151. KWA NINI ISRAEL ILISHINDWA
“Miriamu na Haruni wakanena kinyume na Musa”
Wana wa Israeli walikaa Sinai kwa muda wa miezi kumi na miwili mpaka mwezi wa kumi na nne, tangu walipotoka Misri. Walikuwa wamepokea zile amri kumi za Mungu na sheria nyingine nyingi ambazo zilidhibiti maisha yao ya kila siku na walifundishwa masomo muhimu juu yamtazamo wao kuhusu Mungu na jinsi Mungu alivyowatazama. Huko, walipokea maagizo kwa ajili ya maskani na ukuhani; maagizo ambayo ni muhimu sana kwao wakiwa wateule wa Mungu. Pia, katika Sinai, watu walikubali kutii sheria za Mungu na kutii agano walilopewa na Mungu, akiwafanya kuwa “ufalme wa makuhani na taifa takatifu". Hata hivyo, bado wana wa Israeli walishindwa mara kadhaakufanya mambo ambayo Mungu aliwaagiza. Tunapaswa kuwa tayari kujifunza kutokana na makosa yao ili tuepuke kufanya makosa yaleyale.
Hesabu 10, 11 na 12
KUWEKA PASAKA
Ilipokaribia siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili, Mungu aliwaamuru watu waishike Pasaka. Kwa wakati huu ilikuwa Pasaka ya ukumbusho. Watu hao wangewaeleza watoto wao wadogoa matukio ya usiku wa ajabu mwaka mmoja tu uliopita walipokuwa wakijiandaa kuondoka Misri. Hata katika nyakati zetu, Waisraeli husherehekea sikukuu ya Pasaka kama ukumbusho wa kukombolewa kwao kutoka utumwani katika nchi ya Misri karne nyingi zilizopita.
KUONDOKA KUTOKA SINAI (Hesabu 10:11-36).
Wakati Mungu alipoamua kwamba ulikuwa ni wakati wa Israeli kuondoka kutoka Sinai, wingu juu ya hema liliondoka huku likielekea kwenye njia waliyopaswa kupita. Tarumbeta ilipopigwa, na watu wakiwa wanaendelea kukusanyika, Maskani iligawanywa, na samani zake zikafunikwa na kubebwa kwa namnawaliyoamua wana wa Lawi. Watu wakashusha hema zao, wakakusanya vitu vyao vichache vya safari, wakalichukua jeneza lenye mifupa ya Yusufu. Kisha kwa wingu la utukufu, ishara ya uwepo wa Mungu juu yao (Hesabu 10:12), taifa lilitembea katika makundi manne chini ya uongozi wa Yuda, Rubeni, Efraimu na Dani (Hesabu 10:14-28). Mbele ya kila kundikulikuwa na bendera ya kabila kuu, Yuda - simba; Rubeni - mtu; Efraimu - ng'ombe, na Dani - tai. Safari ya kila siku ilianza na kumalizika kwa maombi (Hesabu 10:35-36).
Wakati wa kuondoka, ni siku kumi na moja tu zilizowatenga wana wa Israeli na nchi ya ahadi (Kumb. 1:2). Hata kuwapa mudazaidi watoto wadogo, wazee na wagonjwa kusafiri, nchi ya Kanani haikuwa mbali. Kilichohitajiwa tu ili waingie bila shida ni kuvumilia kwa subira, kutumainia uwezo wa Mungu kuwaongoza kwenye nchi ya ahadi..
SABABU ZA KUSHINDWA (Hesabu 11).
Lakini sifa hizi zilikosekana miongoni mwa Waisraeli. Ni kweli kwamba walipaswa kupita katika jangwa kavu na kame kati ya Sinai na Kadeshi. Uchovu na hali mbaya ya mazingira ya jangwa ingewasonga sana; lakini uwepo wa Mungu na maono matukufu ya nchi iliyojaa baraka za riziki tele zinazowangoja ziliondoa matatizo hayo.. Lakini ndani ya siku 3 tu manung'uniko yalizuka miongoni mwa watu (Hesabu 11:1) na ingawa hii iliadhibiwa kwa moto kutoka kwa Mungu ambao uliwateketeza wale waliokuwa kwenye ukingo wa kambi, malalamiko mapya yakaibuka.. Kulikuwa na watu wa mataifa mengine kati ya Waisraeli (Hesabu 11:2) ambao walikuwa wamejiunga na watu wa Mungu. Walianza kulinganisha starehe walizoacha huko Misri na hali ngumu ya jangwani. Malalamiko haya yaliathiri na wengine, mpaka kambi nzima ikaingia katika hali ya kutoridhika, na kwa sababu hiyo Musa alihuzunika.
Mwitikio wa kawaida wa wanadamu kwa magumu kama yaliyowakumba Waizraeli,, ni kufanya matatizo ya sasa yaonekane kuwa mabaya zaidi na kutia chumvi furaha ya wakati uliopita. Watu kwa upumbavu wao wakaanza kufikirikwamba utumwa wao huko Misri ulikuwa bora kuliko maisha katika jangwa la Sinai. Walikumbuka samaki, matango, matikitimaji, vitunguu majina vitunguu saumu ambavyo vilitofautiana sana na chakula cha kawaida cha mana walichopokea sasa; walisahau saa nyingi za utumwa, uchungu wa mapigo waliyopata na mauaji ya watoto wao chini ya wasimamizi wa kazi wa Misri.. Walisahau pia kwamba, utajiri wa nchi ya ahadi waliyokuwa wakiiendea ulikuwa mkubwa zaidi kuliko furaha iliyofikiriwa ya Misri (Kumb. 8:7-10).
Kila mtu anayekubali wito wa Kristo kuurithi Ufalme wa Mungu atakuwa chini ya shinikizo wakati mmoja au mwingine kufuata mtindo wa Israeli wa kushindwa.. Ni rahisi kuruhusu matatizo ya sasa kuficha maono yetu ya ufalme ujao. Mashaka yanaweza kuingia akilini mwetu badala ya imani inayohitajika kwa ajili ya “kudumu kwa saburi katika kutenda mema.” Paulo aliwahimiza Warumi kwa maneno haya ambayo yanawahusu wale wote ambao wangeingia katika safari kupitia maisha haya ya sasa ya Ufalme — “Kwa maana ninayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu.” (Warumi 8:18).
MUNGU ANATUMA KWARE (Hesabu 11:33-35).
Musa alikasirika na kufadhaika, na Mungu akawakasirikia watu kwa sababu ya kulalamika kwao. Hata hivyo, Mungu alionyesha uwezo wake wa kuwaandalia mahitaji yao kwa kutuma kware wengi sana ambao walikuja kutua chini katika kambi ya Israeli. Watu kwa pupa walikusanyika zaidi ya walivyohitaji. Walikuwa wamepuuza dhabihu ya kuteketezwa ya kila siku, nyakati za maombi na maombi binafsi, lakini ilipokuja suala la kutosheleza tamaa yao ya chakula, wangeweza kukesha usiku kucha. Tunahitaji kuchunguza ni wapi yalipo masilahi yetu halisi - kwa “chakula” cha kiroho au anasa za muda za kimaisha. Hitaji letu la kweli ni mwongozo wa kila siku wa neno la Mungu ambalo litatuongoza kwenye uzima wa milele. Anasa za ulimwengu si za kudumu. Matokeo ya mwisho ya kutafuta anasa hizo ni kuangamia bila matumaini. Hekima ingetufundisha kufuata mafundisho ya Kristo: “Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa.” (Mt. 5:6 Linganisha. Zab. 119:20).
Hakukuwa na wazo la kumshukuru Mungu kwa ajili ya riziki yake na walipokuwa bado wakila, Mungu alionyesha hasira yake kwa kutuma tauni kati yao, na watu wengi wakafa. Kwa sababu hiyo, mahali pale pakaitwa Kibroth-Hataava, maana yake, “makaburi ya wenye pupa”. (Hes. 11:33-35; Zab. 78:29-31).
MALALAMIKO YA MIRIAM NA Haruni (Hesabu 12).
Jaribujingine lilimngoja Musa. Miriamu na Haruni, dada yake na kaka yake, walimkosoa sana. Tuhumazao zilitokana na wivu. Walitaka sehemu kubwa zaidi ya mamlaka na wajibu ambao alikuwa amepewa Musa.
Tunakumbuka mtazamo wa Musa alipoagizwa awaongoze watu wa Mungu kutoka Misri. Hakujiona kuwa na uwezo. Kujiamini kwake kwa miaka arobaini iliyopita kulikuwa hakuna kitu. Mamlaka ya Mungu, basi, yaliwekwa juu ya mabega ya mtu huyu mnyenyekevu. Soma Hesabu 12:3, "Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa dunia." Ni wazi kwamba, malalamiko ya Miriamu na Haruni yalikuwa ya uongo. Zaidi ya hayo, Mungu asingesema na mtu yeyote mdomo kwa mdomo ila na Musa mtumishi wake (Hesabu 12:6-8). Ni wazi kwamba Musa alipewa mamlaka kwa kuteuliwa na Mungu na alistahili.
Miriamu aliadhibiwa kwa dhambi yake. Wingu la kuwapo kwa Mungu lilipoinuka kutoka kwa wale watatu waliokuwa wamekutana kwenye hema la kukutania, Musa na Haruni walishtuka kuona kwamba Miriamu alikuwa “mweupe kama theluji” (Hesabu 12:10). Haruni alimsihi Musa kwa niaba yake na kukiri dhambi yake mbele yake akiomba msamaha. Musa aliomba kwa Mungu kwa niaba yao na Miriamu akatakaswa na ugonjwa huo baada ya kukaa siku saba nje ya kambi. Kama mtu aliyetengwa na mwenye ukoma alikuwa ishara na onyo la matokeo mabaya yote ya husuda na wivu.
FUNZOKWETU:
Tunapoutafuta Ufalme wa Mungu tunapaswa kusahau anasa za dunia na kuziacha nyuma yetu. Badala ya kulalamika, tunapaswa kushukuru Mungu kila wakati kwa baraka zake.
Wivu wa tabia, uwezo au cheo cha wengine ni tabia inayotokana na kiburi na ubinafsi. Ni moja wapo ya dhambi ambayo ni ya hila zaidi kuliko nyingine nyingi kwa sababu inaweza isionekane kwa nje. Tunapaswa kuchunguza mawazo yetu na msingi wa matendo yetu kwa uangalifu, ili kuondoa mambo kama hayo katika akili zetu kabla ya wakati wa kiti cha hukumu cha Kristo wakati mambo haya yote yatafunuliwa. Tunapaswa kufikiria kwa uangalifu sana juu ya uwepo wa Mungu na kuona yote na kujua yote na katika kushughulika kwetu sisi kwa sisi kuona maneno ya Paulo kama yapatikanayo katika Wafilipi 2:2-5, 19-21; 4:8
MAKTABA YA MAREJEO:
· "Wapi Ilipotokea" (Islip Collyer) Sura 6
· "Musa Mtumishi Wangu" (H. Tennant) Kurasa. 105-114
· "Hadithi ya Biblia" (H. P. Mansfield) Toleo. 2 Kurusa. 62-71
MASWALI YA AYA:
1. Kwa nini sikukuu ya Pasaka iliadhimishwa kila mwaka?
2. Eleza jinsi Israeli walivyopangwa walipokuwa wakiondoka Sinai.
3. Mana ilikuwa ni nini na wana wa Israeli waliitikiaje?
4. Eleza kisa kinachohusu kware huko Kibroth Hataavah. Je, tunaweza kujifunza nini kutokana na tukio hili?
MASWALI YA INSHA:
1. Wakati Israeli walipoondoka Sinai, haikuchukua muda mrefu kabla ya kumtenda Mungu dhambi. Fafanua
a. Jinsi walivyoshindwa na eleza mchango wawatu wa mataifa mengine ("mkutano mchanganyiko").
b. Funzo tunalolipata leo kutokana nakushindwa kwao.
2. Haruni na Miriamu walimuonea wivu Musa. Miriamu alipigwa na ukoma. Nini ilikuwa sababu ya adhabu hii na uoneshe jinsi gani tunaweza kuteswa na tatizo hilina namna ya kuepuka dhambi hii.