Correspondance Course - Lesson 03

Swahili

Somo la 3

Somo: Zaburi 119:1 – 40

Madai ya Biblia

Biblia inadai kuwa ni Neno la Mungu; ni neno lenye ‘pumzi’ ya Mungu (2 Timotheo 3:16). Mungu aliwaongoza watu waliochangia kuiandika, kwa hiyo walichoandika ni ujumbe wake Mungu. Mara nyingi katika Agano la Kale, manabii wanasema: “Bwana Mungu anasema………”

Kama Biblia sio Neno la Mungu, basi haina umuhimu sana. Lakini, kama ni kweli ni ujumbe wa Mungu kwa mwanadamu, basi ni muhimu sana kuisoma na kujaribu kufanya kile inachosema. Kama tunaudharau ujumbe wa Biblia, tunamdharau Muumba wa Enzi yote.

TUNAJUAJE KUWA BIBLIA NI YA KWELI?

Biblia inatabiria mambo yajayo

Hatuwezi kujua litakalotokea kesho. Biblia imesemea katika sehemu nyingi mambo ambayo yangetokea mbeleni, mamia ya miaka kabla hayajatokea. Unabii wa namna hii umetimia kama ilivyosemwa, hata kwa vitu vidogo-vidogo sana. Hapa kuna mifano michache.

Kuzaliwa kwa Yesu:

Katika Mathayo 2 tunasoma kuwa Mamajusi walikuja kwa Herode na kuuliza, “Yuko wapi yeye aliyezaliwa, Mfalme wa Wayahudi?” Sasa Herode aliwauliza wakuu wa Makuhani hili swali, na wakamjibu, ni: “Katika Bethlehemu ya Uyahudi”. Walijuaje? Ni kwa kuwa, mamia ya miaka nyuma, ilikuwa imetabiriwa hivyo na kimojawapo cha vitabu vya Agano la Kale (Mika 5:2).

Kifo cha Yesu

Fungua Zaburi ya 22 na isome kwa uangalifu. Katika Zaburi hii kuna maelezo ya kifo cha Yesu kwa kuwambwa msalabani. Hebu angalia zaidi msitari wa 16, “Wamenizua (wamenipigilia) mikono na miguu”. Angalia tena msitari wa 18, “Wanagawanya nguo zangu, na vazi langu wanalipigia kura”.

Sasa, kama unaisoma Injili ya Yohana 19: 23, 24 utaona kuwa hivyo ndivyo wale askari walivyofanya, baada ya kumpigilia Yesu msalabani. Mwandishi wa Zaburi aliwezaje kusemea vile ambavyo kifo cha Yesu kingetokea mamia ya miaka nyuma, kama aliloandika halikutoka kwa Mungu? Hili ni jambo la ajabu hata zaidi tukizingatia kuwa, katika enzi hizo za mwandika-Zaburi, Wayahudi hawakuwa wakijua chochote kuhusu kuua au kuuawa kwa kupigiliwa msalabani; wahalifu wao waliuawa kwa kupigwa mawe.

Matukio makuu yalitabiriwa

Soma Isaya 13:19, 20. Katika wakati nabii Isaya alipoyaandika maneno haya kuihusu Babeli, Babeli lilikuwa ni taifa kubwa kuliko yote duniani, lenye nguvu na utukufu. Sasa, pale kulipokuwa Babeli nyakati hizo, kumebakia tu mahame kwenye eno ambalo ni nusu-jangwa.               

Imekuwa vile vile kama nabii Isaya alivyosema, mamia ya miaka baada ya unabii huo kutoka. Ni Mungu peke yake ambaye angeweza kujua kuwa mabadiliko makubwa kiasi hicho yangetokea. Kuna mifano mingi kama hii. Ni Mungu pekee awezaye kuyaona ya mbele, na unabii ulioandikwa katika Biblia unathibitisha kuwa, ni Mungu aliyewaambia hao walioandika kitu cha kuandika.

Wataalam wa Kihistoria wanaochimbua chini (Archaelogists), wamevumbua uthibitisho wa vitu vingi vinavyozungumzwa kwenye Biblia. Kwenye mabaki ya kale wamegundua kuwa, miji ya Sodoma na Gomora ni kweli ilikuwapo (Mwanzo 19). Wameigundua pia miji ya Ai, Ashkeloni, Betheli, Bethshemeshi, Gibea, Hazori, Yeriko, Lakishi, Megido, Samaria, Shechemu na mingine mingi iliyotajwa katika Biblia.

Biblia haijabadilika karne zote hizi

Kati ya vitabu vya kale vilivyogunduliwa katika eneo la Dead Sea mwaka 1947 ni gombo la nabii Isaya. Lilikuwa limeandikwa kama miaka 2,000 nyuma. Maandiko ni kama yalivyo kwenye kitabu cha Isaya leo. Ujumbe wa Biblia haubadiliki kufuatana na wakati!

Kitabu cha kale

(Gombo)

Yesu aliliamini Agano la Kale

Wapo watu leo wanaolicheka wazo kuwa Adamu na Hawa walikuwa watu kikweli, na kwamba Nuhu alijenga kweli Safina na kuwaweka wale wanyama wote ndani yake. Wanafikiri wanajua zaidi, kuliko kuamini hadithi kama ile ya Yona kumezwa na samaki mkubwa. Lakini, Yesu aliviamini vitu hivi!

Yesu aliamini mafundisho ya Agano la Kale kuwahusu:

  • Adamu na Hawa                        (Tazama Mathayo 19:4,5)
  • Nuhu na gharika                        (Tazama Luka 17:26, 27)
  • Lutu na mkewe                         (Tazama Luka 17:29-32)
  • Ibrahimu, Isaka na Yakobo         (Tazama Mathayo 8:11)
  • Daudi na Sulemani                    (Tazama Mathayo 12:3, 42)
  • Yona na nyangumi                     (Tazama Mathayo 12:40

 

Hatuwezi kuyapuuza alichosema Bwana Yesu Kristo. Alifufuliwa na Mungu baada ya kufa kwa siku tatu. Hili ni tukio la kweli katika historia, ambalo watu wenye busara walio wengi wanalikubali. Muujiza kama huo ungeweza tu kufanywa kwa uweza wa Mungu.

Hakuna ambaye ameweza kuithibitisha Biblia kusema uongo

Maadui wengi wa Biblia, wakiwepo baadhi ya watu wajanja sana, wamejaribu kufanya hili, lakini wote wameshindwa. Kama ni hivyo, ni lazima tukubali kuwa sio kitabu cha kawaida.

Je, unajua kuwa:

  • Biblia ilichukua karibu miaka 2,000 kuandikwa?
  • Iliandikwa na wachunga-kondoo, wavuvi, daktari, mtengeneza mahema na wengineo?
  • Ina jumla ya vitabu 66, na kwamba 39 kati yake ni vya Agano la Kale na 27 ni vya Agano Jipya?
  • Waandishi hao wote kwa pamoja wanatupa  hadithi moja iliyokamilika; habari ya kusudi la Mungu na wanadamu?
  • Karibu waandishi wote walikuwa Wayahudi?
  • Sehemu kubwa ya Biblia ni juu ya Wayahudi?

Ufuatao ni mwongozo wa juu-juu kukuonesha yaliyomo katika sehemu mbalimbali za Biblia:

AGANO LA KALE

KITABU

YALIYOMO

 

MWANZO

 

 

KUTOKA, MAMBO YA WALAWI, HESABU,

KUMB. LA TORATI

 

YOSHUA---ESTA

 

 

ZABURI---WIMBO ULIO BORA.

 

ISAYA---MALAKI

 

Mwanzo wa dunia na mahusiano ya Mungu na wanadamu wa kwanza.

 

Vitabu hivi vinatuambia jinsi Mungu alivyowateua Wayahudi kuwa watu wake na kuwatoa Misri, na kuwapa nchi ya Kanaani (Israeli).

 

Historia ya Wayahudi inaendelea kuzungumziwa katika vitabu hivi.

 

Hivi ni vitabu vya ushairi na hekima.

 

Hivi ni vitabu vya manabii. Waliwaambia na kuwakumbusha Wayahudi walivyopaswa kumtii Mungu. Wanaongelea pia matukio mengi ya muhimu ambayo yalipaswa kutokea katika historia ya ulimwengu. Baadhi ya haya yanaendelea kutokea katika nyakati zetu hizi, na mengine ni ya mbele zaidi.

 

AGANO JIPYA

KITABU

YALIYOMO

MATHAYO, MARKO, LUKA,  YOHANA

 

MATENDO YA MITUME

 

 

 

WARUMI ---YUDA

 

 

UFUNUO YA YOHANA

Hivi ni vitabu vinne tofauti-tofauti vya maelezo ya maisha ya Kristo, kifo na kufufuka kwake kutoka kwa wafu.

 

Hiki ni juu ya eklesia za kwanza kuanzishwa, na jinsi Wakristo wa karne ya kwanza walivyokuwa. Wanapaswa wawe ndio mwongozo wetu leo.

 

Ni nyaraka (barua) mbalimbali zilizoandikwa na mitume, ili kuyafundisha hayo makanisa machanga.

 

Ni kitabu cha unabii.

(Kama unahitaji orodha kamili ya vitabu vya Biblia, utaipata katika ukurasa wa mwanzoni wa Biblia yako)

Kuna maandiko mengine Mungu aliyojifunua kwayo?

Jibu kwa swali hili ni, “Hapana”. Kuna dini nyingi katika dunia, na nyingi zina vitabu vyake ‘vitakatifu’. Waislamu, kwa mfano, wana Kuruani, wanayoichukulia kuwa ni Neno la Mungu. Wamormoni wana Kitabu cha Mormoni, wanachosema wametumiwa na Mungu. Zipo sehemu za vitabu hivi zinazochukulia baadhi ya mafundisho yake kwenye Biblia, na zinatoa nasaha za maana na za hekima. Lakini, katika maeneo mengi, vitabu hivi havikubaliani na ujumbe wa Biblia.

Sasa si kitu kinachoweza kueleweka, kama Mungu angeweza kusema kitu hiki katika kitabu kimoja, na kitu kingine tofauti katika kitabu kingine. Ni kimoja tu kinachoweza kweli kuwa Neno lenye pumzi ya Mungu, na Biblia inadai ndio hilo Neno.

Biblia – Mwongozo wa maisha ya mwanadamu

Mungu aliona hali ya kusikitisha iliyoko kwa mwanadamu, mdhambi, na akamtuma mwanawe, YESU, kufa, watu waweze kuwa na tumaini la uzima wa milele. Yesu Kristo naye ametuonesha namna tunavyoweza kuishi maisha yanayoweza kumpendeza Mungu. Biblia inayo mifano mingine ya ‘watu wa imani’, na inatuonesha jinsi baadhi yao walivyoshindwa. Habari za Wayahudi zinatuwezesha kujifunza kutoka katika makosa yao.

HITIMISHO

Ni wazo kubwa kuwa, Mungu wa mbinguni ametupa kitabu kusudi tuweze kumjua, na kuishi kwa namna anavyotutaka tuishi. Amewaambia kiuhakika wanaume na wanawake katika kitabu chake hiki sababu ya kuiumba dunia, na vile historia yake itakavyokuwa, mpaka wakati Injili itakapotimizwa, na Mungu kuwa ‘yote katika wote’.

Biblia ni mwongozo ambao Mungu ametupa, unaotuonesha njia ya Uzima wa Milele katika Ufalme wake. Hakuna kitabu kingine kama hiki; sio maandiko yaliyokufa, ni Neno la uzima. Kama tukikisoma kila siku kwa umakini na kwa kuomba, kitayabadili maisha yetu, na kuyafanya yawe ya kumpendeza Mungu.

Muhtasari

  1. Biblia ni kitabu cha kipekee. Kinadai kuwa ni Neno la Mungu kwa mwanadamu.
  2. Biblia inatoa kwa watu tumaini la uzima.
  3. Yesu aliyaamini Maandiko ya Agano la Kale.
  4. Kuna ushahidi mwingi kuwa Biblia ni ya kweli, historia yake imethibitishwa na uvumbuzi wa kisasa. Inayo ndani yake unabii mwingi ambao umetimia.
  5. Biblia inatupa historia ya Mungu anavyoshughulika na mwanadamu, tangu alivyomuumba mtu wa kwanza, mpaka hapo ulimwengu utakapojazwa na Utukufu wake.
  6. Biblia ni hazina ya Mungu kwetu, inayotuonesha namna ya kusihi. Tunapaswa kuisoma kila siku.

Mistari ya kusoma:  Zaburi 1,  Zaburi 22,  2 Timotheo 3

Jifunze kwa moyo:  2 Timotheo 3: 16 – 17

  “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwadibisha katika haki, ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema”.

Swahili Title
Madai ya Biblia - Somo la 03
Swahili file
PDF file
Chichewa file
Arabic file
African text
Christadelphian Bible Mission