–44; Marko 1:21–39

SHABAHA

Kuonyesha jinsi Yesu alivyofundisha kwa mamlaka na kuwaponya wagonjwa huko Kapernaumu kwa nguvu aliyopokea kutoka kwa Mungu. Habari zake zikaenea sana, lakini Yesu hakuruhusu umaarufu umzuie kufanya kazi kuu aliyotumwa kufanya: kuhubiri Habari Njema ya Ufalme wa Mungu.

YESU ANAFUNDISHA KWA MAMLAKA — Marko 1:21–28; Luka 4:31–37

Siku ya Sabato watu walikusanyika katika sinagogi kusikia Maandiko. Yesu akafundisha, nao wakashangaa kwa sababu neno lake lilikuwa na mamlaka. Hakuwa akifundisha kama mtu anayekisia. Alijua Neno la Baba yake, alilitii na alieleza mapenzi ya Mungu kwa uwazi.

Ghafla mtu aliyekuwa na “pepo mchafu” akapaza sauti. Maandiko yanatumia lugha hii kueleza hali yake. Hatupaswi kuigeuza kuwa mafundisho kwamba kulikuwa na malaika waovu waliomwasi Mungu na kumwingia mtu. Yesu alimwamuru anyamaze na kutoka, na yule mtu akapona. Watu walistaajabu kwa sababu kwa neno la Yesu hali hiyo ilikoma. Hii ilikuwa ishara ya nguvu ya Mungu iliyotenda kupitia Mwana wake.

Yesu ndiye “Mtakatifu wa Mungu” (Marko 1:24), aliyewekwa wakfu na Baba yake. Miujiza yake ilithibitisha ujumbe wake na kuonyesha huruma ya Mungu kwa wenye mateso.

YESU AMPONYA MAMA MKWE WA PETRO — Marko 1:29–31

Baada ya kutoka sinagogini, Yesu alienda pamoja na Yakobo na Yohana nyumbani kwa Simoni na Andrea. Mama mkwe wa Simoni alikuwa amelala ana homa, nao wakamwambia Yesu juu yake. Yesu akamkaribia, akamshika mkono na kumwinua; homa ikamwacha. Luka pia anaeleza kwamba Yesu “akaikemea ile homa” (Luka 4:39). Mara moja akawa na nguvu za kuwahudumia waliokuwa nyumbani.

Uponyaji huo ulikuwa kamili. Yesu hakutafuta sifa kwa ajili yake mwenyewe; alitumia nguvu alizopewa kuwasaidia wengine na kumtukuza Mungu.

KUPONYA WAGONJWA JIONI — Luka 4:40–41

Jua lilipotua na Sabato kumalizika, watu walileta wagonjwa wa magonjwa mbalimbali. Yesu akaweka mikono juu ya kila mmoja wao na kuwaponya. Mathayo anaunganisha uponyaji huu na Isaya 53:4: “Mwenyewe alitwaa udhaifu wetu, na kuyachukua magonjwa yetu” (Mathayo 8:17, kwa maana ya KJV).

Miujiza hii haikuwa maonyesho. Ilikuwa sehemu ya ushuhuda kwamba Yesu ndiye Masihi aliyeahidiwa na kwamba Mungu alikuwa akifanya kazi kupitia yeye. Huruma ya Yesu kwa watu walioteseka inaonyesha tabia tunayopaswa kuiga.

YESU ANAONDOKA KAPERNAUMU — Marko 1:35–39; Luka 4:42–44

Asubuhi sana, kabla ya mapambazuko, Yesu alitoka kwenda mahali pa faragha na kuomba. Ingawa alikuwa Mwana wa Mungu, Yesu alikuwa mwanadamu wa kweli. Alichoka, alihitaji kupumzika, na alihitaji kumtegemea Baba yake katika sala. Hakuwahi kutenda dhambi, lakini maisha yake ya utiifu yalikuwa maisha ya kumtegemea Mungu.

Wanafunzi walipompata walimwambia kwamba watu wote walikuwa wakimtafuta. Lakini Yesu akasema, “Imenipasa kuihubiri habari njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia; maana kwa sababu hiyo nalitumwa” (Luka 4:43). Alikataa kufungwa na umaarufu wa sehemu moja. Kazi yake kuu ilikuwa kuhubiri Ufalme wa Mungu.

FUNDISHO KWETU

Yesu alionyesha upendo kwa Mungu kwa moyo wake wote, akili yake yote na nguvu zake zote. Alitumia muda wake kuwafundisha watu, kuwasaidia wenye shida na kusali kwa Baba yake. Nasi hatuna uwezo wa kufanya miujiza kama yeye, lakini tunaweza kuwa wenye huruma, wenye kujali na tayari kuwasaidia wengine.

Tunajifunza pia kwamba sala na Neno la Mungu ni muhimu hata tunapokuwa na shughuli nyingi. Yesu hakuruhusu mahitaji ya watu yamfanye asahau kumtafuta Baba yake. Wala umaarufu haukubadili kusudi lake.

MAELEZO YA NYONGEZA

Yesu mara nyingi aliponya siku ya Sabato, jambo lililosababisha mabishano na baadhi ya viongozi wa dini. Amri ya nne iliwataka Waisraeli kuacha kazi zao siku ya saba na kuikumbuka Sabato kwa Bwana (Kutoka 20:8–11). Yesu hakuwa akivunja mapenzi ya Mungu kwa kutenda mema. Alifundisha kwamba “ni halali kutenda mema siku ya Sabato” (Mathayo 12:12).

Sabato haikukusudiwa kuwazuia watu kuonyesha rehema. Yesu aliweka wazi kwamba utiifu kwa Mungu hauwezi kutenganishwa na huruma kwa watu.

MASWALI

Majibu Mafupi

1. Kwa nini watu walikusanyika katika sinagogi siku ya Sabato?

2. Mafundisho ya Yesu yalitofautianaje na yale ya waandishi?

3. Nini kilitokea ghafla Yesu alipokuwa akifundisha?

4. Yesu alimwambia nini yule mtu mwenye pepo mchafu?

5. Yesu na wanafunzi wake walikwenda wapi baada ya sinagogi?

6. Yesu alimsaidiaje mama mkwe wa Petro?

7. Nini kilitokea jua lilipotua?

8. Yesu alifanya nini mapema asubuhi iliyofuata?

9. Kwa nini Yesu hakubaki Kapernaumu?

Majibu ya Kina

10. (a) Watu wa Kapernaumu walifikiriaje mafundisho ya Yesu? (b) Eleza kilichotokea katika sinagogi.

11. (a) Yesu aliwasaidia watu gani siku hiyo? (b) Mfano wake unatufundisha nini kuhusu kumpenda Mungu na kuwajali wengine?

Majibu ya Nyongeza

12. (a) Sheria ya Musa ilisema nini kuhusu Sabato? (b) Je, Yesu alivunja mapenzi ya Mungu kwa kuponya siku ya Sabato? (c) Kwa nini?

Swahili Title
083 YESU HUKO KAPERNAUMU
African text
CSSA
Translator 1
Veslin
Literature type
Sub type
Sub sub type