Who are the Christadelphians - Lesson 02

Swahili

Somo la 2

WAKRISTADELFIA NI WATU GANI?

Somo: Yohana 15

Lengo la kozi hii ya Biblia ni kuelekeza fikra zako kwenye Maandiko Matakatifu. Lakini, unaweza ukajiuliza Wakristadelfia ni watu gani, kwa hiyo tutakuambia machache juu yetu.

Wakristadelfia ni jumuia pana kimataifa, ya wanaume na wanawake, wanaoisoma Biblia yote na kuikubali kuwa ni Neno lililotoka kwa Mungu. Wanaziamini ahadi zilizopo katika Agano la Kale na Agano Jipya zinazomhusu Bwana Yesu Kristo, na hatma ya ulimwengu. Wanasubiria kurudi kwa Yesu kutoka mbinguni, kuusimamisha Ufalme wa Mungu duniani.

Neno Kristadelfia linatokana na maneno mawili ya Kiyunani (Kigiriki), yenye maana ya ‘Ndugu katika Kristo’.

Wakristadelfia wanaishi wapi?

Kuna Wakristadelfia kwenye nchi zaidi ya 50; wapo Uingereza na maeneo mengi katika Ulaya, wapo kwenye nchi zaidi ya 30 katika Afrika, wapo Mashariki ya Mbali- kutoka India hadi Indonesia, wapo Australia na visiwa vya Bahari ya Pasifiki, wapo Amerika ya Kaskazini na Kusini- kutoka Kanada kwenda chini mpaka Argentina, na katika visiwa vya Karibeani. Ni jumuiya yenye mchanganyiko wa watu wa rangi nyingi na tamaduni tofauti tofauti.

Wanaamini nini?

Wakristadelfia wanachukulia imani yao katika mambo yaliyokuwa yakiaminiwa na kufundishwa na Yesu na wanafunzi wake kama miaka 2000 iliyopita. Ujumbe wa kweli wa Ukristo haujabadilika. Kwa bahati mbaya, katika karne zote hizi zilizopita, makanisa mengi ya Kikristo yameuacha ukweli na kufuata mafundisho yenye misingi yake katika imani za kipagani. Hata hivyo, kwa nyakati mbalimbali kumekuwa na vikundi vidogo-vidogo vilivyoishikilia imani ya kweli.

Kwa mfano katika Ulaya, zaidi ya miaka 400 iliyopita kulikuwa na watu wengi waliojifunza Injili ya kweli kwa kuisoma Biblia wenyewe, wakati ilipochapishwa katika lugha zao za kiasili. Watu hawa walijiita ‘Ndugu katika Kristo’. Cha kuhuzunisha, wengi wao waliteswa au kuuawa kutokana na imani yao. Wengi walilazimika kuzihama nyumba zao, lakini waliibeba Injili na kuisambaza Ulaya na kwenye nchi za ng’ambo.

Haikuchukua muda, hata hivyo, ukweli ukawa tena umechanganywa na mafundisho potofu. Kuna fundisho katika hili: ukweli unadumu tu pale watu wanaompenda Mungu, wanapokuwa wanasoma na kujifunza wenyewe Neno la Mungu.

Jumuiya ya Wakristadelfia ilianzaje?

Katika mwaka 1832 daktari mmoja wa Kingereza kwa jina la John Thomas, aliyekuwa mhudumu wa kanisa, alipanda meli iliyokuwa ikielekea New York, Amerika, kwa kuwa baba yake alitaka kuishi Marekani.

Meli hiyo ilipata msukosuko wa dhoruba kali baharini kiasi kwamba, dokta Thomas alifikiri wangeangamia. Alistukia hakujua vya kutosha juu ya kile hasa kinachomtokea mtu anapokufa. Alijiapia kuwa kama angepona na kuifikia nchi kavu, asingetulia mpaka aupate ukweli wote juu ya uhai baada ya kifo.

Kwa bahati aliweza kufika New York, na akawa mkweli kwa neno lake. Aliitumia miaka kumi na mitano iliyofuata kwa kujifunza Biblia kwa umakini sana, huku akiipima na kuilinganisha na madai ya makundi mbalimbali ya ‘Ukristo’. Alipokuwa amejihakikishia kuwa ameelewa vizuri mambo yaliyoandikwa katika Agano la Kale na Agano Jipya, kumhusu Yesu Kristo na Ufalme wa Mungu unaokuja katika dunia, alifanya mpango akabatizwa kwa kuzamishwa kwenye maji. Alifanya mahubiri mengi ya hadharani katika Amerika na Uingereza, na kuandika vitabu na kuchapisha magazeti ya kidini.

Kati ya wale waliopata mafundisho yake na kujiunga na John Thomas katika kazi yake ya kuhubiri, kulikuwa na bwana mmoja wa Scotland aliyeitwa Robert Roberts. Huyu alisaidia sana katika kuwaweka pamoja walioamini katika vikundu vya wafuasi tunavyoviita ‘Eklesia’. Hili ni neno la Kibiblia lenye maana ya ‘kusanyiko la watu walioitwa’. Wakristadelfia wanapenda kulitumia neno Eklesia zaidi badala ya neno ‘Kanisa’; neno ambalo mara nyingi linatumiwa na wengi kumaanisha jengo, badala ya watu.

Jina Kristadelfia linaweza kuonekana la ajabu kidogo mwanzoni

Jina ‘Mkristadelfia’ au ‘Wakristadelfia’ lilianza kutumiwa kwa mara ya kwanza mwaka 1862, wakati waumini katika Amerika walipoitaka serikali yao ya Marekani iwasamehe kujiunga na jeshi, wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Marekani. Wakiwa wameona haja ya kuwa na jina la kuweza kujitambulisha kama washiriki wa kundi moja (lililo tofauti na madhehebu zingine), John Thomas aliwakumbuka wale Ndugu katika Kristo wa miaka 300 nyuma, hivyo akalibuni jina ‘Christadelphian’ ambalo ni namna ya Kiyunani ya kusema ‘Ndugu katika Kristo’.

Hawa Wakristadelfia wa karne ya 19 walikuwa wakisafiri sana, na walihubiri katika maeneo mengi ya dunia walipokwenda, na ilipofika mwishoni mwa karne hiyo kulikuwa na vikundi vingi vya waumini katika nchi nyingi.

Wakristadelfia wanajipangaje?

Kuna kamati kadhaa zinazopanga mambo kuhusiana na kazi ya kueneza Injili, na zingine za kuwaangalia wagonjwa, wazee na wale walio katika mazingira ya upweke. Tunazo pia ofisi katika nchi chache kwa ajili ya kuchapisha magazeti, vitabu na majalida mbalimbali. Lakini, hatuna wahudumu wa kulipwa, wala Makao-makuu. Mahitaji ya kifedha yanashughulikiwa kwa michango ya hiari inayotoka kwa wanajumuia wetu. Hatuna ‘wachungaji’.

Lakini utapenda kuuliza: kama hakuna mfumo wa uongozi unaotoka Ofisi-Kuu, unaowaunganisha waumini, Wakristadelfia wanajiendeshaje? Jibu ni kwamba, imani ya namna moja tuliyonayo na mambo ya pamoja tunayofanya, ndivyo vitu vinavyotuweka katika ushirika wa namna moja, unaotuunganisha wote.

Kila Eklesia ilipo, inajiendesha yenyewe kwa kuchagua ‘wazee’ wake wanaoongoza mambo. Hao wanapatikana kwa kupiga kura (kwa kawaida) mara moja kwa mwaka. Wale wanaochaguliwa wanalitumikia kusanyiko lao katika kutekeleza majukumu mbalimbali kama ya Ukatibu, kuwa Mweka Hazina, au kuwa Mwenyekiti wa mikutano (kuwa Mwongoza-Ibada).

Hawalipwi kwa kazi wanayofanya na sio ‘makuhani’. Tunaamini ya kuwa, Bwana Yesu, akiwa sasa mbinguni, ndiye aliye pekee Kuhani wetu, ambaye kupitia kwake waumini wote waliobatizwa, wanaweza kutubia dhambi zao kwa njia ya maombi. Wakristadelfia hawajengi majengo makubwa yanayoonekana ki-kanisa. Hata hivyo, kuna baadhi ya Eklesia katika sehemu mbalimbali zenye kumbi zao, au vyumba, wanapokutania na kutangazia imani yao. Kwingineko wanatumia vyumba vya kupanga, au madarasa ya shule au kumbi za kijamii.

Imani moja

Wakristadelfia, bila kujali walipo ni wapi katika dunia, wamesoma na kujifunza Biblia zao wenyewe au kuhubiriwa, na kuja kuamini mambo yanayofanana na ya kuaminika. Kwa zaidi ya miaka 100 tumekuwa na Tamko la Kiimani ambalo kila muumini analikubali kuwa ni msingi wa ushirika wake na waumini wengine.

Tamko hilo ni muhtasari ya mafundisho ya Kibiblia waliyojifunza. Kabla mtu yeyote hajabatizwa kuweza kuwa Mkristadelfia, ni lazima ajiridhishe mwenyewe kuwa ameelewa mafundisho ya muhimu ya Biblia, na ni sharti akubaliane kabisa na imani yetu iliyojengekea kwenye Biblia, na aridhie yale yanayofanyika. Hili ndilo linalowaunganisha Wakristadelfia pamoja. Andiko linasema, kuna:

“Mwili mmoja…Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja” (Waefeso 4:4-5).

Hili limetuwezesha Wakristadelfia popote pale tulipo, kuwa na ushirika wa kufurahia na wa maana sana mmoja kwa mwingine.

Tunataka kuwaje?

Sisi wote tunahitaji msaada wa Mungu. Kitu kimoja tunachokifanya kila siku ni kusoma Biblia. Hili ni jambo la maana kama kupata chakula chetu cha kila siku. Mara moja kila juma tunakutana Kumega-Mkate (kula kipande kidogo cha mkate na kunywa divai kidogo) kwa kuyakumbuka mauti ya Bwana Yesu Kristo. Kwa kufanya hivi tunakuwa tukitekeleza amri ya Yesu, kama alivyotuagiza akisema tufanye hivyo kwa kumkumbuka.

Tunajitahidi kwa kadri ya uwezo wetu, kuweka imani yetu katika matendo kwa kuangalia sana jinsi tunavyoishi. Kwa kuwa Yesu anarudi hivi karibuni, tunapenda tuwe tayari kwa ujio wake. Hili lina maana ya kuishi maisha yaliyo safi katika KWELI; lina maana ya kujiepusha na ulevi, zinaa, kucheza kamari na mambo mengine maovu.

Wakristadelfia ni raia wema katika nchi zao. Wanajitahidi kufanya mema wanayoweza, na hawapambani au kuwapeleka watu mahakamani. Wanakuwa na mke mmoja, na ni kinyume kwao kufanya ngono kabla ya kuoa au kuolewa, au nje ya ndoa. Tunatambua kuwa wengine wanakuwa walishakuwa na wake zaidi ya mmoja kabla ya kubatizwa; jambo hili limejadiliwa katika somo la 33.

Ushirika wa Kibiblia wa Kikristadelfia (CBM)

Ushirika huu, CBM, kama tunavyouita, upo kwa ajili ya kuihubiri Injili ya Ufalme wa Mungu duniani pote. CBM inatangaza kozi za mafunzo na inachapisha machapisho mbalimbali kuwasaidia watu waielewe Biblia. Ni ushirika wenye watumishi wa kujitolea wa Kikristadelfia wanaoifanya kazi hii pamoja na kazi zao zingine. Kusudi lake ni kuwasaidia watu, wanaume kwa wanawake, kujifunza Injili, na kuwatia moyo watubu na kubatizwa, na kuufuata mfano wa Yesu na mitume wake.

Tunataka kukushirikisha imani sahihi, tumaini na furaha

Wakristadelfia wanaamini kikweli kuwa, imani yao ni kielelezo cha Injili ya Kweli, kama ilivyo katika Biblia. Tunatumaini kuwa, wewe nawe unaweza kufurahia kuigundua KWELI. Inaridhisha sana; sio tu kwa sababu ya ukweli uliomo ndani yake, bali inaleta pia tumaini, furaha na upendo katika maisha yako. Mungu akubariki sana katika kumtafuta. Mafundisho kadhaa ya Kibiblia yameandikwa hapo chini.

Mistari ya kusoma: Zaburi 119:130, Mathayo 28:19-20, Yohana 17:3

Jifunze kwa moyo: Yohana 15:13-14

“Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.   Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo”.

Baadhi ya mafundisho ya muhimu ya Biblia:

  • Biblia ni ujumbe wa kweli kutoka kwa Mungu.
  • Kuna Mungu mmoja tu, Muumbaji, ambaye anaongoza mambo yote ya dunia hii.
  • Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu, aliyezaliwa na Mariamu. Alikuwa mtu pekee ambaye hakufanya dhambi. Alikufa msalabani kuwaokoa wale wanaomwamini. Alifufuliwa kutoka kaburini na sasa yupo mbinguni.
  • Yesu atarudi hivi karibuni kutoka mbinguni. Akirudi atausimamisha Ufalme wa Mungu duniani. Atatawala kama Mfalme, na Makao Makuu yake yatakuwa Yerusalemu katika Nchi ya Israeli.
  • Wayahudi ni mashahidi wa Mungu wa kusudi lake, hata kama wapo kati yao ambao hawalitambui hili. Mungu alifanya maagano na Ibrahimu na Daudi ambayo yatatimizwa Yesu atakaporudi.
  • Kifo ni adhabu kutokana na dhambi, na watu wote ni wadhambi. Tumaini pekee la uhai baada ya kifo ni katika miili kufufuliwa kutoka kwenye kaburi katika kurudi kwa Yesu.
  • Kutakuwa na hukumu. Wale walio wafuasi waaminifu wa Yesu watapewa uzima wa milele na watamsaidia kutatua matatizo ya dunia na kuleta amani na mibaraka kwa mataifa yote.
  • Ni lazima tuiamini Injili, tutubie dhambi zetu na tubatizwe. Kama tukiendelea kujitahidi kuzitii amri za Mungu, na kuomba msamaha tunaposhindwa, ndipo tutakapookolewa.
  • Unabii wa Biblia kuhusu matukio duniani kwa nyakati za nyuma na sasa, umetimia na unatimia wote. Ishara zinaonesha kuwa, kurudi kwa Yesu Kristo duniani kumekaribia sana. Ndio maana unapaswa kujifunza Biblia yako sasa.
Swahili Title
Wakristadelfia ni watu gani? - Somo la 02
Swahili file
PDF file
Chichewa file
Arabic file
African text
Christadelphian Bible Mission