CSSA 2-2-18 - BAPTISED INTO MOSES

Swahili

 

168. WAKABATIZWA WAWE WA MUSA

Taifa la Israeli lilikuwa limekaribia kuzaliwa! BWANA alikuwa amefanya Jina lake kuwa kuu katika Misri, na sasa akamwagiza Musa kuwaongoza Israeli kuondoka. Kuvuka Bahari ya Shamu ni tukio lenye maana kamili, na sisi inatubidi kujaribu kuelewa umuhimu wake. Sisi pia, tunaitwa ili kuyacha maisha ya giza, na kubatizwa kwa ajili ya maisha mapya ya “kutembea nuruni”, yaani, kwa kufuata Neno la Mungu.

 

KUTOKA 14

KUIACHA MISRI NYUMA

Pigo la mwisho lilikuwa limevunja upinzani wa Farao. Katika huzuni yao kwa ajili ya wazaliwa wao wa kwanza waliofariki, Wamisri hawakuwazuia tena Waisraeli walipoondoka.

 

Wanaume 600,000 (laki sita) pamoja na wake zao na watoto wakiwemo  pia baadhi ya Wamisri waliotaka kwenda pamoja nao, wakasafiri wakiteremka kuelekea Sukothi na kupiga kambi pale (Kutoka 12:37, 38). Kwa shangwe  kuu wakatengeneza vibanda vyao vya kuishi na wakasherehekea ukombozi wao. Baadaye wakati Israeli ilipoanzishwa katika  nchi ya ahadi walisherehekea tukio hili kwa kukaa katika vibandani kila mwaka wakati wa sikukuu ya vibanda (Walawi 23:39-43).

 

Wakaondoka Sukoti wakasafiri hadi Ethamu ukingoni mwa jangwa (Kutoka 13:20). Mungu sasa alikuwa anaongoza njia kwa nguzo ya wingu  wakati wa mchana na kwa nguzo ya moto wakati wa usiku (mstari 21,22). Ni kwa nini Mungu aliwaongoza kuelekea kusini  maana alikuwa anaweza  kuwaongoza kupitia barabara kuu ya biashara kuelekea kasikazini mashariki?

 

 

Pamoja na kuwaongoza njia hadi ukombozi wa mwisho kutoka Misri, Mungu alifahamu pia kwamba watu hawakuwa tayari kwa ajili ya kupigana vita na kuitamalaki nchi (Kutoka13:17,18; Kumb. 8:2-6). Waltakiwa kujiandaa kama taifa na wapewe sheria. Sinai, pamoja na ukimya wake, umbali wa utisho wa mlima na uwandaa mpana, palifaa kufaa kwa kusudi hili.  Na kwa hiyo ndiko walikoelekea.

 

WANAFUATWA NA FARAO

Musa akawaongoza watu upande wa magharibi wa bahari ya Shamu. Wakaweka kambi yao mahali paitwapo Pi-Hahirothi ambalo lilikuwa  eneo kame lenye milima ya miamba na yenye miteremko mikali kuelekea baharini (Kutoka 14:1-3). Eneo lenyewe lilikuwa la ukimya mzito na la kutisha, nao Israeli “walipoinua macho yao”, wakaona vumbi la  jeshi la Farao likiwafuata! Wakiwa wamezungukwa na milima kila upande, na bahari mbele yao na jeshi kubwa lenye nguvu la Wamisri likiwafuata mbio, Israeli walifadhaika sana. Watu wakashikwa na hofu kuu na wakaogopa sana. Farao alikuwa amesikitikia uamuzi wake wa kuwaachilia waende kwa hiyo “aliwafuatia nyuma kwa haraka”na akadhamiria kuwarejesha na kuwaangamiza Waebrania aliowachukia.

 

Ilikuwa ni mazoea yao kuwaogopa Wamisri, kwa hiyo wakamgeukia Musa na kumlalamikia kuwa aliwaleta huko jangwani kufa! (Kutoka 14:10-12).

 

Lakini, Musa alikuwa mtulivu na mwaminifu. Kwa ujasiri aliwatuliza watu ili wasiogope kwa maneno; “Msiogope, simameni tu, na mkauone wokovu wa BWANA …BWANA Atawapigania ninyi  nanyi mtanyamaza kimya” (Kutoka 14:13,14)

 

UKOMBOZI KUPITIA BAHARI

Mungu akampatia Musa maagizo yake na kisha akaihamisha nguzo ya mawingu na kuiweka kati ya Wamisri na Waisraeli. Wakati Wamisri walipohangaika kupapasa papasa gizani, Waisraeli walipewa nuru kuona, na kujitayarisha kuendelea.

 

Musa akawaongoza wana wa Israeli mpaka ukingo wa Bahari ya Shamu. Usiku kucha upepo wa nguvu kutoka mashariki ulivuma, ukiyafanya maji ya Bahari kusimama kama ukuta na kuweka njia ya kupitia Baharini (mstari 21 soma maelezo ya pembeni)

 

Ilipofika alfajiri mapema –Musa akawapa  wana wa Israeli amri ya kusonga mbele. Wana wa Israeli, wakaupokea mwujiza uliofanyika kwa ajili yao, waliharakisha kuvuka. “Kwa imani wakata  katika Bahari ya Shamu kama katika nchi kavu” (Waebrania 11:29).

 

Wamisri sasa, wakaweza kuona yaliyokuwa yakitendeka, wakajitumbukiza kwenye njia wakiwafuatia! Lakini, bahati mbaya yao, magurudumu ya magari yao ya vita yakachomoka, farasi wakatapatapa ovyo, na walikuwa wamechanganyikiwa kabisa. Ndipo walipotambua  kwamba walikuwa wakipigana na Mungu wa Israeli, ndipo wote wakataharuki sana (Kutoka 14:23-25).

 

Musa akaagizwa kunyosha fimbo yake tena. Alipofanya hivyo, Bahari ikaanguka kingoni mwake juu ya Farao na jeshi lakelote. Hata mmoja wao hakupona!

 

MAISHA MAPYA

Wakiwa huru sasa, wakiwa wamekombolewa kutoka katika utumwa na kupona kifo, Israeli walifurahia ukombozi wao. Wimbo mzuri ajabu wa ukombozi ukaimbwa na Musa na watu wote, kama ulivyoandikwa katika Kutoka 15:1-21. Hakika  BWANA alikuwa ameshinda kwa utukufu mkuu! (mstari 1)

 

Mungu kwa kweli ni mwokozi na mponyaji mwenye kuweza kutenda maajabu katika taabu ya watu wake.

 

Paulo anasema kuvuka huku ni sawa na ubatizo (1Wakorintho 10:1-5). Ni mfano uliokusudiwa ili kutufundisha sisi mambo makuu ya Mungu atakayotenda kwa ajili yetu iwapo kwa imani “tutadumu katika imani” na kuitii amri yake Mungu kwa kukubali kubatizwa (linganisha Kutoka 14:15)

 

Wakati wa “kuzikwa” katika maji ya ubatizo, tunakuwa kama Waisraeli wa kale: Kwa kuyaacha matendo yetu ya zamani. Tunapoibuka kutoka ndani ya maji ili tuishi  “maisha mapya” (Warumi 6:3,4), tunakuwa kama wana wa Israeli  waliokuwa wamesimama kwenye ukingo wa mashariki wa bahari. Ndipo sasa tumekombolewa kutoka utumwani, tukifahamu kuwa Mungu ni mkuu kuliko nguvu za dunia ambayo ilituweka utumwani hapo mwanzo.

 

Mbele yetu linasimama “jangwa la maisha yetu” pamoja na njia nyembamba ambayo inaongoza kwenda kwenye urithi wa milele katika Ufalme wa Mungu. Ukombozi huo unasababisha sisi tumtumikie Mungu kila siku ya maisha yetu, kwa furaha na kwa shukrani. Mungu, ambaye ametenda makubwa mengi kwa ajili yetu,  hakika anastahili kusifiwa nasi kwa kweli.

 

Na nyuma yetu  kuna maisha yetu ya zamani, tuliyoishi katika kiutumikia dhambi. Imani kwa Mungu aliyetukomboa sisi na maisha ya kujiweka wakfu katika kumtumikia Mwokozi wetu mwishowe itatuletea ushindi dhidi ya adui yetu mkuu kuliko wote –kifo (1Wakorintho 15:22, 23; Warumi 6:23).

 

MUHTASARI:

  • Wakati Mungu alipowatoa Israeli kutoka Misri, aliwaongoza kuelekea kusini mpaka jangwani ili kuindoa Misri kutoka kwao, ili kuwalinda kutokana na vita na kuwaanzisha kuwa taifa.

 

  • Sisi pia tunaadabishwa kwa njia ya mateso na majaribu kwa ajili ya kuanza na mwenendo mzuri na kutuweka  kuwa wenye kustahili kwa ajili ya Ufalme.

 

 

  • Kukiwa na milima  upande wa kushoto na upande wa kulia, bahariikiwa mbele, na adui wakiwa nyuma yao, somo kubwa la Mungu alilowafundisha Israeli (na sisi) ni kwamba pasipo yeye hakuna wokovu. Sisi pia tumezoea mkono wa ulinzi wa Mungu, ambaye aatuokoa  tisiangamizwe na watu waliotaka kutuangamiza.

 

  • Wakihofia kifo lakini wakimwamini Mungu, Israeli waliendelea na safari ya kuvuka Bahari ya Shamu na kwa hiyo “wakabatizwa kuwa wa Musa” (1Wakorintho 10:2)

 

 

  • Mara tunapopata kufahamu  ujuzi wa Kweli tunaweza kuokolewa kutoka katika utumwa wa dhambi na kifo, kwa kubatizwa katika Kristo.

 

MAKTABA YA REJEA

“Tumaini la Israeli” (J. Thomas) –  Sehemu 2, sura 4,ukurasa 292-293

“Mkono wa Mungu Usioonekana” (R. Roberts) – sura 14

“Mkufunzi wa  Christdefia” – Maswali na Majibu Na. 58 hadi 63

“Hisoria ya  Biblia” (H.P. Mansfield) ukurasa. 278

“ Maisha  ya Jangwani” (J. Martin) –C.S.S.S. Maelezo

 

MASWALI YA VIFUNGU

  1. Ni kwa nini Mungu aliwaongoza wana wa Israeli kuelekea kusini alipowatoa kutoka Misri?
  2. Je,watu walifanya nini walipofuatwa na Farao? Je,kulikuwa na kosa gani katika hisia zao?
  3. Ni gani Mungu aliwaokoa Israeli kutokana na jeshi la Farao lililokuwa likiwafuatia?
  4. Ni kwa njia gani ubatizo ni kama kule kuvuka kwa wana wa Israeli katika Bahari ya Shamu?

 

MASWALI YA INSHA:

  1. Elezea tendo la kuvuka Bahari ya Shamu na mwisho wa Wamisri.

Kutokana na msingi wa ukombozi wa Israeli pale Bahari ya Shamu elezea tofauti “kati ya maisha tunayoyaacha nyuma tunapobatizwa na katika maisha mapya tunayokuwa nayo ndani ya Kristo.

 

 

 

Swahili Title
168 WAKABATIZWA WAWE WA MUSA
Translator 1
Jonathan Nkombe
Literature type
Sub type
Sub sub type